Tuesday, 26 February 2013

Mulugo: Michango ya CWT hulinda maslahi ya walimu

SERIKALI imesema fedha ambazo walimu huchangia katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hulinda na kutetea maslahi ya walimu wawapo kazini. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliliambia Bunge jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiembesamaki, Waride Bakari Jabu.

“Kwa mujibu wa Sheria namba sita ya mwaka 2004 ya CWT inabainisha wazi kuwa, makato ambayo walimu hukatwa ni kwa ajili ya kulinda na kueteta maslahi wawapo kazini, lakini sheria hiyo haijaelezea mafao ya walimu mara wanapostaafu ama kufariki,” alisema Mulugo.

Aidha, alitoa wito kwa wabunge kuhakikisha wanatoa mapendekezo ya kuwapo kwa mabadiliko ya sheria hiyo na hatimaye walimu hao mara wanapostaafu ama kufariki waweze kupata mafao yao.

Katika swali lake la nyongeza, alitaka kujua walimu wananufaikia vipi pindi wanapostaafu ama kufariki kutokana na wao kuchangia kiasi cha Sh bilioni 2.2 ikiwamo makato ya NSSF kwa kila mwezi.

Alihoji fedha hizo ambazo walimu wanachangia kama zimekuwa zikikaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Akijibu swali hilo, Mulugo, alisema CWT hawakaguliwi na CAG bali hukaguliwa na mamlaka ambaye humchagua wao na wala fedha hizo hazikaguliwi na CAG na baada ya ukaguzi wa mtaalamu huyo ripoti zote za fedha zilizokaguliwa hupelekwa kwa Msajili wa Vyama.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati, alitaka maelezo ya Serikali kuhusiana na kuwapo kwa malalamiko toka kwa walimu kutokana na kukatwa asilimia mbili na Hazina wanapoajiriwa.

Akijibu swali hilo, alikiri kuwapo kwa suala hilo na kudai lipo katika Sheria ya CWT ya mwaka 2004 na fedha hizo hukatwa kutokana na chama hicho kufikisha wanachama zaidi ya asilimia 50.

No comments: