Kuna kisa cha msafiri mmoja aliyeomba mahali pa kulala kwa
mjumbe wa Serikali ya Mtaa ili kesho yake aendelee na safari yake.
Alifika saa 5.00 usiku na kwa kuwa mjumbe alikuwa amekwisha kula,
alichofanya ni kumwandalia msafiri huyo mahali pa kulala, basi.
Alishukuru. Mlo wake usiku ule ulikuwa machungwa
sita aliyonunua njiani. Loo, alipokata la kwanza, lilikuwa limeoza,
alitupa kwenye kona. Lahaula, alipochukua la pili, nalo lilikuwa
limeoza. Balaa, kumbe yote yalikuwa vivyo hivyo.
Haraka aligundua kwamba kilichosababisha akaona
machungwa kuwa yameoza ni kibatari, hivyo, alikizima, akachukua
machungwa yale na kuanza kula gizani, akalala. Heri angelala na njaa
kabisa maana kesho yake aliharisha sana njiani na kutapika; we acha tu!
Kisa hicho kinakaribia kujirudia ndani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) ambacho makada wake waliotangaza nia au kuchukua
fomu za kuwania urais wanachafuana na kujiozesha. Akisimama huyu anasema
yeye tu anafaa, akisimama yule anadai wengine wote bomu, sasa
atapatikana wapi aliye bora?
Edward Lowasa alijizuia alipotangaza nia, lakini
Charles Makongoro alimshona barabara Stephen Wasira. “Mzee Wasira
alifanya kazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Nyerere
aliondoka yeye akabaki, bado yupo. Akaja Ali Hassan Mwinyi akaondoka,
yeye yupo….na sasa huyu Mzee Wetu Jakaya Kikwete anaondoka, atamuaga
yeye atabaki yupo!” Hebu jiulize, ikitokea ‘Bwana Yupo’ ameteuliwa
itakuwaje?
Frederick Sumaye hakutafuna maneno, alisema; “Kama
kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni, nitampisha (katika
mbio za urais).” Alishangiliwa na wafuasi wake huku wakimwambia;
“Hakunaaaa.”
Bernard Membe aliwaambia wanaCCM mkoani Lindi;
“Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi
adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia
nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.” Halafua akadai, “Hata Baba
wa Taifa, Mwalimu Nyerere huko aliko atafurahi endapo nitakuwa rais.”
Yaani Nyerere afurahie Membe kuwa rais kuliko hata mtoto wake Makongoro?
Prof Sospeter Muhongo alisema; “Nafahamu...
sidhani kama kuna mtu mwingine anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu
wanaCCM, nitahakikisha tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa
ya uchumi wa Taifa hili….Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi,
mnanijua vizuri…”
Samuel Sitta alijipigie debe kwa kusema; “Kwa
kifupi ninao uelewa na uzoefu unaolingana na changamoto za kipindi
kigumu cha miaka mitano ijayo yenye mwelekeo wa kutikisa misingi ya
utawala wa nchi yetu… kwa uimara wangu wa uongozi, nitajumuisha nguvu na
maarifa ya wananchi ili tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za
maendeleo kwa ufanisi na tija zaidi.”
Mwigulu Nchemba alisema; “Ahadi yangu kubwa kwenu
ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania
kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye
uchumi wa kati.”
Kauli hizi zimetolewa kirejareja sana, lakini
zitakuja kuwa na madhara makubwa mbele ya safari ndani na nje ya CCM
kuwaaminisha wapigakura kwamba “chungwa teule” halijaoza kiviiile. Hapo
watajitahidi kupiga msasa na kupinga methali isemayo “samaki mmoja
akioza wote wameoza”.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu
ya Taifa na mkutano mkuu wa CCM walioshiriki mwezi huu, kuwaunga mkono
makada wanaowapenda wawe marais, ndiyo mwezi ujao, watashiriki
kumpitisha mmoja akapambane na wa Ukawa kutafuta tiketi ya kuishi Ikulu
ya Magogoni, Dar es Salaam.
Nani akemee? Wazee wa kukemea walijazana Arusha, Butiama, Mwanza, Lindi, Mbeya na kwingineko kuwapiga ‘tafu’ watangazania.
Kingunge Ngombale-Mwiru, mmoja wa makada wenye
hekima wanaotegemewa kutoa ushauri ndani ya CCM yuko katika Timu Lowasa.
Siku Lowasa alipotangaza nia mjini Arusha, Kingunge alikuwapo na
alitoboa siri ya Halmashauri Kuu akisema, Mwenyekiti wa chama hicho,
Rais Kikwete aliwataka wale wenye ugomvi kutafuta suluhu. Vyema. Je,
yeye kuwa kwenye Timu Lowasa ni kusaidia suluhu ipatikane?
Lowasa mwenyewe yuko tayari kwa suluhu? Akijibu
maswali ya wahariri kuhusu kutofautiana na wenzake alisema; “…Kama kuna
mtu ambaye hanipendi ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.” Siku
alipochukua fomu alisema, “Naamini katika ushindi na sina mpango wa
kushindwa.” Waandishi wa habari walipomuuliza kama yupo tayari
kushirikiana na wanasiasa wanaompinga sasa, aliwajibu; “Nitavuka daraja
nitakapofika.” Mmh!
Ndiyo maana nasema zinakaribia siku za CCM kula
gizani chungwa lililooza na kununua msasa ili kulitakatisha kabla ya
kuliuza kwa wananchi.
0658 383 979

No comments:
Post a Comment