Dar es Salaam. Kitendo cha Serikali kutoa kauli
tatu tofauti ndani ya wiki moja kuhusu tarehe ya Kura ya Maoni
kupitisha Katiba Inayopendekezwa, kimeelezwa na watu wa kada mbalimbali
nchini kuwa ni matokeo ya viongozi wa Serikali kukosa uongozi wa pamoja.
Wakizungumza na Mwananchi Jumamosi, wasomi,
wanaharakati, viongozi wa dini na wanasiasa wamesema kauli hizo
zinawachanganya Watanzania, kwamba mpaka sasa hakuna anayejua tarahe
rasmi ya kufanyika Kura ya Maoni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick
Werema alilieleza gazeti hili kuwa kura hiyo ingefanyika Machi 30
mwakani na kwamba upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo
zitafanyika kwa siku 30, kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi
Katiba Inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi
yanayoipinga.
Siku moja baadaye, Rais Kikwete alipokutana na
mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China
alisema endapo mipango yote itakwenda kama inavyoandaliwa, Watanzania
wataipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa Aprili mwakani.
Kauli ya Jaji Werema pia ilipingwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva na kufafanua kuwa
kura ya maoni haiwezi kufanyika Machi 30 mwakani kwa sababu kazi ya
uandikishaji wa Daftari la Wapigakura haitakuwa imekamilika.
Utata umezidi kuongezeka baada ya jana katika
mkutano wake na waandishi wa habari, Jaji Lubuva kusema kuwa Daftari la
Kudumu la Wapigakura litakamilika Aprili 18 mwakani, huku taratibu
zikieleza kwamba kura ya maoni itafanyika baada ya elimu kutolewa kwa
wananchi na hutolewa kati ya miezi mitatu hadi sita.
Awali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi
kukaririwa akisema kuwa Kura ya Maoni ifanyike kabla ya Uchaguzi Mkuu
2015, huku Rais Kikwete akikubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kuwa
kura ya maoni itafanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Faraja Christoms alisema, “Hayo ni matokeo ya kukosekana kwa
uwajibikaji wa pamoja. Sina hakika kama AG ndiye alipaswa kutaja tarehe
ya kura ya maoni, yeye ni mshauri tu.”
Alisema kitendo cha kauli ya AG kutofautiana na
iliyotolewa na rais ambaye amemteua ni ishara mbaya katika utendaji kazi
wa Serikali.
“Wakati mwingine kauli kama hizi zinaweza
kuwavunja moyo walioteuliwa. Nakumbuka Waziri Mkuu Pinda aliwahi kutoa
kauli ya kupinga maelezo ya Waziri wa Ujenzi, Magufuli (John). Tafsiri
ya kilichotokea ni kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Dk Leonard Mtaita alisema kazi iliyobaki ni kuwahamasisha
wananchi wakati wa kupiga kura ya maoni utakapofika kwa maelezo kuwa
kila mtu atapiga kura kutokana na anachokiamini.
Dk Mtaita alisisitiza pia kuboreshwa kwa Daftari
la Wapigakura, akisema kuwa hilo ndilo litakuwa jambo la msingi ili
kuwafanya Watanzania wote wenye sifa waweze kupiga kura, huku akiiomba
Serikali kuhakikisha inasambaza nakala za kutosha za Katiba
Inayopendekezwa.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles
Kitima alisema, Serikali kupuuza mawazo na malalamiko ya watu ni ishara
mbaya, kufafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa ina uhalali wa kisheria
lakini inakosa uhalali wa kisiasa na ili kuokoa mvutano, maridhiano ni
jambo la msingi.
“Wananchi wanaulalamikia mchakato wa Katiba,
pamoja na mvutano unaoendelea, haya malalamiko ya wananchi si ya
kufurahia hata kidogo. Jambo hili linatakiwa kupatiwa ufumbuzi,”
alisema.
Aliongeza, “Rais ndiye anayetakiwa kutueleza
msimamo wake ni nini juu ya suala hili. Je, na yeye atafuata masilahi ya
CCM au atazungumza kama Rais. Kama maridhiano yatakosekana na Katiba
hiyo ikapitishwa, haitadumu muda mrefu kwa sababu watawala wengine
watakaokabidhiwa kijiti wataibadili Katiba hiyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la
kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii, Fordia, Bubelwa Kaiza
alisema tofauti za kauli za viongozi zinaonyesha kuwa mchakato wa kupata
Katiba Mpya uliendeshwa katika taratibu zisizo sahihi, ndio maana
hakuna kauli moja kuhusu siku ya kupiga kura ya maoni.
“Hayo ni majibu kwamba ndani ya serikali kuna
mkanganyiko mkubwa kuhusu suala zima la Katiba Mpya. Hakuna msemaji
sahihi, kila mtu anazungumza lake. Ndio maana hata katika Bunge Maalumu
kila mtu alifanya lake, sheria zilibadilishwa bila kufuatwa kwa
utaratibu,” alisema.
