Friday, 28 March 2014

Siri ya CCM kung’ang’ania Serikali mbili kikatiba

Katika maisha ya kawaida, binadamu ana msimamo wake na hata uamuzi  asiopenda ubadilike.
Katika medani ya siasa nchini msimamo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kuhusu Muungano na muundo  unafahamika. Ni muundo wa kutaka  Serikali mbili ambao chama hicho unakipigania kwa udi na uvumba.
Hata hivyo, msimamo huo ni kinyume na mapendekezo au matakwa ya wengi kama ilivyoainishwa kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
 Tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi na ilipendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Hivi karibuni akifungua Bunge Maalumu la Katiba, Rais Jakaya Kikwete akaunga mkono msimamo wa chama chake, jambo lililoibua mjadala unaoendelea hadi sasa.
Hoja ya Serikali mbili
Kwanini CCM wanataka Serikali mbili na siyo tatu au moja kama ilivyo maoni ya wananchi walio wengi kwa mujibu wa maelezo ya Tume ya Warioba? Makala haya yanachambua hoja hiyo.
 Profesa Bakar Mohammed ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anayesema msimamo wa CCM wa kudai Serikali mbili unatokana na hofu ya uhafidhina wa kuogopa mabadiliko.
Anasema viongozi wengi wa CCM wanasumbuliwa na hofu na woga wa mabadiliko na kwamba wanakuwa wagumu kuyakubali  yanapotaka kutokea.
“Kama mtu unaangalia madaraka zaidi, lazima kunakuwa na woga, na hii ni hulka ya binadamu kuwa na woga wa kuacha kile ulichokizoea… Lakini ukiangalia masilahi ya nchi na kuacha yale yanayokusukuma kusingekuwa na wasiwasi huu unaoonekana sasa,” anasema.
Anasema CCM inachofanya ni kuhakikisha haking’oki madarakani, huku viongozi wake wakiamini kuwa wana sifa za kuongoza na siyo wengineo.
Profesa Bakari anailinganisha hofu ya sasa ya CCM na ile waliyokuwa nayo viongozi wa chama hicho miaka ya 1990 zilipoanza vuguvugu za mabadiliko ya siasa za vyama vingi. Anasema CCM kiliendesha propaganda kuwa mfumo wa vyama vingi haukuwa na tija na ungeleta vita.
Hofu hiyo anasema ndiyo inayokifanya chama hicho kikongwe kuhofia kung’olewa madarakani.
 “Woga huo bado upo, wanaogopa pengine mfumo ukiwa wa Serikali tatu uwezekano wa wao kubaki madarakani utakuwa mdogo,” anafafanua.
Anaongeza kusema kuwa  hofu ya CCM siyo kwa ajili ya masilahi ya nchi,  badala yake inaonekana chama kinaangalia masilahi yake.
Ingekuwa vyema anasema kwa CCM  kueleza madhara yanayoweza kulikumba taifa ikiwa muundo wa Serikali tatu utapita.
 “Wanatoa hoja kuwa mfumo wa Serikali tatu unaweza kusambaratisha nchi, lakini hakuna uhakika kama mfumo huu uliopo nchi hauwezi kusambaratika,” anasema.
Hofu ya kuyumba na kuanguka
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk. Benson Bana anasema siri ya CCM kung’ang’ania Serikali mbili inatokana na hofu ya kuyumba na kuanguka.
Anasema CCM kimekuwa madarakani na mfumo huo kwa miaka 50 na kwamba hofu yao ni kuwa ukiondoa Serikali mbili kinaweza kuyumba na kuachia madaraka.
Anasema misingi ya wanasiasa ni madaraka, na kwamba ukishayapata, huwezi kuyaachia kirahisi.
“Misingi ya wanasiasa ni madaraka… Kuyalinda, kuyahifadhi na kuyatumia madaraka yale kwa namna yoyote…Huwezi kuyaachia madaraka kirahisi. Utafanya ujanja, utatumia mbinu chafu  ili tu kuhakikisha unabaki madarakani, na hiki ndicho wanachofanya CCM,” anasema.
Dk. Bana anasema CCM kingeeleweka na kingekuwa na mwonekano mzuri zaidi endapo wangepigania kuwapo kwa Serikali moja.
“Wangekuwa wanataka muungano imara, endelevu na uliokomaa wangeelekeza katika Serikali moja…Lakini hawataki kwa sababu wanajua moja inaweza ikawanyima uongozi,” anasema.
Dk. Bana anasema ni vyema wananchi wakaelimishwa huu muungano una faida gani na wanafunzi shuleni katika elimu ya uraia waelezwe faida zake.
“Ingekuwa wazi tungejua nani anafaidika na nini, mikopo misaada, nani anachangia nini…Je zile sababu za waasisi za kuungana bado zipo sasa miaka 50 ya Muungano, ule woga kuwa Zanzibar itamezwa bado upo leo?” Anahoji.
Anaongeza kuwa ni vyema kwa watawala kutazama  mazingira ya sasa ya siasa zetu kwa kile anachoeleza kuwa hata Katiba ikipita ikakubali kuwapo wa Serikali mbili, bado wananchi watahoji mantiki ya muundo huo.
Msomi mwingine wa siasa, Dk. Alexander Makuliko  anasema hofu ya CCM ni kuwa ndio iliyouasisi Muungano wa Serikali mbili, hivyo  isingependa hali hiyo ibadilike.
Anaendelea kusema kuwa CCM imezoea mfumo huu na kuwa ikiukosa itaathirika, kwakuwa ni sera yake na imekuwa ikiitekeleza, lakini msimamo wa  wananchi ndiyo kitu cha msingi kuzingatiwa. Hoja zijengwe na zisikilizwe, ubabe hautakiwi, busara inahitajika zaidi.
Anasema pamoja na suala la  Serikali mbili kuwa  ni pimajoto ya  uhai wa CCM,  hata hivyo hoja zinazotolewa katika kutetea msimamo wao ni nzuri tu na zinazoeleweka vyema.
“Sioni kama wanang’ang’ania, lakini ukweli ni kuwa kila chama kina sera yake, na CCM kimeweka sera yake katika suala la Muungano wao wanasema ni Serikali mbili, na siyo tatu…kwamba tatu zitaongeza gharama na mengineyo, ni sababu za msingi kabisa,” anasema.
Anaongeza kuwa hoja zinazotolewa na chama tawala ni kubwa na siyo za kupuuzwa, lakini vilevile kero zinazotajwa kuhusu mfumo wa Muungano uliopo nazo zipo na zinaweza kutatuliwa katika mfumo uliopo.
“Unajua hivi vyama kila kimoja kinataka kuvutia kwake, hata bila rasimu ya Warioba…Ninashauri walete hoja, kisha watu wazipime hizo hoja, kwanini serikali mbili, na wale wa tatu tayari wameleta hoja na ushahidi, watu waachwe wapime,” anasema na kuongeza:
‘’Jambo la msingi kuzingatiwa ni kuwa mawazo ya wananchi wengi yataonekana wakati wa kura za maoni. Angalizo ni  kuhakikisha kuwa kura hiyo isije ikachakachuliwa.’’

