Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele
ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana
na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya
Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa
11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe
kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema:
“Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge
hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani
Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya
wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo
kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba
kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe
wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari,
Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya
Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi
(hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata
kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na
kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti
chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher
Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji
Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili
za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye
mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino
Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza
sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo,
naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo
tutakapotangaziwa tena.”
Licha ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe waliendelea kupaza sauti zao wakisema kwamba walikuwa wanaburuzwa.
Wakati hayo yakitokea, kikosi cha askari wa Bunge
kiliingia ndani ya ukumbi na kusimama katika lango kuu hali iliyoonekana
kuwa ni kuchukua hadhari endapo hali ya usalama ingechafuka.
Baada ya tamko la kuahirisha mkutano, askari hao
waliingia moja kwa moja hadi alipokuwa ameketi Jaji Warioba na
kumsindikiza hadi nje na jitihada za waandishi wa habari kumfuata ili
kupata maoni yake hazikufanikiwa.
Kilichofuata baada ya hali hiyo ni kurushiana
maneno kwa baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Ave Maria Semakafu ambaye nusura
azipige kavukavu na mjumbe mwingine ambaye jina halikuweza kupatikana
mara moja.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe akiwamo Waziri wa
Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani waliamulia ugomvi
huo kabla ya kuwa mkubwa.
Wajumbe walionekana kukaa katika vikundi ndani ya
Bunge huku wakijadiliana juu ya kilichotokea wakati Sitta, Katibu wa
Bunge, Yahaya Khamis Hamad na msaidizi wake, Dk Thomas Kashililah wakiwa
katika kikao cha faragha.
Baada ya kujadiliana kwa nusu saa, Hamad akiwa
ameongozana na Dk Kashililah, alirejea katika ukumbi wa Bunge na
kuwataka wajumbe kutawanyika hadi hapo watakapojulishwa.
Hali hiyo iliibua kelele kutoka kwa wajumbe
wakitaka kujua iwapo waondoke katika maeneo ya Bunge au la. Hamad
alisisitiza kwamba warejee nyumbani hadi hapo watakapojulishwa.

No comments:
Post a Comment