Wapo wanaofuata mkumbo wa kusoma mchepuo (combination)
fulani kwa sababu marafiki zao wengi wameuchagua mchepuo huo. Aidha,
wapo wanaolazimisha kusoma masomo magumu yaliyo nje ya uwezo wao
kiakili.
Kwa mfano, unaweza kupata alama C katika mtihani wa Hisabati (Basic Mathematics), lakini alama hiyo siyo tiketi pekee ya kuchagua kusoma masomo yenye hesabu za kiwango cha juu (Advanced Mathematics).
Waliofeli nao?
Kama ilivyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania,
asilimia 78.91 ya wahitimu wamepata daraja la nne na sifuri. Ni dhahiri
kuwa wanafunzi hawa hawana sifa ya kujiunga na kidato cha tano.
Hata hivyo, huo ndiyo uwe mwisho wa safari
ya kusaka elimu kwa vile tu umefeli? Makala haya yanajaribu kutoa
mapendekezo mbadala yanayoweza kutumiwa na wanafunzi ili kujiendeleza
zaidi kielimu?
Kwanza ieleweke kutokuchaguliwa kidato cha tano au
kufeli kidato cha nne si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu
ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.
Uzoefu unaonyesha hapa nchini kuna watu wengi
baadhi yao leo ni maprofesa maarufu waliowahi kufeli katika madaraja
fulani ya kielimu siku za nyuma, lakini kwa kuwa tu walikuwa na dhamira
ya dhati na kutoa uamuzi sahihi, waliweza kujiendeleza na kufika kiwango
hicho cha elimu kinachotamaniwa na kila mtu.
Nikupe siri moja ninayoifahamu kuhusu wasomi hawa,
baadhi yao waliwahi kuwa walimu wangu pale Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam. Hawa pamoja na wengine kuamua kuanza maisha ya familia au kikazi
lakini walijiendeleza kupitia mfumo usio rasmi.
Unaweza kuihuisha ndoto yako ya kupata elimu kwa kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo na ndiyo maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi.
Rudi tena darasani. Kuna shule nyingi za sekondari
zenye programu maalumu kwa ajili ya watu wanaorudia mitihani ya kidato
cha nne tena kwa bei rahisi.
Zitafute shule hizi ila kuwa makini na vituo vinavyoitwa kwa Kiingereza ‘Tuition Centers’ ambavyo vingi vinajali masilahi kuliko ubora wa elimu.
Chunga jambo hili! Kuna mtindo wa wanafunzi
wanaofeli kidato cha nne na kuamua kuingia kidato cha tano huku
wakirudia mitihani yao. Hawa wanalazimika kusoma masomo ya mitihani
wanayoirudia huku wakisoma pia masomo mapya ya kidato cha tano.
Huku ni kujidanganya, kwa mtindo huu, mwanafunzi husika hawezi
kusoma kwa undani masomo ya kidato cha tano badala yake atakuwa anasoma
‘kimtego mtego’ ili afaulu tu mitihani ya ndani.
Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani
za ngazi ya cheti. Kusomea cheti siyo kuonekana mjinga, kwanza una
uhakika wa kuajiriwa au kujiajiri. Kwa mtu mwenye ndoto ya kusoma zaidi,
kipato cha ajira yako ndicho unachoweza kukitumia kujiendeleza zaidi.
Upo mfano mzuri wa walimu wa shule za msingi
waliosomea ualimu kwa ngazi ya cheti. Wengi hujiendeleza kwa kurudia
mitihani na hatimaye kufika vyuo vikuu.
Siyo ualimu pekee, kwa mujibu wa mfumo wa elimu
nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa kozi za msingi kwa
wahitimu wa kidato cha nne wakiwamo waliopata angalau daraja la nne.
Unachofanya ni kusomea cheti cha msingi kwa mwaka
mmoja, kisha unaendelea kwa kusoma tena cheti cha juu kabla ya kupata
fursa ya kusoma stashahada.
Kwa walio makini mlolongo huu wa elimu unaweza
kukufikisha mbali. Unaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya
kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi hawa kwa sharti la
kuwa vimesajiliwa na Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (NACTE).
Fursa nyingine inayotumiwa na baadhi ya wanafunzi
wanaoishia kidato cha nne ni kusoma masomo ya ufundi katika vyuo
vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya VETA
wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza
zaidi kielimu.
Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya VETA umekua na
kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira iwe
ajira binafsi au ajira rasmi. Kwa mfano, hivi sasa VETA inaendesha kozi
katika sekta za madini, utalii, teknohama na nyinginezo muhimu zama za
sasa.

No comments:
Post a Comment