.. Samuel Sitta awekwa mtegoni

Dodoma/Dar. Suala la ama kutumia kura ya siri au ya wazi kuamua ibara za Rasimu ya Katiba jana liliuteka upya mjadala wa Kanuni za Bunge la Katiba, huku ikielezwa kuwa limewekwa kama mtego kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika kuwania urais.
Sitta ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia CCM, huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wake kisiasa ndani ya chama hicho.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Godbless Lema alimtaka Sitta kuwa makini na maelekezo aliyodai mwenyekiti huyo anapewa katika uendeshaji wa Bunge na kudai pia kuwa, kuna kundi la watu wanaotaka urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 wanaotaka kumkwamisha.
Akichangia hoja ya mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni yaliyotaka kupitishwa mifumo miwili ya kura kwa wazi na siri, Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha alisema kwa mazingira ambayo yanaendelea, Sitta anapaswa kuwa makini na watu wanaompatia maelekezo wakitaka aonekane hafai baadaye.
“Ni vyema ukawa makini na mapendekezo unayoletewa kwa sababu hao wote pamoja na wanachama wa chama chako wanajua kama utaliongoza vizuri Bunge hili, basi unaweza ukapata tiketi ya kugombea urais 2015 ndani ya chama chako, lakini ukishindwa watakudhihaki kuwa umeshindwa, hivyo hutaweza kuliongoza taifa,” alisema Lema huku Sitta aliyeonekana awali akitabasamu, alibadilika na kumtazama mbunge huyo kwa umakini.
Lema alisema miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kamati nyingine za Bunge hilo, kuna watu ambao wanataka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mjadala huo, ilionekana wazi kuwa wajumbe bado wamegawanyika pande mbili – CCM wakionekana kuunga mkono kura ya wazi na upande wa upinzani wakipigia chapuo kura ya siri.
Miongoni mwa waliopigia debe kura ya siri ni John Mnyika aliyesema suala la upigaji kura ni la kikatiba ili kuhakikisha kila mjumbe anapiga kura yake bila kushurutishwa, kushinikizwa wala kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au chombo chochote.
Wajumbe hao walikuwa wanajadili mapendekezo yaliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, baada ya juzi kuzua mvutano uliosababisha Bunge hilo kuvunjika ili kusubiri maridhiano ya pande zinazopingana.
Mapendekezo ya Kanuni
Kificho alisema, mapendekezo hayo yamefikiwa kutokana na masharti ya kanuni ya 59 (1) na 87 (1) kwamba kanuni ya 38 (1) iweke utaratibu wa kupiga kura ama ya wazi au ya siri, ambao utatekelezwa na mwenyekiti kwa kushauriana na katibu.
Alisema wakati wa kupiga kura ya siri kila mjumbe atapiga kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’  kwa kutumia karatasi ya kupigia kura itakayokuwa imeandaliwa na katibu kwa ajili ya hilo.
Mjumbe Michael Laizer alisema wamechoshwa  na malumbano juu ya kura za wazi au siri, hivyo iwapo kuna wajumbe ambao hawataki mapendekezo ya kamati waondoke.
Naye Ezekiel Olouch alisema utaratibu unaopendekezwa na kamati haujawahi kufanyika mahala popote duniani.
Alisema kura ya siri imekuwa ikitumika kuamua mambo ya msingi na kuepusha mpasuko katika jamii hasa katika masuala ambayo yanaweza kuligawa taifa.
Mohamed Raza alisema msimamo wake ni kupiga kura ya wazi kwani wengi wanajua msimamo wake ambao ametoka nao Zanzibar.
Joshua Nassari alisema anashangazwa kuona Taifa linarejeshwa katika karne ya 18 katika upigaji wa kura kwa kung’ang’ania kura ya wazi wakati wao wamechaguliwa kwa kura za siri.
“Mwenyekiti wewe tumekuchagua kwa siri wajumbe wote wamepatikana kwa siri, iweje leo kulazimisha kura ya wazi ili wajumbe wa CCM watakaopiga kura za siri wachukuliwe hatua,” alisema Nassari.

Tuhuma nzito bungeni,ni za rushwa dhidi ya Waziri Mkuu Pinda

Dar es Salaam. Hali ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya wajumbe wa kundi la 201.
Katika tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa serikali mbili.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli tupu.
Vilevile baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi hilo walicharuka na kujaribu kujitetea huku mmojawapo akitishia kuwa iwapo Wenje asingeomba radhi, asingetoka ndani ya Bunge hilo.
Hoja ilipoanzia
Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani “walilia” sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa kama mganga wa jadi.
Ingawa hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.
Kuhusu rushwa, Wenje alisema:“…Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika usiku. Hii haikubaliki.”
Baada ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.
Profesa Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.
“Kuna kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.
“Kwa sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje aniombe radhi,” alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira, huku kukiwa na sauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.
Makamu mwenyekiti pia alifanya jitihada za kuwataka wajumbe kuwa wavumilivu, huku akitoa nafasi kwa Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza kwamba ni tuhuma nzito. 
Kawambwa alisema: “Ni kweli nilikutana nao; ni wajumbe ambao wanatoka kwenye taasisi zinazojihusisha na masuala ya elimu, lakini mbona wameshafanya mikutano yao mingine mingi ambayo mimi hawakuniita. Kama mtu akiwa hana hoja bora akae chini.”
Makamu Mwenyekiti alimtaka Wenje aombe radhi kutokana na kauli yake, lakini katika hali ya kushangaza mjumbe huyo alisisitiza kwamba Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamekiri.
“Maghembe amekiri aliwaita wafugaji na wavuvi ndiyo waliokula chakula cha rushwa, pia wapo wengine walienda kwa Waziri Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi mama mmoja siwezi kumtaja jina hapa alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa jina lake mwenyekiti baadaye. Aliambiwa kwamba anatoa siri… hoja iliyojadiliwa huko ilikuwa ni kwamba msimamo ni wa serikali mbili… rushwa ya chakula, maji na bahasha walipewa,” alisema Wenje na kusababisha kulipuka kwa kelele zaidi.
Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.
Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.
Baada ya Wenje kukaa, baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 walichachamaa wakitaka kutetea hadhi yao, akiwamo mjumbe kutoka kundi la wafugaji, Esther Juma aliyesema hawatendewi haki kama kundi kusema kwamba walihongwa.
Alisema yeye ana ng’ombe 3,000 na asingeweza kwenda kupokea rushwa ya chakula na kumtaka mbunge huyo kuwaomba radhi la sivyo asingetoka mlangoni.
Wakati mjadala huo ukiendelea, mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa ametoka kwa udhuru, alirejea kimya kimya, na kumtaka Wenje kueleza iwapo anadhani kauli yake haikuwaudhi baadhi ya wajumbe.
Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.
Kauli hiyo ilimfanya Sitta kutangaza kuwa anapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge na uamuzi utakaotolewa atautangaza bungeni.

Tuesday, 25 March 2014

Baada ya matokeo Fanya uamuzi sahihi kujiendeleza kielimu

Wapo wanaofuata mkumbo wa kusoma mchepuo (combination) fulani kwa sababu marafiki zao wengi wameuchagua mchepuo huo. Aidha, wapo wanaolazimisha kusoma masomo magumu yaliyo nje ya uwezo wao kiakili.
Kwa mfano, unaweza kupata alama C katika mtihani wa Hisabati (Basic Mathematics), lakini alama hiyo siyo tiketi pekee ya kuchagua kusoma masomo yenye hesabu za kiwango cha juu (Advanced Mathematics).
Waliofeli nao?
Kama ilivyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, asilimia 78.91 ya wahitimu wamepata daraja la nne na sifuri. Ni dhahiri kuwa wanafunzi hawa hawana sifa ya kujiunga na kidato cha tano.
Hata hivyo, huo ndiyo uwe mwisho wa safari ya kusaka elimu kwa vile tu umefeli? Makala haya yanajaribu kutoa mapendekezo mbadala yanayoweza kutumiwa na wanafunzi ili kujiendeleza zaidi kielimu?
Kwanza ieleweke kutokuchaguliwa kidato cha tano au kufeli kidato cha nne si ishara mbaya maishani na wala haijawa sababu ya kuanza kuamini kuwa umeshafeli kimaisha.
Uzoefu unaonyesha hapa nchini kuna watu wengi baadhi yao leo ni maprofesa maarufu waliowahi kufeli katika madaraja fulani ya kielimu siku za nyuma, lakini kwa kuwa tu walikuwa na dhamira ya dhati na kutoa uamuzi sahihi, waliweza kujiendeleza na kufika kiwango hicho cha elimu kinachotamaniwa na kila mtu.
Nikupe siri moja ninayoifahamu kuhusu wasomi hawa, baadhi yao waliwahi kuwa walimu wangu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hawa pamoja na wengine kuamua kuanza maisha ya familia au kikazi lakini walijiendeleza kupitia mfumo usio rasmi.
Unaweza kuihuisha ndoto yako ya kupata elimu kwa kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo na ndiyo maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi.
Rudi tena darasani. Kuna shule nyingi za sekondari zenye programu maalumu kwa ajili ya watu wanaorudia mitihani ya kidato cha nne tena kwa bei rahisi.
Zitafute shule hizi ila kuwa makini na vituo vinavyoitwa kwa Kiingereza ‘Tuition Centers’ ambavyo vingi vinajali masilahi kuliko ubora wa elimu.
Chunga jambo hili! Kuna mtindo wa wanafunzi wanaofeli kidato cha nne na kuamua kuingia kidato cha tano huku wakirudia mitihani yao. Hawa wanalazimika kusoma masomo ya mitihani wanayoirudia huku wakisoma pia masomo mapya ya kidato cha tano.
Huku ni kujidanganya, kwa mtindo huu, mwanafunzi husika hawezi kusoma kwa undani masomo ya kidato cha tano badala yake atakuwa anasoma ‘kimtego mtego’ ili afaulu tu mitihani ya ndani.
Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani za ngazi ya cheti. Kusomea cheti siyo kuonekana mjinga, kwanza una uhakika wa kuajiriwa au kujiajiri. Kwa mtu mwenye ndoto ya kusoma zaidi, kipato cha ajira yako ndicho unachoweza kukitumia kujiendeleza zaidi.
Upo mfano mzuri wa walimu wa shule za msingi waliosomea ualimu kwa ngazi ya cheti. Wengi hujiendeleza kwa kurudia mitihani na hatimaye kufika vyuo vikuu.
Siyo ualimu pekee, kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa kozi za msingi kwa wahitimu wa kidato cha nne wakiwamo waliopata angalau daraja la nne.
Unachofanya ni kusomea cheti cha msingi kwa mwaka mmoja, kisha unaendelea kwa kusoma tena cheti cha juu kabla ya kupata fursa ya kusoma stashahada.
Kwa walio makini mlolongo huu wa elimu unaweza kukufikisha mbali. Unaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi hawa kwa sharti la kuwa vimesajiliwa na Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (NACTE).
Fursa nyingine inayotumiwa na baadhi ya wanafunzi wanaoishia kidato cha nne ni kusoma masomo ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya VETA wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza zaidi kielimu.
Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya VETA umekua na kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira iwe ajira binafsi au ajira rasmi. Kwa mfano, hivi sasa VETA inaendesha kozi katika sekta za madini, utalii, teknohama na nyinginezo muhimu zama za sasa.

Sitta ‘amkataa’ Warioba bungeni

Dodoma. Jaribio la kutaka kumrejesha bungeni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili ajibu masuala yaliyoibuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kufungua Bunge limegonga mwamba.
Uamuzi wa kukataa ombi hilo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mjumbe wa Bunge, Julius Mtatiro, akisema hadhani kama ni sahihi ombi hilo kutekelezwa.
Awali Mtatiro aliomba mwongozo kwa mwenyekiti, akitaka kujua iwapo kuna haja ya kumrejesha Jaji Warioba kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja za Rais Kikwete ambazo zimekinzana na maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.
Mtatiro alisema: “Mtoa hoja mahususi alikuwa ni Jaji Warioba na Rais Kikwete alialikwa kama mgeni rasmi kufungua Bunge, lakini badala yake alikuja kujibu hotuba ya Warioba.
“Kwa sababu Rais alikaribishwa kama mgeni rasmi, lakini  alijibu  hoja za Warioba, je, hatuoni kama kuna haja ya kumrejesha mtoa hoja mahususi aje kujenga hoja  kutokana na alichosema Rais Kikwete?” alihoji Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF.
Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema tayari amepokea kwa maandishi kutoka kwa baadhi ya wajumbe kuzungumzia suala hilo, jambo ambalo litafanyika lakini si kwa kumwita tena Jaji Warioba.
“Tunapenda kupata muda wa kuzungumzia  suala hili ili kuliweka sawa, hotuba zote mbili ambazo ni muhimu zitaandaliwa ili kupitiwa kuona kama malalamiko yanayotolewa yana hoja,” alisema Sitta.
Tangu Rais Kikwete ahutubie Bunge Ijumaa na kutoa hoja kinyume na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, hasa muundo wa Muungano, kumeibuka mijadala ya ama kuipinga au kuiunga mkono, huku wengine wakieleza kuwa imekiuka sheria.

CCM yaliteka Bunge la Katiba

Dodoma. Sasa ni wazi kwamba serikali mbili zimeonyeshwa taa za kijani baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukamata uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba.
Jana kamati 14 za Bunge hilo ziliwachagua viongozi wake; Mwenyekiti na Makamu na 12 kati yake zilichukuliwa na wajumbe kutoka CCM, chama ambacho tayari kimeweka wazi msimamo wake kuunga mkono Muungano kuwa ni serikali mbili.
Miongoni mwa waliochaguliwa wenyeviti ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), Steven Wassira na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu ambao wamekuwa mstari wa mbele kupigia chapuo mfumo huo badala ya serikali tatu zinazopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Wengine ni Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango – Malecela, Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai, Mbunge wa Viti Maalumu, Kidawa Khamid Salehe, Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha na Mbunge wa Mlalo, Hassan Ngwilizi.
Wengine wa CCM ni Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah na aliyewahi kuwa Waziri katika serikali zilizopita Paul Kimiti. Pia wamo Mbunge wa Wawi ambaye alifukuzwa uanachama na chama chake cha CUF, Hamad Rashid Mohamed na Mwenyekiti wa kundi la wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais, Francis Michael.
Katika uchaguzi wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, aliyekuwa mwenyekiti wa Muda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alichaguliwa mwenyekiti na makamu wake, Dk Susan Kolimba.
Kamati ya Uandishi wa Katiba ilimchagua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na makamu wake, Mgeni Hassan Juma. Kwa kupata nafasi hizo ni dhahiri kwamba ‘mapishi’ ya uendeshaji wa Bunge hilo yatafanywa na CCM kwani mwenyekiti wake Samuel Sitta na makamu mwenyekiti Samia Suluhu Hassan pia ni makada wa chama hicho.
Wenyeviti hao wataungana na Sitta pamoja na Hassan kuunda Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambayo ndiyo itakuwa na mamlaka ya kupanga ratiba na miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge hilo.
Waliochaguliwa kuwa makamu wenyeviti ni Profesa Makame Mbarawa, Shamsa Mwangunga, Fatma Mussa Juma, Dk. Sira Ubwa Mamboya, Assumpter Mshama, Dk. Maua Daftari na Waride Bakar Jabu. Wengine ni Biubwa Yahya Othaman, William Ngeleja, Salimin Awadh Salimin, Yusuf Massauni na Thuwayba Kisasi.
Mbowe atimuliwa
Katika uchaguzi huo, mjumbe wa Bunge hilo, Freeman Mbowe alitimuliwa katika kamati alikokwenda kushiriki uchaguzi kwa madai kwamba hakuwa mjumbe.
Mbowe alisema kabla ya uchaguzi huo alimfuata Mwenyekiti Sitta kumwomba wafanye marekebisho katika kamati tatu za Bunge.
Alisema waliafikiana kuwa Godbless Lema aliyekuwa Kamati namba saba ahamieKamati namba mbili na AnnaMary Stella Mallac aliyekuwa Kamati namba mbili ahamie Kamati namba sita.
Alisema kwa makubaliano hayo yeye (Mbowe) alihamia Kamati namba saba akitokea Kamati namba sita.
“Nilivyoingia katika ukumbi wa Igada, wajumbe walianza kuguna mara wakaanza kuzozana wakitaka wajumbe ambao hawakuwamo kwenye orodha ya kamati hiyo kutoka nje,” alisema na kuongeza;
“Waliamua kuitana majina, lakini hawakuona jina langu wakanitaka nitoke nje, nikawaeleza makubaliano kati yangu na Mwenyekiti (Sitta) lakini hawakuafiki walisisitiza nitoke ndani ya ukumbi huo.”
Alisema hatua hiyo iliwafanya makatibu wasaidizi kuitwa na kuelezwa kilichotokea ambapo waliwasiliana na Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hemed ambaye aliwajibu kuwa bado hajapokea taarifa za mabadiliko hayo na kuwataka wasubiri awasiliane na Sitta.
“Wakati nikiendelea kusubiria
jibu, mmoja wa wajumbe aliendelea kupaza sauti akitaka niondolewe ili waweze kupiga kura,” alisema.
Alisema hali hiyo ilimfanya yeye na baadhi ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani, akiwamo Profesa Abdallah Safari kususia uchaguzi huo na kuondoka.
Mbowe alisema baada ya muda walifuatwa na makatibu wakiwaomba samahani warudi ukumbini kwa sababu wamepokea maelezo kutoka kwa Sitta. Sitta alithibitisha tukio hilo, lakini alisema halikuathiri matokeo ya uchaguzi kwa sababu kuondoka kwao hakukuathiri akidi inayotakiwa.

