Sheikh Mohammed anasema serikali ndio inawanyanyasa wananchi
wake kwa kupitisha sheria ambazo zinawazuia kunufaika na rasilimali za
taifa lao ambazo Mungu amewapa.
“Wachimbaji wadogo wamepewa migodi yenye ukubwa wa
mita 50 kwa 50 lakini mchimbaji mmoja mkubwa amepewa eneo kubwa zaidi
ya eka tano halafu inapitishwa sheria ya kuchimba kwenda chini jambo
ambalo haliwezekani huku ni kuwazuia wachimbaji wadogo kupata madini”
alisema.
Alisema kwa sasa shughuli nyingi za msikiti huo
zimesimama kwani wananchi wa Mirerani hawana fedha za kutoa sadaka
tofauti na miaka ya nyuma ambapo sadaka ziliwezesha ujenzi wa msikiti
huo, shule na kuwa na miradi.
Padri Aloyce Kitomali wa Kanisa la Katoliki
Mirerani, alisema kanisa hilo lilikuwa na uwezo wa kukusanya sadaka
katika ibada moja zaidi ya milioni moja lakini sasa hata Sh500, 000
hazipatikani kwani waumini hawana fedha.
Anasema miradi mingi ya kanisa hilo, sasa
imezorota kwani wananchi wengi wanategemea madini ya tanzanite ambayo
sasa hayapatikani na inasemekana anayepata ni mwekezaji.
“Wananchi hapa wengi wana hali ngumu ya maisha
tofauti ya miaka ya nyuma kwani uchumi wao ulitegemea sana madini ya
Tanzanite” alisema.
Osca Gunewe ambaye ni Katibu wa Bodi ya shule ya
Kanisa la Pentekoste, anasema uchumi wa mji wa Mirerani unategemea
madini ya Tanzanite hivyo kwa hali iliyopo sasa ni muhimu Serikali
kuwasaidia wakazi wa mji huo.
Gunewe ambaye aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji wa Kata
ya Mirerani, anasema ingewezekana kuwasaidia watu wa Mirerani hata kwa
kutolewa ajira kwa vijana wa Mirerani katika migodi ya mwekezaji.
Anasema lakini kampuni hiyo, haiajiri vijana wa
Mirerani na hivyo sasa wapo mitaani tu kwani hata migodi ya wachimbaji
wadogo mingi imesimama na ambayo inaendelea na kazi, inachukua vijana
wachache sana.
Omar Awadhi alikuwa Mwenyekiti wa Serikali ya
Kijiji cha Mirerani miaka 10 iliyopita, anasema, maisha ya Mirerani sasa
yamebadilika na hata uchangiaji shughuli za maendeleo umepungua sana.
Anasema Mirerani licha ya utajiri wote, haina hata huduma ya maji safi,
kwani ndoo moja inauzwa kati ya Sh400 na 500.
Awadhi anasema maji hayo yanatolewa Wilaya ya Hai
Mkoa wa Kilimanjaro kitu ambacho siyo sahihi kulingana na utajiri wa
tanzanite ambayo inapatikana Mirerani pekee duniani.
“Tatizo hapa ni mwekezaji kama madini haya
yangechimbwa na wachimbaji wadogo pekee hali isingekuwa hivi, kwani watu
wengi wangepata madini japo kidogo kidogo lakini yangeendelea kuujenga
Mji wa Mirerani na hata mikoa ya jirani,” anasema.
Robo tatu ya migodi ya wachimbaji wadogo imesimama
Mayala Raurenti ni Ofisa Madini, Mirerani. Anakiri
uchimbaji wa madini hayo kuzorota kwa wachimbaji wadogo, lakini anasema
chanzo ni mahitaji makubwa ya teknolojia.
Raurenti anasema madini katika maeneo ya kitalii B
na D vinavyomilikiwa na wachimbaji wadogo tofauti na miaka ya nyuma
sasa yapo mbali na hivyo kuhitaji teknolojia za kisasa.
Hivi sasa wachimbaji wadogo, wamepungua kutokana
na upatikanaji madini kuwa mgumu na kuanza kutumia mashine badala ya
watu katika kupandisha michanga juu ya mgodi na hata kuchimba.
Mihayo Franeis ni Ofisa wa Miamba (jiolojist)
katika machimbo ya Tanzanite Mirerani. Anasema kati ya migodi zaidi ya
400 ya wachimbaji wadogo ni migodi 120 tu ndiyo inachimbwa kila siku.
Anasema hali hiyo, ,imesababisha kupungua sana kwa
wachimbaji wadogo kwani pia migodi hiyo, ambayo awali ilikuwa
inawafanyakazi zaidi ya 4,000 sasa hawafiki 500.
“Mgodi ambao ulikuwa na wachimbaji wadogo 100 sasa
wapo 15 hii inatokana na matumizi ya teknolojia za kisasa katika
uchimbaji,” anasema.
Anasema hata mamia ya vijana ambao walikuwa
wamejiajiri kuchambua michanga na kupata dhahabu sasa hawapo na ndio
sababu watu wamepungua sana Mirerani. Anasema kitalu B kina migodi 183
na kitalu D kina migodi 368 lakini ambayo inachimbwa kila siku si zaidi
ya migodi 120 hivyo ndio sababu mji kama wa Mirerani uliokuwa unategemea
madini hayo umebadilika.
Hata hivyo, anakiri licha ya migodi kuwa michache
inayochimbwa bado upatikanaji madini siyo kama zamani kwa kuwa miamba
ipo mbali zaidi kwa migodi mingi.
“Ni kweli migodi mingi ya wachimbaji wadogo
haipati madini, tatizo ni kuwa maeneo mengi yamechimbwa tayari na sasa
madini yapo chini zaidi hivyo gharama za uchimbaji ni kubwa,” anasema.
Akizungumzia malalamiko ya wachimbaji kuwa madini
mengi yapo eneo la mwekezaji alisema siyo sahihi kwani madini yote yapo
kwenye miamba katika eneo la Mirerani lakini kwa maeneo ya wachimbaji
wadogo yapo chini zaidi.
Serikali sasa yalia kukosa kodi Mirerani.
Martha Umbulla ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro. Anakiri
hali ngumu ya maisha Mirerani lakini anasema hata kodi kutoka katika
madini hayo, wilaya hiyo hainufaiki kwa sasa.
“Wakazi wa Mirerani wanategemea madini, sasa
hayapatikani hivyo uchangiaji maendeleo siyo mzuri lakini Serikali
tungeweza kupata hata kodi kutoka kwa wachimbaji hasa mwekezaji lakini
hatupati,” anasema.
Anafafanua kuwa kodi ya mapato ya madini hayo,
wachimbaji wanalipa Arusha kutokana na mji wa Mirerani kutokuwa na ofisi
za Mamlaka ya kodi (TRA).
Alisema Serikali inafanyia kazi matatizo ya
Mirerani ili kuona wananchi wataishi vipi na kutokwama shughuli mbali
mbali za kiuchumi. Huu ndiyo mji wa Mirerani ambao sasa upo hoi na
wananchi wanalia kila kona baada ya kushindwa kunufaika na madini ya
Tanzanite.

No comments:
Post a Comment