Tuesday, 26 February 2013

HILI SUALA LA UDINI LITATUFIKISHA WAPI NDUGU WATANZANIA?


HAKI YA KUCHINJA Waislamu, Wakristo wapigana mapanga *Mchungaji auawa kinyama, saba wajeruhiwa *Kisa ng'ombe, mbuzi waliochinjwa na Mkristo

SAKALA la nani mwenye haki ya kuchinja kati ya Wakristo na Waislamu, jana lilichukua sura mpya katika Kijiji cha Buselesele, Wilaya ya Chato, mkoani Geita baada ya kutokea vurugu kubwa
na kusababisha mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste,
Mathayo Kachila (48) na watu wengine saba kujeruhiwa.

Vurugu hizo zilitokea jana kijijini hapo kuanzia saa tatu asubuhi katika Soko Kuu la Buselesele, baada ya mtu mmoja ambaye inadaiwa ni Mkristo, kuchinja ngombe mmoja, mbuzi wawili.

Inadaiwa kuwa, Mchungaji Kachila alishambuliwa na kundi la Waislamu jirani na msikiti wakati akiwasindikiza wageni wake
baada ya vurugu hizo kupamba moto.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Paul Kasagabo, alithibitisha taarifa za kifo hicho na kuongeza kuwa, watu wengine saba walijeruhiwa vibaya kutokana na vurugu hizo.

“Chanzo cha vurugu ni mwananchi mmoja ambaye inadaiwa ni Mkristo aliyefahamika kwa jina moja la Obadia, kuchinja ngo'mbe mmoja, mbuzi wawili na nyama hizo kuuzwa katika bucha ambayo nje ilifungwa kitambaa chenye ujumbe unaosema 'Yesu tena bucha', ambayo anaimiliki hivyo hali hiyo iliwachukiza Waislamu.

“Katika vurugu hizi, bucha ya mtu anayelalamikiwa ilivunjwa pamoja na dula lililokuwa likitoa huduma ya M-Pesa na mwili
wa Mchungaji Kachila umehifadhiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Geita,” alisema.

Kamanda Kasagabo aliongeza kuwa, hadi sasa hakuna mtu ambaye amekamatwa kutokana na vurugu hizo ila jeshi hilo linaendelea kuwasaka wahusika ili waweze kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Ernest Nkwabi, alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa Mchungaji huyo hospitalini hapo na majeruhi saba.

“Tumepokea mwili mmoja wa marehemu na majeruhi saba ambao kati yao, wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya.

“Mwili wa marehemu una majeraha ya kukatwa na panga mara nne kichwani, mkono wa kushoto na kiganga chake chote kukatwa katwa hivyo kusababisha avuje damu nyingi,” alisema.

Aliwataja majeruhi waliopelekwa Hospitali ya Bugando kuwa ni Ramadhan Paschal (36), aliyejeruhiwa vibaya katika fuvu la kichwa upande wa mbele na Said Ntamopagafe (47) ambaye amejeruhiwa mguu wa kulia kwa kukatwa mapanga.

Alisema majeruhi wawili Vicent Raymond (18) na Yassin Rajab (56), bado wamelazwa hospitalini hapo wakiendelea na matibabu
na wengine wawili walitibiwa na kuruhusiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, alisema vurugu hizo zimedhibitiwa kijijini hapo na hali ya utulivu kurudi kama kawaida ambapo wananchi wanaendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
Share on linkedin Share on facebook Share on twitter Share on email More Sharing Services 0

CHADEMA wambana JK tatizo la udini


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi, ameitaka Serikali iwaeleze Watanzania kwanini inafumbia mambo tatizo la udini linaloendelea nchini.


Bw. Arfi aliyasema hayo mjini Dodoma jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mwanga Bar, Kata ya
Uhuru na kusisitiza kuwa, tatizo hilo linaweza kuiweka nchi
mahali pabaya kwa siku za usoni.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, bado haijachukua hatua zozote ili kuepusha machafuko yanayoweza
kutokea na kusababisha amani iliyopo kuwa historia.

“Awali Chama cha Wananchi CUF kilionekana cha Waislamu hivyo Wakristo wakakiogopa na kukimbia udini...hivi sasa CCM inadai CHADEMA ni chama cha Wakristo.

“Kutokana na propaganda hizi, tayari yameanza kutokea machafuko ambayo Wakristo na Waislamu wanapigana mapanga, tunamtaka Rais Kikwete alieleze Taifa kwanini chama chake kinasimamia
zaidi masuala ya udini,” alisema Bw. Arfi.


Aliongeza kuwa, baada ya mbinu za CCM kudai CHADEMA ni chama cha kikabila, sasa wameibuka na mbinu mpya wakidai
chama chao cha Wakristo jambo ambalio si kweli.

Alisema hivi sasa, CCM inatumia mamilioni ya fedha za wananchi katika mambo yasiyo na tija kwa jamii na Taifa badaya ya fedha hizo kuelekezwa katika sekta ya elimu ili kuongeza ufaulu wa
wanafunzi kwa lengo la kuongeza wataalamu.

“Tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika katika sekta ya elimu, zinasema uwekezaji mdogo katika sekta hii imechangia watoto wengi kuanza kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma
wala kuandika lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho Taifa, Bw. Benson Kigaila, aliwataka viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2012.

Ole wenu mnaoona dini ni bora kuliko Mungu!

CHRISTIANS and Muslims in Tanzania can be partners in building a society shaped by the values taught by God: tolerance, justice, peace and concern for the poorest and the weakest.” Hiyo ni kauli ya kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani wakati huo, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II aliyoitoa kwa Watanzania alipozuru nchini Septemba mwaka 1990.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, ujumbe huu ulitaka kumaanisha kwamba, “Wakristu na Waislamu wa Tanzania wanaweza kuwa wadau katika kujenga jamii yenye maadili ya Kimungu; uvumilivu, haki, amani na kuwajali maskini na wanyonge.”

Nimelazimika kuanza na nukuu hii ili kuwaonyesha tu wafuasi wa kweli wa dini hizi jinsi walivyo na jukumu kubwa katika kuunda jamii yenye uvumilivu na mshikamano wa dhati ambao ndio msingi wa namna Mungu anavyotaka tuishi.

Kwa ufahamu mdogo nilionao kuhusu Uislamu (ninaweza kusahihishwa katika hili), ni kwamba jina tu lenyewe linamaanisha unyenyekevu na zaidi sana Uislamu ni dini ya amani na ukiwasikiliza baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu wanasema Waislamu pia wamefundishwa namna ya kuishi na watu wasio wa dini yao kwa amani.

Na kwa kweli ziko baadhi ya hadithi zinashuhudia kuwa hata Mtume Mohamad (S.A.W) alipata msaada kwa namna moja ama nyingine kutoka kwa Wakristo na watu wengine wasio Waislamu, wakati anahamia Madina toka Makka.

Lakini pia katika Ukristu, upo msingi mmoja mkubwa wa imani yao, wanatakiwa wawapende jirani zao kama nafsi zao na zaidi sana wanatakiwa wawapende hata adui zao kwa sababu upendo ndiyo amri yao kuu.

Yako masimulizi katika Injili kwamba Bwana Yesu aliwaambia wale wote wanaomfuata na kuamini katika yeye kuwa wanaweza kuwa na uwezo hata wa kuhamisha milima, lakini kama wanatindikiwa na upendo ni kazi bure, utaona ni jinsi gani upendo ulivyo sehemu muhimu ya imani hii.

Bahati mbaya tuliyonayo katika jamii yetu kwa sasa, tumeanza kutumia dini hizi badala ya kuwa daraja la kutuunganisha, kutumia tofauti zetu kama njia ya kutuweka pamoja zaidi, sasa tunatumia tofauti za dini zetu kama sababu ya kuwa maadui na kujenga matabaka hasimu katika jamii yetu.

Kipo kitu kimoja ambacho viongozi na wafuasi wa imani hizi wanatakiwa watambue kuwa ni mpango wa Mungu wanayesema wanamwabudu, kutuumba tukiwa tunatofautiana.

Jinsi ambavyo tunatofautiana sura zetu na mawazo yetu ndivyo ambavyo tunatakiwa tutarajie tutatofautiana katika mitazamo ya mambo mbalimbali ikiwemo ya imani. Hili Mungu wanayemwabudu analijua na ndiyo maana kuna mbingu na jehanamu.

Sasa kama Mungu mwenye kuwaumba Binadamu hawa pamoja na uwezo wake wote usio na mipaka, lakini amewaacha binadamu hawa hawa waamue kuishi maisha watakayo kwa utashi wao binadamu mwingine ni nani mpaka atake watu wote waamini kama anavyoamini yeye?

Wataalamu wa elimu ya genetic wanatuambia kuwa ili kuwe na mtu ambaye anafanana na wewe kwa kila kitu, yaani sura, mawazo unayowaza wewe na yeye awaze hivyo na muwe na mtazamo unaofanana kwa kila kitu, ni lazima mzaliwe watoto laki tatu katika familia ya baba mmoja na mama mmoja, mtoto wa laki tatu na moja ndiye atakuwa anafanana kwa kila kitu na yule mzaliwa wa kwanza wa familia hiyo.

Hapa tunaweza kuona ni jinsi gani haiwezekani kutaka kufananisha mitazamo, kwa kuwa ni Mungu pekee na mwenye uwezo wa kila jambo chini na juu ya jua aliyeamua kutuwekea tofauti hizi na sisi hatuna namna wala uwezo wa kufanya vinginevyo, tunachoweza kufanya ni kutaka kuziishi tofauti hizo kwa manufaa yetu na kuifanya Tanzania iwe sehemu nzuri ya kuishi kila mmoja wetu apendavyo bila kuingilia uhuru wa mtu.

Kwa hakika ni uendawazimu na ujinga wa kiimani kutaka au hata kuthubutu tu kuwaza mikakati na mbinu za kuwafanya watu wote wawe Wakristu au Waislamu, hilo halitawezekana kwa sababu ni Mungu aliyedhamiria kutufaya tutofautiane namna hii, hizi tofauti zetu hatukuchagua wenyewe, tumejikuta kwa njia mbalimbali tuna mitazamo hiyo inayokinzana ambayo siyo lazima itufanye tupigane.

Dini hizi ni kama zinataka kuharibu taifa hili kama tu ambavyo dini zimeharibu mataifa mengine mengi yaliyotukuka kwa kuwa na amani na mshikamano na nguvu za kiuchumi.

Madai yanayoendelea sasa ya nani ana haki ya kuchinja kuliko mwingine, yanaweza kuwa ya msingi kulingana na imani za watu na hapa sitaki kuingia katika mtego wa kupuuza imani ya mtu, lakini hivi waumini hawa wamejiuliza ni kwa kiasi gani maisha ya mtu yana thamani kuliko hiyo nyama wanayogombania kuchinja?

Haiwezekani kwamba, Waislamu na Wakristu ambao hawazidi asilimia 50 ya Watanzania wote wanataka ndiyo wawe madereva wa nchi hii, wapo pia Watanzania wenye haki zao ambao wana haki ya kuishi kwa amani na hapa ndiyo wajibu wa Serikali unapoingia.

Katika hiki, Serikali haiwezi kukwepa wajibu wake katika damu za Watanzania zilizomwagika. Kwa sababu ni kweli kwamba, Serikali imetajwa legelege mno katika kusimamia mambo ya msingi ya taifa, hatimaye tumejikuta tunaliingiza taifa katika hali ambayo kama tukipuuzia kuchukua hatua za makusudi kulimaliza hili, tutaingia katika zama ambazo tunaweza tusitoke huko.

Tumeshindwa kuvumiliana kwa sababu ya vibaraka na uzembe wa Serikali kutotambua wajibu wake, ama imeamua kuupuuza kwa makusudi na sijui ni kwa maslahi ya nani.

Ole wetu tusipochukua hatua mujarabu kwa wakati na wananchi na wafuasi wa dini hizi wanaoshabikia mambo kama vile Yanga na Simba, wasifikiri hii ni ngoma ya kitoto.

Nchi hii ikilipuka wote tutakuwemo bila kujali nani anamwabudu nani kwa imani gani.

Yale tuliyozoea kuyaona kwenye mchakato wa Katiba, watu wanagombania kila mtu awe na mamlaka juu ya Katiba dhidi ya wenzao, hili nao lilikuwa Salamu ya jinsi gani tumefika hapa, kila jambo siku hizi tunahitaji kuliangalia kwa jicho la dini kwa manufaa ya dini zetu, hili halitatufikisha siyo tu tuendako kama taifa, bali hata wanaomwamini hawatafika kwa Mungu wao kwa mtindo huu.

Hili hata kwenye haki za kikatiba pia, hatuwezi kuwa waumini safi wa dini zetu kama tunapoandika Katiba kila mtu anataka imtambue yeye zaidi kuliko wengine, wako watoto wa mitaani, hawa wanatakiwa Waislamu na Wakristu wanaokwenda kutoa maoni kwenye Tume ya kuratibu maoni ya Katiba wawatetee.

Wako watoto wadogo wanaodhulumiwa haki, hawa hawawezi kusema kwenye Katiba, wakuwasemea ni sisi Waislamu na Wakristu tunaomjua Mungu kwa sababu Mungu kawaweka hawa katikati yetu ili aone sisi aliotujalia zaidi kuliko wao, tunatumia vipi neema hizo kwa manufaa ya wenzetu wasiojiweza.

Tuzifanye dini zetu ziwe sehemu ya kutupatanisha kwa msingi wa uvumilivu kwa sababu Mungu mwenyewe mwenye dini hizi tunazotumia kumwabudu ni mvumilivu kuliko tunavyoweza kufikiri.

Jaribu kujiuliza wewe unayetaka dini yako tu ndiyo iwe bora kuliko ya wengine, unadai huwezi kuvumilia wenye imani tofauti na wewe, hebu fikiria Mungu angekuwa siyo mvumilivu hata kwa nukta moja.

Wewe kiongozi wa dini unayehamasisha watu wa imani yako wawachukie na wasifungamane na wengine, jiulize kwa siku moja unawaza na kufanya mangapi ambayo Mungu angeamua kukushughulikia hapo hapo ungeweza kudumu kwa muda gani?

Mungu anavyotupenda tumezungukwa na mifano mingi sana ya jinsi dini na tofauti zozote za kijamii zimesababisha machafuko katika nchi za wenzetu, lakini sijui kwanini hatutaki kujifunza.

Migogoro inayozaa vita za kidini au za kikabila huwa inaanza namna hii kwa kukosa uvumilivu miongoni mwa wanajamii, tujue kwamba hata mbuyu ulipoanza kuchipua ardhini ulikuwa mdogo na dhaifu kama mchicha, lakini baada ya muda ukawa ulivyo.

Chokochoko za kidini tunaweza kuziona ndogo na zinafanywa na wapuuzi, hivyo haziwezi kutuletea madhara na mitafaruku katika jamii.

Tutakuwa tunajidanganya, tusipokuwa macho na kuchukua hatua sasa mambo yakishashika kasi sina hakika tutakimbilia wapi, lakini walau nina hakika na jambo moja kwamba, machafuko yakianza hakuna atakayebaki salama, si Muislamu au Mkristo.

Ole wao wanaoziona dini ni bora kuliko Mungu.

Katiba mpya ifute mfumo wa ‘Westminister’ - Kujenga Umoja na Utambulisho wa Kitaifa


WAKATI tunajadili utungaji wa Katiba mpya ya Tanzania, ni vizuri tukatafakari kwanza misingi itakayotuongoza katika kuandaa maudhui ya Katiba hiyo. Katika waraka huu napenda kutoa mawazo machache kuhusiana na suala hilo. Napendekeza misingi ifuatayo:

Kujenga umoja na utambulisho wa kitaifa, Kupanua uhuru na haki za msingi za raia, kupanua demokrasia, kuweka mfumo wa uwazi wa utawala na uongozi na kudhibiti ufisadi, kuimarisha uchumi na uzalishaji, kujenga umoja na ushirikiano wa kikanda na hatimaye umajumui wa Afrika nzima.

Kabla sijajadili misingi hiyo, nizungumzie kidogo suala la mchakato wa kuandaa Katiba. Katiba ni chombo chenye mamlaka juu ya kila mtu na kila chombo katika jamii.

Katiba lazima itawale mamlaka zote kuanzia kwa Rais hadi kwa balozi wa nyumba kumi na kuishia kwa mtu binafsi. Katiba sharti itawale asasi zote kuanzia Bunge hadi mahakama, polisi, asasi za kiraia na kidini, n.k.

Ndiyo maana haifai kwa Katiba kuamuliwa na vyama vya siasa ambavyo ni vikundi vyenye maslahi maalumu ndani ya Katiba hiyo.
Kujenga Umoja na Utambulisho wa Kitaifa
Katiba yoyote ile ya nchi huwa na jukumu la kujenga utaifa na utambulisho wa Taifa linalohusika na hivyo kuchunga na kulinda usalama na uzalendo wa Taifa hilo. Ndiyo maana Katiba za mataifa mengi hutaja mipaka ya nchi, Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya/za Taifa na lugha nyingine rasmi kama zipo.

Katiba za baadhi ya nchi hutaja hata hati za maandishi za lugha yao na vipengele muhimu vya utamaduni wa Taifa, kama vile dini, mila na kadhalika. Katiba ya sasa ya Tanzania inataja baadhi ya mambo haya lakini si yote. Kwa mfano haitaji Lugha ya Taifa!

Kujenga utambulisho na utaifa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa kuweka misingi imara ya umoja inayokubalika kwa wananchi wote wa makundi na matabaka yote, kujenga uzalendo, mapenzi ya nchi na moyo wa kuwa tayari kuitetea na kuifia nchi ikibidi.

Ni wazi kwamba, suala la kuruhusu uraia wa nchi mbili au zaidi ambalo linapigiwa debe sana hivi sasa na baadhi ya watu, inabidi litazamwe kwa kuzingatia msingi huu wa uzalendo na maslahi ya Taifa: Mathalan, itakuwaje iwapo raia wa Marekani (au nchi nyingine), ambaye pia ni raia wa Tanzania, atatumwa na Rais wake wa Marekani na kupewa nyenzo zote kuja kututawala na kutekeleza matakwa ya nchi yake (ya Marekani) hapa kwetu? Utamzuiaje?

