Dar es Salaam. Hali ya sintofahamu ilitokea jana baada ya
wanachama wa Chama cha Albino Tanzania (Tas) kumshambulia kiongozi wao,
Ernest Kimaya wakati wakiwa njiani kuelekea Ikulu ambako Rais Jakaya
Kikwete aliwaita kwa mazungumzo.
Pembeni ya barabara inayopakana na Ikulu, karibu
na jengo la Wizara ya Elimu wakati wakielekea kumuona Rais Kikwete,
wanachama hao walianza kumshambulia Kimaya wakidai kuwa si kiongozi
halali, lakini aliokolewa na maofisa usalama waliokuwapo katika tukio
hilo.
Wanachama hao walitaka kushinikiza na wao kumwona
Rais Jakaya Kikwete badala ya viongozi 15 ambao ndiyo waliotakiwa
wamwone Rais na kuzungumza naye. Saa moja baadaye, viongozi hao wa Tas
waliingia Ikulu kuonana na Rais Kikwete.
Wanachama hao walikuwa wakimtaka Kimaya aachie wadhifa wake kwa kuwa si kiongozi.
Kimaya alizomewa muda wote na kumvuta nguo na
baadhi ya wanachama hao ambao walimtuhumu kuwa anajinufaisha na vifo vya
albino vinavyozidi kutokea nchini.
Hata hivyo, Kimaya alishindwa kujizuia na kutaka
kupigana na baadhi watu waliokuwa wakimzonga na kumtukana. Maofisa
usalama walimchukua na kumwondoa eneo la tukio ili vurugu zisiendelee.
Baadhi ya wanachama wa Tas walisema viongozi wao
wamejikusanya wenyewe kwenda Ikulu bila kuwashirikisha na kuwa hawafanyi
mikutano ya mara kwa mara zaidi ya kuwaita kwenye maandamano.
Mmoja wa albino hao, Nuru Iddi alisema hawana
imani na viongozi wao kwa sababu muda wao wa kuwepo madarakani uliisha
tangu mwaka jana.
Alisisitiza kuwa tangu wakati huo hawajafanya uchaguzi wowote na viongozi wametulia ili waendelee kujinufaisha.
“Albino akiuawa kule Mwanza mimi ndiyo napata
uchungu, siyo hawa viongozi... wao wanapokea michango mingi kutokana na
vifo vya wenzetu lakini hawafanyi jambo lolote la maana kulinda maisha
yetu,” alisema mwanachama huyo.
Iddi aliongeza kuwa wao ndiyo walitakiwa kuonana
na Rais Kikwete ili wamueleze hali halisi na nini cha kufanya ili
kulinda maisha yao.
Aliulaumu uongozi wa Tas kwa kutowashirikisha wao kama wanachama kutoa maoni ambayo yangewasilishwa kwa Rais.
Naye Mwalimu Matimbwa alisisitiza kuwa viongozi wao wako nje ya
muda kikatiba. Alisema mwaka 2006 kulikuwa na kisa kimoja tu cha mauaji
ya albino lakini mpaka sasa idadi imefikia 78. Aliushutumu uongozi wa
Tas kutodhibiti ongezeko hilo la mauaji ya albino.
“Nasikia uchungu sana ninapoona wenzangu wanauawa
lakini baadhi yetu wanajinufaisha na mauaji hayo. Hatuwezi kushinda vita
hivi kama hatuna uongozi thabiti. Tunataka uchaguzi ufanyike haraka
sana,” alisisitiza Matimbwa.
Matimbwa aliongeza kuwa katiba yao inataka
uchaguzi ufanyike kila baada ya miaka mitano lakini uchaguzi huo
haukufanyika mwaka jana.
Kimaya alikiri kuwa walitakiwa kufanya uchaguzi
mwaka 2014, lakini walikubaliana na wanachama kuwa uongozi uliokuwepo
madarakani kwa ngazi ya wilaya, mikoa na taifa uendelee na kazi.
“Sisi tupo madarakani kihalali kwa sababu
wanachama wenyewe ndiyo walipendekeza kuwa tuendelee kuongoza. Hili ni
kundi la wahuni tu, siyo wanachama wetu,” alisema kiongozi huyo kabla ya
kushambuliwa na wanachama waliokuwa wakipiga kelele wakisema
“hatumtambui, aachie kiti huyo”.
Kimaya alifafanua kuwa mara ya mwisho walifanya
uchaguzi mwaka 2009, lakini mwaka jana walishindwa kufanya uchaguzi kwa
sababu kulikuwa na mwingiliano wa mambo.
Rais Kikwete aliandaa chakula cha mchana na
viongozi wa Tas, Ikulu jijini Dar es Salaam. viongozi wa Tas walipata
nafasi ya kuongea naye juu ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
yanayoshika kasi nchini kwa sasa.

No comments:
Post a Comment