Serikali juzi iliwasilisha bungeni Muswada wa Sheria unaotishia
uhuru wa vyombo vya habari, lakini ikauchomoa baadaye jioni baada ya
kugundua kwamba umestukiwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hatua hiyo ya Serikali ya kuwasilisha Muswada wa
Sheria ya Takwimu unaoonekana kulenga kukwamisha vyombo vya habari
katika kupata takwimu na kuzitumia katika habari na taarifa zinazotolewa
kwa wananchi, imeonekana kwa wengi katika tasnia ya habari kama
uthibitisho kwamba pengine Serikali haina dhamira ya kuona wananchi
wanapata haki ya kupata habari.
Moja ya kifungu cha muswada huo kilicholalamikiwa
na wabunge wengi ni Ibara ya 37 (4), ambacho kinaeleza kwamba wadau na
vyombo vya habari vitakavyotoa takwimu bila kibali cha Ofisi ya Takwimu
watakwenda jela miaka mitatu pamoja na faini ya Sh10 milioni au vyote
kwa pamoja.
Inasikitisha kuona kwamba adhabu hiyo kubwa kupita
kiasi imeungwa mkono na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na
Biashara, ambayo iliwasilisha maoni yake bungeni juzi.
Adhabu ya kosa hilo awali ilikuwa kifungo cha
mwaka mmoja, lakini katika hali ya kushangaza Kamati hiyo ilipendekeza
iongezwe hadi miaka mitatu eti kuzuia tabia ya baadhi ya watu kutoa
takwimu za uongo na kwa makusudi ili kupotosha jamii.
Hakuna anayepinga kuwapo umuhimu wa kuipa mamlaka
zaidi na kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutekeleza majukumu yake
ya kitakwimu kwa ufanisi, wala hakuna anayepinga uanzishwaji wa mfumo
thabiti wa utoaji wa takwimu unaokusudia kuboresha na kuimarisha takwimu
rasmi nchini.
Jambo hilo tumekuwa tukilisisitiza mara kwa mara na kwa kweli tunadhani Serikali imechelewa sana kuanza kuchukua hatua.
Hata hivyo, tunadhani Serikali inafanya makosa
kudhani kwamba uchapishaji wa takwimu zisizo sahihi unatokana na watu
kutaka kupotosha jamii na kuleta machafuko.
Ni kweli kwamba katika mazingira fulani takwimu
zisizo sahihi zinaweza kusababisha vurugu, lakini pia lazima tukubali
kwamba Serikali yenyewe ndiyo inapaswa kubeba lawama kwa uzagaaji wa
takwimu zinazokinzana na zisizo sahihi.
Tangu tupate uhuru Serikali haijawahi siyo tu kuwa
na utamaduni wa kuheshimu na kutunza takwimu, bali pia kuweka mazingira
ya kuboresha ukusanyaji wa takwimu kwa kuweka mfumo thabiti na
kuboresha Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Hivyo kama ni kupotosha takwimu, Serikali ndiyo
imekuwa mpotoshaji namba moja. Hii imetokana na kutokuwapo mfumo wa
kuainisha takwimu kutoka katika wizara, taasisi za Serikali, sekta ya
umma na sekta binafsi kama inavyofanyika katika nchi nyingi duniani. Kwa
mfano, hatudhani kama Serikali inazo takwimu sahihi kuhusu Deni la
Taifa hivi sasa.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba muswada huo wa
Sheria ya Takwimu uliochomolewa bungeni juzi ulilenga kuvibana vyombo
vya habari na kuminya uhuru na haki ya wananchi kupata habari.
Kwa miaka minane sasa, Serikali imekuwa ikisuasua kupeleka
bungeni Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari, hata
baada ya kuihakikishia jumuiya ya kimataifa mara kwa mara kwamba muswada
huo ungepelekwa bungeni.
Tunadhani Muswada wa Sheria wa Takwimu ni
mwendelezo wa mkakati wa Serikali wa kuvibana vyombo vya habari. Bunge
litafanya vyema kuukataa iwapo Serikali itaurudisha ukiwa na maudhui
yaleyale yaliyoufanya uchomolewe bungeni juzi.

No comments:
Post a Comment