Hatusemi kwamba kiongozi asiyekuwa na uraia wa nchi ya kigeni hawezi kutumiwa na nchi hiyo kutekeleza maslahi yake katika nchi anayoiongoza. Tunawafahamu viongozi vibaraka wengi waliotumiwa hivyo. Tunachosema hapa ni kwamba, tusiwarahisishie maadui zetu mchakato wa kupata vibaraka miongoni mwetu.

Suala la utamaduni sharti lipewe uzito kikatiba, maana bila utamaduni hakuna Taifa na njia ya uhakika ya kumdhibiti na kumtawala mtu ni kumteka kitamaduni na kiakili.

Hapa suala la lugha sharti lipewe uzito unaostahiki; Lugha ya Taifa, Kiswahili ipewe nafasi muhimu kikatiba na lugha za kijamii na za kigeni tunazozihitaji zisisahaulike. Katiba itaje wazi kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na lugha rasmi ya kwanza na Kiingereza ni lugha rasmi ya pili.

Katiba ielekeze kwamba itatungwa sheria mahsusi itakayofafanua nafasi, dhima na matumizi ya lugha ya Taifa na lugha nyinginezo katika jamii.
Kupanua Uhuru na Haki za Raia
Katiba inapaswa kulinda uhuru na haki za raia ambazo ni pamoja na haki za kuishi, kuheshimiwa kama binadamu, kufanya kazi na kupata malipo ya haki kwa kazi hiyo, kupewa pensheni ya uzeeni, kujumuika, kusafiri, kuishi popote, kuabudu au kutokuabudu.

Haki za lugha na utamaduni pia zinahusika hapa. Na haki hizo lazima ziwe ni kwa raia wote bila kujali jinsi, kabila, rangi, dini, cheo, umri au nasaba.

Katiba ya sasa inatoa haki hizo kwa kiasi fulani. Katiba ijayo ingefaa isisitize na kufafanua zaidi haki hizi za msingi.
Kumtaja Mungu katika Katiba
Hapa tunaweza kueleza kuwa pendekezo la Jaji Mstaafu Barnabas Samatta, katika kongamano moja kuwa Katiba mpya itaje Mwenyezi Mungu halikubaliki kwa sababu linakwenda kinyume na uhuru wa kuabudu tunaouzungumzia.

Kwa kuwa Katiba tayari inatoa uhuru wa kuabudu, hakuna sababu ya kuufunga uhuru huo kwa kuuhusisha na imani fulani maalumu, zile zinazozingatia dhana ya Mungu. Ni vyema Katiba iendelee kutofungamana na imani ya dini yoyote.
Kupanua Demokrasia
Katika ulimwengu wa sasa na ujao, utawala wa kidemokrasia hauepukiki. Hivyo tunahitaji Katiba inayotambua haki na haja hiyo ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Demokrasia tunayozungumzia hapa ni demokrasia pana inayojumuisha wananchi wote wa makundi yote. Hatuzungumzii demokrasia ya vyama vya siasa tu.

Katiba yetu ya sasa kwa kiasi kikubwa inajikita katika demokrasia ya vyama badala ya demokrasia ya Umma. Labda hili linahitaji ufafanuzi zaidi.

Miaka kadha iliyopita makundi mbalimbali ya wanasiasa, yalianza kufanya kampeni ya kutaka majimbo ya uchaguzi yaongezwe ili kuimarisha uwakilishi na demokrasia.

Tulishuhudia madiwani wa halmashauri mbalimbali, wakipitisha maazimio ya kuongeza majimbo ya udiwani na ubunge. Baadhi ya wabunge na vyama vyao vilevile walipendekeza majimbo mapya yaanzishwe.

Kampeni hiyo ilifanikiwa kwa kiasi fulani na majimbo mapya kadha yaliundwa, japo ilitolewa tahadhari kuwa jengo la sasa la Bunge mjini Dodoma halina nafasi ya kuongeza wabunge wengi. Msingi wa kampeni hii ni dhana potofu kuwa demokrasia maana yake ni kuwa na wawakilishi wengi wa vyama katika Bunge na mabaraza ya madiwani.

Mtazamo huu wa kimajimbo kuhusu uwakilishi unadaiwa kutokana na mfumo wa Westminister, yaani mfumo wa Bunge la Uingereza. Hii ni kweli kwa kiasi fulani tu.

Waingereza wana utaratibu wa uwakilishi wenye historia ya karne nyingi za mapambano ya kitabaka na kikatiba kati ya mamwinyi, mabwanyenye, watwana na wafanyakazi na kati ya ufalme wa England na falme za Wales, Scotland na Ireland, ambazo kwa pamoja zinaunda Ufalme wa Muungano wa Uingereza (UK).

Baada ya miaka mingi ya kupambana na kumwaga damu na baadhi ya viongozi na wafalme kukatwa vichwa, hatimaye Waingereza walikubaliana kuwa na Bunge lenye chemba au mabaraza mawili ili kuzingatia maslahi ya pande zote.

Mabaraza hayo ni lile la Mamwinyi (House of Lords) na lile la Makabwela (House of Commons). Wajumbe wa Baraza la Mamwinyi hawachaguliwi na wananchi na hujumuisha mamwinyi wenye kumiliki ardhi kubwa na viongozi wakuu wa Kanisa la Uingereza. Wajumbe wa Baraza la Makabwela huchaguliwa majimboni.

Mapambano ya kudai demokrasia nchini Uingereza, vilevile yaliibua vyama vikuu viwili, Conservative (chenye kuwakilisha maslahi ya mamwinyi na mabwanyenye) na kile cha Labour (ambacho awali kiliwakilisha maslahi ya matabaka ya wazalishaji wafanyakazi na vibarua.

Siku za karibuni, kimezuka chama kingine kikuu cha tatu, Liberal Democrats, ambacho kimetokana na muungano wa vyama vidogo viwili vya Liberal Party na Social Democratic Party, hicho ni chama cha kiliberali cha mrengo wa kati.

