Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) umeibua shutuma dhidi ya uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba
kwamba unawarubuni kwa fedha baadhi ya wajumbe wa umoja huo ili kuipigia
kura Katiba inayopendekezwa.
Kamati ya Ufundi ya Ukawa, ilisema jana kuwa
wajumbe wanaorubuniwa wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa ahadi ya kupewa zaidi
ya Sh500 milioni ni wa CUF na wengine wanne wa Chadema wanaotoka
Zanzibar.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya
Khamis Hamad alikanusha madai hayo, akisema hajasikia kitu kama hicho na
ndiyo kwanza alikuwa anasikia hilo kutoka kwa mwandishi wa habari
hizi... “Hakuna kitu kama hicho, hilo jambo ndiyo nalisikia kutoka
kwako.”
Kutokana na madai hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Ukawa, John Mnyika alisema kamati hiyo ilianza kikao cha siku mbili
kuanzia jana kujadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa uongozi wa juu
wa umoja huo.
Licha ya Mnyika kukataa kutaja majina ya wajumbe
waliorubuniwa, wajumbe wa Chadema wanaotokea Zanzibar ni Zeudi Abdallah
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha),
Maryam Msabaha, Mwanamrisho Abama na Raya Ibrahim. “Tumewataka wajumbe
wetu wote kukusanya ushahidi na kuuwasilisha kwa viongozi wa Ukawa,”
alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema Bara.
Aliongeza, “Chadema ina wajumbe wanne, watatu ni
wabunge wa kawaida na mmoja wa kuteuliwa na Rais (Kundi la 201).
Tumepata taarifa kutoka kwa wajumbe hao kwamba wanapigiwa simu na
uongozi wa Bunge ukiwataka wasaini karatasi za kupigia kura ili uongozi
wa Bunge uchakachue kura.
“Tumeanza kikao kujadili suala hili ila tumeamua
kwanza tuueleze umma kupitia vyombo vya habari juu ya ‘uharamia’
unaofanywa na Bunge la Katiba linaloongozwa na Sitta (Samuel) na Makamu
wake Samia (Suluhu Hassan).”
Ukiukaji kanuni
Akinukuu Kifungu cha 36 (3) cha Kanuni za Bunge la
Katiba, Mnyika alisema si sahihi Sitta kutaka wajumbe waliopiga kura ya
‘hapana’ kuitwa katika Kamati ya Mashauriano na uamuzi huo ni kinyume
na kanuni...
“Ni kama kuwatisha tu wajumbe.”
Kanuni hiyo inasema; “Endapo baada ya ibara ya
Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa upya kupigiwa kura, theluthi mbili ya
wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote
kutoka Tanzania Zanzibar haikufikiwa, basi ibara hiyo itapelekwa kwenye
Kamati ya Mashauriano ili kupata mwafaka.”
Sitta awataje
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha
wa CUF, Joran Bashange alimtaka Sitta kutaja majina ya wajumbe wa CUF
na Chadema waliopiga kura... “Tunamtaka awataje kwa majina maana ujanja
wake na wenzake tumeshaujua na tuna ushahidi wote.”
Bashange alisema mpaka sasa hakuna mjumbe wa Bunge
hilo ambaye ni mjumbe wa Ukawa aliyepiga kura kupitisha Katiba
inayopendekezwa.
“Ndiyo maana walibadili kanuni ili kuruhusu
wajumbe kupiga kura kwa faksi na baruapepe ili kufanya ‘uharamia’ wa
kuiba kura,” alisema.

No comments:
Post a Comment