Saturday, 29 August 2015

Lowassa: Wanawake nguzo ya mabadiliko

 
 
Mke wa Mgombea wa Urais wa Chadema, Mama Regina Lowassa akiwasalimia wanawake  walioshindwa kuingia katika ukumbi uliopo katika Jengo LAPF Kijitonyama baada ya ukumbi huo kufurika, wakati wa mkutano wa Mgombea Urais, Edward Lowassa alipokuwa akizungumza na wanawake wa Dar es Salaam, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa amesema mabadiliko katika Taifa hili ni jambo la lazima na linalohitaji nguvu ya wanawake ili kulifanikisha kwa maendeleo ya Watanzania wote.
Lowassa alisema hayo jana kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za wanawake, ulioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na kutumia nafasi hiyo kuomba kura kwa wanawake na kuwataka wamtafutie kura kwa watu wengine.
Alisema anaamini kuwa wanawake katika umoja wao, ndiyo nguzo kubwa ya mabadiliko na wakiamua kufanya hivyo hakuna wa kupinga. Alisema wanawake wanakabiliwa na shida mbalimbali ambazo zinahitaji mabadiliko ya kimfumo.
“Nimekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 30, nina uzoefu kwamba mwanamke akisema anakupa kura anakupa kweli. Wanawake mtanipa kura zenu?” Lowassa aliwauliza wanawake waliohudhuria kwenye mkutano huo nao kwa pamoja walijibu “umepataaa”
Alisema anakusudia kuleta maendeleo kwa kasi kubwa ambayo hakuna anayeweza kufikia akitaka ifike mahali Watanzania waache woga wa kutafuta mabadiliko ya kweli.
Lowassa aliwataka wanachama wengine wa CCM kujiunga na upinzani kwa madai kwamba ndiko yalipo mabadiliko ya kweli. Aliendelea kunukuu kauli ya Mwalimu Julius Nyerere aliyowahi kuisema mwaka 1995, kwamba: “Wananchi wanataka mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Aliongeza: “Hawa wenzangu wa CCM waje Ukawa. Huku hakuna noma, waje tu wajiunge na gurudumu la mabadiliko,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wanawake waliohudhuria katika mkutano huo.
Awali, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alizindua salamu mpya itakayotumika katika kampeni zake nchi nzima. Alisema salamu hiyo inaambatana na ishara ya kuzungusha mikono kumaanisha mabadiliko.
“Lowassa amekuwa chachu ya mabadiliko nchini na ametuunganisha wote licha ya tofauti zetu, sasa napendekeza salamu mpya tutakayoitumia kwenye kampeni, nikisema Lowassa, mnazungusha mikono yenu kumaanisha mabadiliko,” Mbowe alielekeza na salamu hiyo ilianza kutumika papo hapo.
Alisema katika utafiti wake, amebaini kuwa wanawake wengi wamekuwa hawafiki kwenye mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa sababu ya kusukumwa, kukanyagwa na kudhalilishwa kijinsia, hali aliyosema sasa itabadilishwa.
Alisema kuanzia sasa watatenga maeneo maalumu ya kukaa wanawake kwenye mikutano yao yote ya hadhara kuanzia siku ya uzinduzi wa kampeni zao kesho katika Viwanja vya Jangwani.
“Kuja kwa Lowassa ni mpango wa Mungu. Alitoka alikotoka na kuja kuwaunganisha wanawake, wasichana, wanaume na vijana nchi nzima. Hatuna budi kumuunga mkono ili atuletee mabadiliko tunayoyahitaji,” alisema Mbowe.
Regina Lowassa alonga
Mke wa mgombea urais wa Ukawa, Regina Lowassa ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatishwa mara kwa mara na shangwe za wanawake, alitumia muda huo kuwaombea kura wagombea urais wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mama Lowassa alibainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini ikiwamo mfumo mbaya wa elimu ambao haumuandai mwanafunzi kujitegemea na kukosekana kwa huduma bora za afya kwa wajawazito.
Alisema Tanzania bado iko nyuma kiuchumi kwa sababu Serikali imeshindwa kutengeneza mazingira wezeshi kwa wanawake ili wanufaike na rasilimali zilizopo.
Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia alisema wanawake ni wengi wana nguvu kubwa ya kuamua nani awe rais, hivyo kuwataka kumpa kura mgombea wa Ukawa ili akalijenge Taifa.
Ilivyokuwa
Licha ya ratiba ya mkutano huo kuonyesha ungeanza saa 8.00 mchana, wanawake wengi walifika kuanza saa tano asubuhi na kutumia muda mwingi kuimba nyimbo za kumsifu Lowassa nje ya Jengo la LAPF.
Baadhi ya watu walisikika wakiimba; “Kama siyo Kikwete, Lowassa tungempata wapi?” huku wengine wakisema “CCM siyo chama, kingekuwa chama Lowassa asingehama.”
Ilipofika saa nane mchana, idadi ya watu iliongezeka kiasi kwamba walinzi waliokuwa wakilinda lango la kuingilia ukumbini walilazimika kutumia nguvu ya ziada kuwazuia waliokuwa wanataka kuingia ndani.
Kutokana na idadi ya watu kuendelea kuongezeka, ilimbidi mshereheshaji kuomba vijana wa ulinzi wa Red Brigade kusaidia kuwazuia watu waliokuwa wanataka kuingia ndani wakati ukumbi umeshajaa.
Walinzi walilazimika kufunga milango na kutangaza kuwa Lowassa na viongozi alioambatana nao watazungumza na watu walio nje ya ukumbi kwanza, ndipo waingie ndani ili wote wasikie anataka kuwaambia nini.
Hata baada ya kuzungumza nao, wafuasi hao wa Ukawa waliendelea kufuatilia mkutano huo kupitia televisheni zilizofungwa nje ya ukumbi huo.
Waimbaji wa nyimbo za injili, Bahati Bukuku na Jeni Miso, walikuwa kivutio kwa wafuasi hao kutokana na nyimbo walizoiimba za kutaka mabadiliko huku msanii wa filamu Jackline Wolper akimzawadia Lowassa keki ya siku ya kuzaliwa. Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953.
Wanachama walonga
Mkazi Kitunda, Magdalena William (41) alisema amefika eneo la kongamano kuanzia saa 2.30 asubuhi ili asikose nafasi ya kuona kila kinachofanywa na kuamuliwa kwa ajili yao.
Zakia Haule (37), mkazi wa Magomeni, alisema hakuenda kwenye shughuli zake ili kuungana na wenzake kuleta mabadiliko kwa pamoja. Akiwa mwenye furaha na kujiamini, alisema amejipanga kuipigia kura Ukawa.
Mkazi wa Tabata, Siwatu Mussa (42) aliyefika saa nane mchana na kushindwa kuingia ukumbini alisema: “Nitakaa hadi nimuone anatoka, najipanga kwa ajili ya Jangwani naona nitakuwa wa kwanza, siku hiyo sitaki kupitwa na kitu.”
Tofauti na inavyokuwa watu wanapoingia mpirani, zinapobaki dakika nne au tano kuanza kuondoka, jana hakuna aliyefanya hivyo hadi Lowassa alipomaliza kuzungumza.
Imeandikwa na Peter Elias, Goodluck Eliona na Kalunde Jamal

No comments: