Tabora.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk
Willibroad Slaa amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisitafute dawa ya
mawaziri ‘Mizigo’ badala yake wamwajibishe aliyewateua hao wanaowaita
mzigo.
Alisema badala
ya kuwahangaisha Watanzania kwa kujadili majina ya mawaziri mizigo,
wanapaswa kuchukua hatua za kinidhamu kama wana uhakika na mawaziri hao
na kushauri kuangalia upatikanaji wao hadi kufikia nafasi hizo nyeti za
kuwatumikia watu.
Akihutubia
mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui mjini Tabora
juzi,Dk Slaa alisema kinachoendelea ndani ya Serikali hivi sasa ambacho
kinaitwa ‘mawaziri mizigo’ ni moja ya dalili ya tatizo katika mamlaka
ya uteuzi alibainisha pia kuwa, kuwatimua mawaziri hao siyo dawa bali kushughulikia chanzo cha tatizo.
Amesema kwa muda mrefu Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa lawamani kutokana na kushindwa kazi kwa mawaziri wake, jambo ambalo Dk Slaa amesema, limetokana na kutofanyika kwa umakini wa kuzingatia vigezo, bali uswahiba.
Alisisitiza
kuwa kinachofanyika sasa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
kuzunguka nchi nzima na kutaja majukwaani mawaziri mzigo ni njia ya
kusukuma agenda
ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri,lakini rais anapaswa kuchukua
uamuzi sahihi wakati wa kuwawajibisha hao ‘mizigo’ ambao ni maswahiba.
Dk Slaa
anaendelea na ziara ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama hicho mkoani
Tabora,juzi alitembelea maeneo ya Ugoweko, Kakola na Tabora mjini na
kudai kuwa mabadiliko ya mara
kwa mara ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Rais Kikwete hayana
tija kwa Watanzania na ni dalili za tatizo la ukosefu wa uwajibikaji.

No comments:
Post a Comment