Alifafanua kuwa ni ngumu kwa kila jambo linalohusu
Katiba kwenda vizuri kwa sasa kwa sababu mchakato uliharibika baada ya
kuanza vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba
Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema elimu ya uraia inatakiwa
kutolewa miezi mitatu hadi sita kabla ya kufanyika Kura ya Maoni, si
siku 30 alizozitaja Jaji Werema.
“Huwezi kutoa elimu ya uraia kwa siku 30, mfano
Zimbabwe walitumia miezi sita kutoa elimu ya uraia. Mchakato huu
umeingiliwa na wajanja, si riziki tena, ni kama mtu aliyejifungua mtoto
aliyekufa,” alisema.
Kibamba alisema Nec ilieleza kuwa kufikia Mei
ndiyo itakuwa imemaliza kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura, kwamba
kitendo cha Jaji Werema kueleza kuwa Kura ya Maoni itafanyika Machi
mwakani, ni ishara ya ‘ukambale’.
“Waziri Mkuu (Pinda) alisema Katiba ipatikane
kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, Rais Kikwete akakubaliana na TCD kuwa ni
2016, jana (juzi) Jaji Werema anatueleza kuwa ni Machi mwakani,
tumsikilize nani?”
Alisema tarehe ya kura ya maoni kwa mujibu wa
sheria inatakiwa kutangazwa na Rais si Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kibamba alisisitiza kuwa Serikali bora ni ile inayojiendesha kwa
uwajibikaji wa pamoja.
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
(TLS), Felix Kibodya alisema, “Tamko la Serikali kwa jambo kama hilo
huwa ni moja na si kila kiongozi kutoa tamko lake. Ndiyo maana tarehe
ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, si
mtu mwingine.”
Alisema huenda mkanganyiko ulioibuka juu ya tarehe rasmi ya kura
ya maoni unatokana na nchi kutowahi kuendesha zoezi la upigaji wa kura
hiyo.
“Sheria inaeleza wazi kuwa rais atatangaza tarehe
rasmi siku 84 baada ya kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa. Ili muda
usogezwe mbele ni lazima sheria ibadilishwe, nadhani hilo linaweza
kufanyika katika kikao kijacho cha Bunge,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa
Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi alisema mchakato
wa Katiba ni suala la kisheria na kisiasa, hivyo kama Rais alikutana na
wanasiasa na kukubaliana, ingekuwa jambo jema kama makubaliano hayo
yangezingatiwa.
“Kama ni suala la sheria, sheria husika
inabadilishwa lakini kama ni suala la makubaliano ya wanasiasa, pia
lilitakiwa kuzingatiwa. Kwa sasa kuna mvutano mkali, sijui nini
kitatokea,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk Willbrod Slaa alisema jambo hilo linatokana na viongozi wa
Serikali kugawanyika huku akitolea mfano kauli ya Rais Kikwete kuwa
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ungefanyika Februari mwakani, lakini
baadaye Waziri Pinda akatangaza kuwa utafanyika Desemba 14 mwaka huu.
“Nchi inayokuwa na viongozi ambao kila mmoja
anatoa kauli yake haiwezi kuwa na mshikamano. Wao hawana umoja halafu
wanataka Watanzania kuwa na umoja, hilo litawezekana kweli?” alihoji Dk
Slaa.
Aliongeza, “Hata kura ya maoni ikifanyika leo
haina maana tena kwa sababu Katiba Inayopendekezwa imeondolewa mambo ya
msingi yaliyotokana na maoni ya wananchi. Wanasema Katiba hii ni bora
barani Afrika, sijui nani kawadanganya. Dk Slaa alisisitiza kuwa ili hali iwe shwari ni
lazima kura ya maoni ifanyike wakati ambao Nec itakuwa imeliboresha
Daftari la Wapigakura. “Watambue kuwa safari ya kudai Katiba Mpya ndiyo
inaanza sasa kwa sababu Katiba Inayopendekezwa ni mali ya CCM, si
Watanzania.”
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa
Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema, “Kama tunaamini kuwa
Katiba Inayopendekezwa siyo nzuri, umefikia wakati wa kuwaachia wananchi
wapige kura. Kama ni nzuri wataipitisha na kama hawaikubali
wataikataa.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa
Gaudence Mpangala alisema, “Tangu mwanzo niliupinga mchakato wa Katiba
na matokeo yake imezaliwa Katiba Inayopendekezwa isiyokuwa na maoni
muhimu ya Watanzania. Sikubaliani na mchakato wa kura ya maoni.”
Profesa Mpangala alisema mchakato wa kupata Katiba
Mpya unatakiwa kurudiwa mwaka 2016 kwa maelezo kuwa Katiba
itakayopatikana haitakuwa na ridhaa kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma),
Hashim Rungwe alisema, “Hayo ni matokeo ya nchi kuwa na sheria mbovu.
Katiba yetu pamoja na sheria za nchi hii hazieleweki. Rais amepewa
madaraka makubwa kiasi kwamba wengine wakitoa kauli hata kama wanaweza
kufanya hivyo, kauli zao zinaonekana si kitu mbele ya kauli ya Rais.”







