Dodoma.Sakata
la wabunge waliochukua posho kwa ajili ya safari za mafunzo nje ya nchi
na kuacha kusafiri, limeingia hatua mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda kuwataka wazirudishe.
Katika orodha
ya wabunge wanaotajwa katika sakata hilo, wamo baadhi ya wabunge wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Mapinduzi (CCM)
na Chama cha NCCR-Mageuzi.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki
iliyopita mjini Dodoma na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM)
wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (Laac).
Keissy alisema
baadhi ya wabunge wanapaswa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kuchukua posho za safari za nje ya
nchi lakini hawakwenda safari hizo.
Mbunge huyo
alifafanua kuwa mbali na kutokwenda kabisa safari hizo, lakini wapo
ambao walikwenda na hawakukaa siku zote zilizopangwa.
“Tunawajua na
wapo humu ndani,” alisema huku baadhi ya wabunge wakipaza sauti wakitaka
awataje, lakini yeye akasema siyo jukumu lake kuwataja kwani Ofisi ya
Bunge inawajibika kufanya hivyo.
Mbunge huyo alienda mbali na kudai mbunge mmoja alikatisha safari ya kwenda Marekani na kuamua kwenda Dubai kwa safari binafsi ambayo haikuwepo katika ratiba ya ziara hiyo ya mafunzo.
Habari za
uhakika zilizopatikana jana zilisema wabunge wanane walichukua posho ya
safari ya kati ya Sh5 milioni na Sh6 na Spika amewaandikia barua
akiwataka warudishe fedha hizo.
Majina ya
wabunge hao tunayo, lakini kwa sababu za maadili ya uandishi wa habari,
gazeti hili halitaweza kuwataja kwa kuwa hawakupatikana ili kujibu
tuhuma hizo kama maadili yanavyoelekeza.
Akizungumza na
gazeti hili ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, Kaimu Katibu wa
Bunge, John Joel, alisema kuwa Spika ameshaliona jambo hilo na kulichukulia hatua za kiutawala.
“Spika
amewaandikia barua akiwataka kurejesha fedha zote za safari ambazo
hawakwenda. Ni lazima wazirudishe hakuna namna,” alisema Joel ambaye pia
ni Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge.
Alipoulizwa
kuhusiana na majina yao na kiasi walichochukua, Joel alisema hilo ni
jambo la kiutawala na kwamba Spika ndiyehuarifiwa na kamati kuhusiana na
wabunge ambao hawakusafiri.
“Spika ndiye anayearifiwa na
wenyeviti wa kamati husika juu ya wabunge waliosafiri na wasiosafiri
kwa sababu wao ndiyo wanapanga safari na sisi tunawapa posho,” alisema.
Akizungumzia
malalamiko ya wabunge juu ya baadhi ya wabunge wasiofika bungeni kusaini
ili wapate posho ya kikao, Joel alisema tatizo hilo limepungua kwa
kiasi kikubwa.
“Lilikuwepo
lakini limepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kugundua wakifika kwenye
malipo majina yao waliosainiwa yamekatwa,” alisema Joel.
Alipoulizwa
kuhusiana na tatizo hilo la kupokea posho za safari za nje ya nchi bila
kwenda, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu
alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo.
“Lakini muhimu
hapa ni Bunge kuandaa utaratibu wa kurejesha mrejesho wa jinsi
walivyozitumia na hapo ndipo watagundulika wabunge wanaosafiri kweli na
muda waliokaa mahali husika,” alisema Lissu.
Mbunge wa
Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye anatajwa kuwemo
kwenye orodha ya wabunge waliopokea posho bila kusafiri, alikiri na
tayari alishamuandikia barua Katibu wa Bunge akimueleza kwamba
hakusafiri na kuomba utaratibu wa kurejesha fedha hizo.
Nasari alisema
yeye alikuwa Jimboni kwake kwa shughuli za wananchi wake, hivyo
hakuweza kusafiri na suala hilo alilifikisha mapema kwa Katibu ili ampe
maelekezo namna ya kurejesha fedha hizo.

No comments:
Post a Comment