Friday, 28 March 2014

Tuhuma nzito bungeni,ni za rushwa dhidi ya Waziri Mkuu Pinda

Dar es Salaam. Hali ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa serikali mbili.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi hilo walicharuka na kujaribu kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa iwapo Wenje asingeomba radhi, asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani “walilia” sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa kama mganga wa jadi.
Ingawa hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.
Kuhusu rushwa, Wenje alisema:“…Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika usiku. Hii haikubaliki.”
Baada ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.
“Kwa sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje aniombe radhi,” alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira, huku kukiwa na sauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.
Makamu mwenyekiti pia alifanya jitihada za kuwataka wajumbe kuwa wavumilivu, huku akitoa nafasi kwa Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza kwamba ni tuhuma nzito. 
Kawambwa alisema: “Ni kweli nilikutana nao; ni wajumbe ambao wanatoka kwenye taasisi zinazojihusisha na masuala ya elimu, lakini mbona wameshafanya mikutano yao mingine mingi ambayo mimi hawakuniita. Kama mtu akiwa hana hoja bora akae chini.”
Makamu Mwenyekiti alimtaka Wenje aombe radhi kutokana na kauli yake, lakini katika hali ya kushangaza mjumbe huyo alisisitiza kwamba Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamekiri.
“Maghembe amekiri aliwaita wafugaji na wavuvi ndiyo waliokula chakula cha rushwa, pia wapo wengine walienda kwa Waziri Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi mama mmoja siwezi kumtaja jina hapa alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa jina lake mwenyekiti baadaye. Aliambiwa kwamba anatoa siri… hoja iliyojadiliwa huko ilikuwa ni kwamba msimamo ni wa serikali mbili… rushwa ya chakula, maji na bahasha walipewa,” alisema Wenje na kusababisha kulipuka kwa kelele zaidi.
Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.
Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.
Baada ya Wenje kukaa, baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 walichachamaa wakitaka kutetea hadhi yao, akiwamo mjumbe kutoka kundi la wafugaji, Esther Juma aliyesema hawatendewi haki kama kundi kusema kwamba walihongwa.
Alisema yeye ana ng’ombe 3,000 na asingeweza kwenda kupokea rushwa ya chakula na kumtaka mbunge huyo kuwaomba radhi la sivyo asingetoka mlangoni.
Wakati mjadala huo ukiendelea, mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa ametoka kwa udhuru, alirejea kimya kimya, na kumtaka Wenje kueleza iwapo anadhani kauli yake haikuwaudhi baadhi ya wajumbe.
Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta kutangaza kuwa anapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge na uamuzi utakaotolewa atautangaza bungeni.

