Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta
amesema kushamiri kwa vitendo vya watu wachache kujitajirisha na wengine
kununua uongozi, kunatokana na Katiba ya sasa kutokuwa na meno ya
kupambana na rushwa na ufisadi.
Amesema vitendo hivyo vitakoma kama nchi ikiwa na
Katiba nzuri, itakayowezesha kutungwa kwa sheria nzuri zitakazowabana
mafisadi na watoa rushwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili nyumbani kwake Dodoma juzi, Sitta alisema: “Siridhiki na Katiba ya
sasa inavyoshughulikia rushwa na ufisadi. Katika nchi yetu inaonekana ni
rahisi mtu kujitajirisha kwa kutumia cheo chake na baada ya hapo
kununua uongozi. Katika nchi maskini jambo hili ni hatari kubwa.”
Aliongeza, “Katiba lazima ielekeze kwamba iko
tofauti kati ya kufanya biashara na kuongoza watu. Haiwezekani ukawa na
biashara kubwa zinazochukua zabuni za Serikali na ukaendelea kuwa
kiongozi wa Serikali, nchi nyingi zimetenganisha mambo haya.”
Alisema rushwa ni hatari na inaweza kusababisha
nchi kukosa amani, kwa sababu wananchi maskini watafika mahali hawataona
uhalali wa maisha ya watu wanaowaongoza.
“Nimeipenda Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, imeeleza wazi kuhusu suala la uadilifu hivyo
lazima zitungwe sheria zitakazowabana watu kutokutumia madaraka yao
vibaya,” alisema.
Sitta ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, alisema ni hatari kuwa na mfanyakazi wa Serikali mwenye
kampuni binafsi ambayo inapewa tenda za Serikali.
“Sisemi kuwa watu wasiwe wafanyabiashara, mtu
akiamua kuhudumia umma anatakiwa kuweka mali na biashara zake katika
mfumo wa kuendesha biashara hiyo bila yeye kuwa mhusika wa moja kwa
moja. Hivyo, ndivyo wanavyofanya mataifa kama Uingereza na Marekani,”
alisema Sitta.
Alisema taarifa nyingi za maendeleo katika nchi za
Afrika zinaeleza kuwa nchi za bara hilo zinakwama kupiga hatua
kimaendeleo kwa sababu ya rushwa.
“Rushwa inajenga mtandao ambao unashuka hadi ngazi
za chini. Watumishi wa chini wakiona mikataba mibovu inawanufaisha
wakubwa nao hutafuta mianya katika maeneo yao. Ikiwa hivyo wanaopata
shida ni wananchi wanyonge,” alisema na kuongeza;
“Sisi wakubwa tunaweza kutoa rushwa na tukaishi
vizuri ila watu maskini kutoa rushwa ni ngumu. Elimu yetu siyo nzuri,
huduma za afya nazo hivyo hivyo kutokana na kushamiri kwa rushwa,”
alisisitiza.
Alisema ni ajabu kuona vitabu vyenye makosa
vinatumika katika shule mbalimbali nchini na hata ukifuatilia unabaini
kuwa aliyetoa vitabu hivyo alitoa rushwa Wizara ya Elimu.
“Asilimia 40 ya dawa tunazotumia hapa Tanzania ni ‘feki’. Yaani
unaandikiwa dawa ambazo hazina maana katika matibabu. Hali hii ni
matokeo ya kuwa na mfumo mbovu ambao unahitaji kubadilishwa. Katiba Mpya
inatakiwa kuzungumzia kiundani suala la uadilifu, kuwe na sheria
zitakazozuia mtu kujinufaisha kutokana na wadhifa wake,” alisema.
Alisema rushwa ikiwa tabia ndani ya nchi, uchumi
unakwama kwa sababu mapato ya Serikali badala ya kwenda kutatua matatizo
ya wananchi yanakwenda katika zabuni za ovyo na kutajirisha wachache
ambao nao wana tabia ya kutorosha fedha nje ya nchi.
“Mnachangia mfumo wa mapato ya Serikali lakini
fedha zinatoroshwa nje ya nchi. Katika Afrika misaada inayotoka nje ni
kidogo kuliko fedha zinazotoroshwa kwa rushwa. Kuna faida gani kujisifia
kuwa Waziri wa Fedha kasaini mikataba wakati rushwa inatoka zaidi
kuliko fedha inayoingia?” alihoji Sitta.
Alisema Tanzania imeathirika na rushwa, huku
akitolea mfano jinsi wakulima wanavyokuwa na madeni hewa yanayowafanya
washindwe kuendesha shughuli zao.
“Ni hatari kuwa na vijana waliokata tamaa kwa
sababu ya kutokuwapo ajira. Tatizo la ajira ni kutokukua haraka kwa
uchumi. Uchumi wetu utaweza kukua kwa haraka na kupunguza umaskini kama
hatutaingia mikataba mibovu na tutakomesha rushwa,” alisema.
Alisema nchi ambayo viongozi wake wanapokea rushwa
ni lazima itapata wawekezaji uchwara kwa sababu wanajua hata
wakiboronga hakuna wa kuwafanya jambo lolote.
“Kama ni barabara watajenga tu hata kwa kiwango
cha chini kwa sababu wanajua hata ikiharibika wao watakuwa wameshalipwa
fedha zao na aliyetoa zabuni naye atakuwa ameshachukua chake,” alisema

No comments:
Post a Comment