Vipo vyama vingine vidogo vidogo, lakini havina athari kubwa kiutawala. La muhimu kufahamu kuhusu mfumo huu wa Uingereza ni kwamba, vyama vyote vinavyoshika utawala huendeleza takriban sera zilezile za uchumi, utaifa na mambo ya nje na hakuna hata kimoja kwa sasa kinachowakilisha maslahi ya mnyonge.

Jingine la kukumbuka ni kwamba mfalme au malkia wa Uingereza, ni nguzo mojawapo ya Bunge la Uingereza kama alivyo Rais hapa kwetu.

Hivyo, madai ya kwamba Tanzania inafuata mfumo wa Westminister yana walakini maana hayasemi ukweli wote. Hata hivyo, kuna jambo moja la Westminister ambalo Tanzania na nchi nyingi za Jumuiya ya Madola zinaling’ang’ania, nalo ni uwakilishi na utawala kupitia katika vyama.

Huu ni utaratibu ulioletwa kwetu na nchi za Magharibi nasi tukaupokea na kuukubali bila kuusaili. Lakini je, utaratibu huu unahakikisha kuwapo kwa mfumo bora wa uwakilishi wa makundi yote ya wananchi?

Mugyabuso Mulokozi ni Profesa Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Viongozi wapunguze anasa kunusuru maisha ya mama na mtoto

NI Jumatano nyingine tena, tunakutana katika safu yetu ya Jicho la Mtanzania. Jumatano ya leo safu hii itajikita katika suala la afya ya mama na mtoto kwa kuijadili hospitali yetu ya taifa Muhimbili.

Sote tunafahamu kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndiyo hospitali mama katika nchi yetu. Ni hospitali ambayo magonjwa sugu hutibiwa, ina wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali za afya pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa.

Binafsi, pamoja na kuwa mkazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu, sijawahi kupata nafasi ya kufika katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu bali kusindikiza wagonjwa au kwenda kuona. Mara ya kwanza kufika hospitalini hapo nilimsindikiza rafiki yangu wa karibu aliyekuwa akiuguliwa na mtoto wake mchanga.

Mwanaye huyo, alizaliwa katika hospitali hiyo akiwa hajatimiza umri wa kuzaliwa (pre mature), kutokana na matatizo ya uvimbe tumboni mwa mama yake. Wakati mama wa mtoto anaruhusiwa kurudi nymbani aliambiwa na daktari wake kuwa ataendelea kuhudhuria kliniki chini ya uangalizi wa daktari bingwa wa watoto hapo Muhimbili mpaka daktari wake atakaporidhishwa na maendeleo ya mtoto ndipo atapewa ruhusu ya kuhudhuria kliniki nyingine.

Siku nilifika Muhimbili nikiwa na rafiki yangu, mwanaye alikuwa ameugua ghafla na hivyo kulazimika kuwahishwa hospitalini Muhimbili.

Tukiwa kitengo cha huduma za dharura, mama na mtoto walipokelewa na kuingizwa ndani kwa ajili ya kuonwa na daktari. Tulimsubiri mapokezi kwa takribani saa nne ndiyo akatoka huku akitueleza kuwa mtoto ameandikiwa kulazwa. Ilibidi tena tusubiri kwa karibu saa moja ili gari la kuwapeleka wodini kufika.

Tulipofika wodini tulikutana na daktari wa zamu ambaye naye alichukua maelezo kabla ya mama kuonyeshwa wodi. Baadaye alimwita muuguzi na kumwambia amtafutie kitanda lakini muuguzi baada ya kuzunguka huko na kule alirejea na kueleza hakukuwa na kitanda isipokuwa anaweza kutoa msaada wa kumtafutia kitanda ambacho itabidi atumie na mgonjwa mwingine.

Kitanda kilipopatikana tulimpeleka mtoto na mama yake wodini. Kitanda ambacho alitakiwa kukitumia kilikuwa tayari kina mtoto wa umri kama miaka miwili akiwa amelala na mama yake.

Muuguzi alimwamsha mama aliyekuwa amelala na kumwambia kuwa itabidi atumie kitanda hicho pamoja na mwenziye.

Wakati huo, nilikuwa nikijaribu kuangalia uwezekano wa kitanda kile ambacho ni kidogo kutumiwa na watu wanne. Kimsingi uwezekano ulikuwa mdogo kwani hata huyo mama tuliyemkuta akitumia na mwanaye walikuwa wamelala kwa kujibana.

Mama tuliyemkuta aliamka kwa upendo na kushauri mke wa rafiki yangu amlaze mtoto na wao wakae macho mpaka asubuhi kwa sababu isingewezekana kulala wote kitandani hapo kutokana na udogo wa kitanda.

Moyoni nilisikitishwa na hali ile. Rafiki yangu aliniomba ushauri wa kumuhamisha mgonjwa wetu pale kutokana na mazingira tuliyoyaona na baada ya kujadiliana tulikwenda kumwomba daktari atupe ruhusa na kurudi siku inayofuata asubuhi, jambo ambalo alilikubali baada ya kutazama hali ya mtoto na pia kuangalia mazingira ya pale wodini.

Nilijiuliza maswali mengi, lakini kubwa lilikuwa iwapo Serikali yetu ina dhamira ya dhati ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Jibu lililonijia haraka ni kwamba pamoja na tatizo la ufinyu wa bajeti ambalo nchi yetu inakabiliana nalo, bado Serikali haijaweza kuonyesha nia ya dhati ya kutokomeza vifo hivi ambavyo vinaweza kuepukika.

Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika uliofanyika Kampala nchini Uganda mwaka 2010, viongozi wa Afrika walikubali kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya afya kwa kupanua wigo wa afya ya mama na mtoto. Raisi Jakaya Kikwete, alitamka kuwa kupunguza vifo vya akina mama na wototo ni kipaumbele namba moja kwa Tanzania.

Lakini takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa vifo vya watoto wachanga bado viko juu. Jumla ya watoto 32 hufa kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa wakiwa hai ikiwa na maana kuwa vifo vya watoto wachanga 44,000 hutokea kila mwaka sawa sawa na asilimia 47 ya vifo vyote vya watoto wachanga.

Kimsingi, maisha ya watoto hasa chini ya mwaka mmoja hutegemea sana maisha ya mama zao au kwa lugha nyingine ni kuwa kama mtoto wa chini ya mwaka mmoja atafiwa na mama yake, uwezekano wa yeye kuishi unakuwa ni mdogo na ndiyo maana afya ya mama ina uhusiano wa karibu na ya motto.

Niliwaza mambo mengi kutokana na ile hali niliyoiona pale Muhimbili. Kwanza niliwaza kuwalaza watoto wawili wagonjwa ambao umri wao unapishana sana. Mmoja ana miaka miwili mwingine kwa wakati huo alikuwa hajafikisha hata umri ambao kwa kawaida mtoto anatakiwa kuzaliwa japokuwa tayari alikuwa ameshazaliwa akiwa na karibu mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa maelekezo ya daktari wake, mtoto huyo alitakiwa kupata uangalizi wa karibu sana na kuwekwa kwenye mazingira safi na salama bila ya kushikwa au kuonwa na watu tofauti na wazazi wake ambao walishapewa masharti ya kumtunza kwani mwili wake ulikuwa bado ni dhaifu, hivyo ni rahisi kwake kupata magonjwa, lakini siku hiyo alilazwa na mgonjwa mwingine.

Kwa upande mwingine sote tunafahamu kuwa, malaria ni ugonjwa namba moja unaosababisha vifo vya maelfu ya Watanzania kila mwaka. Kina mama wale ambao walikuwa wameamua kukesha wakiwaangalia watoto kutokana na kukosa vitanda vya kulalia, walikuwa kwenye hatari ya kupata malaria kutokana na mbu jambo ambalo siyo tu ni hatari kwa afya zao bali hata kwa afya za watoto wao ambao wanawategemea.

Tukitazama kwa pamoja hii ya Hospitali ya Taifa ikiwa katika hali hiyo, nyingine hali ikoje? Waliopata nafasi ya kutembelea Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke wanaweza kuwa mashahidi wazuri wa hali mbaya za hospitali hizo.

Haina shaka kwamba, kama viongozi wetu na familia zao wangekuwa wanatibiwa katika hospiali zetu hizi, pengine wangeona umuhimu wa kuboresha hali ya utoaji huduma kwa hospitali hizi.

Mameya wa Jiji na viongozi wengine wa manispaa zetu wanatembelea magari ya gharama aina ya Toyota VX V8. Haya ni magari ya kifahari na yenye gharama kubwa. Fedha hizi zinaweza kujenga wodi kubwa kwa ajili ya akina mama wajawazito pamoja na kuwawekea vitanda na vifaa vingine muhimu.

Hakuna sababu kwa viongozi wetu kutumia magari ya gharama kubwa kama haya kama taifa limekusudia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Viongozi wetu wakiamua akina mama na watoto wasife kwa kukosa huduma na vifaa tiba inawezekana iwapo watakubali kuachana na anasa walizozikumbatia sasa.

Mulugo: Michango ya CWT hulinda maslahi ya walimu

SERIKALI imesema fedha ambazo walimu huchangia katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hulinda na kutetea maslahi ya walimu wawapo kazini. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliliambia Bunge jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiembesamaki, Waride Bakari Jabu.

“Kwa mujibu wa Sheria namba sita ya mwaka 2004 ya CWT inabainisha wazi kuwa, makato ambayo walimu hukatwa ni kwa ajili ya kulinda na kueteta maslahi wawapo kazini, lakini sheria hiyo haijaelezea mafao ya walimu mara wanapostaafu ama kufariki,” alisema Mulugo.

Aidha, alitoa wito kwa wabunge kuhakikisha wanatoa mapendekezo ya kuwapo kwa mabadiliko ya sheria hiyo na hatimaye walimu hao mara wanapostaafu ama kufariki waweze kupata mafao yao.

Katika swali lake la nyongeza, alitaka kujua walimu wananufaikia vipi pindi wanapostaafu ama kufariki kutokana na wao kuchangia kiasi cha Sh bilioni 2.2 ikiwamo makato ya NSSF kwa kila mwezi.

Alihoji fedha hizo ambazo walimu wanachangia kama zimekuwa zikikaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Akijibu swali hilo, Mulugo, alisema CWT hawakaguliwi na CAG bali hukaguliwa na mamlaka ambaye humchagua wao na wala fedha hizo hazikaguliwi na CAG na baada ya ukaguzi wa mtaalamu huyo ripoti zote za fedha zilizokaguliwa hupelekwa kwa Msajili wa Vyama.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati, alitaka maelezo ya Serikali kuhusiana na kuwapo kwa malalamiko toka kwa walimu kutokana na kukatwa asilimia mbili na Hazina wanapoajiriwa.

Akijibu swali hilo, alikiri kuwapo kwa suala hilo na kudai lipo katika Sheria ya CWT ya mwaka 2004 na fedha hizo hukatwa kutokana na chama hicho kufikisha wanachama zaidi ya asilimia 50.

Vyombo vya habari vyashutumiwa kesi ya Lulu


ARAZA la Habari Tanzania (MCT), limevishutumu vyombo vya habari kwa kuandika habari zenye mwelekeo wa kumhukumu msanii Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, kwamba amemuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Akisoma tamko la Kamati ya Maadili ya MCT Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema wamesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza kwa baadhi ya vyombo vya habari katika kuripoti kuhusu kifo cha msanii, marehemu Kanumba.

Alisema hatua hiyo ni ukiukwaji mkubwa uliovuka mipaka wa maadili ya uandishi wa habari.

Alisema vyombo hivyo vimemhukumu msichana Lulu kuwa amemuua msanii huyo bila kuzingatia kwamba kufanya hivyo ni kosa.

Alisema ukiukwaji huo umejitokeza baada ya msichana huyo kufikishwa mahakamani ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii yaliandika vichwa vya habari vinavyomhukumu moja kwa moja Lulu kama ni muuaji.

“Kwa mujibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari, mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa hadi atiwe hatiani na mahakama.

“Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika kwa waandishi na wahariri wote kujiepusha na habari au vichwa vya habari vinavyohukumu ambavyo vinaonekana kushawishi au kushinikiza uamuzi wa mahakama,” alisema Jaji Mihayo.

Aidha, alionya kesi ya msanii huyo si rahisi kama wengi wanavyofikiri na vyombo vya habari vifanye kazi yake kwa mujibu wa taaluma na viache kuongozwa na taarifa za pembeni, zikiwamo za katika mitandao.

Naye, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, aliwataka waandishi wa habari kuchunguza undani wa kifo cha marehemu Kanumba kwa sababu kinaingilia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Nawakumbusha waandishi wenzangu, tuzame zaidi kulitazama suala hili, tukio limetokea kwa utatanishi, habari ya kifo cha Kanumba inaingilia masuala ya kijinsia, maana jamii inalishwa sumu kwamba kuna mmoja ambaye ni malaya na mwingine sivyo, hii si sawa,” alisema Kajubi.

Serikali yafanya kufuru

*Yapandisha mishahara ya vigogo ghafla Waziri Kombani adai imefuata taratibu,Wengine waongezewa Sh milioni moja
SERIKALI imefanya marekebisho ya mishahara kwa watumishi wake kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Sambamba na hilo, mishahara ya viongozi wa Serikali kwa mwaka huo wa fedha, nayo imefanyiwa marekebisho.

Marekebisho hayo ni kwa mujibu wa waraka wenye kumbukumbu namba S/AC 205/ 399/ 01/ 44, kutoka Ofisi ya Rais Ikulu (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), uliotolewa Julai 25, mwaka huu.

Waraka huo, umesambazwa kwa wakuu wote wa idara za Serikali, wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wakurugenzi wa halmashauri zote za wilaya nchini.

Waraka huo, uliosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu (Utumishi), Hab Mkwizu, umehusisha pia marekebisho ya ngazi za mishahara kwa viongozi hao wa Serikali.

Kwa mujibu wa waraka huo, ngazi za mishahara zilizokuwa zinaanzia TGS I hadi TGS Q, zimebadilishwa na sasa zitasomeka LSS (E) 1 hadi LSS (E) 9.

Watumishi na viongozi wa Serikali walionufaika na marekebisho hayo, ni pamoja na makatibu wakuu wa wizara, manaibu wao pamoja na wakurugenzi wa idara zote za Serikali. Marekebisho hayo yameanza kutekelezwa Julai, 2012.

Hata hivyo, marekebisho hayo yamelalamikiwa na baadhi ya watumishi wa Serikali, wakidai kuwa hayana uwiyano unaoeleweka kati ya mishahara ya wamtumishi wa Serikali.

Marekebisho hayo yanaoneshwa katika kiambatanisho namba 1 cha waraka huo, ambapo watumishi na viongozi hao wameongezewa mshahara usiopungua 400,000.

Mfano mshahara wa mtumishi wa ngazi TGS P, umepanda kutoka Sh 3, 216, 000 hadi Sh 4, 500, 000 katika ngazi mpya ya LSS (E) 9, ongezeko ambalo ni zaidi ya Sh milioni moja.

Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikosoa marekebisho hayo na kusema kuwa, hayana uwiyano mzuri kati ya mshahara wa mtumishi na mtumishi mwingine.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, amekiri kuwapo kwa marekebisho hayo ya mishahara kwa watumishi na viongozi wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Kombani alisema, marekebisho hayo ni ya kawaida na kwamba yanawagusa watumishi wote wa Serikali bila kubagua.

“Serikali ikifanya marekebisho ya mishahara, inafanya hivyo kwa watumishi wake wote. Hatuchagui nani aongezewe nani asiongezewe ni wote,” alisema.

Alisema vigezo vilivyotumika katika marekebisho hayo, ni pamoja na aina ya kazi, uzoefu na muda aliotumia mtumishi kukaa kazini.

“Unauliza kwanini watumishi wengine wamepewa nyongeza kubwa na wengine kidogo, ndugu yangu sifa zinatofautiana, mtumishi anayeanza kazi leo, hawezi kulipwa mshahara na mtumishi aliyepo kazini kwa miaka 20,” alisema.

Alipoulizwa ni sababu zipi zilizoifanya Serikali kurekebisha ngazi ya mshahara kutoka TGS na sasa kutumia ngazi mpya ya LSS, Waziri Kombani alisema. “Hayo ni masuala ya kitaalamu zaidi.”

Kombani alikiri kima cha chini cha mshahara ni kidogo na kueleza kuwa, Serikali ipo katika majadiliano.

“Kima cha chini kilipanda kutoka Sh 130, 000 hadi Sh 170, 000. Tunajua kima hiki hakitoshi lakini tupo katika majadiliano,” alisema.

Chadema waonyesha picha za video alivyouawa Mwangosi



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonyesha picha za mnato na video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alivyouawa.

Picha hizo zilionyeshwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichohudhuriwa pia na waandishi wa habari. Kikao hicho cha Kamati Kuu kilikuwa ni cha dharura na kilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.


Wakati picha hizo zikionyeshwa wazi wazi, viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari, walishindwa kujizuia kwani baadhi yao walijikuta wakiangua vilio wakionyesha kusikitishwa na jinsi Mwangosi alivyouawa.

Katika tukio hilo, Mbowe ni kati ya waliolia na ilifika wakati akanyanyuka kutoka meza kuu na kwenda nje ya ukumbi, ili asiendelee kushuhudia Mwangosi alivyouawa.

Wakati picha hizo zikionyeshwa kwa zaidi ya masaa mawili, askari polisi walioshiriki kumuua Mwangosi walionekana wazi wazi na pia Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana pia eneo la tukio akishuhudia Mwangosi akiuawa.

Kwa mujibu wa picha hizo, mwandishi wa habari aliyeanza kukamatwa na askari polisi na kupata kipigo ni Godfrey Mushi wa Gazeti la Nipashe.

Picha hizo za video zilionyesha kuwa, baada ya Mushi kukamatwa, Mwangosi alikwenda kumuokoa mwenzake huyo na alipofika eneo la tukio, askari hao walianza kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda Kamuhanda.

