Dar es Salaam. Shughuli za kiserikali katika Wizara ya Mambo ya
Ndani na ofisi jirani, jana zilisimama kwa siku nzima kutokana na
hekaheka zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema pale
mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipojisalimisha polisi.
Hekaheka hizo ziliibuka kuanzia saa 5.10 asubuhi
baada ya Mbowe akiongozana na wanasheria wa chama hicho, kufika katika
ofisi za Makao Makuu ya Polisi ambako pia zipo ofisi za wizara hiyo
kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza
kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya Mbowe kuwasili, alifika Mkurugenzi wa
Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, Benson
Kigaira na alipojitambulisha akakataliwa kuingia.
Baadaye waliwasili mawakili, Profesa Abdallah
Safari na Mabere Marando ambao waliruhusiwa kuingia, kisha wakafuata
Mbowe, John Mnyika na wanasheria wengine akiwamo John Malya na Peter
Kibatala.
Wakati huo, Barabara ya Garden inayokatiza mbele
ya wizara hiyo ilikuwa imefungwa na wafuasi wa Chadema walikuwa
wamezuiliwa kwa mbali. Kila mwananchi aliyefika katika jengo hilo
kupatiwa huduma, alijibiwa na askari waliokuwa na mbwa na silaha kuwa,
“hakuna shughuli yoyote inayofanyika hadi kesho (leo)”.
Hali hiyo iliendelea hadi saa 9:10 alasiri baada
ya Mbowe aliyehojiwa kwa saa mbili kuhusu tuhuma za uchochezi kuachiwa
kwa dhamana.
Baada ya kuachiwa, Mbowe alisindikizwa kwa msafara
wa magari manne ya polisi akielekea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,
ambako alipanda ndege kwenda Afrika Kusini kwa shughuli za kichama.
Ilivyokuwa
Ombi lililotolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema (Bara), John Mnyika kuwataka wanachama wa Chadema kujitokeza
kumsindikiza Mbowe polisi, liliitikiwa kwani zaidi ya wanachama 100
walijitokeza katika ofisi hizo.
Walianza kukusanyika mmoja baada ya mwingine nje
ya makao mkuu ya jeshi hilo kuanzia saa 4:30 asubuhi na kujichanganya
katika kundi la waandishi wa habari, hali iliyosababisha askari polisi
waliokuwa na bunduki na mabomu ya machozi kuwataka wanahabari
wajitambulishe kwa kuonyesha vitambulisho ili wawatenge na wafuasi hao.
Licha ya juhudi hizo, hawakufanikiwa kuwatawanya
wanachama hao ambao awali, walijieleza kuwa walikuwa wamefuata hati zao
za kusafiria katika Ofisi za Uhamiaji zilizopo eneo hilo.
Hali ilibadilika baada ya Mbowe kufika katika
ofisi hizo akiwa katika msafara wa magari matano huku ukiongozwa na
Mnyika na wanachama hao kuanza kuimba nyimbo za chama hicho na kumsifu
kiongozi wao.
Msafara huo ulizuiwa kwenye lango la ofisi hizo na askari wa FFU
waliwazuia viongozi wengine, wakisema anayetakiwa kuingia ndani ni
Mbowe na wanasheria wake pekee.
Baada ya gari la Mbowe kuingia, viongozi na baadhi
ya wafuasi wa chama hicho nao walipenya kwa nguvu getini na kuingia
ndani ya uzio huku wakisema ‘people’s power’ (nguvu ya umma). Kitendo
hicho kiliwatibua FFU na kuanza kutumia nguvu kuwatoa nje, hali iliyozua
vurugu kubwa.
Kutokana na mvutano huo, askari zaidi wa FFU
waliokuwa katika Land Rover mbili wakiwa na mbwa waliongezeka na kuanza
kuwashushia kipigo wafuasi hao huku wakiwataka kusimama umbali wa mita
100 kutoka lilipo jengo hilo.
Baada ya kutolewa ndani ya uzio baadhi ya wafuasi
wa Chadema walikaa chini wakisema hawatafanya vurugu na wako tayari
kuingia ndani wakiwa wamenyoosha mikono juu.
Katika kundi la wafuasi hao walikuwamo pia baadhi
ya wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini), Mchungaji
Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana).
Wabunge waliofika baadaye na kuruhusiwa kuingia ndani ni Suzan Lyimo (Viti Maalumu) na Halima Mdee (Kawe).
