Dar es Salaam. Siku moja baada ya Bunge Maalumu
la Katiba kupitisha Katiba inayopendekezwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Katiba hiyo
bado ina maswali mengi kuliko majibu, hasa katika muungano na mgombea
binafsi.
Amesema licha ya Zanzibar kuridhia mambo kadhaa
kuwekwa katika orodha ya mambo ya muungano, hali inaweza kuwa tofauti
ukifikia wakati wa Zanzibar kubadili Katiba yao ili kuwezesha
utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Juzi Bunge hilo lilipitisha Katiba inayopendekezwa
kwa tofauti ya kura mbili na kuhitimisha kwa sasa mchakato wa kuandika
Katiba hadi mwaka 2016 ambapo litafanyika zoezi la upigaji wa kura ya
maoni.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana, Jaji
Warioba alisema, “Wasiwasi wangu ni juu ya muungano kwa sababu katika
masharti ya mpito ni lazima Zanzibar ifanye marekebisho ya Katiba yake.
Rasimu inayopendekezwa inasema Tanzania itakuwa nchi moja pamoja na
madaraka ya rais kugawa nchi. Kwa maana hiyo lazima Katiba ya Zanzibar
ibadilike.”
Alisema katika mambo ya muungano, Katiba
inayopendekezwa imeliweka suala la kodi ambalo halikuwamo katika rasimu
iliyotolewa na Tume ya Katiba, kusisitiza kuwa kitendo hicho hakitajibu
swali la ‘Tanganyika kuvaa koti la Muungano’.
“Wameongeza kodi ya mapato, ushuru wa forodha na
bidhaa katika mambo ya muungano. Maana yake ni kwamba kodi yote
inayokusanywa, ikiwamo ya kutoka Zanzibar itaingizwa kwenye mfuko wa
muungano,”alisema.
Aliongeza, “Wakati huo huo Zanzibar imepewa uwezo
wa kusimamia mambo yake yenyewe na ili iweze kulitekeleza hilo ni lazima
iwe na vyanzo vyake vya mapato. Sasa watasimamiaje wakati mapato yote
yanaingia kwenye mfuko wa muungano.”
Alisema ili suala hilo liweze kutekelezwa ni
lazima Zanzibar ibadili Katiba yake na kusisitiza kuwa utakapofika
wakati wa kubadili Katiba ya Zanzibar, jambo hilo linaweza kukwama.
“Sioni kama Wazanzibar watakubali suala hili. Kama
mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yatakwama, ni wazi kuwa Katiba
inayopendekezwa haitatekelezeka. Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar
yanategemea maridhiano ya Wazanzibari wenyewe na kumbuka kuwa CUF na CCM
wanavutana sana,” alisema Jaji Warioba.
Akifafanua hilo, alisema mabadiliko ya Katiba ya
Zanzibar lazima yapate theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi na kusisitiza kuwa kwa mvutano wa vyama hivyo viwili
visiwani Zanzibar, itakuwa kazi ngumu kupitisha jambo hilo.
“Katiba ya Zanzibar isipobadilishwa kero za
muungano zinazozungumzwa zitaendelea. Kazi iliyopo sasa ni kufikiria
maridhiano kuhusu muungano, lazima tuhakikishe Zanzibar imekubali
kubadili katiba yake na kuridhia mapato yake kuingizwa katika mfuko wa
muungano,” alisema.
Aliongeza, “Kama ambavyo Tanzania Bara
waliitegemea Zanzibar kupitisha Katiba inayopendekezwa, ni lazima pia
ihakikishe kuwa Zanzibar inakubali kubadili Katiba yake.”
Kuhusu mgombea huru Jaji Warioba alisema, “Katiba
inayopendekezwa imeweka masharti ya mgombea ubunge na kutaja sifa za
ziada za mgombea huru ambazo ukizitazama kwa undani utabaini kuwa
wanamkataa mgombea huru kistaarabu.”
Alisema sifa hizo za ziada walitakiwa kuwekewa na wagombea wengine, si mgombea huru pekee.
“Mfano ni kutoruhusu mtu kutoka katika chama cha siasa kisha kugombea kama mgombea huru,” alisema.
Jaji Warioba aliyataja baadhi ya mambo ya msingi
yalikuwamo katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingizwa
tena katika Katiba inayopendekezwa kuwa ni malengo muhimu ya kisiasa,
kiuchumi, kiutamaduni na kimazingira.
No comments:
Post a Comment