Rais Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo mjini Igunga juzi, ambapo alisema kati ya walimu watakaoajiriwa na kusambazwa, 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu, Rais Kikwete alisema mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu, ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.
Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee inahitaji walimu 285.
Hii itakuwa mara ya pili, Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379, walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246, walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu.
Wakati shule za Serikali, zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459, hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.
Rais Kikwete aliwaambia wananchi kuwa Serikali, inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi.
Pia alizungumzia suala la huduma ya maji, akisema Serikali imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete alisema kufuatia kuzinduliwa kwa mradi wa Maji wa Bulenya, mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70.
CWT YAJIBU
Akizungumzia ajira mpya za walimu, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania, Ezekiel Oluochi, alisema Serikali imefanya jambo la maana, lakini imechelewa kuchukua hatua haraka.
“Naipongeza Serikali, lakini kimsingi natofautina na Serikali katika hili, imechelewa sana kutoa ajira kwani takwimu zinaonyesha kuna upungufu wa walimu 150,000 kwa shule za msingi na 50,000 shule za sekondari.
“Mpaka sasa walimu waliopo ni 234,054, tunahitaji walimu 200,000, kwa maana hiyo walimu waliopo hivi sasa ni asilimia 90,” alisema Oluochi.
Aliitaja mikoa ambayo, inakabiliwa na uhaba wa walimu, kuwa ni Shinyanga, Singida na Arusha katika wilaya za Ngorongoro, Longido na Monduli.
Aliitaja mikoa mingine na wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Dodoma (Kondoa), Kagera (Muleba), Mwanza (Ukerewe, Misungwi), Tabora (Uyui, Sikonge na Urambo), Lindi (Kilwa, Nachingwe, Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini na Lindi Vijijini).
Alisema mikoa ya Mtwara na Lindi, ina hali mbaya zaidi kuliko mingine Tanzania.
“Sababu kubwa ya mikoa hii kuwa na hali mbaya, inatokana na mazingira magumu wanayokutanayo walimu wapya wanaopangiwa huko.
“Asilimia 12 ya walimu wapya wanaoajiriwa, wanaacha kazi hasa wa shule za msingi na walimu wenye shahada ambao wengi wao wanapelekwa vijijini na kujikuta hawatimizi ndoto zao,” alisema Oluochi.
Alisema kama kweli Serikali imedhamiria kumaliza tatizo hilo, basi kuanzia sasa ihakikishe walimu wapya wote wanalipwa stahiki zao, ikiwa ni pamoja na nauli, posho ya siku saba na fedha za kusafirishia mizigo ya tani moja na nusu, kama sheria inavyotaka.
No comments:
Post a Comment