Sunday, 16 March 2014

Tunahitaji kubadilika ili kuondoa umaskini

Nakumbuka nilipokuwa bado kijana katika mkoa nilioishi kulikuwa na matajiri kadhaa ambao sisi tuliwaona wametuzidi. Wengine walikuwa jamaa zetu, hivyo kuwafahamu kwa karibu zaidi namna walivyokuwa wakiendesha maisha yao na namna walivyokuwa wakifurahia maisha yao ya kutokukosa vitu vidogo vidogo.
Sehemu kubwa zaidi ya matajiri hao sasa hawapo tena katika hali hiyo ya kuwa navyo. Wengi wao sasa ni wahitaji, wakiishi maisha ya kubangaiza. Tukiwaacha wao hata sisi wengine japo siyo matajiri, lakini huenda tumewahi kushika ‘vipesa’ wakati fulani, lakini pesa hizo zikashindwa kabisa kubadilisha maisha yetu.
Hali hii inahitaji kujitafakari kwani haina maana kuzungumzia nchi kujitoa katika umaskini wakati watu wake hawana mpango wa kujitoa katika umaskini huo. Tujiulize, inakuwaje tunaendelea kuwa maskini hata pale ambapo tunapata fursa ya kuwa na fedha?
Majibu kwa swali hili yapo mengi, lakini leo tuangalie yale yanayoendeana na tabia.
Wengi wetu tuna tabia ya kutokuweka akiba. Tabia hii wanayo wakulima, wafanyakazi hata wafanyabiashara. Mtu akibarikiwa kuwa na ziada ya pesa, basi badala ya kufikiria namna pesa hizo zitakavyozalisha zaidi, pesa hizo zitatafutiwa matumizi zaidi.
Matumizi hayo mara nyingi siyo ya kuzipeleka kwenye eneo la uwekezaji ili mtu apate faida zaidi bali ni kwenye eneo la ulaji. Kwetu sisi pesa zaidi maana yake ni sherehe zaidi, ununuzi zaidi na mbwembwe nyingine nyingi zisizokuwa na tija. Mwishowe ziada yote iliyopatikana inayeyuka na kumrudisha mtu katika hali ile ile aliyokuwa nayo kabla ya fedha kumtembelea.
Hakika hii inahuzunisha; hebu fikiria leo mtu anawakaribisha kwenye sherehe ya ubatizo wa mwanawe ambayo inakuwa kubwa kuliko hata ya Tanzania kufikisha miaka 50, halafu kesho mtu huyo huyo anakugongea na kukuomba au kukukopa fedha ya kununulia unga wa ugali.
Yanatupata haya kwa sababu fedha inatuwasha pale inapokuwa mikononi mwetu. Wakati wenzetu wanachambua faida na hasara watakazozipata kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali, sisi tunachambua kicheko tutakachokuwa nacho katika matanuzi ambayo hata kuyapanga hatupangi bali yanakuja hapo hapo baada ya kupata fedha.
Siamini kama kweli mtu alipanga kuwajengea vimada nyumba bora za kuishi halafu yeye na familia yake wakakosa sehemu ya kuishi. Naamini fedha zilipokuwa mkononi zilimtia upofu na zilimharibu akili yake, hata akatenda hayo. Tumewasikia wale waliopata ufahamu baada ya kufilisika na wakataka kuzimiliki nyumba hizo bila mafanikio.
Wao wanateseka kwa kukosa makazi, lakini wale waliowapa starehe za muda wanaishi katika nyumba za kifahari. Hata kama makazi yapo hizo fedha si zingewekezwa kwenye maeneo yanayozalisha fedha zaidi?
Uzalishaji huo si ungemwezesha sasa mtu kuishi uzee wake mwema? Uzee ambao mtu angekuwa anatumia muda mwingi sasa kuwaombea na kuwabariki watoto wake, badala ya kila siku kuwalaani kwa madai kwamba hawamjali.
Tabia nyingine inayotuvuruga sana ni ya kujionyesha. Katika kujionyesha huko mtu ananunua au anajenga, hata kile ambacho hana sababu nacho. Mtu alikuwa na friji yake inayomtosha kwa matumizi ya nyumbani kwake leo fedha imemtembelea basi atakwenda kununua friji kubwa, utafikiri anataka kuweka kuku wa kuuza.
Friji hiyo kubwa inaishia kuwekwa maji, atajenga nyumba kubwa zaidi yenye ghorofa mbili, halafu vyumba vingine vinaishia kuwa makazi ya mende. Inasikitisha sana pale watu wanapokuwa wamezeeka halafu nyumba hiyo ipo mahali ambapo familia haiwezi hata kubadilisha matumizi ya nyumba hizo yaani badala ya kuishi, labda wafanye hoteli au wapangishe.
Utakuta mtu kaishiwa kabisa, lakini hajui jinsi ya kuitumia nyumba hiyo ambayo kwa sasa inatumika kwa asilimia 10 tu. Ukijiuliza kwa nini mtu aliwekeza kwenye jumba kama hilo, jibu utakalopata ni alitaka watu wajue kwamba naye ana fedha.
Tunahitaji kweli vitu vyote tunavyovinunua? Hakuna siku tunajutia viatu na nguo nyingi tulizozijaza katika nyumba zetu, ambazo kwa kuwa zimepitwa na wakati zimejaza makabati yetu na hatuna za kuzifanyia?
Hivi kweli mtu unakosa hata fedha ya kununulia dawa, lakini ndani ya nyumba una vitu chungu mzima ulivyovinunua kwa kujionyesha na sasa havikuzalishii chochote, hiyo kweli ni akili?
Tunapenda sana kuwaiga wazungu, nafikiri tuwaige pia tabia yao ya kupenda kuweka akiba kwa ajili ya kuwekeza au kwa ajili matumizi ya baadaye. Tujifunze pia kufanya vitu kwa kiasi, tuache tabia ya kujionyesha, kwani tabia hii inatufanya tusifikiri vizuri katika kuwekeza fedha tuzipatazo.
Tusipobadilika, tutaishia kama tulivyo; leo mtu anapigiwa makofi kwa kuvaa vizuri, kutembelea magari ya kifahari, kuishi kwenye nyumba ya kifahari na kufanya sherehe kubwa kubwa halafu baada ya muda mfupi, anakuwa omba omba au kopa kopa asiyerudisha fedha anazokopa.
Hii haikubaliki hata kidogo. Tujizoeshe tabia mbadala nayo ni ya kuweka akiba na kununua vitu kwa mahitaji siyo kwa fahari.

No comments: