Dar es Salaam. Makada wa CCM waliotangaza nia
au kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na chama hicho kuwania urais,
wameeleza jinsi rushwa, ufisadi na udhaifu katika ukusanyaji kodi huku
wakijinadi kuwa wao ndiyo wataondoa uovu huo iwapo watapitishwa kushika
nafasi hiyo ya juu kisiasa.
Lakini hakuna hata mmoja aliyeiponda Serikali kwa
kushindwa kudhibiti rushwa, ambayo baadhi walishasema kuwa imekithiri
hata kwenye chama hicho tawala, huku mmoja akisema kuwa iwapo CCM
itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Kati ya waliotangaza nia na kuchukua fomu, makada
11 ni mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne wakiwamo mawaziri waandamizi
walioshika nafasi za juu na waliofanya kazi katika awamu zote nne.
Pia wamo makada waliokuwamo kwenye Baraza la
Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, lakini wakaondoka kwa sababu
tofauti, huku kundi jingine likihusisha watendaji wakuu wa zamani wa
Idara ya Usalama wa Taifa.
Lakini bado tatizo hilo la rushwa limekuwa
likitumiwa na makada hao wa CCM wanaowania urais wakati wakijinadi kwa
wanachama wao kwamba watafumua mfumo uliopo, kusuka upya sheria na
kuimarisha taasisi za fedha ili watuhumiwa wakubwa wa rushwa wafikishwe
kortini na kufungwa, badala ya kuwakamata walarushwa wadogowadogo pekee.
Katika hotuba zao wakati wanatangaza nia mbele ya
umati wa wafuasi wao na mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua
fomu, makada hao, mbali ya kueleza mikakati tofauti ya namna ya
kuimarisha uchumi wamekosoa mfumo wa sheria kwamba unawalinda mafisadi
wakubwa ambao hawakamatwi hadi kwa kibali maalumu.
Kwa mfano, akitangaza nia ya kuwania urais
kijijini kwao Butiama, Charles Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema anaomba kibali cha kuisaidia CCM
ikomeshe rushwa, na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe
Watanzania, anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.
“Kosa la Rais Jakaya Kikwete ni kuwapenda sana
marafiki zake. Kwa bahati mbaya, baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka,”
alisema Makongoro ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliwaambia
wafuasi wake mkoani Lindi kwamba ili kutekeleza utawala bora, hawezi
kukaa kimya kuona rushwa, ubadhirifu, ufisadi vikichukua nafasi katika
utawala wake.
“Ninawatumia salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi
kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha Watanzania wanachukia rushwa na
kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na mpokeaji rushwa. Kama ni
watumishi wa umma, watakwenda na maji...,” alisema mbunge huyo wa Mtama.
Ahadi ya kukomesha rushwa pia ilitolewa na Waziri
wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyesema kwamba anataka kulifanyia Taifa
mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na
kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
“Ili kukomesha tatizo la rushwa, hatuna budi
kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” alisema Sitta
kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, Tabora.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba alisema akifika Ikulu, ili kupambana na rushwa, “nitafanya
mabadiliko ya kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii ikiwamo kuipa meno
Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa
moja kwa moja mahakamani”.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen
Wasira alionyesha kukiri kuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuwania
urais, wamo wenye kashfa za rushwa, lakini akajitenga nao kujionyesha
kuwa hana doa hilo.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa
lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya
kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea
anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea,”
alisema waziri huyo mkongwe na kuongeza:
“Kumbukeni sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyinginezo.”
Wasomi wawashangaa
Lakini kauli na ahadi hizo za makada hao wa CCM
wanaotaka kuingia Ikulu zimewashangaza wachambuzi waliofuatwa na
Mwananchi ili kutoa maoni yao kuhusu hoja za wagombea.
