Sunday, 23 March 2014

Tanzania inahitaji watumishi wafanyakazi wa aina gani?

Mwanzo wa maendeleo ya kweli kwa nchi yoyote duniani kama historia
inavyodhirisha, ni pale watumishi na wafanyakazi wanapobadilika na kujitambua kutokana na kuwepo sera na mifumo ya usimamizi nautendaji kazi inayotambua nafasi, stahili au haki, wajibu na majukumu ya kila mtu katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Kwa jumla, wataalamu wa nadharia na tasnia ya rasilimali watu wanasema
Kwamba, kazi kubwa ya wanaosimamia rasilimali watu ni kuhakikisha kila shughuli katika taasisi husika anapatikana mtu sahihi, mwenye elimu na ujuzi sahihi, wakati sahihi na atakayepewa kazi sahihi ili aifanye kwa usahihi pia.
Hata hivyo, rasilimali watu kama somo ni somo pana na katika miaka ya leo imeanza kuaminika kwamba kiongozi wa taasisi anayepwaya katika elimu na ujuzi wa rasilimali watu hawezi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama ilivyo kwa yule aliyesheheni nidhamu na nadharia husika.
Kazi ya kusimamia au kuongoza rasilimali watu inaanzia na mipango, ugawanyaji kazi na wajibu, utafutaji watu kujaza nafasi zilizo wazi, mahojiano ya kutathmini sifa na uwezo wa mtu kama unaendana na jinsi alivyo na uchaguaji miongoni mwa walioomba kazi idadi ya watu wanaotakikana kwa kazi fulani.
Menejimenti ya rasilimali watu inajumuisha pia mambo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi, uchukuaji wa hatua za kinidhamu, afya na usalama wa wafanyakazi pamoja na mikakati yote inayoihakikishia taasisi kuendelea hata kama waliopo kwa wakati huo wataondoka au kufa.
Kampuni au idara ya Serikali au taasisi iwayo kwa hiyo ina maana kwamba utendaji kazi wake na sifa yake aghalabu, utatokana na aina ya watu walioajiriwa. Ukiajiri watu wa ovyo na utendaji wa taasisi husika nao pia utakuwa ni wa ovyo. Ukiajiri watumishi au wafanyakazi wazuri basi uwezekano wa taasisi hiyo kuwa na utendaji mzuri nao ni mkubwa pia.
Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba wale wote waliopewa dhamana ya kuajiri wafanyakazi au watumishi wapya lazima wawe wanaojua kila linalopaswa kujulikana juu ya mbinu zote zinazotumika katika nadharia na utendaji kazi katika tasnia ya rasilimali watu ili kuhakikisha kwamba watumishi watarajiwa wote wanapepetwa kwa namna ambayo chuya au chafu wote unaondolewa na panabakia nafaka nzima na safi.
Hili linahitaji kwa kiasi kikubwa ugwiji katika masuala ya saikolojia na sosholojia. Elimu zinazoweza kuwang’amua watu walivyo na watakavyokuwa kwa kuangalia historia yao ya kimaisha na kikazi.
Polisi wanapolalamika kwamba wameajiri askari polisi ambao wanashirikiana na majambazi kuwaibia na kuwadhuru wananchi ilhali tunajua kazi ya polisi inatakiwa iwe nini, hapo kunaonyesha kuna walakini mkubwa katika namna wafanyakazi katika eneo husika awanavyochambuliwa na mwishowe kuajiriwa.
Mamlaka za kodi na mapato zinavyolalamika kuna wafanyakazi walioiva na kupevuka kwa rushwa, pia tatizo ni hilo hilo, yaani, jinsi watumishi wao wanavyopatikana na jinsi wanavyochujwa ili wabakie wale walio safi.
Benki na sekta ya fedha inapolalamika juu ya wizi kushamiri katika mabenki kwa ushirkiano kati ya wafanyakazi wa taasisi za kifedha na wafanyabiashara au hata wezi ni ishara kwamba kuna ajira mbovu katika sekta husika.
Tunapolalamika juu ya utendaji kazi katika hospitali, shuleni, vyuoni na kadhalika jambo hili pia huwa ni dalili ya kuwepo kwa walakini katika masuala ya haki na wajibu wa watumishi wahusika.
Tumalizie kwa kusema kwamba rasilimali watu ambayo nchi inabahatika kuwa nayo haitoki juu mbinguni. Rasilimali hiyo inatokana na jamii iliyopo katika nchi husika.
Hivyo ni vigumu kuona kama jamii yenyewe inajikita katika uongo, ubabaishaji, uzembe, ubinafsi, uvivu, umbeya, maneno bila vitendo, kula usichokipanda na ila za kila aina, ni kwa vipi jamii hiyo inaweza kuwa na wafanyakazi wanaohitaji kuiondoa jamii yao kutoka kwenye hatua ya chini kabisa kimaendeleo na kuipeleka kwenye hatua ya juu kabisa kimaendeleo!

No comments: