Dodoma/Dar. Suala la ama kutumia kura ya siri
au ya wazi kuamua ibara za Rasimu ya Katiba jana liliuteka upya mjadala
wa Kanuni za Bunge la Katiba, huku ikielezwa kuwa limewekwa kama mtego
kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika kuwania urais.
Sitta ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika
kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia CCM, huku
akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wake kisiasa ndani ya
chama hicho.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Godbless Lema alimtaka
Sitta kuwa makini na maelekezo aliyodai mwenyekiti huyo anapewa katika
uendeshaji wa Bunge na kudai pia kuwa, kuna kundi la watu wanaotaka
urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 wanaotaka kumkwamisha.
Akichangia hoja ya mapendekezo ya mabadiliko ya
kanuni yaliyotaka kupitishwa mifumo miwili ya kura kwa wazi na siri,
Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha alisema kwa mazingira ambayo
yanaendelea, Sitta anapaswa kuwa makini na watu wanaompatia maelekezo
wakitaka aonekane hafai baadaye.
“Ni vyema ukawa makini na mapendekezo unayoletewa
kwa sababu hao wote pamoja na wanachama wa chama chako wanajua kama
utaliongoza vizuri Bunge hili, basi unaweza ukapata tiketi ya kugombea
urais 2015 ndani ya chama chako, lakini ukishindwa watakudhihaki kuwa
umeshindwa, hivyo hutaweza kuliongoza taifa,” alisema Lema huku Sitta
aliyeonekana awali akitabasamu, alibadilika na kumtazama mbunge huyo kwa
umakini.
Lema alisema miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ya
CCM na kamati nyingine za Bunge hilo, kuna watu ambao wanataka kugombea
urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika mjadala huo, ilionekana wazi kuwa wajumbe
bado wamegawanyika pande mbili – CCM wakionekana kuunga mkono kura ya
wazi na upande wa upinzani wakipigia chapuo kura ya siri.
Miongoni mwa waliopigia debe kura ya siri ni John
Mnyika aliyesema suala la upigaji kura ni la kikatiba ili kuhakikisha
kila mjumbe anapiga kura yake bila kushurutishwa, kushinikizwa wala
kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au chombo chochote.
Wajumbe hao walikuwa wanajadili mapendekezo
yaliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za
Bunge, Pandu Ameir Kificho, baada ya juzi kuzua mvutano uliosababisha
Bunge hilo kuvunjika ili kusubiri maridhiano ya pande zinazopingana.
Mapendekezo ya Kanuni
Kificho alisema, mapendekezo hayo yamefikiwa
kutokana na masharti ya kanuni ya 59 (1) na 87 (1) kwamba kanuni ya 38
(1) iweke utaratibu wa kupiga kura ama ya wazi au ya siri, ambao
utatekelezwa na mwenyekiti kwa kushauriana na katibu.
Alisema wakati wa kupiga kura ya siri kila mjumbe
atapiga kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ kwa kutumia karatasi ya kupigia kura
itakayokuwa imeandaliwa na katibu kwa ajili ya hilo.
Mjumbe Michael Laizer alisema wamechoshwa na malumbano juu ya
kura za wazi au siri, hivyo iwapo kuna wajumbe ambao hawataki
mapendekezo ya kamati waondoke.
Naye Ezekiel Olouch alisema utaratibu unaopendekezwa na kamati haujawahi kufanyika mahala popote duniani.
Alisema kura ya siri imekuwa ikitumika kuamua
mambo ya msingi na kuepusha mpasuko katika jamii hasa katika masuala
ambayo yanaweza kuligawa taifa.
Mohamed Raza alisema msimamo wake ni kupiga kura ya wazi kwani wengi wanajua msimamo wake ambao ametoka nao Zanzibar.
Joshua Nassari alisema anashangazwa kuona Taifa
linarejeshwa katika karne ya 18 katika upigaji wa kura kwa kung’ang’ania
kura ya wazi wakati wao wamechaguliwa kwa kura za siri.
“Mwenyekiti wewe tumekuchagua kwa siri wajumbe
wote wamepatikana kwa siri, iweje leo kulazimisha kura ya wazi ili
wajumbe wa CCM watakaopiga kura za siri wachukuliwe hatua,” alisema
Nassari.

No comments:
Post a Comment