Monday, 24 March 2014

Ndugai: Taifa lina tatizo la mgawanyo wa rasilimali

Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameomba ushauri kwa Seneta Amos Wako wa Kenya kuhusu mgawanyo wa rasilimali za taifa.
Ombi hilo la Ndugai, ambaye ni mjumbe wa Bunge la Katiba, lilitokana na historia aliyoitoa seneta huyo wa Busia Mashariki nchini Kenya, iliyotokana na uzoefu alioipata katika Mchakato wa kuunda na kuandika katiba ya nchi hiyo.
Mwishoni mwa wiki, Seneta Wako alieleza bungeni kuwa changamoto zilizokuwa zikiikabili Kenya wakati ikiandika Katiba yake, ni pamoja na wananchi kulalamikia mfumo wa mgawanyo wa rasilimali.
“Kulikuwa na madai kwamba hakukuwa na usawa katika kugawa keki ya taifa, maeneo yenye viongozi yalidaiwa kupendelewa kwa kuwa na huduma nzuri za kijamii kuliko mengine,” alieleza Seneta Wako.
Ndugai alipopata nafasi ya kuuliza swali, alisema tatizo la mgawanyo wa rasilimali lililokuwako Kenya, lipo hata hapa nchini lipo kwa kiwango kikubwa.
“Mikoa mingi inalalamikia uduni wa huduma kwa jamii. Kwa uzoefu wako unashauri nini kifanyike kutatua changamoto hii,” aliuliza Ndugai.
Seneta Wako alisema mgawanyo wa madaraka na rasilimali za taifa nchini Kenya unaendelea kushughulikiwa kupitia Utawala wa Majimbo, ingawa aliasa kwamba kinachofaa kwa wengine haimaanishi kitafaa kwa Tanzania.
Alisisitiza kuwa ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania utatokana na Watanzania wenyewe kwa sababu ndio wanaofahamu mila, desturi na mfumo mzima wa maisha yao.

Sunday, 23 March 2014

Tanzania inahitaji watumishi wafanyakazi wa aina gani?

Mwanzo wa maendeleo ya kweli kwa nchi yoyote duniani kama historia
inavyodhirisha, ni pale watumishi na wafanyakazi wanapobadilika na kujitambua kutokana na kuwepo sera na mifumo ya usimamizi nautendaji kazi inayotambua nafasi, stahili au haki, wajibu na majukumu ya kila mtu katika kuchangia maendeleo ya nchi.
Kwa jumla, wataalamu wa nadharia na tasnia ya rasilimali watu wanasema
Kwamba, kazi kubwa ya wanaosimamia rasilimali watu ni kuhakikisha kila shughuli katika taasisi husika anapatikana mtu sahihi, mwenye elimu na ujuzi sahihi, wakati sahihi na atakayepewa kazi sahihi ili aifanye kwa usahihi pia.
Hata hivyo, rasilimali watu kama somo ni somo pana na katika miaka ya leo imeanza kuaminika kwamba kiongozi wa taasisi anayepwaya katika elimu na ujuzi wa rasilimali watu hawezi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama ilivyo kwa yule aliyesheheni nidhamu na nadharia husika.
Kazi ya kusimamia au kuongoza rasilimali watu inaanzia na mipango, ugawanyaji kazi na wajibu, utafutaji watu kujaza nafasi zilizo wazi, mahojiano ya kutathmini sifa na uwezo wa mtu kama unaendana na jinsi alivyo na uchaguaji miongoni mwa walioomba kazi idadi ya watu wanaotakikana kwa kazi fulani.
Menejimenti ya rasilimali watu inajumuisha pia mambo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi, uchukuaji wa hatua za kinidhamu, afya na usalama wa wafanyakazi pamoja na mikakati yote inayoihakikishia taasisi kuendelea hata kama waliopo kwa wakati huo wataondoka au kufa.
Kampuni au idara ya Serikali au taasisi iwayo kwa hiyo ina maana kwamba utendaji kazi wake na sifa yake aghalabu, utatokana na aina ya watu walioajiriwa. Ukiajiri watu wa ovyo na utendaji wa taasisi husika nao pia utakuwa ni wa ovyo. Ukiajiri watumishi au wafanyakazi wazuri basi uwezekano wa taasisi hiyo kuwa na utendaji mzuri nao ni mkubwa pia.
Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba wale wote waliopewa dhamana ya kuajiri wafanyakazi au watumishi wapya lazima wawe wanaojua kila linalopaswa kujulikana juu ya mbinu zote zinazotumika katika nadharia na utendaji kazi katika tasnia ya rasilimali watu ili kuhakikisha kwamba watumishi watarajiwa wote wanapepetwa kwa namna ambayo chuya au chafu wote unaondolewa na panabakia nafaka nzima na safi.
Hili linahitaji kwa kiasi kikubwa ugwiji katika masuala ya saikolojia na sosholojia. Elimu zinazoweza kuwang’amua watu walivyo na watakavyokuwa kwa kuangalia historia yao ya kimaisha na kikazi.
Polisi wanapolalamika kwamba wameajiri askari polisi ambao wanashirikiana na majambazi kuwaibia na kuwadhuru wananchi ilhali tunajua kazi ya polisi inatakiwa iwe nini, hapo kunaonyesha kuna walakini mkubwa katika namna wafanyakazi katika eneo husika awanavyochambuliwa na mwishowe kuajiriwa.
Mamlaka za kodi na mapato zinavyolalamika kuna wafanyakazi walioiva na kupevuka kwa rushwa, pia tatizo ni hilo hilo, yaani, jinsi watumishi wao wanavyopatikana na jinsi wanavyochujwa ili wabakie wale walio safi.
Benki na sekta ya fedha inapolalamika juu ya wizi kushamiri katika mabenki kwa ushirkiano kati ya wafanyakazi wa taasisi za kifedha na wafanyabiashara au hata wezi ni ishara kwamba kuna ajira mbovu katika sekta husika.
Tunapolalamika juu ya utendaji kazi katika hospitali, shuleni, vyuoni na kadhalika jambo hili pia huwa ni dalili ya kuwepo kwa walakini katika masuala ya haki na wajibu wa watumishi wahusika.
Tumalizie kwa kusema kwamba rasilimali watu ambayo nchi inabahatika kuwa nayo haitoki juu mbinguni. Rasilimali hiyo inatokana na jamii iliyopo katika nchi husika.
Hivyo ni vigumu kuona kama jamii yenyewe inajikita katika uongo, ubabaishaji, uzembe, ubinafsi, uvivu, umbeya, maneno bila vitendo, kula usichokipanda na ila za kila aina, ni kwa vipi jamii hiyo inaweza kuwa na wafanyakazi wanaohitaji kuiondoa jamii yao kutoka kwenye hatua ya chini kabisa kimaendeleo na kuipeleka kwenye hatua ya juu kabisa kimaendeleo!

