Warsal, Poland. Kampuni ya Ursus ya Poland imesema ina mkakati
wa kujenga kiwanda cha kutengeneza matrekta Tanzania kwa kushirikiana na
kampuni ya Suma JKT.
Rais wa Bodi ya Ursus, Karol Zarajczyk alisema
hayo jijini Warsaw jana wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokutana na
wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza Tanzania.
Zarajczyk alisema wanataka kujenga kiwanda hicho
kwa kuwa wametambua Tanzania ina fursa ya kufungua milango ya kibiashara
kwa nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.
Alisema lengo jingine la kampuni hiyo
inayotengeneza matrekta ni kutoa mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya
kutunza matrekta hayo, ili waone umuhimu wake katika sekta ya kilimo.
“Barani Afrika tulianza kupeleka matrekta Ethiopia, Ghana na Guinea. Sasa hivi tumeamua kwenda Tanzania na Zambia.
“Nia yetu siyo kujenga tu kiwanda, bali pia kutoa huduma kwa wakulima juu ya uendeshaji na utunzaji wa matrekta hayo,” alisema.
Alisema wako tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa
Tanzania waliopo vyuoni ili waweze kuunganisha matrekta hayo, kuyafanyia
ukarabati na kutengeneza vipuri vyake wakati kunapokuwa na ulazima wa
kufanya hivyo.
“Tunapenda kujenga kiwanda mahali ambapo itakuwa
rahisi kupata vijana wa kuajiriwa ili iwe rahisi kuwafundisha teknolojia
tunayoitumia kutengeneza matrekta,” alisema.
Kwa upande wake, Pinda alisema atawasilisha
maelezo hayo kwa waziri anayehusika na sekta hiyo ili mawasiliano rasmi
ya kujenga kiwanda hicho yafanyike.

No comments:
Post a Comment