Madini na maisha ya wananchi
Haiingii akilini kuona kampuni za kigeni
zinazochimba madini Tanzania zinawekeza nchi za nje, huku wananchi wa
Tanzania wakiendelea kuwa maskini.
Nafahamu kuwa mimi siyo mwandishi wa kwanza
kuandika suala la madini Tanzania, lakini haimaanishi kwamba tufunge
mdomo au tutupe kalamu zetu.
Madini ni miongoni mwa rasilimali zenye thamani
kubwa, hivyo kama zitawekewa sheria na usimamizi mzuri, taifa linaweza
kunufaika sana kimaendeleo.
Tanzania tunazalisha madini ya aina nyingi kama dhahabu, almasi, rubi, tanzanite, ulanga nk.
Katika uzalishaji huo, kuna baadhi ya migodi
inamilikiwa na wachimbaji wadogo wazalendo na mingine inamilikiwa na
wachimbaji wakubwa hususani kampuni za kigeni na mingine inamilikiwa kwa
ubia baina ya wageni na wazawa au mengine ya wazawa.
Ulinzi wa madini yetu
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 ibara ya 27 ibara ndogo ya 1 inaeleza kuwa kila mwanachi ana
jukumu la kulinda mali ya nchi ikiwa ni pamoja na madini. Hii ndiyo
kusema kwamba kwa kuacha madini kuchimbwa kiholela, wananchi na Serikali
yenyewe haijitendei haki. Madini ni mali ya yote inapaswa kuwanufaisha
wote.
Madini katika pato la taifa
Hivi karibuni kuna michango mbalimbali inaendelea
bungeni kuijadili bajeti, hatujaelezwa kwa kina mapato yanayotokana na
madini, miaka yote tumeendelea kuwa tegemezi.
Wasomi wanaongezeka, ajira haziongezeki, deni la
taifa nalo linazidi kupanda. Tuna rasilimali nyingi zikiwamo madini,
lakini ni kama yametushinda kujinufaisha, sasa tunakimbilia sekta ya
gesi. Rais wa Botswana, Festus Mogae tarehe 7, Juni, 2006 alisema: “Kwa
watu wetu, kila almasi inayouzwa inawakilisha chakula mezani, mazingira
mazuri ya kuishi, afya bora, maji safi, barabara kuunganisha jamii zetu
na vingi zaidi.”
Kasoro za sheria za madini Tanzania
Sheria inayosimamia madini Tanzania ni Sheria ya Madini ya mwaka
2010 Na.14 pamoja na kanuni zake mbalimbali zinazohusu mazingira
zilitolewa na gazeti la Serikali Na. 403 la tarehe 5/11/2010 inayohusu
kanuni za mazingira.
Sheria hizo zinahitaji kupitiwa upya kwa sababu ya kasoro zake kadhaa zinazoonekana.
Moja ya kasoro hizo ni kwamba katika maombi ya
kupewa leseni za uchimbaji madini kama watu wana sifa sawa za kupewa,
wanaangalia nani wa kwanza kuomba, kama wameomba siku moja wataangalia
mazingira husika.
Tunahitaji kufanya mabadiliko na sheria hiyo kutamka kuwa utaifa ndiyo kitu cha msingi cha kuangalia.
Tumeona wiki iliyopita mjini Dodoma, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alikuwa akizindua
kampeni ya Uzalendo, mambo haya ya uzalendo yasambae katika sekta zote
mpaka za madini.
Mbili, waziri ana mamlaka makubwa sana kwenye
sheria hii ya madini, anasaini mikataba kwa niaba ya Watanzania; kifungu
cha 15 cha sheria ya madini ya mwaka 2010 kinamruhusu waziri husika
kuamua kugawa maeneo ya uchimbaji kwa zabuni au kawaida.
Madaraka ni makubwa sana ukizingatia na unyeti wa
sekta. Kumpa mtu madaraka makubwa kiasi hicho ni kuweka mwanya wa
rushwa. Tatu, kamishna wa madini kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha sheria
no. 14 ya mwaka 2010 ya madini huteuliwa na Rais tu. Hii ni nafasi
nyeti inatakiwa kuwa ya wazi na ya kiushindani, Watanzania waombe nafasi
hiyo, mwenye uwezo mkubwa ndiyo apewe nafasi.
Kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka
2010 kinakataza mtu yeyote zaidi ya mmiliki halali wa leseni ya madini,
kumiliki, kusafirisha au kuuza madini, jambo kama hili pia linapaswa
kuangaliwa, kwa sababu kwa namna moja ama nyingine kinazuia watu wengine
kujiingiza kwenye biashara hii.
Kifungu cha 18 (3) kinakataza mtu yeyote
kusafirisha nje ya nchi madini au sampuli za madini bila kuwa na leseni
ya madini, kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi na uthibitisho wa
malipo ya mrabaha. Sheria kama hii inapaswa kuangaliwa, kwani angeweza
kuruhusiwa tu yeyote ili mradi awe anafuata taratibu nyingine za
biashara.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010, mtu yeyote atakayekiuka sheria kuhusiana na
umiliki na biashara ya madini akipatikana na hatia atatozwa faini ya
kiasi kisichozidi Sh10 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au
adhabu zote mbili.
Kwa kampuni, adhabu iliyopo kwa mujibu wa sheria
kwa kosa hilo ni kulipa faini isiyozidi Sh50 milioni. Wataalamu wa
madini wanabainisha kuwa faini iliyowekwa na sheria na adhabu yake ni
ndogo sana ukilinganisha na thamani ya madini.
Kifungu cha 6 (4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka
2010, kinampa mamlaka kamishna wa madini kutaifisha madini
yaliyopatikana kinyume cha sheria, pamoja na vifaa vilivyotumika
kuzalisha madini hayo. Sheria ilipaswa kueleza zaidi juu ya uhifadhi na
uuzaji wa madini hayo.
Tano, sheria ya madini kifungu cha 25 (1) inaeleza kuwa ripoti
inayotolewa na wamiliki wa haki miliki za migodi ni siri, kwa nini
ripoti iwe siri? Kwa nini isiwekwe wazi mfano kwenye tovuti ya wizara na
kufanya kila mwananchi ajionee kinachoendelea kwenye rasilimali ya nchi
yao. Mikataba ni siri, ripoti kutoka kwa wamiliki nayo ni siri.
Waswahili wanasema “halali haina siri, haramu ndiyo ina siri.”
Hizi ni baadhi ya kasoro kwenye sheria ya madini. Haya mambo yawekwe wazi kila mmoja ajue kinachoendelea.
Maeneo ya migodi yatangazwe wazi, kila mtu
agombanie kwa ushindani ulio sawa. Maeneo ya madini yaianishwe na
yatangazwe, watu wagombanie kwa usawa, kipaumbele wapewe wazawa wenye
sifa na uwezo, tusiwabeze Watanzania juu ya hili.
Kwa mfano kwa sasa tunataka kujikita kwenye
kuchimba urani, lakini imefahamika kuwa madini hayo ya urani yana hatari
kubwa kwa binadamu kutokana na kuwa na mionzi yenye madhara. Lazima
tujifunze kutoka kwenye uchimbaji wa madini mengine kama dhahabu,
almasi, Tanzanite na chokaa, ambao ulisababisha wananchi kupata magonjwa
ya ngozi, saratani, uchafuzi wa maji na vifo vya mifugo na wanyama
wengine wa porini na majini.
Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na 403 la tarehe
5/11/2010 kanuni ya 7 na 8 zinakataza uchafuzi wa mazingira, lakini
kanuni ya tisa inasema ukifanya kosa la uchafuzi faini haitazidi milioni
moja au kifungo kisichozidi miezi sita, najiuliza hiyo adhabu kweli
inaonyesha nia ya dhati ya kulinda mazingira kweli?
Jibu jepesi, hapana, tutunze mazingira yetu, madini yana thamani sana lakini hata mazingira yetu yana thamani kubwa sana.
Kwa kifupi, baada ya mikataba hiyo kutomnufaisha
mwananchi, Serikali haina budi kuangalia mapungufu hayo katika sheria na
kuyafanyia kazi ili madini na rasilimali nyingine ziwe na usimamizi
thabiti na wenye manufaa kwa kila Mtanzania.