Warioba:‘Tumemaliza kazi yetu’

Dodoma. Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi waamue.
Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Jaji Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Alisema wamemaliza jukumu walilopewa na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge.
Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali, wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada ya kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa 1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Alisema hajui lengo la Rais kufanya alichofanya lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni ya wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012), inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda kosa kinyume na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000 (milioni mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.
Sheria hiyo inaendelea kuelekeza, (4) Hatua zozote zilizochukuliwa chini ya kifungu hiki hazitachukuliwa kuwa zimefikia ukomo na zitaendelea kuwa na nguvu ya kisheria hata baada ya Sheria hii kukoma kutumika.”
Profesa Baregu alisema sheria imezungumzia mtu yeyote, hajui kwa Rais inakuwaje.
“Sijui ameona Bunge halitoshi, haliwezi kung’amua mambo au limepungukiwa kiasi cha kushindwa kumudu majukumu yake? Sielewi ila amevunja sheria na amelivunjia Bunge hadhi yake kiasi kwamba hata kazi yake inaweza isiaminike,” alieleza.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete amejipa jukumu la kujibu na kujadili hoja za rasimu na hivyo kuwa sehemu ya Bunge Maalumu.
Alisema wakati wabunge wanahimizwa kutumia mfumo wa maafikiano katika kuamua mambo, Rais amewajengea msingi wa mgawanyiko na chuki, hali itakayoathiri mpango wa kulipatia taifa Katiba inayotokana na wananchi.
Profesa Baregu alitaja baadhi ya kauli za Rais Kikwete ambazo zinaweza kuathiri mchakato kuwa ni kujirudia kwa kauli; “Nyie ndiyo mnaotunga Katiba (Wabunge wa Bunge Maalumu) kazi imebaki kwenu.” na maelekezo kwamba serikali tatu zitapatikana, lakini labda baada ya yeye (Rais Kikwete) kuondoka madarakani.
Jaji Ramadhan
Jaji Ramadhani alisema wao Tume wamemaliza kazi yao na kwamba sasa wanawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi waamue.
“Tumemaliza kazi yetu na sasa tunawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ikitokea wajumbe wa Bunge hilo wakihitaji ufafanuzi wa jambo lolote, yeye binafsi anaahidi kutoa ushirikiano.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni juzi, alisema yeye alikuwa Arusha akishughulika na vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na kwamba hakuwa amepata muda wa kuipitia na kuitafakari kwa kiwango cha kuizungumzia.
“Ninasoma na kuitazama kupitia vyombo vya habari na ninafahamu nyie wanahabari huwa mnalenga pale palipowakuna. Hivyo nikitulia na kupata hotuba halisi aliyotoa nikaitafakari; nitaizungumzia,” alieleza.
Rais Kikwete akizindua Bunge juzi mjini Dodoma, alisema rasimu ya pili iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba ina makosa mengi ya kiuandishi.
Alisema ina mambo mengi, baadhi yalitakiwa kuwekwa kwenye Sheria.
“Mbolea, mbegu, pembejeo vyote vimewekwa humo, hata umri na haki ya mtoto kupewa jina vinawekwa humo, yakiwekwa yote kama yalivyo, serikali haitaweza kuyatekeleza itashtakiwa mahakamani kila wakati,” alieleza.
Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu kusoma neno kwa neno, mstari kwa mstari na kujiridhisha na mambo watakayoidhinisha yaingie kwenye Katiba itakayopendekezwa.
Alisema watakachoona kinafaa kurekebishwa, kuboreshwa au kufutwa wasisite kufanya hivyo kwa sababu inatakiwa Katiba bora, inayotekelezeka na ambayo haitalalamikiwa kiasi cha kulazimika kuibadilisha muda mfupi baada ya kupitishwa.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, alisema wakichagua Serikali tatu watatakiwa kuondoa mambo yote yanayoweza kukanganya utendaji wa Serikali za washirika na ile ya Muungano. Lakini wakichagua Serikali mbili, mengi yatatekelezeka.
Rais Kikwete alisema serikali zote mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba kutatua mambo matatu kati ya sita ambayo bado hayajatatuliwa kutoka kwenye orodha ya kero 31 za Muungano zilizoainishwa na Zanzib