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu
cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema wengi waliotangaza
nia ya kuwania urais wanatoka kwenye mfumo wa rushwa, hivyo itakuwa kazi
ngumu kwao kuiondoa. “Tanzania imefikia ngazi ambayo rushwa imekuwa
mfumo wa utawala. Ikifikia hatua hiyo kuindoa ni kazi kubwa kwa sababu
kupiga vita mfumo si suala dogo, hawa watiania walishindwa huko
serikalini, watawezaje sasa?” alihoji.
Alisema wengi kati ya wagombea hao wanatoka katika
mfumo wa rushwa ambao wameujenga wenyewe, hivyo si kazi rahisi
kuimaliza kwa sababu kuna kulindana na kustahimiliana.
“Kulindana ni utamaduni wa mfumo huo wa rushwa.
Ndiyo wameujenga na walikuwa ndani ya mfumo, ndiyo maana wanashindwa
kueleza watatumia mbinu gani
kuondoa mfumo huo,” alisema.
Alisema anahitajika mtu shupavu kuiondoa rushwa
hapa nchini kwa sababu imeshaota mizizi kwenye mfumo wa utawala, na
kwamba kusema tu wataimaliza hakuna ukweli wowote.
“Ufisadi unaofanywa na viongozi wa Serikali,
vigogo na wanasiasa zina athari kubwa kwa uchumi wa nchi hii,” alisema
Profesa Mpangala.
Mawazo hayo yanalingana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania, Hamad Salim ambaye alisema ni vigumu kwa wanaotaka kuwania
urais kuimaliza rushwa kwa sababu wote wanafanya kazi katika mfumo
uliojaa rushwa.
“Wao wenyewe wanaingia madarakani kupitia mfumo wa
rushwa, sidhani kama wataweza kuung’ata mkono ambao unawalisha. Kama
mchakato mzima wa kuingia madarakani kama vile kuchukua fomu, kupiga
kura, kutafuta wadhamini wote umejaa rushwa, wataweza kuiondoa?”
alihoji.
Alisema ahadi wanazozitoa watia nia ni vigumu
kutekelezeka kwa sababu wanapambana na mfumo wao wenyewe na kazi ya
kuumaliza ufisadi si ya mtu mmoja wala ya siku moja.
Salim alisema inashangaza baadhi ya watangazania
kukusanya watu wanaowaunga mkono, kuandaa kampeni na kuandaa watu wa
kuwashangilia.
Alisema watangazania hao wanatoa ahadi zao kama
kampeni tu na wakiingia madarakani hawatafanya kazi kulingana na
walichoahidi bali kwa kuangalia ilani ya CCM.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa UDSM, Dk Benson
Bana aliwataka watangazania hao kuacha kutumia kigezo cha rushwa kama
njia ya kupata kura na badala yake wazungumzie sera nyingine.
Dk Bana alisema Watanzania hawatamchagua kiongozi
kwa sera zake za kutaka kuondoa rushwa kwani nao wanafahamu kuwa CCM
imejaa rushwa.
“Watanzania hawamchagui mtu kwa kigezo cha kupambana na rushwa, hicho ni kimbelembele tu, waache kimbelembele,” alisema.
Dk Bana pia alisema watangazania hao waiache
Takukuru ifanye kazi yake na wasiwadanganye wananchi kuwa wao ni
mabingwa wa kupambana na tatizo hilo.
Lakini mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa
Fedha(IFM) kitivo cha kompyuta na mifumo ya hesabu, Dk Eliamani Sedoyeka
aliliangalia tatizo la rushwa kuwa ni silka na hivyo ni vigumu
kuthibitisha iwapo mgombea ana au hana tatizo hilo.
Dk Sedoyeka alisema kiongozi anayesema atapambana
na rushwa anatakiwa kupimwa kwa rekodi yake ya uongozi kwa kuangaliwa
iwapo aliweza kukemea, kuadhibu, au kukataa rushwa katika mazingira
yoyote yale.
“Kwa mfano wapo watu wanajiweka karibu na
matajiri, wanapewa fedha na matajiri za kufanya kampeni, je watakuja
kulipa vipi hisani za matajiri watakapoingia madarakani? Hayo ndiyo
mazingira,” alisema

No comments:
Post a Comment