Miongoni mwa walioathirika na hekaheka hizo ni
wanahabari ambao pamoja na kuonyesha vitambulisho na kamera, baadhi yao
walishushiwa kipigo na askari hao.
Katika kipigo hicho, mwandishi wa Habari wa Gazeti
la Tanzania Daima, Josephat Isango na Mwandishi gazeti la Hoja, Shamimu
Ausi walijeruhiwa. Isango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na
jicho la kulia.
Wakati Isango alisema alivamiwa na askari wawili
wa FFU na kwamba hata alipojitambulisha na kuwaonyesha kitambulisho
waliendelea kumpiga, Ausi alisema alipigwa rungu usoni na akashangazwa
na nguvu kubwa iliyotumika wakati awali, aliruhusiwa kusimama katika
eneo alipokuwa akiendelea na kazi.
Baada ya vurugu hizo waandishi wa habari na
wafuasi wa chama hicho walitakiwa kusimama katika makutano ya Barabara
ya Ghana na Ohio umbali wa mita 100 kutoka yalipo makao makuu ya jeshi
hilo kusubiri mahojiano yaishe.
Ilipofika saa 8.45, Mwanasheria wa Chadema, Tundu
Lissu alitoka nje ya ofisi hizo na kuzungumza na waandishi wa habari na
wafuasi wa chama hicho.
Alisema mahojiano kati ya Mbowe na Jeshi la Polisi
yalikwenda vizuri huku akiongozwa na wanasheria na kwamba polisi
wamekubali kumpa dhamana lakini kabla hajaondoka, wafuasi wote
wanatakiwa kuondoka eneo hilo bila maandamano.
“Polisi wanaomba mtawanyike, hawataki maandamano, wao
watamsindikiza hadi makao makuu ya chama yaliyopo Kinondoni, mkifanya
maandamano watatumia nguvu kuyazuia na hilo hawataki litokee. Nawaomba
mtawanyike,” alisema Lissu.
Baada ya tangazo hilo, wafuasi hao kwa shingo upande, walikubali ushauri huo na kuondoka katika eneo hilo saa 9.00 alasiri.
Ilipofika saa 9.20 Mbowe alitoka katika ofisi hizo
akisindikizwa na magari ya polisi aina ya Land Rover zilizojaa askari
na baadaye ilielezwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
aliyekuwa makao makuu ya chama hicho kuwa mwenyekiti huyo alikwenda moja
kwa moja Uwanja wa Ndege kwa safari ya kikazi Afrika Kusini.
Mtikila azua gumzo
Wakati hekaheka zikiendelea, Mwenyekiti wa DP,
Mchungaji Christopher Mtikila alifika katika ofisi hizo saa 7.26 akiwa
katika Bajaj lakini alizuiwa kuingia ndani na akaondoka.
Akizungumza na wanahabari, Mtikila alisema, “Ni lazima Watanganyika tuidai Tanganyika yetu kwa gharama yoyote, aluta continua.”
Makao Makuu
Baada ya kuondoka eneo hilo, wafuasi wa Chadema
walikwenda katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa,
Kinondoni na kupewa maelekezo na Dk Slaa na Lissu.
Lissu alisema Mbowe anatuhumiwa kwa uchochezi kwa
kauli yake kuhusu kufanyika maandamano nchi nzima, huku akisisitiza kuwa
tuhuma alizopewa “ni za wizi wa kuku”.
“Mbowe aliposema kufanyika maandamano alikuwa na
maana kuwa maandamano hayo yatafanyika baada ya Chadema kutoa taarifa,
kauli yake haikuwa ya uchochezi hata kidogo,” alisema Lissu.
Aliongeza, “Kama polisi wakitueleza ni sheria ipi
inakataza maandamano, sheria ipi inalazimisha wanaotaka kuandamana
lazima wawe na kibali na sheria ipi inakataza watu kugoma, watakuwa na
ruksa ya kumfunga Mbowe.”
Kwa upande wake, Dk Slaa alisema, “Mbowe baada ya
kutoka polisi ameomba nimwagie kwa wanachama wa Chadema. Amekwenda
Afrika Kusini katika mkutano wa chama. Safari yake ilikuwa imepangwa
tangu juzi na ingeahirishwa kama angenyimwa dhamana leo.”Dk Slaa alimwagiza Kigaira kuhakikisha kuwa wanachama wawili wa chama
hicho waliokamatwa na polisi wanaachiwa kwa dhamana. Zoezi la kufanya
maandamano likifanyika kama hivi Taifa hili litabadilika,” alisema.

No comments:
Post a Comment