Tuesday, 25 March 2014

Baada ya matokeo Fanya uamuzi sahihi kujiendeleza kielimu

Wapo wanaofuata mkumbo wa kusoma mchepuo (combination) fulani kwa sababu marafiki zao wengi wameuchagua mchepuo huo. Aidha, wapo wanaolazimisha kusoma masomo magumu yaliyo nje ya uwezo wao kiakili.
Kwa mfano, unaweza kupata alama C katika mtihani wa Hisabati (Basic Mathematics), lakini alama hiyo siyo tiketi pekee ya kuchagua kusoma masomo yenye hesabu za kiwango cha juu (Advanced Mathematics).
Waliofeli nao?
Kama ilivyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, asilimia 78.91 ya wahitimu wamepata daraja la nne na sifuri. Ni dhahiri kuwa wanafunzi hawa hawana sifa ya kujiunga na kidato cha tano.
Hata hivyo, huo ndiyo uwe mwisho wa safari ya kusaka elimu kwa vile tu umefeli? Makala haya yanajaribu kutoa mapendekezo mbadala yanayoweza kutumiwa na wanafunzi ili kujiendeleza zaidi kielimu?
Kwanza ieleweke kutokuchaguliwa kidato cha tano au kufeli kidato cha nne si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.
Uzoefu unaonyesha hapa nchini kuna watu wengi baadhi yao leo ni maprofesa maarufu waliowahi kufeli katika madaraja fulani ya kielimu siku za nyuma, lakini kwa kuwa tu walikuwa na dhamira ya dhati na kutoa uamuzi sahihi, waliweza kujiendeleza na kufika kiwango hicho cha elimu kinachotamaniwa na kila mtu.
Nikupe siri moja ninayoifahamu kuhusu wasomi hawa, baadhi yao waliwahi kuwa walimu wangu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hawa pamoja na wengine kuamua kuanza maisha ya familia au kikazi lakini walijiendeleza kupitia mfumo usio rasmi.
Unaweza kuihuisha ndoto yako ya kupata elimu kwa kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo na ndiyo maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi.
Rudi tena darasani. Kuna shule nyingi za sekondari zenye programu maalumu kwa ajili ya watu wanaorudia mitihani ya kidato cha nne tena kwa bei rahisi.
Zitafute shule hizi ila kuwa makini na vituo vinavyoitwa kwa Kiingereza ‘Tuition Centers’ ambavyo vingi vinajali masilahi kuliko ubora wa elimu.
Chunga jambo hili! Kuna mtindo wa wanafunzi wanaofeli kidato cha nne na kuamua kuingia kidato cha tano huku wakirudia mitihani yao. Hawa wanalazimika kusoma masomo ya mitihani wanayoirudia huku wakisoma pia masomo mapya ya kidato cha tano.
Huku ni kujidanganya, kwa mtindo huu, mwanafunzi husika hawezi kusoma kwa undani masomo ya kidato cha tano badala yake atakuwa anasoma ‘kimtego mtego’ ili afaulu tu mitihani ya ndani.
Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani za ngazi ya cheti. Kusomea cheti siyo kuonekana mjinga, kwanza una uhakika wa kuajiriwa au kujiajiri. Kwa mtu mwenye ndoto ya kusoma zaidi, kipato cha ajira yako ndicho unachoweza kukitumia kujiendeleza zaidi.
Upo mfano mzuri wa walimu wa shule za msingi waliosomea ualimu kwa ngazi ya cheti. Wengi hujiendeleza kwa kurudia mitihani na hatimaye kufika vyuo vikuu.
Siyo ualimu pekee, kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa kozi za msingi kwa wahitimu wa kidato cha nne wakiwamo waliopata angalau daraja la nne.
Unachofanya ni kusomea cheti cha msingi kwa mwaka mmoja, kisha unaendelea kwa kusoma tena cheti cha juu kabla ya kupata fursa ya kusoma stashahada.
Kwa walio makini mlolongo huu wa elimu unaweza kukufikisha mbali. Unaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi hawa kwa sharti la kuwa vimesajiliwa na Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (NACTE).
Fursa nyingine inayotumiwa na baadhi ya wanafunzi wanaoishia kidato cha nne ni kusoma masomo ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya VETA wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza zaidi kielimu.
Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya VETA umekua na kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira iwe ajira binafsi au ajira rasmi. Kwa mfano, hivi sasa VETA inaendesha kozi katika sekta za madini, utalii, teknohama na nyinginezo muhimu zama za sasa.

Sitta ‘amkataa’ Warioba bungeni

Dodoma. Jaribio la kutaka kumrejesha bungeni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili ajibu masuala yaliyoibuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kufungua Bunge limegonga mwamba.
Uamuzi wa kukataa ombi hilo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mjumbe wa Bunge, Julius Mtatiro, akisema hadhani kama ni sahihi ombi hilo kutekelezwa.
Awali Mtatiro aliomba mwongozo kwa mwenyekiti, akitaka kujua iwapo kuna haja ya kumrejesha Jaji Warioba kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja za Rais Kikwete ambazo zimekinzana na maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Mtatiro alisema: “Mtoa hoja mahususi alikuwa ni Jaji Warioba na Rais Kikwete alialikwa kama mgeni rasmi kufungua Bunge, lakini badala yake alikuja kujibu hotuba ya Warioba.
“Kwa sababu Rais alikaribishwa kama mgeni rasmi, lakini  alijibu  hoja za Warioba, je, hatuoni kama kuna haja ya kumrejesha mtoa hoja mahususi aje kujenga hoja  kutokana na alichosema Rais Kikwete?” alihoji Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF.
Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema tayari amepokea kwa maandishi kutoka kwa baadhi ya wajumbe kuzungumzia suala hilo, jambo ambalo litafanyika lakini si kwa kumwita tena Jaji Warioba.
“Tunapenda kupata muda wa kuzungumzia  suala hili ili kuliweka sawa, hotuba zote mbili ambazo ni muhimu zitaandaliwa ili kupitiwa kuona kama malalamiko yanayotolewa yana hoja,” alisema Sitta.
Tangu Rais Kikwete ahutubie Bunge Ijumaa na kutoa hoja kinyume na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, hasa muundo wa Muungano, kumeibuka mijadala ya ama kuipinga au kuiunga mkono, huku wengine wakieleza kuwa imekiuka sheria.

CCM yaliteka Bunge la Katiba

Dodoma. Sasa ni wazi kwamba serikali mbili zimeonyeshwa taa za kijani baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamata uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jana kamati 14 za Bunge hilo ziliwachagua viongozi wake; Mwenyekiti na Makamu na 12 kati yake zilichukuliwa na wajumbe kutoka CCM, chama ambacho tayari kimeweka wazi msimamo wake kuunga mkono Muungano kuwa ni serikali mbili.
Miongoni mwa waliochaguliwa wenyeviti ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu ambao wamekuwa mstari wa mbele kupigia chapuo mfumo huo badala ya serikali tatu zinazopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Wengine ni Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango – Malecela, Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Khamid Salehe, Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Wengine wa CCM ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah na aliyewahi kuwa Waziri katika serikali zilizopita Paul Kimiti. Pia wamo Mbunge wa Wawi ambaye alifukuzwa uanachama na chama chake cha CUF, Hamad Rashid Mohamed na Mwenyekiti wa kundi la wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais, Francis Michael.
Katika uchaguzi wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, aliyekuwa mwenyekiti wa Muda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alichaguliwa mwenyekiti na makamu wake, Dk Susan Kolimba.
Kamati ya Uandishi wa Katiba ilimchagua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na makamu wake, Mgeni Hassan Juma. Kwa kupata nafasi hizo ni dhahiri kwamba ‘mapishi’ ya uendeshaji wa Bunge hilo yatafanywa na CCM kwani mwenyekiti wake Samuel Sitta na makamu mwenyekiti Samia Suluhu Hassan pia ni makada wa chama hicho.
Wenyeviti hao wataungana na Sitta pamoja na Hassan kuunda Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambayo ndiyo itakuwa na mamlaka ya kupanga ratiba na miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge hilo.
Waliochaguliwa kuwa makamu wenyeviti ni Profesa Makame Mbarawa, Shamsa Mwangunga, Fatma Mussa Juma, Dk. Sira Ubwa Mamboya, Assumpter Mshama, Dk. Maua Daftari na Waride Bakar Jabu. Wengine ni Biubwa Yahya Othaman, William Ngeleja, Salimin Awadh Salimin, Yusuf Massauni na Thuwayba Kisasi.
Mbowe atimuliwa
Katika uchaguzi huo, mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe alitimuliwa katika kamati alikokwenda kushiriki uchaguzi kwa madai kwamba hakuwa mjumbe.
Mbowe alisema kabla ya uchaguzi huo alimfuata Mwenyekiti Sitta kumwomba wafanye marekebisho katika kamati tatu za Bunge.
Alisema waliafikiana kuwa Godbless Lema aliyekuwa Kamati namba saba ahamieKamati namba mbili na AnnaMary Stella Mallac aliyekuwa Kamati namba mbili ahamie Kamati namba sita.
Alisema kwa makubaliano hayo yeye (Mbowe) alihamia Kamati namba saba akitokea Kamati namba sita.
“Nilivyoingia katika ukumbi wa Igada, wajumbe walianza kuguna mara wakaanza kuzozana wakitaka wajumbe ambao hawakuwamo kwenye orodha ya kamati hiyo kutoka nje,” alisema na kuongeza;
“Waliamua kuitana majina, lakini hawakuona jina langu wakanitaka nitoke nje, nikawaeleza makubaliano kati yangu na Mwenyekiti (Sitta) lakini hawakuafiki walisisitiza nitoke ndani ya ukumbi huo.”
Alisema hatua hiyo iliwafanya makatibu wasaidizi kuitwa na kuelezwa kilichotokea ambapo waliwasiliana na Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hemed ambaye aliwajibu kuwa bado hajapokea taarifa za mabadiliko hayo na kuwataka wasubiri awasiliane na Sitta.
“Wakati nikiendelea kusubiria
jibu, mmoja wa wajumbe aliendelea kupaza sauti akitaka niondolewe ili waweze kupiga kura,” alisema.
Alisema hali hiyo ilimfanya yeye na baadhi ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani, akiwamo Profesa Abdallah Safari kususia uchaguzi huo na kuondoka.
Mbowe alisema baada ya muda walifuatwa na makatibu wakiwaomba samahani warudi ukumbini kwa sababu wamepokea maelezo kutoka kwa Sitta. Sitta alithibitisha tukio hilo, lakini alisema halikuathiri matokeo ya uchaguzi kwa sababu kuondoka kwao hakukuathiri akidi inayotakiwa.

Monday, 24 March 2014

Ndugai: Taifa lina tatizo la mgawanyo wa rasilimali

Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameomba ushauri kwa Seneta Amos Wako wa Kenya kuhusu mgawanyo wa rasilimali za taifa.
Ombi hilo la Ndugai, ambaye ni mjumbe wa Bunge la Katiba, lilitokana na historia aliyoitoa seneta huyo wa Busia Mashariki nchini Kenya, iliyotokana na uzoefu alioipata katika Mchakato wa kuunda na kuandika katiba ya nchi hiyo.
Mwishoni mwa wiki, Seneta Wako alieleza bungeni kuwa changamoto zilizokuwa zikiikabili Kenya wakati ikiandika Katiba yake, ni pamoja na wananchi kulalamikia mfumo wa mgawanyo wa rasilimali.
“Kulikuwa na madai kwamba hakukuwa na usawa katika kugawa keki ya taifa, maeneo yenye viongozi yalidaiwa kupendelewa kwa kuwa na huduma nzuri za kijamii kuliko mengine,” alieleza Seneta Wako.
Ndugai alipopata nafasi ya kuuliza swali, alisema tatizo la mgawanyo wa rasilimali lililokuwako Kenya, lipo hata hapa nchini lipo kwa kiwango kikubwa.
“Mikoa mingi inalalamikia uduni wa huduma kwa jamii. Kwa uzoefu wako unashauri nini kifanyike kutatua changamoto hii,” aliuliza Ndugai.
Seneta Wako alisema mgawanyo wa madaraka na rasilimali za taifa nchini Kenya unaendelea kushughulikiwa kupitia Utawala wa Majimbo, ingawa aliasa kwamba kinachofaa kwa wengine haimaanishi kitafaa kwa Tanzania.
Alisisitiza kuwa ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania utatokana na Watanzania wenyewe kwa sababu ndio wanaofahamu mila, desturi na mfumo mzima wa maisha yao.

Sunday, 23 March 2014

Tanzania inahitaji watumishi wafanyakazi wa aina gani?

Mwanzo wa maendeleo ya kweli kwa nchi yoyote duniani kama historia
inavyodhirisha, ni pale watumishi na wafanyakazi wanapobadilika na kujitambua kutokana na kuwepo sera na mifumo ya usimamizi nautendaji kazi inayotambua nafasi, stahili au haki, wajibu na majukumu ya kila mtu katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Kwa jumla, wataalamu wa nadharia na tasnia ya rasilimali watu wanasema
Kwamba, kazi kubwa ya wanaosimamia rasilimali watu ni kuhakikisha kila shughuli katika taasisi husika anapatikana mtu sahihi, mwenye elimu na ujuzi sahihi, wakati sahihi na atakayepewa kazi sahihi ili aifanye kwa usahihi pia.
Hata hivyo, rasilimali watu kama somo ni somo pana na katika miaka ya leo imeanza kuaminika kwamba kiongozi wa taasisi anayepwaya katika elimu na ujuzi wa rasilimali watu hawezi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama ilivyo kwa yule aliyesheheni nidhamu na nadharia husika.
Kazi ya kusimamia au kuongoza rasilimali watu inaanzia na mipango, ugawanyaji kazi na wajibu, utafutaji watu kujaza nafasi zilizo wazi, mahojiano ya kutathmini sifa na uwezo wa mtu kama unaendana na jinsi alivyo na uchaguaji miongoni mwa walioomba kazi idadi ya watu wanaotakikana kwa kazi fulani.
Menejimenti ya rasilimali watu inajumuisha pia mambo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi, uchukuaji wa hatua za kinidhamu, afya na usalama wa wafanyakazi pamoja na mikakati yote inayoihakikishia taasisi kuendelea hata kama waliopo kwa wakati huo wataondoka au kufa.
Kampuni au idara ya Serikali au taasisi iwayo kwa hiyo ina maana kwamba utendaji kazi wake na sifa yake aghalabu, utatokana na aina ya watu walioajiriwa. Ukiajiri watu wa ovyo na utendaji wa taasisi husika nao pia utakuwa ni wa ovyo. Ukiajiri watumishi au wafanyakazi wazuri basi uwezekano wa taasisi hiyo kuwa na utendaji mzuri nao ni mkubwa pia.
Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba wale wote waliopewa dhamana ya kuajiri wafanyakazi au watumishi wapya lazima wawe wanaojua kila linalopaswa kujulikana juu ya mbinu zote zinazotumika katika nadharia na utendaji kazi katika tasnia ya rasilimali watu ili kuhakikisha kwamba watumishi watarajiwa wote wanapepetwa kwa namna ambayo chuya au chafu wote unaondolewa na panabakia nafaka nzima na safi.
Hili linahitaji kwa kiasi kikubwa ugwiji katika masuala ya saikolojia na sosholojia. Elimu zinazoweza kuwang’amua watu walivyo na watakavyokuwa kwa kuangalia historia yao ya kimaisha na kikazi.
Polisi wanapolalamika kwamba wameajiri askari polisi ambao wanashirikiana na majambazi kuwaibia na kuwadhuru wananchi ilhali tunajua kazi ya polisi inatakiwa iwe nini, hapo kunaonyesha kuna walakini mkubwa katika namna wafanyakazi katika eneo husika awanavyochambuliwa na mwishowe kuajiriwa.
Mamlaka za kodi na mapato zinavyolalamika kuna wafanyakazi walioiva na kupevuka kwa rushwa, pia tatizo ni hilo hilo, yaani, jinsi watumishi wao wanavyopatikana na jinsi wanavyochujwa ili wabakie wale walio safi.
Benki na sekta ya fedha inapolalamika juu ya wizi kushamiri katika mabenki kwa ushirkiano kati ya wafanyakazi wa taasisi za kifedha na wafanyabiashara au hata wezi ni ishara kwamba kuna ajira mbovu katika sekta husika.
Tunapolalamika juu ya utendaji kazi katika hospitali, shuleni, vyuoni na kadhalika jambo hili pia huwa ni dalili ya kuwepo kwa walakini katika masuala ya haki na wajibu wa watumishi wahusika.
Tumalizie kwa kusema kwamba rasilimali watu ambayo nchi inabahatika kuwa nayo haitoki juu mbinguni. Rasilimali hiyo inatokana na jamii iliyopo katika nchi husika.
Hivyo ni vigumu kuona kama jamii yenyewe inajikita katika uongo, ubabaishaji, uzembe, ubinafsi, uvivu, umbeya, maneno bila vitendo, kula usichokipanda na ila za kila aina, ni kwa vipi jamii hiyo inaweza kuwa na wafanyakazi wanaohitaji kuiondoa jamii yao kutoka kwenye hatua ya chini kabisa kimaendeleo na kuipeleka kwenye hatua ya juu kabisa kimaendeleo!

Warioba:‘Tumemaliza kazi yetu’

Dodoma. Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi waamue.
Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Jaji Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Alisema wamemaliza jukumu walilopewa na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge.
Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali, wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada ya kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa 1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Alisema hajui lengo la Rais kufanya alichofanya lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni ya wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012), inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda kosa kinyume na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000 (milioni mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.
Sheria hiyo inaendelea kuelekeza, (4) Hatua zozote zilizochukuliwa chini ya kifungu hiki hazitachukuliwa kuwa zimefikia ukomo na zitaendelea kuwa na nguvu ya kisheria hata baada ya Sheria hii kukoma kutumika.”
Profesa Baregu alisema sheria imezungumzia mtu yeyote, hajui kwa Rais inakuwaje.
“Sijui ameona Bunge halitoshi, haliwezi kung’amua mambo au limepungukiwa kiasi cha kushindwa kumudu majukumu yake? Sielewi ila amevunja sheria na amelivunjia Bunge hadhi yake kiasi kwamba hata kazi yake inaweza isiaminike,” alieleza.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete amejipa jukumu la kujibu na kujadili hoja za rasimu na hivyo kuwa sehemu ya Bunge Maalumu.
Alisema wakati wabunge wanahimizwa kutumia mfumo wa maafikiano katika kuamua mambo, Rais amewajengea msingi wa mgawanyiko na chuki, hali itakayoathiri mpango wa kulipatia taifa Katiba inayotokana na wananchi.
Profesa Baregu alitaja baadhi ya kauli za Rais Kikwete ambazo zinaweza kuathiri mchakato kuwa ni kujirudia kwa kauli; “Nyie ndiyo mnaotunga Katiba (Wabunge wa Bunge Maalumu) kazi imebaki kwenu.” na maelekezo kwamba serikali tatu zitapatikana, lakini labda baada ya yeye (Rais Kikwete) kuondoka madarakani.
Jaji Ramadhan
Jaji Ramadhani alisema wao Tume wamemaliza kazi yao na kwamba sasa wanawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi waamue.
“Tumemaliza kazi yetu na sasa tunawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ikitokea wajumbe wa Bunge hilo wakihitaji ufafanuzi wa jambo lolote, yeye binafsi anaahidi kutoa ushirikiano.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni juzi, alisema yeye alikuwa Arusha akishughulika na vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na kwamba hakuwa amepata muda wa kuipitia na kuitafakari kwa kiwango cha kuizungumzia.
“Ninasoma na kuitazama kupitia vyombo vya habari na ninafahamu nyie wanahabari huwa mnalenga pale palipowakuna. Hivyo nikitulia na kupata hotuba halisi aliyotoa nikaitafakari; nitaizungumzia,” alieleza.
Rais Kikwete akizindua Bunge juzi mjini Dodoma, alisema rasimu ya pili iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba ina makosa mengi ya kiuandishi.
Alisema ina mambo mengi, baadhi yalitakiwa kuwekwa kwenye Sheria.
“Mbolea, mbegu, pembejeo vyote vimewekwa humo, hata umri na haki ya mtoto kupewa jina vinawekwa humo, yakiwekwa yote kama yalivyo, serikali haitaweza kuyatekeleza itashtakiwa mahakamani kila wakati,” alieleza.
Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu kusoma neno kwa neno, mstari kwa mstari na kujiridhisha na mambo watakayoidhinisha yaingie kwenye Katiba itakayopendekezwa.
Alisema watakachoona kinafaa kurekebishwa, kuboreshwa au kufutwa wasisite kufanya hivyo kwa sababu inatakiwa Katiba bora, inayotekelezeka na ambayo haitalalamikiwa kiasi cha kulazimika kuibadilisha muda mfupi baada ya kupitishwa.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, alisema wakichagua Serikali tatu watatakiwa kuondoa mambo yote yanayoweza kukanganya utendaji wa Serikali za washirika na ile ya Muungano. Lakini wakichagua Serikali mbili, mengi yatatekelezeka.
Rais Kikwete alisema serikali zote mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba kutatua mambo matatu kati ya sita ambayo bado hayajatatuliwa kutoka kwenye orodha ya kero 31 za Muungano zilizoainishwa na Zanzib

