Dar es Salaam. Wakati CCM ikielekea katika kipindi kigumu cha
kuamua mgombea wake wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Makongoro
Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
amezungumzia taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja
kuwa na mpango wa kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.
CCM, ambayo imeshika nchi tangu kurejeshwa kwa
siasa za vyama vingi, hujikuta katika wakati mgumu kila wakati
inapotakiwa kutoa mgombea wa kurithi nafasi ya Rais aliye madarakani
baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Tayari wanachama wanne wa chama hicho tawala
wameshatangaza rasmi kuwania urais huku wengine sita wakifungiwa kwa
makosa ya kudaiwa kuanza kampeni mapema, huku kukiwa na mlolongo wa watu
wanaotajwa kuwa na mpango wa kujitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwamo
Makongoro, ambaye imeelezwa kuwa ameshauriwa kuchukua uamuzi huo
kujaribu kukinusuru chama kutokana na makundi yanayoonekana kujitokeza
katika mbio hizo.
“Mimi si mtabiri, siwezi kukwambia nitagombea au
la, lakini uamuzi wangu utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na
CCM,” alisema Makongoro ambaye ni ofisa wa zamani wa Jeshi la Wananchi
(JWTZ) na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Vyanzo hivyo vya habari vimeeleza kuwa mkakati wa
kuhakikisha Makongoro anakuwa rais, unaratibiwa na baadhi ya makada
waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere.
Mkakati huo pia unatajwa kuwa ulianza pale
alipochaguliwa kuwa mbunge wa Eala. Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Lazaro Nyalandu ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii na
Hamisi Kigwangala (mbunge) wametangaza nia ya kuomba ridhaa ya CCM
kuwapitisha kuwania urais.
Hata hivyo, upinzani mkubwa unaonekana kuwa kwa
vigogo ambao hawajatangaza nia hiyo na ambao wanatumikia adhabu ya
kufungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kutokana na kikiuka taratibu za chama
hicho.
Miongoni mwa ambao hawajajitokeza ni Waziri Mkuu
wa zamani, Edward Lowassa, ambaye wafuasi wake wamekuwa wakijitokeza
katika siku za karibuni kueleza wazi msimamo wao kuwa ndio chaguo
sahihi, na Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Pia yumo Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu,
Frederick Sumaye, Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri wa
Kilimo na Chakula, Steven Wasira na Naibu Waziri wa Fedha-Sera, Mwigulu
Nchemba, ambaye alionywa na chama hicho dhidi ya safari zake mikoani
zilizodaiwa kuwa na dalili za kampeni.
Kauli ya Makongoro
Akizungumza na gazeti hili, Makongoro hakuonyesha
kukataa wala kukubali kuhusu uamuzi wa kugombea nafasi hiyo iliyoshikwa
na baba yake kwa takribani miaka 25.
“Ninachoweza kutabiri kwa sasa ni iwapo nina njaa
basi lazima nitakula au simba akitokea lazima nikimbie. Kama nina
usingizi na kuna kitanda karibu lazima nitalala lakini mambo mengine
siwezi kuyasemea,” alisema Makongoro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa
Arusha Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi. Alisema anasubiri
siku ambayo CCM itatangaza mchakato wa kuchukua fomu ndipo hatma yake
itajulikana.
Makongoro ni nani
Makongoro ni mtoto wa tatu wa familia ya Hayati
Nyerere na Januari 30 mwaka huu alitimiza miaka 56 tangu azaliwe.
Alipata mafunzo ya uongozi wa kijeshi Monduli kati ya mwaka 1980 na
1982.
Luteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi alipata
elimu ya sekondari ya juu na ya kawaida kwenye Shule ya Sekondari ya
Wavulana ya Tabora wakati elimu ya msingi alisomea katika shule tatu
tofauti za Arusha, Bunge na Isike kati ya mwaka 1971 na 1978.
Mwaka 1995 Makongoro alihama CCM na kujiunga na
NCCR Mageuzi na katika uchaguzi wa kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za
vyama vingi, Makongoro alishinda ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, lakini
hakumaliza kipindi chake kutokana na ubunge huo kupingwa mahakamani na
hatimaye kutenguliwa.
Aprili 7, 2012 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimchagua kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki.
Maoni ya wachambuzi
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, mwenyekiti wa
Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema masuala ya urais wa
Makongoro aulizwe mwenyewe.
“Sitaki kuulizwa kuhusu hilo, mimi si meneja wa
kampeni wa hao watu. Nitoe kabisa katika hilo,” alisema Butiku, ambaye
ni miongoni mwa watu waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere wakati wa
utawala wa awamu ya Kwanza.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru
alisema hawezi kutoa maoni yoyote hadi pale Makongoro atakapoamua
kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Benson Bana alisema iwapo Makongoro anahitaji kuwa rais,
basi angepata kwanza ushauri wa wazee kutoka Butiama.
“Kwangu mimi Makongoro hana sifa ya kuwa rais,
kwani kuna vigezo gani vinavyoangaliwa? Angeomba ushauri kwanza hata kwa
kina Butiku,” alisema Dk Bana.
Alisema kwa anavyofahamu, CCM huchagua viongozi
wazalendo, wenye maadili na historia za kupendeza wala si viongozi
kutokana na koo zao au umaarufu tu. Kadhalika Dk Bana alisema mchakato
wa kumpata rais ajaye ni mgumu hivyo akaitaka CCM isikurupuke.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alisema
haoni tatizo kwa mtoto huyo wa muasisi wa Taifa kwa kuwa ana sifa zote
za uongozi na hana sifa ya ‘uchafu.’
“Ukizungumzia usafi wa viongozi, hana neno. Anaweza kuwa kiongozi mzuri tu na pia ana haki kikatiba,” alisema.
Profesa Mpangala alisema licha ya watu kukosoa
kuwa watoto wa viongozi wa zamani wanatengenezwa kuwa viongozi, lakini
kama mtu ana sifa basi hana budi kugombea.

No comments:
Post a Comment