Kujenga umoja na utambulisho wa kitaifa, Kupanua uhuru na haki za msingi za raia, kupanua demokrasia, kuweka mfumo wa uwazi wa utawala na uongozi na kudhibiti ufisadi, kuimarisha uchumi na uzalishaji, kujenga umoja na ushirikiano wa kikanda na hatimaye umajumui wa Afrika nzima.
Kabla sijajadili misingi hiyo, nizungumzie kidogo suala la mchakato wa kuandaa Katiba. Katiba ni chombo chenye mamlaka juu ya kila mtu na kila chombo katika jamii.
Katiba lazima itawale mamlaka zote kuanzia kwa Rais hadi kwa balozi wa nyumba kumi na kuishia kwa mtu binafsi. Katiba sharti itawale asasi zote kuanzia Bunge hadi mahakama, polisi, asasi za kiraia na kidini, n.k.
Ndiyo maana haifai kwa Katiba kuamuliwa na vyama vya siasa ambavyo ni vikundi vyenye maslahi maalumu ndani ya Katiba hiyo.
Kujenga Umoja na Utambulisho wa Kitaifa
Katiba yoyote ile ya nchi huwa na jukumu la kujenga utaifa na utambulisho wa Taifa linalohusika na hivyo kuchunga na kulinda usalama na uzalendo wa Taifa hilo. Ndiyo maana Katiba za mataifa mengi hutaja mipaka ya nchi, Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya/za Taifa na lugha nyingine rasmi kama zipo.
Katiba za baadhi ya nchi hutaja hata hati za maandishi za lugha yao na vipengele muhimu vya utamaduni wa Taifa, kama vile dini, mila na kadhalika. Katiba ya sasa ya Tanzania inataja baadhi ya mambo haya lakini si yote. Kwa mfano haitaji Lugha ya Taifa!
Kujenga utambulisho na utaifa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa kuweka misingi imara ya umoja inayokubalika kwa wananchi wote wa makundi na matabaka yote, kujenga uzalendo, mapenzi ya nchi na moyo wa kuwa tayari kuitetea na kuifia nchi ikibidi.
Ni wazi kwamba, suala la kuruhusu uraia wa nchi mbili au zaidi ambalo linapigiwa debe sana hivi sasa na baadhi ya watu, inabidi litazamwe kwa kuzingatia msingi huu wa uzalendo na maslahi ya Taifa: Mathalan, itakuwaje iwapo raia wa Marekani (au nchi nyingine), ambaye pia ni raia wa Tanzania, atatumwa na Rais wake wa Marekani na kupewa nyenzo zote kuja kututawala na kutekeleza matakwa ya nchi yake (ya Marekani) hapa kwetu? Utamzuiaje?
Hatusemi kwamba kiongozi asiyekuwa na uraia wa nchi ya kigeni hawezi kutumiwa na nchi hiyo kutekeleza maslahi yake katika nchi anayoiongoza. Tunawafahamu viongozi vibaraka wengi waliotumiwa hivyo. Tunachosema hapa ni kwamba, tusiwarahisishie maadui zetu mchakato wa kupata vibaraka miongoni mwetu.
Suala la utamaduni sharti lipewe uzito kikatiba, maana bila utamaduni hakuna Taifa na njia ya uhakika ya kumdhibiti na kumtawala mtu ni kumteka kitamaduni na kiakili.
Hapa suala la lugha sharti lipewe uzito unaostahiki; Lugha ya Taifa, Kiswahili ipewe nafasi muhimu kikatiba na lugha za kijamii na za kigeni tunazozihitaji zisisahaulike. Katiba itaje wazi kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na lugha rasmi ya kwanza na Kiingereza ni lugha rasmi ya pili.
Katiba ielekeze kwamba itatungwa sheria mahsusi itakayofafanua nafasi, dhima na matumizi ya lugha ya Taifa na lugha nyinginezo katika jamii.
Kupanua Uhuru na Haki za Raia
Katiba inapaswa kulinda uhuru na haki za raia ambazo ni pamoja na haki za kuishi, kuheshimiwa kama binadamu, kufanya kazi na kupata malipo ya haki kwa kazi hiyo, kupewa pensheni ya uzeeni, kujumuika, kusafiri, kuishi popote, kuabudu au kutokuabudu.
Haki za lugha na utamaduni pia zinahusika hapa. Na haki hizo lazima ziwe ni kwa raia wote bila kujali jinsi, kabila, rangi, dini, cheo, umri au nasaba.
Katiba ya sasa inatoa haki hizo kwa kiasi fulani. Katiba ijayo ingefaa isisitize na kufafanua zaidi haki hizi za msingi.
Kumtaja Mungu katika Katiba
Hapa tunaweza kueleza kuwa pendekezo la Jaji Mstaafu Barnabas Samatta, katika kongamano moja kuwa Katiba mpya itaje Mwenyezi Mungu halikubaliki kwa sababu linakwenda kinyume na uhuru wa kuabudu tunaouzungumzia.
Kwa kuwa Katiba tayari inatoa uhuru wa kuabudu, hakuna sababu ya kuufunga uhuru huo kwa kuuhusisha na imani fulani maalumu, zile zinazozingatia dhana ya Mungu. Ni vyema Katiba iendelee kutofungamana na imani ya dini yoyote.
Kupanua Demokrasia
Katika ulimwengu wa sasa na ujao, utawala wa kidemokrasia hauepukiki. Hivyo tunahitaji Katiba inayotambua haki na haja hiyo ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Demokrasia tunayozungumzia hapa ni demokrasia pana inayojumuisha wananchi wote wa makundi yote. Hatuzungumzii demokrasia ya vyama vya siasa tu.
Katiba yetu ya sasa kwa kiasi kikubwa inajikita katika demokrasia ya vyama badala ya demokrasia ya Umma. Labda hili linahitaji ufafanuzi zaidi.
Miaka kadha iliyopita makundi mbalimbali ya wanasiasa, yalianza kufanya kampeni ya kutaka majimbo ya uchaguzi yaongezwe ili kuimarisha uwakilishi na demokrasia.
Tulishuhudia madiwani wa halmashauri mbalimbali, wakipitisha maazimio ya kuongeza majimbo ya udiwani na ubunge. Baadhi ya wabunge na vyama vyao vilevile walipendekeza majimbo mapya yaanzishwe.
Kampeni hiyo ilifanikiwa kwa kiasi fulani na majimbo mapya kadha yaliundwa, japo ilitolewa tahadhari kuwa jengo la sasa la Bunge mjini Dodoma halina nafasi ya kuongeza wabunge wengi. Msingi wa kampeni hii ni dhana potofu kuwa demokrasia maana yake ni kuwa na wawakilishi wengi wa vyama katika Bunge na mabaraza ya madiwani.
Mtazamo huu wa kimajimbo kuhusu uwakilishi unadaiwa kutokana na mfumo wa Westminister, yaani mfumo wa Bunge la Uingereza. Hii ni kweli kwa kiasi fulani tu.
Waingereza wana utaratibu wa uwakilishi wenye historia ya karne nyingi za mapambano ya kitabaka na kikatiba kati ya mamwinyi, mabwanyenye, watwana na wafanyakazi na kati ya ufalme wa England na falme za Wales, Scotland na Ireland, ambazo kwa pamoja zinaunda Ufalme wa Muungano wa Uingereza (UK).
Baada ya miaka mingi ya kupambana na kumwaga damu na baadhi ya viongozi na wafalme kukatwa vichwa, hatimaye Waingereza walikubaliana kuwa na Bunge lenye chemba au mabaraza mawili ili kuzingatia maslahi ya pande zote.
Mabaraza hayo ni lile la Mamwinyi (House of Lords) na lile la Makabwela (House of Commons). Wajumbe wa Baraza la Mamwinyi hawachaguliwi na wananchi na hujumuisha mamwinyi wenye kumiliki ardhi kubwa na viongozi wakuu wa Kanisa la Uingereza. Wajumbe wa Baraza la Makabwela huchaguliwa majimboni.
Mapambano ya kudai demokrasia nchini Uingereza, vilevile yaliibua vyama vikuu viwili, Conservative (chenye kuwakilisha maslahi ya mamwinyi na mabwanyenye) na kile cha Labour (ambacho awali kiliwakilisha maslahi ya matabaka ya wazalishaji wafanyakazi na vibarua.
Siku za karibuni, kimezuka chama kingine kikuu cha tatu, Liberal Democrats, ambacho kimetokana na muungano wa vyama vidogo viwili vya Liberal Party na Social Democratic Party, hicho ni chama cha kiliberali cha mrengo wa kati.
Vipo vyama vingine vidogo vidogo, lakini havina athari kubwa kiutawala. La muhimu kufahamu kuhusu mfumo huu wa Uingereza ni kwamba, vyama vyote vinavyoshika utawala huendeleza takriban sera zilezile za uchumi, utaifa na mambo ya nje na hakuna hata kimoja kwa sasa kinachowakilisha maslahi ya mnyonge.
Jingine la kukumbuka ni kwamba mfalme au malkia wa Uingereza, ni nguzo mojawapo ya Bunge la Uingereza kama alivyo Rais hapa kwetu.
Hivyo, madai ya kwamba Tanzania inafuata mfumo wa Westminister yana walakini maana hayasemi ukweli wote. Hata hivyo, kuna jambo moja la Westminister ambalo Tanzania na nchi nyingi za Jumuiya ya Madola zinaling’ang’ania, nalo ni uwakilishi na utawala kupitia katika vyama.
Huu ni utaratibu ulioletwa kwetu na nchi za Magharibi nasi tukaupokea na kuukubali bila kuusaili. Lakini je, utaratibu huu unahakikisha kuwapo kwa mfumo bora wa uwakilishi wa makundi yote ya wananchi?
Mugyabuso Mulokozi ni Profesa Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment