Dar es Salaam. Baada ya Bunge la Katiba juzi
kufanikiwa kupata theluthi mbili ya wajumbe wa pande zote mbili za
Muungano na kupitisha Katiba inayopendekezwa, sasa msuguano kuhusu
Katiba unaonekana kuhamia uraiani.
Msuguano kuhusu Katiba hiyo unatarajiwa kuendelea
mitaani, ndani ya vyama vya siasa na kwenye majukwaa kutokana na tofauti
ya mitizamo iliyoibuka kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopitishwa.
Ingawa matokeo ya kura za ushindi yalipokewa kwa
furaha na wajumbe waliokuwapo bungeni kwa kucheza na kurusha vijembe kwa
wapinzani, huenda kibarua kitakuwa kigumu kwa CCM itakapolazimika
kupambana na wananchi, wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini
‘waliojeruhiwa’ na mwenendo wa Bunge.
Bunge hilo liliendeshwa kwa upinzani mkali kutoka
kwa makundi mbalimbali ya watu waliokuwa wakitaka lisimamishwe kwa madai
kuwa limechakachua maoni yao kama yalivyopendekezwa kwenye Rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
CCM na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar
CCM iliingia doa baada ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kuzua
kizaazaa bungeni Jumatano wiki iliyopita kwa kupiga kura ya hapana
katika ibara 22 kwenye Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
Mwanasheria huyo ambaye awali alijiondoa kwenye
Kamati ya Uandishi kwa kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa yanakwenda,
alizomewa na baadhi ya wajumbe na kulazimika kutolewa ukumbini akiwa
chini ya ulinzi wa askari wa Bunge.
Akizungumza na gazeti hili, Othman alisema kuwa
alichofanya kilikuwa ni utashi wake kwa kuwa Serikali ilitamka kwenye
Baraza la Wawakilishi na hata nje ya Baraza kuwa haikuwa na msimamo.
“Kwa hiyo kama Serikali haikuwa na msimamo kwa
maana ya upande, maana yake ni ipi pengine unisadie… nilipiga kura kwa
kuzingatia utashi wangu na maoni yangu,” alinukuliwa Othman.
Ingawa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta
alimtetea Othmani kwa kusema wajumbe hawakupiga kura kwa kutumia vyeo
vyao, kwa namna wajumbe walivyoonyesha jazba imeonyesha kuwa CCM
itapaswa kusafishwa taswira iliyochafuka.
Sitta na viongozi wa dini
Kwa upande mwingine, Sitta amejikuta akiingia
kwenye ‘vita’ na viongozi wa dini, baada ya kuwataka waumini wa
madhehebu mbalimbali kuupuza nyaraka zilizotolewa na viongozi hao kwa
kuwa hazina utukufu wowote wa Mwenyezi Mungu.
Sitta alisema baadhi ya viongozi wa dini wanalenga kuliingiza
taifa kwenye machafuko na kwamba yeye hatakuwa tayari kuvumilia hali
hiyo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT),
Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA).
Huku akiwa na waraka huo mkononi, Sitta alisema
kuwa lugha iliyotumika haina staha na haikupaswa kutumiwa na watu
wanaohubiri dini duniani.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Askofu Msaidizi wa
Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema kauli ya Sitta
inaonyesha kuwa amechoshwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.
“Sikutarajia kiongozi kama huyo kutoa kauli mbaya
kama hiyo kwa Taifa zima. Sikutegemea mheshimiwa kama huyo kusema
maneno kama hayo… Huenda ana stress (msongo wa mawazo). Hata ikiwa
hivyo, hakupaswa kutoa kauli nzito kama hiyo. Anatakiwa kufahamu kuwa
waraka huo umetoka kwa Wakristo wote hapa nchini,” alisema Askofu
Kilaini.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika
jana alisema kitendo cha Sitta na wenzake kushindwa hata kuelewa waraka
wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa
kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa.
Hata hivyo, jana Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki (TEC) Father Raymond Saba, amesema bado wanaendelea kutafakari
kauli ya Sitta na kwamba kwa sasa hawajatoa taarifa yoyote.
Akizungumzia kauli ya Sitta, Mhadhiri wa Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kauli ya kiongozi
huyo imeongeza mpasuko wa dini nchini hasa kuhusu mahakama ya kadhi.
“Viongozi wa dini wameipokea kauli ya Serikali kwa
kuwa tu alisema ni kiongozi wa Serikali, lakini itatokea shida kama
ahadi yao haitatekelezwa,” alisema Salim.
Sitta na Jaji Warioba
Sitta amejikuta kwenye vita ya maneno na Jaji Warioba huku kila mmoja akisisitiza kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu
kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) hivi
karibuni, Jaji Warioba alisema ataingia mitaani kuitetea Rasimu ya
Katiba iliyokuwa imebeba maoni ya wananchi.
Alisema kuwa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu.
Hata hivyo, akizungumza jana na gazeti hili
alisema kuwa Katiba hiyo imeacha maswali mengi kuliko majibu hasa kwa
upande wa Zanzibar.
Sitta alalamikia kutukanwa
Sitta atakuwa na kibarua kingine cha kujisafisha
mbele ya wananchi ambao alikaririwa akisema kuwa wamekuwa wakimtumia
meseji za matusi za ya 50 kila siku.
Kwa nyakati tofauti wananchi wasiojulikana
wamekuwa wakiandika meseji za matusi kwenye mitandano na simu kwa kile
wanachosema kuwa Sitta amelazimisha maoni ya CCM yatawale Bunge.
Wananchi wasubiri waelezo zaidi
Baadhi ya wananchi waliohojiwa kuhusu mwenendo wa
Bunge hilo, waliwalaumu wajumbe wa Bunge waliokuwa wakisema walipiga
kuwa kwa niaba ya wananchi kwenye majimbo yao.
Walihoji ni lini wajumbe hao ambao ni wabunge wao
walikwenda kuwauliza iwapo wanataka kupiga kura ya hapana au ndiyo dhidi
ya Katiba iliyopendekezwa?
‘Mimi nimesikia tu mbunge wetu (anamtaja) amesema
wananchi wake wamechagua kura ya ndiyo. Ni nani alimtuma kwenda kuwa
tunataka Katiba hiyo wakati maoni yetu tulitoa tofauti, “ Yohana Change
mkazi wa Vwawa, Mbozi.
Mwanaidi Suleiman alisema haelewi nini
kilichotokea bungeni, kwa kuwa matarajio aliyokuwa nayo kuhusu Katiba
yameyeyuka baada ya kusikia mambo mengi yamekataliwa.
“Nafuu kama wangeondoa mambo mengine, lakini siyo
serikali tatu na uraia wa nchi mbili. Mimi hayo niliyaona makubwa sana,
kama hayapo sasa Katiba itahusu nini?” alihoji Mwanaidi.
Chadema na wanachama wake.
Hali ya hewa ndani ya Chadema ilichafuka baada
ya Sitta kusema kuwa kuna wajumbe wawili wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutoka Zanzibar walikubali kupiga kura kinyume na msimamo wa
vyama vyao.
Sitta alisema kuwa kati ya wajumbe hao, mmoja alikubali kupiga kura na kusema yuko tayari hata kufukuzwa na chama chake.
“Sasa wale wanaotumia mbinu za ovyoovyo ili
mchakato huu usikamilike wanapoteza muda, maana ukizuia maji huku,
yanaelekea kwenye mkondo mwingine,” alisema Sitta.
Taarifa hizo zilionekana kuwalenga wabunge wa Viti
Maalumu, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Abama ambao kwa nyakati tofauti
walithibitishwa kutafutwa ili apige kura.
“Kweli nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi
kuwataja na wananitaka nipige kura na wengine walifika mpaka nyumbani
lakini mimi siwezi kushiriki maana nikifanya hivyo dhamiri yangu
itanishtaki,” alisema Msabaha.
Naye Abama alisema kuwa alikuwa amepewa ilani na
viongozi wake kwamba anatafutwa ili akapige kura, hivyo aliamua kukaa
ndani kukwepa mtego huo.
Kauli hizo mbili tofauti zinauachia Ukawa maswali
magumu yanayohitaji majibu ili kubaini iwapo kuna usaliti wowote
umefanyika au la.
Wabunge wengine ambao wanaweza kukukumbana na
matatizo ndani ya chama hicho ni Mbunge John Shibuda (Maswa Mashariki),
Said Arfi (Mpanda Mjini) ambao walikiuka uamuzi wa Ukawa kutoshiriki
Bunge hilo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana
alisema kuwa suala la wasaliti wa chama linatarajiwa kuzungumzwa kwenye
vikao vya ndani.
“Siwezi kulitolea uamuzi suala hilo, baada ya
kumaliza uchanguzi sasa litazungumzwa ndani ya vikao vya chama na
kutolewa uamuzi,” alisema Dk Slaa.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro
alisema kuwa Sitta alipaswa kuwataja wajumbe kutoka Ukawa waliokubali
kupiga kura, lakini hakufanya hivyo.
“Juzi amechukua kura zao na hawataji ni kina nani
wala walipiga kura kwa njia gani. Hata akijiongezea hizo kula mbili feki
bado BMK upande wa Zanzibar wanabakiwa na kura 145 tu na siyo 146,”
alisema Mtatilo.
Wanananchi waikataa rasimu
Naye Joseph Lyimo kutoka Manyara,
amesema kuwa baadhi ya wakazi wa mkoani humo, wamesema Bunge la Katiba
limepitisha rasimu ya Katiba bila maridhiano kwa baadhi ya wajumbe hivyo
kusababisha hofu ya kupatikana kwa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya
wananchi.
Wakizungumza jana na mwandishi wa habari hizi,
wananchi hao walidai kuwa rasimu hiyo iliyopitishwa bungeni juzi
haikukidhi maoni yaliyotolewa kwenye tume ya Warioba kwani ibara 28
zimefutwa na kuwapo ibara mpya 42.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Abdalah Mtengeti
alisema kwenye Tume ya Warioba wananchi walipendekeza mbunge awe na
ukomo wa madarakani kwa miaka 15, lakini sasa wabunge hao wameridhia
asiwe na mwisho wa utawala.
“Wananchi hawawezi tena kumwajibisha mbunge
waliyemchagua wao wenyewe kama walivyopendekeza awali pia hakuna ukomo
wa mbunge tena hivyo atatawala hadi mwenyewe aseme sigombei tena,”
alisema Mtengeti.
Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Manyara, Frank
Oleleshwa alisema rasimu hiyo ya wabunge haikujali maoni ya wananchi
kwani walipendekeza kufutwa kwa vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya
lakini, wabunge wameridhia.
“Pia wananchi walipendekeza kuwepo na Serikali
tatu ikiwamo kurudisha Tanganyika ili kuwapo na usawa wa nchi, lakini
wabunge wamegoma hilo na kuridhia Rais wa Zanzibar awe makamu wa pili wa
Rais,” alisema Oleleshwa.
CCM, CUF Zanzibar
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai walipozungumza na
gazeti hili kwa nyakati tofauti visiwani humo, Mazrui alisema kwamba
mambo yaliyopitishwa na Bunge la Katiba katika rasimu hiyo yanagongana
na Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ikiwamo suala
la mamlaka ya ugawaji mikoa aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa
kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Alisema Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
utekelezaji wake utakuwa mgumu kwa baadhi ya mambo Zanzibar mpaka Katiba
ya Zanzibar ifanyiwe tena marekebisho na kabla ya kufanyika hivyo
lazima kuitishwe kura ya maoni kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Vuai Ali Vuai alisema kwamba kama viongozi wote watafanya kazi kwa
kuzingatia sheria na katiba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa(SUK)
haitoyumba kwa sababu hakuna mshindi wala mshindwa baada ya rasimu ya
katiba kupitishwa.
“Matokeo ya kura ya rasimu ya katiba, ni ushindi
wa wazanzibari wote na watanzania kwa ujumla, na hakuna mshindi wala
mshindwa” alisema Vuai ambaye pia alikuwa mjumbe wa bunge maalum la
katiba.

No comments:
Post a Comment