Dk
Wilbroad Slaa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa
Serena jijini Dar es Salaam leo; Slaa amebainisha kuachana na siasa za
vyama.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo Dk. Wilbroad Slaa amesema leo kuwa amejiondoa kwenye siasa na
hatajiunga na chama kingine chochote cha siasa ila ataendelea
kuwatumikia Watanzania kwa namna yoyote.
Dk Slaa
amesema alichukua uamuzi huo tangu Julai mwaka huu baada ya kutofautiana
na chama chake juu ya masharti ya kumpokea mgombea wa urais kupitia
Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Dk.
Slaa akizungumza jijini Dar es Salaam leo, amekiri kushiriki vikao
kujadili ujio wa waziri mkuu huyo wa zamani lakini alishangazwa na
viongozi waandamizi wa chama chake kuharakisha kumpokeea pasipo kutimiza
masharti aliyopendekeza.
“Sina tabia ya
kuyumbishwa….sina chuki na mtu yoyote lakini sipendi siasa za
udanganyifu na propaganda,” amesema Dk. Slaa na kusema ameachana na
siasa tangu 28 Julai, 2015 baada ya kuona misingi ya chama alichoshiriki
kukijenga imepotoshwa.
Sharti la kwanza ambalo Dk.
Slaa alitaka lizingatiwe ni kiongozi huyo wa zamani ndani ya serikali ya
CCM kujisafisha kwenye tuhuma ya kashfa ya Richmond aliyohusishwa nayo
akiwa kama Waziri Mkuu.
Aidha, Slaa alitaka ajue
Lowassa ataongeza thamani gani ndani ya Chadema, ikiwa ni pamoja na
viongozi watakaojiunga toka chama tawala.
Baada ya
Lowassa kutokidhi vigezo tajwa, huku akiwataja viongozi waliojiunga
Chadema wakitokea CCM wakiwa ni “mizigo” ndani ya chama tawala,
amejiweka kando na Chadema.
DK Slaa ametumia takribani
saa mbili kueleza msimamo wake na matatizo anayoyaona kwa Lowassa na
waziri mkuu mstaafu ambaye naye amejiunga na upinzani, Frederick Sumaye
kuwa hawafai na si watu safi.

No comments:
Post a Comment