SAKALA la nani mwenye haki ya kuchinja kati ya Wakristo na Waislamu, jana lilichukua sura mpya katika Kijiji cha Buselesele, Wilaya ya Chato, mkoani Geita baada ya kutokea vurugu kubwa
na kusababisha mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste,
Mathayo Kachila (48) na watu wengine saba kujeruhiwa.
Vurugu hizo zilitokea jana kijijini hapo kuanzia saa tatu asubuhi katika Soko Kuu la Buselesele, baada ya mtu mmoja ambaye inadaiwa ni Mkristo, kuchinja ngombe mmoja, mbuzi wawili.
Inadaiwa kuwa, Mchungaji Kachila alishambuliwa na kundi la Waislamu jirani na msikiti wakati akiwasindikiza wageni wake
baada ya vurugu hizo kupamba moto.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Paul Kasagabo, alithibitisha taarifa za kifo hicho na kuongeza kuwa, watu wengine saba walijeruhiwa vibaya kutokana na vurugu hizo.
“Chanzo cha vurugu ni mwananchi mmoja ambaye inadaiwa ni Mkristo aliyefahamika kwa jina moja la Obadia, kuchinja ngo'mbe mmoja, mbuzi wawili na nyama hizo kuuzwa katika bucha ambayo nje ilifungwa kitambaa chenye ujumbe unaosema 'Yesu tena bucha', ambayo anaimiliki hivyo hali hiyo iliwachukiza Waislamu.
“Katika vurugu hizi, bucha ya mtu anayelalamikiwa ilivunjwa pamoja na dula lililokuwa likitoa huduma ya M-Pesa na mwili
wa Mchungaji Kachila umehifadhiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Geita,” alisema.
Kamanda Kasagabo aliongeza kuwa, hadi sasa hakuna mtu ambaye amekamatwa kutokana na vurugu hizo ila jeshi hilo linaendelea kuwasaka wahusika ili waweze kufikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Ernest Nkwabi, alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa Mchungaji huyo hospitalini hapo na majeruhi saba.
“Tumepokea mwili mmoja wa marehemu na majeruhi saba ambao kati yao, wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya.
“Mwili wa marehemu una majeraha ya kukatwa na panga mara nne kichwani, mkono wa kushoto na kiganga chake chote kukatwa katwa hivyo kusababisha avuje damu nyingi,” alisema.
Aliwataja majeruhi waliopelekwa Hospitali ya Bugando kuwa ni Ramadhan Paschal (36), aliyejeruhiwa vibaya katika fuvu la kichwa upande wa mbele na Said Ntamopagafe (47) ambaye amejeruhiwa mguu wa kulia kwa kukatwa mapanga.
Alisema majeruhi wawili Vicent Raymond (18) na Yassin Rajab (56), bado wamelazwa hospitalini hapo wakiendelea na matibabu
na wengine wawili walitibiwa na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, alisema vurugu hizo zimedhibitiwa kijijini hapo na hali ya utulivu kurudi kama kawaida ambapo wananchi wanaendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
Share on linkedin Share on facebook Share on twitter Share on email More Sharing Services 0
No comments:
Post a Comment