Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutia saini hati ya dharura ili
Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho na kuondoa tozo ya
kodi kwa laini za simu imeliacha Bunge katika fadhaa na fedheha kubwa.
Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2013
lilishuhudia wabunge wa chama tawala wakitumia wingi wao bungeni
kupitisha kodi hiyo ambayo iliamsha hasira na vilio kutoka kwa wananchi
kutoka kila kona ya nchi.
Tunasema hatua hiyo ya Rais imeleta fadhaa na
fedheha kwa Bunge kutokana na kuwapo matukio mengi ya aina hiyo katika
kipindi kifupi, ambapo Bunge limekuwa likipitisha miswada mingi muhimu
kwa ushabiki wa kisiasa badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa.
Rais kwa kuwasitiri wabunge wa chama chake amekuwa akitia saini miswada
hiyo na kuwa sheria, lakini baadaye amekuwa akisikiliza hoja za
wapinzani na kulazimika kurudisha sheria hizo bungeni ili zifanyiwe
marekebisho.
Siyo nia yetu hata kidogo kuorodhesha hapa sheria
zote ambazo Rais amezirudisha bungeni kufanyiwa marekebisho katika miaka
ya hivi karibuni. Hata hivyo, wasomaji wetu watakumbuka kuwa, moja ya
sheria nyeti zilizorudishwa bungeni ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo ndiyo hasa iliyoanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya yapata
miezi 18 iliyopita. Kama tulivyosema hapo juu, muswada wa sheria hiyo na
miswada mingine mingi muhimu ilipitishwa na Bunge kwa ushabiki wa
kisiasa na kiitikadi, kwa maana ya hoja za wabunge wa upinzani kuzimwa
au kujadiliwa kwa kejeli, vijembe na matusi na hatimaye kupuuzwa.
Ni katika muktadha huo, Sheria ya Fedha ya mwaka
2013 iliyoanzisha tozo ya kodi kwa laini za simu inapaswa kuangaliwa.
Bunge kwa staili hiyohiyo ya ushabiki wa kisiasa na kiitikadi
lilipitisha muswada wa sheria hiyo, huku wabunge wa upinzani wakipinga
na kuainisha athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa. Ni kweli Rais
alisaini muswada huo na kuwa sheria, lakini kutokana na athari zake kwa
uchumi na wananchi kwa jumla, sasa ameirudisha bungeni kwa hati ya
dharura akitaka ifanyiwe marekebisho na kuifuta kodi hiyo mara moja.
Ni aibu kwa Bunge, Serikali na Kamati ya Bajeti
iliyobuni tozo hiyo kutoona mapema madhara ambayo yangesababishwa na
kodi hiyo ya Sh1,000 (kwa kila laini ya simu kila mwezi) kwa wananchi
maskini ambao wanahangaika kupata mlo mmoja kwa siku. Spika wa Bunge,
Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutojua hali halisi
ilivyo, hasa vijijini walikaririwa bungeni wakitetea kwa nguvu hoja ya
kuwekwa kwa tozo hiyo, wakidai kila mwananchi anao uwezo wa kuilipa
kila mwezi.
Kutokana na utata uliosababishwa na tozo hiyo,
kodi hiyo ilikuwa haijaanza kulipwa mpaka sasa, licha ya Bunge kupitisha
muswada huo Julai, mwaka huu. Rais Kikwete baadaye aliingilia kati kwa
kuagiza mamlaka zote husika kukutana mara moja kumaliza mvutano wa kodi
hiyo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya kodi ili kuziba pengo la Sh178
bilioni ambazo zingetokana na kodi kwenye laini za simu. Ni matarajio
yetu kwamba Bunge letu litakuwa limepata somo la kutosha, hivyo litakuwa
makini siku zijazo kwa kuhakikisha linapitisha miswada pasipo hila wala
ushabiki wa kisiasa.

No comments:
Post a Comment