Dodoma.Kamati
ya Bunge ya kuchunguza athari za Operesheni Tokomeza Ujangili
inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake leo, ambayo inaelezwa kuwa
imependekeza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya vigogo kadhaa wa Serikali.
Taarifa
ya kamati hiyo ndogo itasomwa leo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Mazingira na Maliasili itakapokuwa inawasilisha taarifa yake ya utendaji
kazi bungeni.
Wajumbe
wengi wa kamati hiyo ndogo wanatokana na Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Mazingira na Maliasili. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi
alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa uchunguzi wa kamati hiyo umegundua
udhaifu mkubwa katika wizara na idara za Serikali.
Kamati
hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli imependekeza
kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya maofisa waandamizi wa Wizara za
Maliasili na Utalii na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mjumbe huyo alisema
kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, watakaoguswa na ripoti
hiyo ni baadhi ya maofisa waandamizi wanaosimamia wanyamapori na hata wale wa maliasili.
Kamati
hiyo iliyoanza kazi Novemba 25, mwaka huu inawasilisha ripoti yake
baada ya kumaliza kazi ya kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo mawaziri
watatu ambao wizara zao zilihusika moja kwa moja na operesheni hiyo.
Mawaziri waliohojiwa katika Hoteli ya Bahari Beach,
Dar es Salaam ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi na
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Hata
hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilisema kuna uwezekano mkubwa
taarifa hiyo ‘ikamkaanga’ Dk Mathayo kutokana na mapendekezo ya wabunge
katika mkutano wa 13.
Wabunge
walikerwa zaidi na kauli ya Dk Mathayo alipopata fursa ya kuchangia
taarifa ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili na kuishia
kuwapa pole wafugaji ambao mifugo yao iliuawa kwa risasi.
Katika
operesheni hiyo, wabunge walipaza sauti wakidai wapo raia wasio na
hatia waliouawa na kuteswa, huku mifugo ikiporwa na mingine kama ng’ombe
ikiuawa kwa kupigwa risasi.
Mbunge
wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ndiye aliyekuwa mwiba kwa mawaziri hao
aliposema ana kitabu kilichosheheni ushahidi dhidi ya vitendo vya
ukiukaji wa haki za binadamu. Habari zaidi zinasema kamati hiyo ya
uchunguzi imelazimika kutofanyia shughuli zake katika kumbi za Bunge ili
kukwepa vishawishi kutoka kwa watu wa karibu na vigogo wanaotuhumiwa.
“Wamejificha katika hoteli moja tangu waliporudi Dodoma wiki
iliyopita ili kuandaa ripoti yao kwa sababu hawataki kuingiliwa
ingiliwa na hili ndilo linalowatia hofu mawaziri,” alisema mjumbe huyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, pamoja na kasoro za operesheni hiyo, ilisaidia
kuwabaini maofisa walioko katika mtandao wa ujangili na baadhi yao
walikamatwa na nyara za Serikali.
Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel alithibitisha kuwasilishwa kwa ripoti hiyo
leo wakati kamati itakapowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli
zake... Hata hivyo, alisema hana uhakika wa asilimia 100. Ripoti hiyo
itawasilishwa huku kukiwa na vuguvugu la kung’olewa kwa mawaziri saba
wanaodaiwa mzigo katika utendaji wao na tayari wamehojiwa na Kamati Kuu
ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana wiki iliyopita chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete.
Mbali
na vuguvugu hilo, ripoti ya uchunguzi pia inawasilishwa wakati tayari
Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri watatu wajipime kama bado
wanatosha kuongoza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mawaziri
hao ni Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia
na Manaibu wake, Aggrey Mwanry na Kassim Majaliwa. Ripoti kama hiyo
inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo na Lembeli ndiyo iliyochangia
kumng’oa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kutokana na kashfa ya ugawaji vitalu vya uwindaji.

No comments:
Post a Comment