Tuesday, 18 March 2014

Bunge lachafuka, Warioba asimama bila kuwasilisha Rasimu ya Katiba

Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa 11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema: “Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari, Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi (hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo, naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo tutakapotangaziwa tena.”
Licha ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe waliendelea kupaza sauti zao wakisema kwamba walikuwa wanaburuzwa.
Wakati hayo yakitokea, kikosi cha askari wa Bunge kiliingia ndani ya ukumbi na kusimama katika lango kuu hali iliyoonekana kuwa ni kuchukua hadhari endapo hali ya usalama ingechafuka.
Baada ya tamko la kuahirisha mkutano, askari hao waliingia moja kwa moja hadi alipokuwa ameketi Jaji Warioba na kumsindikiza hadi nje na jitihada za waandishi wa habari kumfuata ili kupata maoni yake hazikufanikiwa.
Kilichofuata baada ya hali hiyo ni kurushiana maneno kwa baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Ave Maria Semakafu ambaye nusura azipige kavukavu na mjumbe mwingine ambaye jina halikuweza kupatikana mara moja.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe akiwamo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani waliamulia ugomvi huo kabla ya kuwa mkubwa.
Wajumbe walionekana kukaa katika vikundi ndani ya Bunge huku wakijadiliana juu ya kilichotokea wakati Sitta, Katibu wa Bunge, Yahaya Khamis Hamad na msaidizi wake, Dk Thomas Kashililah wakiwa katika kikao cha faragha.
Baada ya kujadiliana kwa nusu saa, Hamad akiwa ameongozana na Dk Kashililah, alirejea katika ukumbi wa Bunge na kuwataka wajumbe kutawanyika hadi hapo watakapojulishwa.
Hali hiyo iliibua kelele kutoka kwa wajumbe wakitaka kujua iwapo waondoke katika maeneo ya Bunge au la. Hamad alisisitiza kwamba warejee nyumbani hadi hapo watakapojulishwa.

Sunday, 16 March 2014

Tunahitaji kubadilika ili kuondoa umaskini

Nakumbuka nilipokuwa bado kijana katika mkoa nilioishi kulikuwa na matajiri kadhaa ambao sisi tuliwaona wametuzidi. Wengine walikuwa jamaa zetu, hivyo kuwafahamu kwa karibu zaidi namna walivyokuwa wakiendesha maisha yao na namna walivyokuwa wakifurahia maisha yao ya kutokukosa vitu vidogo vidogo.
Sehemu kubwa zaidi ya matajiri hao sasa hawapo tena katika hali hiyo ya kuwa navyo. Wengi wao sasa ni wahitaji, wakiishi maisha ya kubangaiza. Tukiwaacha wao hata sisi wengine japo siyo matajiri, lakini huenda tumewahi kushika ‘vipesa’ wakati fulani, lakini pesa hizo zikashindwa kabisa kubadilisha maisha yetu.
Hali hii inahitaji kujitafakari kwani haina maana kuzungumzia nchi kujitoa katika umaskini wakati watu wake hawana mpango wa kujitoa katika umaskini huo. Tujiulize, inakuwaje tunaendelea kuwa maskini hata pale ambapo tunapata fursa ya kuwa na fedha?
Majibu kwa swali hili yapo mengi, lakini leo tuangalie yale yanayoendeana na tabia.
Wengi wetu tuna tabia ya kutokuweka akiba. Tabia hii wanayo wakulima, wafanyakazi hata wafanyabiashara. Mtu akibarikiwa kuwa na ziada ya pesa, basi badala ya kufikiria namna pesa hizo zitakavyozalisha zaidi, pesa hizo zitatafutiwa matumizi zaidi.
Matumizi hayo mara nyingi siyo ya kuzipeleka kwenye eneo la uwekezaji ili mtu apate faida zaidi bali ni kwenye eneo la ulaji. Kwetu sisi pesa zaidi maana yake ni sherehe zaidi, ununuzi zaidi na mbwembwe nyingine nyingi zisizokuwa na tija. Mwishowe ziada yote iliyopatikana inayeyuka na kumrudisha mtu katika hali ile ile aliyokuwa nayo kabla ya fedha kumtembelea.
Hakika hii inahuzunisha; hebu fikiria leo mtu anawakaribisha kwenye sherehe ya ubatizo wa mwanawe ambayo inakuwa kubwa kuliko hata ya Tanzania kufikisha miaka 50, halafu kesho mtu huyo huyo anakugongea na kukuomba au kukukopa fedha ya kununulia unga wa ugali.
Yanatupata haya kwa sababu fedha inatuwasha pale inapokuwa mikononi mwetu. Wakati wenzetu wanachambua faida na hasara watakazozipata kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali, sisi tunachambua kicheko tutakachokuwa nacho katika matanuzi ambayo hata kuyapanga hatupangi bali yanakuja hapo hapo baada ya kupata fedha.
Siamini kama kweli mtu alipanga kuwajengea vimada nyumba bora za kuishi halafu yeye na familia yake wakakosa sehemu ya kuishi. Naamini fedha zilipokuwa mkononi zilimtia upofu na zilimharibu akili yake, hata akatenda hayo. Tumewasikia wale waliopata ufahamu baada ya kufilisika na wakataka kuzimiliki nyumba hizo bila mafanikio.
Wao wanateseka kwa kukosa makazi, lakini wale waliowapa starehe za muda wanaishi katika nyumba za kifahari. Hata kama makazi yapo hizo fedha si zingewekezwa kwenye maeneo yanayozalisha fedha zaidi?
Uzalishaji huo si ungemwezesha sasa mtu kuishi uzee wake mwema? Uzee ambao mtu angekuwa anatumia muda mwingi sasa kuwaombea na kuwabariki watoto wake, badala ya kila siku kuwalaani kwa madai kwamba hawamjali.
Tabia nyingine inayotuvuruga sana ni ya kujionyesha. Katika kujionyesha huko mtu ananunua au anajenga, hata kile ambacho hana sababu nacho. Mtu alikuwa na friji yake inayomtosha kwa matumizi ya nyumbani kwake leo fedha imemtembelea basi atakwenda kununua friji kubwa, utafikiri anataka kuweka kuku wa kuuza.
Friji hiyo kubwa inaishia kuwekwa maji, atajenga nyumba kubwa zaidi yenye ghorofa mbili, halafu vyumba vingine vinaishia kuwa makazi ya mende. Inasikitisha sana pale watu wanapokuwa wamezeeka halafu nyumba hiyo ipo mahali ambapo familia haiwezi hata kubadilisha matumizi ya nyumba hizo yaani badala ya kuishi, labda wafanye hoteli au wapangishe.
Utakuta mtu kaishiwa kabisa, lakini hajui jinsi ya kuitumia nyumba hiyo ambayo kwa sasa inatumika kwa asilimia 10 tu. Ukijiuliza kwa nini mtu aliwekeza kwenye jumba kama hilo, jibu utakalopata ni alitaka watu wajue kwamba naye ana fedha.
Tunahitaji kweli vitu vyote tunavyovinunua? Hakuna siku tunajutia viatu na nguo nyingi tulizozijaza katika nyumba zetu, ambazo kwa kuwa zimepitwa na wakati zimejaza makabati yetu na hatuna za kuzifanyia?
Hivi kweli mtu unakosa hata fedha ya kununulia dawa, lakini ndani ya nyumba una vitu chungu mzima ulivyovinunua kwa kujionyesha na sasa havikuzalishii chochote, hiyo kweli ni akili?
Tunapenda sana kuwaiga wazungu, nafikiri tuwaige pia tabia yao ya kupenda kuweka akiba kwa ajili ya kuwekeza au kwa ajili matumizi ya baadaye. Tujifunze pia kufanya vitu kwa kiasi, tuache tabia ya kujionyesha, kwani tabia hii inatufanya tusifikiri vizuri katika kuwekeza fedha tuzipatazo.
Tusipobadilika, tutaishia kama tulivyo; leo mtu anapigiwa makofi kwa kuvaa vizuri, kutembelea magari ya kifahari, kuishi kwenye nyumba ya kifahari na kufanya sherehe kubwa kubwa halafu baada ya muda mfupi, anakuwa omba omba au kopa kopa asiyerudisha fedha anazokopa.
Hii haikubaliki hata kidogo. Tujizoeshe tabia mbadala nayo ni ya kuweka akiba na kununua vitu kwa mahitaji siyo kwa fahari.

Sitta: Katiba inaruhusu kununua uongozi

Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amesema kushamiri kwa vitendo vya watu wachache kujitajirisha na wengine kununua uongozi, kunatokana na Katiba ya sasa kutokuwa na meno ya kupambana na rushwa na ufisadi.
Amesema vitendo hivyo vitakoma kama nchi ikiwa na Katiba nzuri, itakayowezesha kutungwa kwa sheria nzuri zitakazowabana mafisadi na watoa rushwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Dodoma juzi, Sitta alisema: “Siridhiki na Katiba ya sasa inavyoshughulikia rushwa na ufisadi. Katika nchi yetu inaonekana ni rahisi mtu kujitajirisha kwa kutumia cheo chake na baada ya hapo kununua uongozi. Katika nchi maskini jambo hili ni hatari kubwa.”
Aliongeza, “Katiba lazima ielekeze kwamba iko tofauti kati ya kufanya biashara na kuongoza watu. Haiwezekani ukawa na biashara kubwa zinazochukua zabuni za Serikali na ukaendelea kuwa kiongozi wa Serikali, nchi nyingi zimetenganisha mambo haya.”
Alisema rushwa ni hatari na inaweza kusababisha nchi kukosa amani, kwa sababu wananchi maskini watafika mahali hawataona uhalali wa maisha ya watu wanaowaongoza.
“Nimeipenda Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imeeleza wazi kuhusu suala la  uadilifu hivyo lazima zitungwe  sheria zitakazowabana watu kutokutumia madaraka yao vibaya,” alisema.
Sitta ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema ni hatari kuwa na mfanyakazi wa Serikali mwenye kampuni binafsi ambayo inapewa tenda za Serikali.
“Sisemi kuwa watu wasiwe wafanyabiashara, mtu akiamua kuhudumia umma anatakiwa kuweka mali na biashara zake katika mfumo wa kuendesha biashara hiyo bila yeye kuwa mhusika wa moja kwa moja. Hivyo, ndivyo wanavyofanya mataifa kama Uingereza na Marekani,” alisema Sitta.
Alisema taarifa nyingi za maendeleo katika nchi za Afrika zinaeleza kuwa nchi za bara hilo zinakwama kupiga hatua kimaendeleo kwa sababu ya rushwa.
“Rushwa inajenga mtandao ambao unashuka hadi ngazi za chini. Watumishi wa chini wakiona mikataba mibovu inawanufaisha wakubwa nao hutafuta mianya katika maeneo yao. Ikiwa hivyo wanaopata shida ni wananchi wanyonge,” alisema na kuongeza;
“Sisi wakubwa tunaweza kutoa rushwa na tukaishi vizuri ila watu maskini kutoa rushwa ni ngumu. Elimu yetu siyo nzuri, huduma za afya nazo hivyo hivyo kutokana na kushamiri kwa rushwa,” alisisitiza.
Alisema ni ajabu kuona vitabu vyenye makosa vinatumika katika shule mbalimbali nchini na hata ukifuatilia unabaini kuwa aliyetoa vitabu hivyo alitoa rushwa Wizara ya Elimu.
“Asilimia 40 ya dawa tunazotumia hapa Tanzania ni ‘feki’. Yaani unaandikiwa dawa ambazo hazina maana katika matibabu. Hali hii ni matokeo ya kuwa na mfumo mbovu ambao unahitaji kubadilishwa. Katiba Mpya inatakiwa kuzungumzia kiundani suala la uadilifu, kuwe na sheria zitakazozuia mtu kujinufaisha kutokana na wadhifa wake,” alisema.
Alisema rushwa ikiwa tabia ndani ya nchi, uchumi unakwama kwa sababu mapato ya Serikali badala ya kwenda kutatua matatizo ya wananchi yanakwenda katika zabuni za ovyo na kutajirisha wachache ambao nao wana tabia ya kutorosha fedha nje ya nchi.
“Mnachangia mfumo wa mapato ya Serikali lakini fedha zinatoroshwa nje ya nchi. Katika Afrika misaada inayotoka nje ni kidogo kuliko fedha zinazotoroshwa kwa rushwa. Kuna faida gani kujisifia kuwa Waziri wa Fedha kasaini mikataba wakati rushwa inatoka zaidi kuliko fedha inayoingia?” alihoji Sitta.
Alisema Tanzania imeathirika na rushwa, huku akitolea mfano jinsi wakulima wanavyokuwa na madeni hewa yanayowafanya washindwe kuendesha shughuli zao.
“Ni hatari kuwa na vijana waliokata tamaa kwa sababu ya kutokuwapo ajira. Tatizo la ajira ni kutokukua haraka kwa uchumi. Uchumi wetu utaweza kukua kwa haraka na kupunguza umaskini kama hatutaingia mikataba mibovu na tutakomesha rushwa,” alisema.
Alisema nchi ambayo viongozi wake wanapokea rushwa ni lazima itapata wawekezaji uchwara kwa sababu wanajua hata wakiboronga hakuna wa kuwafanya jambo lolote.
“Kama ni barabara watajenga tu hata kwa kiwango cha chini kwa sababu wanajua hata ikiharibika wao watakuwa wameshalipwa fedha zao na aliyetoa zabuni naye atakuwa ameshachukua chake,” alisema