Tuesday, 26 February 2013

Viongozi wapunguze anasa kunusuru maisha ya mama na mtoto

NI Jumatano nyingine tena, tunakutana katika safu yetu ya Jicho la Mtanzania. Jumatano ya leo safu hii itajikita katika suala la afya ya mama na mtoto kwa kuijadili hospitali yetu ya taifa Muhimbili.

Sote tunafahamu kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndiyo hospitali mama katika nchi yetu. Ni hospitali ambayo magonjwa sugu hutibiwa, ina wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali za afya pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa.

Binafsi, pamoja na kuwa mkazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu, sijawahi kupata nafasi ya kufika katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu bali kusindikiza wagonjwa au kwenda kuona. Mara ya kwanza kufika hospitalini hapo nilimsindikiza rafiki yangu wa karibu aliyekuwa akiuguliwa na mtoto wake mchanga.

Mwanaye huyo, alizaliwa katika hospitali hiyo akiwa hajatimiza umri wa kuzaliwa (pre mature), kutokana na matatizo ya uvimbe tumboni mwa mama yake. Wakati mama wa mtoto anaruhusiwa kurudi nymbani aliambiwa na daktari wake kuwa ataendelea kuhudhuria kliniki chini ya uangalizi wa daktari bingwa wa watoto hapo Muhimbili mpaka daktari wake atakaporidhishwa na maendeleo ya mtoto ndipo atapewa ruhusu ya kuhudhuria kliniki nyingine.

Siku nilifika Muhimbili nikiwa na rafiki yangu, mwanaye alikuwa ameugua ghafla na hivyo kulazimika kuwahishwa hospitalini Muhimbili.

Tukiwa kitengo cha huduma za dharura, mama na mtoto walipokelewa na kuingizwa ndani kwa ajili ya kuonwa na daktari. Tulimsubiri mapokezi kwa takribani saa nne ndiyo akatoka huku akitueleza kuwa mtoto ameandikiwa kulazwa. Ilibidi tena tusubiri kwa karibu saa moja ili gari la kuwapeleka wodini kufika.

Tulipofika wodini tulikutana na daktari wa zamu ambaye naye alichukua maelezo kabla ya mama kuonyeshwa wodi. Baadaye alimwita muuguzi na kumwambia amtafutie kitanda lakini muuguzi baada ya kuzunguka huko na kule alirejea na kueleza hakukuwa na kitanda isipokuwa anaweza kutoa msaada wa kumtafutia kitanda ambacho itabidi atumie na mgonjwa mwingine.

Kitanda kilipopatikana tulimpeleka mtoto na mama yake wodini. Kitanda ambacho alitakiwa kukitumia kilikuwa tayari kina mtoto wa umri kama miaka miwili akiwa amelala na mama yake.

Muuguzi alimwamsha mama aliyekuwa amelala na kumwambia kuwa itabidi atumie kitanda hicho pamoja na mwenziye.

Wakati huo, nilikuwa nikijaribu kuangalia uwezekano wa kitanda kile ambacho ni kidogo kutumiwa na watu wanne. Kimsingi uwezekano ulikuwa mdogo kwani hata huyo mama tuliyemkuta akitumia na mwanaye walikuwa wamelala kwa kujibana.

Mama tuliyemkuta aliamka kwa upendo na kushauri mke wa rafiki yangu amlaze mtoto na wao wakae macho mpaka asubuhi kwa sababu isingewezekana kulala wote kitandani hapo kutokana na udogo wa kitanda.

Moyoni nilisikitishwa na hali ile. Rafiki yangu aliniomba ushauri wa kumuhamisha mgonjwa wetu pale kutokana na mazingira tuliyoyaona na baada ya kujadiliana tulikwenda kumwomba daktari atupe ruhusa na kurudi siku inayofuata asubuhi, jambo ambalo alilikubali baada ya kutazama hali ya mtoto na pia kuangalia mazingira ya pale wodini.