Tuesday, 18 March 2014

Bunge lachafuka, Warioba asimama bila kuwasilisha Rasimu ya Katiba

Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana jioni alisimama kwa dakika tatu mbele ya kipaza sauti lakini akashindwa kuwasilisha Rasimu ya Katiba kutokana na vurugu zilizojitokeza bungeni.
Vurugu hizo zilitokea muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kumwalika kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa muda wa dakika 120.
Jaji Warioba alisimama kwenye mimbari ya Bunge saa 11:02 jioni tayari kuhutubia lakini kabla ya kufanya hivyo, wajumbe kadhaa walisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti.
Waliosimama ni Profesa Ibrahimu Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sitta aliwanyima fursa akisema: “Hakuna mwongozo hapa, naomba Mwenyekiti uendelee, waheshimiwa wabunge hakuna mwongozo naomba Mwenyekiti uendelee kwa ajili ya hansard.”
Kauli hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa kwani Jaji Warioba alipowasha kipaza sauti tayari kuanza kuhutubia, baadhi ya wajumbe walianza kupiga kelele, wengine makofi na kugonga meza hivyo kumfanya ashindwe kufanya kazi hiyo ya uwasilishaji.
Waliokuwa mstari wa mbele kupinga Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa sehemu kubwa walikuwa ni wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Jaji Warioba akiwa anatafakari mbele ya mimbari, Sitta aliwasha kipaza sauti na kumtaka aendelee kuwasilisha Rasimu ya Katiba ... “Endelea Mwenyekiti, endelea kwa ajili ya kumbukumbu rasmi (hansard).”
Lissu akisikika akijibu kauli hiyo akisema: “Fuata kanuni mwenyekiti... fuata kanuni mwenyekiti,… huku akipiga kelele na kugonga meza na wakati huo Profesa Lipumba akiwa amewasha kipaza sauti chake kutaka kuzungumza huku naye akiendelea kupiga meza kwa nguvu.
Wengine waliosimama ni Mchungaji Christopher Mtikila, Ezekiel Oluoch, Philimon Ndesamburo, Moses Machali na Mchungaji Peter Msigwa.
Dakika tatu zilikatika huku kukiwa hakuna dalili za hali kutulia na kuona hivyo, Jaji Warioba aliamua kuondoka kwenye mimbari na kuketi kimya akiwa na Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhani.
Baada ya hapo, Sitta alisimama na kuwasha kipaza sauti na kusema: “Waheshimiwa wajumbe, katika mazingira haya tuliyonayo, naomba kutangaza kuwa nasitisha shughuli za Bunge hadi hapo tutakapotangaziwa tena.”
Licha ya kauli hiyo, baadhi ya wajumbe waliendelea kupaza sauti zao wakisema kwamba walikuwa wanaburuzwa.
Wakati hayo yakitokea, kikosi cha askari wa Bunge kiliingia ndani ya ukumbi na kusimama katika lango kuu hali iliyoonekana kuwa ni kuchukua hadhari endapo hali ya usalama ingechafuka.
Baada ya tamko la kuahirisha mkutano, askari hao waliingia moja kwa moja hadi alipokuwa ameketi Jaji Warioba na kumsindikiza hadi nje na jitihada za waandishi wa habari kumfuata ili kupata maoni yake hazikufanikiwa.
Kilichofuata baada ya hali hiyo ni kurushiana maneno kwa baadhi ya wajumbe akiwamo Dk Ave Maria Semakafu ambaye nusura azipige kavukavu na mjumbe mwingine ambaye jina halikuweza kupatikana mara moja.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe akiwamo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani waliamulia ugomvi huo kabla ya kuwa mkubwa.
Wajumbe walionekana kukaa katika vikundi ndani ya Bunge huku wakijadiliana juu ya kilichotokea wakati Sitta, Katibu wa Bunge, Yahaya Khamis Hamad na msaidizi wake, Dk Thomas Kashililah wakiwa katika kikao cha faragha.
Baada ya kujadiliana kwa nusu saa, Hamad akiwa ameongozana na Dk Kashililah, alirejea katika ukumbi wa Bunge na kuwataka wajumbe kutawanyika hadi hapo watakapojulishwa.
Hali hiyo iliibua kelele kutoka kwa wajumbe wakitaka kujua iwapo waondoke katika maeneo ya Bunge au la. Hamad alisisitiza kwamba warejee nyumbani hadi hapo watakapojulishwa.