Picha hizo zinaonyesha kuwa, kabla Mwangosi hajauawa, polisi mmoja alipitisha bunduki yake miguuni kwa polisi mwenzake kisha Mwangosi akauawa.

Baada ya tukio hilo, picha hizo zinaonyesha kuwa, baadhi ya askari polisi waliokuwa wakimpa kipigo Marehemu Mwangosi, walikimbia na kuacha mwili wa marehemu ukiwa vipande vipande.

Kwa mujibu wa picha hizo, polisi hao walipokuwa pembeni, wenyewe kwa wenyewe walianza kulaumiana huku baadhi yao wakimlaumu muuaji na kusema umefanya nini hicho?.

Baada ya hapo, mmoja wa polisi hao alisikika akisema twende tukamchukue mwenzetu na walipofika mahali alipokuwa mwenzao ambaye alikuwa amejeruhiwa kwa bomu lililomuua Mwangosi, gari ya Kamanda Kamuhanda ilisogea karibu na kumpakia askari polisi aliyejeruhiwa.

Picha hizo za video ambazo zinaonekana zilirekodiwa kwa umakini wa hali ya juu, zinaonyesha baada ya mauaji hayo, askari walishikwa na butwaa huku baadhi yao wakionekana kushika pua.

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya askari ambao ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walionekana katika mkanda huo wa video, wakifungua kofia zao zilizokuwa zimefunika uso na macho yao, ili waone vizuri maiti ya Mwangosi iliyokuwa vipande vipande.

Wakati wakivua kofia hizo, baadhi yao walikuwa wakinawa nyuso zao kutokana na moshi uliokuwa umesambaa eneo la tukio wakati walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA.

Pia picha hizo, zilionyesha askari polisi mmoja akiwa amevaa kiraia, huku shingoni akiwa na skafu ya CHADEMA lakini baada ya vurugu kuanza, askari huyo alionekana akiivua skafu hiyo na kuiweka mfukoni.

Alipoivua na kuiweka katika mfuko wa nyuma wa kaptula aliyokuwa amevaa, mwenzake mmoja akampa kofia ya kujikinga na moshi kisha askari huyo akachomoa bastola kwa ajili ya mapambano.

Pamoja na picha hizo kuwaonyesha askari polisi walivyotekeleza tukio hilo, Kamanda wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wa CHADEMA, Benson Kigaila, alionekana pia akijibizana na ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Iringa kuhusu wafuasi wa CHADEMA kuwepo katika Kijiji cha Nyololo kilichopo Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Vile vile, picha hizo za video, awali zilionyesha marehemu Mwangosi alivyokuwa akimuuliza Kamanda Kamuhanda kuhusu sheria ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na maswali hayo yalionyesha jinsi kamanda huyo wa polisi alivyokuwa amechukizwa nayo.

Kutokana na picha hizo, Mbowe alisema huo ni ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi Jeshi la Polisi lilivyokuwa limedhamiria kuua.

Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA itatoa tamko zito leo kuonyesha ni hatua gani zitachukuliwa baada ya kifo cha Mwangosi.

Serikali yamwaga ajira kwa walimu

SERIKALI imetangaza kumwaga ajira mpya za walimu 28,746 katika shule za msingi na sekondari, kuanzia mwezi huu. Hatua hiyo, itapunguza nusu ya ukosefu wa walimu katika shule za Serikali.

Mpaka sasa, Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo Serikali inasema italimaliza katika miaka michache ijayo, kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbalimbali kuhitimu masomo.

Rais Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo mjini Igunga juzi, ambapo alisema kati ya walimu watakaoajiriwa na kusambazwa, 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu, Rais Kikwete alisema mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu, ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.

Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee inahitaji walimu 285.

Hii itakuwa mara ya pili, Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo hilo.

Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379, walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246, walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu.

Wakati shule za Serikali, zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459, hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.

Rais Kikwete aliwaambia wananchi kuwa Serikali, inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi.

Pia alizungumzia suala la huduma ya maji, akisema Serikali imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete alisema kufuatia kuzinduliwa kwa mradi wa Maji wa Bulenya, mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70.
CWT YAJIBU
Akizungumzia ajira mpya za walimu, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania, Ezekiel Oluochi, alisema Serikali imefanya jambo la maana, lakini imechelewa kuchukua hatua haraka.

“Naipongeza Serikali, lakini kimsingi natofautina na Serikali katika hili, imechelewa sana kutoa ajira kwani takwimu zinaonyesha kuna upungufu wa walimu 150,000 kwa shule za msingi na 50,000 shule za sekondari.

“Mpaka sasa walimu waliopo ni 234,054, tunahitaji walimu 200,000, kwa maana hiyo walimu waliopo hivi sasa ni asilimia 90,” alisema Oluochi.

Aliitaja mikoa ambayo, inakabiliwa na uhaba wa walimu, kuwa ni Shinyanga, Singida na Arusha katika wilaya za Ngorongoro, Longido na Monduli.

Aliitaja mikoa mingine na wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Dodoma (Kondoa), Kagera (Muleba), Mwanza (Ukerewe, Misungwi), Tabora (Uyui, Sikonge na Urambo), Lindi (Kilwa, Nachingwe, Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini na Lindi Vijijini).

Alisema mikoa ya Mtwara na Lindi, ina hali mbaya zaidi kuliko mingine Tanzania.

“Sababu kubwa ya mikoa hii kuwa na hali mbaya, inatokana na mazingira magumu wanayokutanayo walimu wapya wanaopangiwa huko.

“Asilimia 12 ya walimu wapya wanaoajiriwa, wanaacha kazi hasa wa shule za msingi na walimu wenye shahada ambao wengi wao wanapelekwa vijijini na kujikuta hawatimizi ndoto zao,” alisema Oluochi.

Alisema kama kweli Serikali imedhamiria kumaliza tatizo hilo, basi kuanzia sasa ihakikishe walimu wapya wote wanalipwa stahiki zao, ikiwa ni pamoja na nauli, posho ya siku saba na fedha za kusafirishia mizigo ya tani moja na nusu, kama sheria inavyotaka.