Nilijiuliza maswali mengi, lakini kubwa lilikuwa iwapo Serikali yetu ina dhamira ya dhati ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Jibu lililonijia haraka ni kwamba pamoja na tatizo la ufinyu wa bajeti ambalo nchi yetu inakabiliana nalo, bado Serikali haijaweza kuonyesha nia ya dhati ya kutokomeza vifo hivi ambavyo vinaweza kuepukika.

Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika uliofanyika Kampala nchini Uganda mwaka 2010, viongozi wa Afrika walikubali kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya afya kwa kupanua wigo wa afya ya mama na mtoto. Raisi Jakaya Kikwete, alitamka kuwa kupunguza vifo vya akina mama na wototo ni kipaumbele namba moja kwa Tanzania.

Lakini takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa vifo vya watoto wachanga bado viko juu. Jumla ya watoto 32 hufa kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa wakiwa hai ikiwa na maana kuwa vifo vya watoto wachanga 44,000 hutokea kila mwaka sawa sawa na asilimia 47 ya vifo vyote vya watoto wachanga.

Kimsingi, maisha ya watoto hasa chini ya mwaka mmoja hutegemea sana maisha ya mama zao au kwa lugha nyingine ni kuwa kama mtoto wa chini ya mwaka mmoja atafiwa na mama yake, uwezekano wa yeye kuishi unakuwa ni mdogo na ndiyo maana afya ya mama ina uhusiano wa karibu na ya motto.

Niliwaza mambo mengi kutokana na ile hali niliyoiona pale Muhimbili. Kwanza niliwaza kuwalaza watoto wawili wagonjwa ambao umri wao unapishana sana. Mmoja ana miaka miwili mwingine kwa wakati huo alikuwa hajafikisha hata umri ambao kwa kawaida mtoto anatakiwa kuzaliwa japokuwa tayari alikuwa ameshazaliwa akiwa na karibu mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa maelekezo ya daktari wake, mtoto huyo alitakiwa kupata uangalizi wa karibu sana na kuwekwa kwenye mazingira safi na salama bila ya kushikwa au kuonwa na watu tofauti na wazazi wake ambao walishapewa masharti ya kumtunza kwani mwili wake ulikuwa bado ni dhaifu, hivyo ni rahisi kwake kupata magonjwa, lakini siku hiyo alilazwa na mgonjwa mwingine.

Kwa upande mwingine sote tunafahamu kuwa, malaria ni ugonjwa namba moja unaosababisha vifo vya maelfu ya Watanzania kila mwaka. Kina mama wale ambao walikuwa wameamua kukesha wakiwaangalia watoto kutokana na kukosa vitanda vya kulalia, walikuwa kwenye hatari ya kupata malaria kutokana na mbu jambo ambalo siyo tu ni hatari kwa afya zao bali hata kwa afya za watoto wao ambao wanawategemea.

Tukitazama kwa pamoja hii ya Hospitali ya Taifa ikiwa katika hali hiyo, nyingine hali ikoje? Waliopata nafasi ya kutembelea Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke wanaweza kuwa mashahidi wazuri wa hali mbaya za hospitali hizo.

Haina shaka kwamba, kama viongozi wetu na familia zao wangekuwa wanatibiwa katika hospiali zetu hizi, pengine wangeona umuhimu wa kuboresha hali ya utoaji huduma kwa hospitali hizi.

Mameya wa Jiji na viongozi wengine wa manispaa zetu wanatembelea magari ya gharama aina ya Toyota VX V8. Haya ni magari ya kifahari na yenye gharama kubwa. Fedha hizi zinaweza kujenga wodi kubwa kwa ajili ya akina mama wajawazito pamoja na kuwawekea vitanda na vifaa vingine muhimu.

Hakuna sababu kwa viongozi wetu kutumia magari ya gharama kubwa kama haya kama taifa limekusudia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Viongozi wetu wakiamua akina mama na watoto wasife kwa kukosa huduma na vifaa tiba inawezekana iwapo watakubali kuachana na anasa walizozikumbatia sasa.

No comments: