Moshi. Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kilimanjaro
(KNCU), kimemjia juu mrajisi wa vyama hivyo nchini kwa kile ilichodai
kukwamisha ustawi na maendeleo yake.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na
mwenyekiti wa KNCU, Maynard Swai wakati akisoma hotuba yake katika
mkutano mkuu maalumu ulioitishwa kwa shinikizo la mrajisi huyo, Dk Audax
Rutabanzibwa.
Licha ya kupokea lawama hizo, Dk Rutabanzibwa
aliyekuwa mwenyekiti katika mkutano huo hakuweza kujibu malalamiko
yaliyoelekezwa kwake na mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo aliwaachia wajumbe wa mkutano huo
kufanya uamuzi kwa njia ya kura kama bodi ya uongozi iendelee au ing’oke
ambapo kura 83 zilikataa na 68 zikitaka ing’oke.
Swai alisema ofisi ya mrajisi huyo imekuwa kikwazo cha maendeleo kwa KNCU .
“Mfano, shamba la Garagagua lilitakiwa kuuzwa Mei
2014, wajumbe mlisharidhia lakini kutokana na ukiritimba wa ofisi ya
mrajisi imekwama,” alisema Swai. Swai aliitaja mipango mingine kuwa ni
ujenzi wa hosteli ya kisasa na hoteli kwenye eneo la makao makuu ya
KNCU.
“Sina nia ya kuifundisha au kuikumbusha ofisi ya
Mrajisi wajibu wake kiutendaji lakini ina wajibu wa kushauri na
kusimamia ushirika ili uendelee kushamiri nchini kwa manufaa ya
wanachama,”alisema.
Lakini Swai alisema hata tume mbalimbali za
uchunguzi zilizotumwa KNCU katika kipindi kifupi cha miaka miwili na
Mrajisi, hazijawahi kutoa mrejesho wa matokeo ya uchunguzi huo.
“Kifungu 57(1) cha sheria namba 6 ya Ushirika ya
mwaka 2013 imeweka bayana kuwa ikiwa kuna uchunguzi au ukaguzi umefanywa
dhidi ya chama cha Ushirika, Mrajisi atapaswa kutoa matokeo ya
uchunguzi huo,”alisema Swai.
KNCU kimeshangazwa pia na hatua ya Mrajisi
kutoamini ukaguzi uliofanywa na COASCO ambacho ni chombo cha Serikali
kuhusu kiasi cha hasara ambayo KNCU ilipata wakati wa mdororo wa uchumi
duniani mwaka 2008.
Katika hesabu hizo, KNCU ilionyesha kupata hasara
ya zaidi ya Sh765 milioni wakati uhakiki uliofanywa na hazina ulionyesha
KNCU kilipata hasara ya Sh250 milioni.
“Mrajisi aliagiza kufuatiliwa kwa tofauti hii huku
akionesha kutokuwa na imani na hesabu zilizokaguliwa na COASCO jambo
ambalo linashangaza kama Serikali haiwezi kuamini kazi iliyofanywa na
chombo chake,” alisisitiza Swai.
Swai alisema tofauti hiyo ilifanyiwa kazi na KNCU na taarifa
kurejeshwa kwa Mrajisi lakini hawajaona mawasiliano yoyote yanayoonyesha
ufuatiliaji wa suala hilo hiyo inadhihirisha namna Mrajisi
alivyoshindwa kuitetea KNCU.
Mwenyekiti huyo alipigilia msumari zaidi pale
alipodai hata mkutano huo mkuu maalumu ulioitishwa na Mrajisi ni batili
na unakiuka kifungu namba 55(9) cha sheria ya Ushirika.
“Sheria iko wazi kuwa hesabu zikishawasilishwa na
kujadiliwa na kisha kupitishwa na mkutano mkuu, uamuzi wao (wajumbe)
kuhusiana na hesabu hizo unakuwa wa mwisho,”alisema Swai.
Swai alisema ilikuwa ni batili kisheria, kwa
Mrajisi kushinikiza kuitishwa kwa mkutano huo ili kujibu hoja za ukaguzi
ambazo alidai hazikupatiwa majibu ya kutosha na KNCU wakati wenye mali
walisharidhika na majibu hayo.

No comments:
Post a Comment