Sunday, 30 November 2014

Tumejifunza nini kutokana na kashfa hizi?

Tanzania imekumbwa na kashfa nyingi kubwa tangu ipate uhuru wake.
Kashfa hizi mbali ya kulitikisa taifa zimeliachia taifa maumivu makali ya upotevu wa fedha na kusababisha baadhi ya mawaziri na viongozi wa juu wa Serikali kung’olewa.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeiongoza nchi tangu mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa), kashfa zilizoitikisa nchini ni pamoja na Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS) na Kashfa ya Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya Epa, Kashfa ya Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na hii ya sasa ya uchotaji mabilioni katika Akaunti ya Escrow.
Kwa hakika, kashfa hizi ni nyingi mno, ambazo zinatakiwa kutupa funzo la kudhibiti mianya ya kutokea kashfa nyingine.
Hata hivyo, inavyoonekana hatujajifunza kitu mbali ya kutokea kashfa hizo. Hii inadhihirishwa na jinsi kashfa ya escrow ilivyoshughulikiwa na Bunge letu.
Kama kuna kitendo cha aibu ambacho Bunge letu linakifanya mjini Dodoma ni kile kilichofanyika Ijumaa usiku cha baadhi ya wabunge na kiti cha Spika kuonyesha kuwalinda watuhumiwa wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ilikuwa inashangaza kuona baadhi ya wabunge ambao wananchi wamewapa dhamana ya kuwawakilisha katika chombo hicho kikuu cha uamuzi, wakijadili kashfa hiyo kwa itikadi za vyama.
Pia, lilichefua zaidi watu wengi waliokuwa wakishuhudia Bunge hilo kupitia redio na televisheni, baada ya baadhi ya wabunge kupendekeza adhabu nyepesi kwa watuhumiwa.
Ilikuwa kama mchezo wa kuingiza kuona mbunge akisema; “Mheshimiwa Spika mtuhumiwa huyu ni mtu mzuri hana ubaya wowote, hivyo naona asichukuliwe hatua.”
Wengine walilazimika kupotosha ukweli ilimradi kuwalinda watuhumiwa kwa madai kwamba fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, siyo fedha za umma.
Wabunge wengine wakaenda mbali zaidi ya kueleza kuwa tuhuma za kuwapo wizi wa fedha hizo umeibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na wapinzani wenzake una lengo baya na Serikali.
Hata, wengine wakafikia mahali pa kusema kuwa wabunge wa CCM ambao watapitisha au kuunga mkono kuchukuliwa hatua kwa Waziri wa Nishati na Madini na watuhumiwa wengine basi siyo wana CCM.
Pia, jambo lingine la kushangaza ni kuona Spika Anne Makinda akimchagua kupendekeza adhabu anayostahili kuchukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi baada ya kubainika kuwa alishindwa kuzuia au alizembea kuishauri Serikali kuhusu kuchotwa kwa fedha za escrow, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye naye ni mmoja wa watuhumiwa wa sakata hilo.
Kwa ujumla mambo hayo yote yalivuruga mjadala mzima na kufikia mahali hata Spika Makinda kushindwa kufanya maamuzi yanayotakiwa.
Wabunge wa upinzani waliona wazi kuwa wabunge wa CCM walikuwa wakijaribu kuwalinda watuhumiwa kitu ambacho walikiona hakina tija kwa taifa.
Hali hiyo ndiyo iliyofanya baadhi ya wabunge wa upinzani kusimama na kuimba, kupinga kiti cha Spika kujaribu kuwalinda watuhumiwa.
Nini kimetufikisha hapo? Matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na Serikali kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea, Serikali hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao.
Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani, kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii.
Nadhani kinachotakiwa kufanyika ni wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa, wanatakiwa kujitathmini upya.
Nasema wajitathimini upya kwa sababu haiwezekani kila mara nchi iingie katika kashfa ambazo tunaweza kuzizuia.
Kama hatua madhubuti zingeweza kuchukuliwa basi hakuna mtu ambaye angeweza kuingiza nchi katika aibu hii.
Kwa mfano kama waziri fulani angekuwa ameshafungwa miaka kumi jela kwa kuiibia serikali, naamini hakuna kiongozi wa serikali angekuwa na hamu ya kujiingiza katika ubadhirifu wa mali za umma. Kutokana na tabia ya kulindana ambayo ipo hivi sasa kila kiongozi anajua kuwa hata kama atapora mali ya umma sana sana akichukuliwa hatua itakuwa ni kuondolewa madarakani na yeye kubakia akiponda mali aliyoiba.

No comments: