Wengi mtakubaliana nami kwamba kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi kimekwenda kwenye kiwango kingine kabisa, na hasa ukizingatia mpaka sasa kuna makada zaidi ya 30 ambao wameonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama.
Wengi wamekuwa na maswali ya kiuchokozi hapa na
pale kwamba unadhani wimbi hili kubwa la wagombea tafsiri yake ni nini?
Nimejitahidi mara zote kusema kuna tafsiri zaidi ya moja, mosi ni
uhalisia kwamba wana CCM wako huru kuweka mawazo yao hadharani, pili,
demokrasia iko pana katika chama kwamba yeyote ambaye anaona anaenea
katika nafasi basi anayo fursa ya kujitokeza na kutangaza nia na
hatimaye kuomba kukubalika na chama.
Tatu, ni kwamba huenda watu hawajui maana hali ya
tafsiri ya urais kama taasisi na Rais kama kiongozi mkuu wa nchi na
majukumu yake, huenda watu wanauona urais kwa maana ya kusafiri kila
pahala, kufungua miradi, kutoa hotuba, kutoa maelekezo, kupita kwenye
msafara wakati wengine tunasubiri foleni, kutuma watu wakafanye kazi
kana kwamba watu hawajui wanalopaswa kutenda.
Wengine wanadhani pia ukiwa Rais kazi ya
kuwashughulikia wauza dawa za kulevya, kushughulikia wala rushwa na
ufisadi ndio hasa itakuwa kazi yao, hawa nawaona wakitembea na pingu,
bakora za mibungo na magereza yanayotembea ili kila watakaye mbaini basi
watamfunga papo hapo, wapo watangaza nia ambao nikienda kwenye vichwa
vya kwa kutafakari nawaona wakiwaza hivi.
Nne, ni kwamba huenda kuna watu wahuni pia, watu
wasio na mapenzi mema na taifa hili, watu ambao wamegeuza nafasi ya
urais bidhaa ya mnadani. Hawa wako pale kuhakikisha wanakuwa Rais,
haijalishi sote tunajua urais mtu hupewa kama dhamana na wananchi,
lakini wapo ambao tayari wameshajiona marais, hii ni kuwakosea
wapigakura, na zaidi kukikosea heshima Chama cha Mapinduzi.
Hawa watu wa namna hii wao hawajali demokrasia kwa
maana ya utawala wa watu kwa watu na watu wenyewe yaani kiingereza
“democracy”, watu hawa ni genge la wajanja wachache ambao wanataka
kushika madaraka ya nchi, maslahi yao ya msingi ni wao wenyewe
kiingereza mtindo huu tunaita “mobocracy”.
Kisiasa- Tanzania iko Njiapanda
Wengi wanahoji dira ya Taifa hili ni ipi? Taifa
halina dira, ninaposema hivi wengi mtasema kwamba mbona tunayo ile
inaitwa “vision 2025”, ni kweli lakini ile ni dira ya Tanzania Bara
pekee, na Tanzania Bara si Taifa, utaniambia pia “vision 2020” nakubali
lakini hiyo inahusu Zanzibar pekee, sasa na mimi nitakuuliza je iko
vision moja ambayo inazungumzia Taifa la Tanzania?
Kwanza nikitizama vision 2020 na 2025 utagundua
bado hazina sifa ya kuwa Dira. Dira ni waraka ambao, Taifa kwa mwafaka
limesema huko ndiko tunakotaka kwenda. Ukisoma vizuri hizi nyaraka mbili
kila moja iko huru, nikimaanisha Ukisoma vision 2025 inazungumza kana
kwamba Tanzania Bara ndio Jamhuri na Muungano na vivyo hivyo ukisoma
vision 2020 unaona Zanzibar inajizungumza yenyewe kana kwamba ni huru.
Kwangu mimi kitendo cha nchi moja kuwa na dira mbili na zisizosomana ni
sawasawa kabisa na kuwa na ndege moja yenye marubani wawili wasio na
uelewa wa pamoja wa wanakwenda wapi. Juzi juzi hapa kule nchini
Ujerumani kitendo cha kuwa na marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja
ndege inapaswa kwenda wapi kilipelekea ajali mbaya kabisa, rubani mmoja
anajua tunatakiwa kuwafikisha salama abiria wakati rubani mwingine ana
mipango ya kutoa uhai wa abiria na yeye mwenyewe kwa kuigongesha kwa
makusudi ndege kwenye milima.
Mzee Warioba alijaribu kututengenezea dira katika
Rasimu ya Katiba Toleo la Pili, lakini Katiba Inayopendekezwa ikasema
hata serikali isipofanya chochote katika utekelezaji wake isihojiwe
kokote hata mahakamani na mtu yeyote asiwe na mamlaka ya kuhoji juu ya
utekelezwaji wa dira hiyo, sasa hapo ni dira au kiini macho?
Taasisi za Mamlaka ya nchi hasa Bunge ni dhaifu,
unakumbuka wakati wa Bunge Maalum wengi ya wabunge walitaka mikataba
isipelekwe Bungeni, baada ya Bunge maalum wakazinduka wakataka mikataba
ya TPDC, wakanyimwa, roho ikawauma sana hata wakatenda kinyume na
mamlaka yao na kuelekeza Polisi iwakamate viongozi wa shirika la mafuta,
walitenda kwa hasira, kiko wapi leo? Kitendo kile kikawafanya watake
mikataba ipitie bungeni kupata ukubalifu, hawa ni wale wale ambao wengi
wao walifuta masharti ya rasimu ya Warioba yaliyosema mikataba ya madini
iridhiwe na bunge.
Wakati Bunge likiwa na mtanziko wa kimamlaka, hali
iko dhahiri shahiri kwamba kuna upungufu wa utamaduni wa kidemokrasia
(democratic culture), tumeacha kuwa watu wa majadiliano (dialogue),
hatujengi hoja bali tunapiga makelele na kushutumiana wakati wote,
Mwalimu Nyerere alipata kusema “argue, don’t shout”. Hatujengi muafaka,
hatufanyi maridhiano, hatuna uelewa wa pamoja katika masuala ya msingi,
hatuna uhimilivu (tolerance) lakini inaonekana tuna uhimilivu kwa mambo
kama rushwa, ufisadi, mauaji ya albino na vikongwe n.k.
Tumeanza kushuhudia roho mbaya ya utengano (negative devisive
force), ukabila, ukanda, udini, ubara na uzanzibari. Umeshuhudia hata
watangaza nia tayari wameanza kujipanga kikanda hii ni hatari kwa ustawi
wa umoja wa kitaifa.
Inaanza kuonekana uongozi si dhamana tena bali
mali ya watu fulani. Utumishi wa umma unafanya kazi kwa woga. Maadili ya
Taifa, binafsi na ya viongozi ni tatizo kubwa, hata pale Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi inapowafuatilia wale wanaokiuka miiko ya uongozi
utagundua nguvu zake zina ukomo mkubwa.
Kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na
mmomonyoko wa maadili, angalia namna ambavyo watangaza nia wanatumia
fedha nyingi, swali la kujiuliza ni fedha zao binafsi? Na kama si zao
waliowapa wana maslahi gani na nafasi ambayo watangaza nia hawa
wanaitafuta? Muungano wetu bado una changamoto nyingi, Serikali mbili
hazieleweki, siyo tu kwenye Katiba ya 1977 bali hata kwenye Katiba
Inayopendekezwa. Watu wa Tanzania Bara wanauona Muungano kama mzigo na
watu wa Tanzania Zanzibar wanauona Muungano kama Kero. Kuvurugwa kwa
mchakato wa kupata Katiba Mpya ni huzuni nyingine inayoongeza njia panda
ya kisiasa
Kiuchumi- Tanzania njiapanda
Umma wa watanzania hauna mali za pamoja,
tulibinafsisha kila kitu na mashirika ya umma yaliyosalia ni hohehahe,
mfano ni shirika la ndege la Taifa “Air Tanzania”, Shirika la Reli (TRL)
ni shida nyingine kubwa licha ya kwamba tuna ubia na watu wengine.
Tuna Shirika la Nyumba (NHC), hili linakimbia kwa
kasi baada ya maboresho makubwa ya kiutendaji, lakini nawapa indhari
kwamba uchumi wa Marekani ulianguka kwa uwekezaji usiotabirika katika
makazi na nyumba, tuwe macho.
Sekta binafsi ni dhaifu, sekta binafsi imeingia
katika huduma na si uzalishaji, tizama kampuni ambazo zinaonekana vinara
ni makampuni ya simu.
Haya hayazalishi, haya yanatoa huduma na
yanachukua fedha za Watanzania maskini zaidi kuliko hata faida ambayo
tunanufaika nayo moja kwa moja kama wananchi maskini na wasio na ajira.
Angalia ongezeko kubwa la mabenki, unadhani
wanufaikaji ni wakulima na wafanyabiashara ndogondogo ambao kwa kiasi
kikubwa wanaangukia katika sifa za watu wasio kopesheka, Tuamke, benki
ni nzuri lakini lazima tuwe na uchumi ambao unabeba watu wake.
Hakuna viwanda vya kutosha vya uzalishaji
kunakopelekea tatizo la ajira na kupoteza fedha za kigeni (hakuna
exports za kutosha), mchele wa mbeya na kwingineko tunao lakini
tunaagiza, sukari ya kutoka Mtibwa, Kilombero na Kagera tunayo lakini
tunaagiza, tunayo gesi lakini bado tunaagiza mafuta mazito. Halafu dola
ya kimarekani ikifika zaidi ya shilingi 2000 tukiuliza tunaambiwa huko
duniani dola imeimarika zaidi, kweli?
Sekta binafsi iliyo dhaifu haiwezi kusimamia demokrasia na kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwapo.
Na hapa niwaseme kidogo Taasisi ya Sekta Binafsi
(TPSF) kwamba wameona Bunge Maalum lilivyoendeshwa na namna ambavyo
Katiba Inayopendekezwa imedhoofisha maadili ya viongozi na kuvuruga Dira
ya Taifa kwa kuiwekea vikwazo, lakini kwani umesikia wakikemea au
wakishauri kitaalamu madhara ya kubomoa misingi ya maadili na
uwajibikaji katika Katiba? Nawapa changamoto, na wao wajitafakari.
Mkazo haujawekwa katika uchumi wa kujitegemea unaozingatia
ukuaji wa kilimo kinachotoa malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo
vinachakata malighafi kuwa bidhaa zilizochakatwa au bidhaa kamili ambazo
ziko tayari kurudi na kutumika katia sekta nyinginezo ikiwemo kilimo
Kukosekana kwa uchumi imara unaojitegemea
kunazalisha watu masikini wengi zaidi katika Taifa letu. Tuna walipakodi
wachache na tuna walaji wengi katika Taifa lakini pia mianya ya
wanaokula zaidi yaw engine kinyume cha sheria ni wengi zaidi na
kusababisha chakula wanachokusanya wachache wetu ama kinaliwa na
wachache wetu kinyume na sheria na matokeo yake hakitoshelezi mahitaji
yetu kama Taifa. Tunalo pia Tatizo la kuwa na vyanzo mbadala mbali na
hivi vya sasa vya mapato ya Taifa na Serikali, na bado tunalo tatizo la
kampuni za madini kutokutoa kodi ya mapato kutoka faida zao.
Wengi wanasema wanatoa kodi lakini ni kodi
wanazokatwa wafanyakazi wao na sio kodi inayokatwa kutokana na shughuli
za ushalishaji wa kampuni. Kwenye gesi ni eneo linguine ambalo ukiachia
kwamba limegubikwa na sintofahamu juu ya namna mikataba yake imefungwa
hasa katika ngazi ya utafutwaji wa gesi ni kizungumkuti kingine
kinachotuweka kwenye njiapanda kama Taifa.
Rais tunayemtaka awamu ya tano
Tunataka Rais ambaye anajua tuko njia panda, ana
ana uwezo na mamlaka ya kukemea kwasababu na yeye ni mwadilifu “moral
authority”. Tunataka kiongozi ambaye anakubalika na jamii na jamii
inamwona kama sehemu ya majibu ya changamoto zao. Hatutaki watu
wajitembeze kwetu, tunajua tunataka Rais ambaye atasimamia masilahi
yetu.
Leo karibu kila mtia nia, nasikia huyu kapata pesa
kule, huyu kapata pale, huyu hela za wizi, huyu kapokea fedha chafu,
huyu kachukua za watu wabaya na kadharika. Watanzania tuache ushabiki,
tusimame na tuwe wamoja katika hili. Rais wetu akiletwa na watu maana
yake si wetu ni wao. Tafakari

No comments:
Post a Comment