Oktoba mwaka huu Watanzania wanatarajia kumpokea rais mpya wa
awamu ya tano kwa imani kuwa atakata kiu kubwa ya watu wanaopenda kuona
wanawekewa mazingira mazuri ya kuondokana na umaskini.
Uzoefu wa awamu nne zilizopita, umeonyesha kuwa
pamoja na vyama vinavyowasimamisha wagombea kwenye kiti cha rais kuwa na
sera zao, kila aliyengia alikuwa na aina yake ya mabadiliko katika
uchumi nchi.
Anayeingia madarakani katika kipindi hiki, anaweza
akawa ana majukumu makubwa zaidi kuliko wengine waliopita maana
Watanzania wengi wana mambo mengi ambayo wanahisi yangetatuliwa, nchi
itaingia kwa haraka kwenye mafanikio na kuondokana na umaskini
uliokithiri.
Hadi sasa, Watanzania zaidi ya 30 wamejitokeza
kupitia CCM na CUF, wakiwa na mawazo mbalimbali ya kutatua matatizo ya
Watanzania kiuchumi, iwapo watapewa ridhaa ya kukalia kiti cha rais.
Yafuatayo ni sehemu ya maelezo ya baadhi yao ambao
katika maelezo yao wanawahakikishia Watanzania watazifanya ndoto zao za
maendeleo kuwa kweli.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa anasema
akifanikiwa kuingia Ikulu atahakikisha analiondolea taifa sifa mbaya ya
kuombaomba na kulifanya kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika. “Tunapaswa
kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania
aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote
zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa
maendeleo tunayoyazungumzia,” anasema Lowassa.
Anasema anataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi
wa utajiri unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira ili kuwawezesha
Watanzania kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe anasema akipewa ridhaa hiyo, atazishirikisha
sekta binafsi na umma katika kuendesha uchumi na kuziwezesha kupata
mitaji mikubwa.
Anasema ana mpango wa kuvifufua viwanda na kuboresha kilimo, ili mazao yanayozalishwa yanunuliwe hapahapa nchini.
“Hatutaki tena kusafirisha malighafi nje halafu
tunaletewa bidhaa zilezile zilizosindikwa. Haya mapinduzi ya viwanda ni
lazima, mara tu nikiingia Ikulu Oktoba mwaka huu,” anasema.
Anasema kasi ya kufanikisha maendeleo ya viwanda
itachochewa na uwepo wa gesi asilia iliyovumbuliwa mikoa ya Kusini,
itakayopunguza gharama za upatikanaji wa nishati ya umeme.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba anasema atahakikisha anakukuza uchumi kwa
kuwa na serikali ya watu waadilifu. Anasema atahakikisha kuwa Serikali
inaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi kisiasa, kiuchumi
na kijamii. “Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda
serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila
chembe ya uonevu wala ulegevu. Nitaunda serikali ya mawaziri 18, ambayo
haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo
wake,” anasema Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina anasema anataka nafasi hiyo ya
juu nchini ili akasimamia makusanyo ya kodi yatokanayo na rasilimali za
taifa yanakuwa mara tatu. Anasema kuwa Tanzania ina uchumi mzuri lakini
unaharibiwa na mfumo wa utawala uliopo. “Kwa sasa Taifa linakusanya Sh12
trilioni kwa mwaka, lakini mimi nitahakikisha makusanyo hayo
yanaongezeka mara tatu ya hapo. Sasa makusanyo yanashindikana kutokana
na kuwapo kwa mianya mingi ambayo inaruhusu wizi wa mali za umma,”
anasema. Mpina anasema Tanzania siyo maskini ila umaskini uliopo
unasababishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wizi, matumizi mabaya ya
madaraka na mikataba mibovu inayofanywa na watu binafsi na serikali.
Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala anaamini kuwa
uchumi unajengwa kwa kuyapa umuhimu mambo makubwa matatu; huduma za
jamii, elimu na maji. Anasema ataboresha miundombinu ya reli, barabara,
bandari na viwanja vya ndege.
“Kazi ya kujenga uchumi na maendeleo ninaamini
tunaiweza, tukiamua. Uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo; sema tuna
upungufu katika kuchukua hatua za kutenda,” anasema.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen
Wasira anasema Tanzania inahitaji miundombinu mingi kuanzia vinu vya
kufulia umeme hadi mifumo ya usambazaji maji safi na mawasiliano ya
simu. “Utawala wangu utaweka kipaumbele cha hali ya juu mpanguo huo ili
kuhakikisha uwapo wa miundombinu ya uhakika na gharama nafuu kwa ajili
ya wazalishaji na walaji kuendana na ukuaji wa juu unaomfaidisha kila
mmoja,” anasema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu anasema ili kufanikiwa kiuchumi nchi, inahitaji rasilimali
watu, hivyo ameahidi kutumia nguvu katika kufanikisha jambo hilo.
Anasema anataka nchi ipige hatua kutoka hapa ilipo iende mbali zaidi
kupitia sekta mbalimbali zikiwemo elimu na afya.
Waziri Nyalandu anaeleza atatumia nguvu kubwa
kuwekeza katika rasilimali watu ambayo ni muhimu kama ilivyo kuongeza
nguvu za kuwawezesha Watanzania kuwekeza katika jamii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba anasema
iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu, atawavusha Watanzania kutoka katika
hali ya uchumi mdogo uliopo hivi sasa na kuwaingia katika ulio wa kati.
“Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili,
nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu
wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia,” anasema
Nchemba.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Entrepreneurship
Limited, Boniphace Ndengo anasema Tanzania inaweza kufikia kiwango cha
uchumi mzuri utakaoleta ustawi kwa wananchi wengi.
Ndengo anasema alianza biashara ya mghahawa mdogo
Mtaa wa Uhuru mjini Musoma, lakini hivi sasa anaitwa mwekezaji hivyo
kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo nchini, anakusudia kujenga
Tanzania kuwa kituo bora cha kimataifa cha utalii na kuifanya kuwa nchi
ya uchumi wa kati.
Mjumbe wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ally anasema atatokomeza rushwa kwa kuwa ni adui wa uchumi.
Amina anataja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na
kuinua uchumi, kuongeza mapato, kupambana na rushwa, huduma za jamii
kuondoa matabaka ya walionacho na wasionacho na kudhibiti mapato ili
yaendane na matumizi.
Balozi Ally Karume anasema Tanzania ili iweze
kujenga uchumi imara, inahitaji kiongozi mwenye mbinu na uwezo wa
kupambana na rushwa na ufisadi kwa vile ndiyo adui wakubwa wa maendeleo
yake.
“Uhuru wa kujituma ni muhimu sana kwa kila mtu. Siyo mtu anataka
kuuza njugu wewe unamwambia huna leseni. Unamuuliza leseni kwani
anataka kuendesha gari? Mtu akitaka kuendesha gari ndiyo mdai leseni,
lakini siyo kuuza njugu lazima watu wapewe uhuru wa kujituma,” anasema
Balozi Karume.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast
Enterpreneurship, Boniphace Ndengo anasema adui mkubwa wa taifa ni
rushwa na ujinga ambao ‘umezaa’ ufisadi, hivyo atakapoingia madarakani
anapiga vita rushwa ili kukuza uchumi.
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal anasema
kwa kuwa yeye ni mwanasayansi atatumia taaluma hiyo kuleta maendeleo
nchini. “Hakuna uamuzi uliokuwa sahihi zaidi ya uamuzi wa kisayansi.
Mimi siku zote uamuzi wangu unafuata utaratibu huo, ndivyo nilivyolelewa
na kufunzwa na nitaendelea kuongozwa kisayansi,” anasema.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema: “Nitahakikisha
uchumi wa wanyonge unainuka. Kwa hiyo katika mpango wa miaka mingine
mitano, tutajikita kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tukifanya hivi
umaskini utapungua kwa kiwango kikubwa na ajira zitapatikana.” Monica
Mbega anasema akifanikiwa kuwa rais wa Tanzania atafanyia utafiti
changamoto za awamu zilizopita na kuhakikisha anazitafutia suluhu ya
kudumu.
Monica anasema pia atakabiliana na viashiria vya
uvunjifu wa amani ambavyo vinatishia kuvuruga mipango ya maendeleo.
Viashiria hivyo anavitaja kuwa ni uhasama, mauaji ya albino, wizi,
ubaguzi wa dini na ukabila.
“Tutazungumzia upendo na umoja kuanzia ndani ya
familia ndio kitovu kitakachosaidia kujenga amani. Amani itajengwa na
upendo misamaha na umoja,” anasema.
Waziri wa Ofisi wa Rais (Kazi Maalumu) Profesa
Mark Mwandosya anasema atakuza uchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha
kilimo cha kisasa, kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya shughuli za
kilimo.
Anasema atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa
kujisimamia na kwamba Serikali itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya
Watanzania waone matunda ya kukua kwa uchumi. “Serikali itakuwa injini
ya kukua Kwa uchumi kwa kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye
kazi kwa ufanisi na kulipa kodi nzuri kwa Serikali,’’ anasema.
Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo
anasema ataondoa umaskini nchini kwa kutumia uchumi wa gesi. “Nitafuta
umaskini kwa kutumia uchumi wa gesi ambao utakuwa unamilikiwa na
Watanzania wenyewe. Gesi nimesomea kwa hiyo ninafahamu mambo haya
vizuri. “Tena kutokana na juhudi zangu za kuhamasisha vijana wapelekwe
nje kusoma masomo ya gesi, nategemea mwakani tutakuwa na wataalamu wengi
zaidi watakaoweza kufanya kazi kwenye sekta hii.”
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja anasema
atapambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi, ambayo ni
umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
“Maendeleo ya kweli ya nchi yetu hayawezi kuletwa na sekta ya umma peke
yake, bali yataletwa kwa kushirikisha kikamilifu sekta binafsi. Ni
muhimu rais wa awamu ya tano awe na weledi wa kutosha kuhusu utendaji wa
sekta ya umma na binafsi,” anasema.

No comments:
Post a Comment