Sunday, 22 December 2013

Wabunge wa CCM wamgomea Waziri Mkuu Pinda

Dodoma. Wabunge wa CCM jana mchana walimgomea Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge (Party Cocas) ya chama hicho, Mizengo Pinda na kushinikiza mawaziri watatu ambao wizara zao zimetajwa kushindwa kusimamia vyema Operesheni Tokomeza Ujangili wajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa mawaziri walioshinikizwa kujiuzulu wenyewe ni pamoja na Balozi Khamisi Kagasheki ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dk Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani)  na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni jana kiliitishwa na Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu kwa lengo lililoelezwa ni kuwapoza wabunge.
Chanzo cha habari kutoka katika kikao hicho kilisema kuwa wabunge hao walitaka mawaziri hao kujiuzulu wenyewe ili kukinusuru chama  mbele ya wananchi.
“Tumemtaka Waziri Mkuu akakae na wenzake na kutuambia kama wanajiuzulu au la na kutupa jibu kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, mtasikia wenyewe baadaye ndani ya Bunge,”kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa kikao hicho na wabunge kurejea bungeni, Pinda hakurejea bungeni, badala yake ilidaiwa kwamba alikuwa na kikao katika ofisi zake zilizopo bungeni.
Hadi  saa 11.25 alasiri  wakati kikao cha Bunge kikiendelea Waziri Mkuu alikuwa hajarejea bungeni, huku ikielezwa kwamba katika kikao alichokuwepo hakikuwahusisha mawaziri wanne waliokuwa katika shinikizo la kujiuzulu.


Malipo ya fidia yawatoa machozi wananchi Dar

Dar es Saalam. Wananchi wa Mji Mpya Majohe, Guluka Kwalala na Ulongoni katika Manispaa ya Ilala  wameiomba Serikali kuingilia kati na kumwamuru mwekezaji wa ujenzi wa njia ya umeme wa  kilovoti 220 kutoka Somanga Mtama  mpaka Kinyerezi, Kilwa Enegy kuwalipa gharama zinazoendana na hali ya maisha ya sasa.
Ombi hilo walilitoa  jana walipokuwa wakijadili kuhusu  dodoso la uhakiki wa mali zao na malipo, walilopewa lilivyokuwa na  upungufu, mapunjo ya mali zao hasa thamani  za nyumba kuwa kidogo  tofauti na gharama  za ujenzi na ununuzi wa kiwanja walizotumia.
Utathmini wa mali na nyumba za wananchi unadaiwa kufanywa na kampuni binafsi iliyofahamika kwa jina la Joransa, ambapo tathmini katika maeneo hayo ilifanyika mwaka 2011 na kutolewa ahadi kuwa malipo ya fidia yangeanza kulipwa baada ya miezi mitatu .
.Baruani Kanoze  akilalamikia kulipwa  fedha kidogo tofauti na thamani ya mali zake, alisema mwekezaji huyo awali aliwahi kusema kuwa atawalipa kwa kiwango kinachoendana na gharama za maisha zilivyo kwa wakati husika jambo ambalo limewashangaza sana. hasa kulingana na kiwango cha malipo kilichotolewa.
‘Ni jambo ambalo haliingii akilini baada ya kuangalia karatasi za tathmini na kukuta gharama zilivyowekwa za viwanja na kupangisha nyumba, kiwanja umewekewa Sh1 milioni na gharama ya kupanga nyumba eti Sh20,000 kwa mwezi, sijui unakwenda kupanga wapi nyumba’ alisema mkazi wa Guluka Kwalala ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
 Alisema yeye anamiliki nyumba ya vyumba  vitano, yenye umeme, choo bora pamoja na  kisima cha maji alivyovijenga   kwa zaidi ya Sh40 milioni,  kwenye dodoso la uhakiki wa mali  anaambiwa thamani ya nyumba yake ni Sh6 milioni.
Aidha, walishauri kuliko Serikali kujiingiza katika maafa kwa kukubali mradi huo utekelezwe wakati wananchi hawajaridhika na fidia ao, ni vyema ikafanyika tathmini nyingine ambayo itakuwa ya haki .
Hata hivyo, uongozi wa Kilwa Energy ulipotafutwa kufafanua malipo hayo ya wananchi, simu zao hazikuweza kupatikana.

Kufutwa kodi ya simu, Bunge aibu tupu

Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutia saini hati ya dharura ili Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho na kuondoa tozo ya kodi kwa laini za simu imeliacha Bunge katika fadhaa na fedheha kubwa.
Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2013 lilishuhudia wabunge wa chama tawala wakitumia wingi wao bungeni kupitisha kodi hiyo ambayo iliamsha hasira na vilio kutoka kwa wananchi kutoka kila kona ya nchi.
Tunasema hatua hiyo ya Rais imeleta fadhaa na fedheha kwa Bunge kutokana na kuwapo matukio mengi ya aina hiyo katika kipindi kifupi, ambapo Bunge limekuwa likipitisha miswada mingi muhimu kwa ushabiki wa kisiasa badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa. Rais kwa kuwasitiri  wabunge wa chama chake amekuwa akitia saini miswada hiyo na kuwa sheria, lakini baadaye amekuwa akisikiliza hoja za wapinzani na kulazimika kurudisha sheria hizo bungeni ili zifanyiwe marekebisho.
Siyo nia yetu hata kidogo kuorodhesha hapa sheria zote ambazo Rais amezirudisha bungeni kufanyiwa marekebisho katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, wasomaji wetu watakumbuka kuwa, moja ya sheria nyeti zilizorudishwa bungeni ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo hasa iliyoanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya yapata miezi 18 iliyopita. Kama tulivyosema hapo juu, muswada wa sheria hiyo na miswada mingine mingi muhimu ilipitishwa na Bunge kwa ushabiki wa kisiasa na kiitikadi, kwa maana ya hoja za wabunge wa upinzani kuzimwa au kujadiliwa kwa kejeli, vijembe na matusi na hatimaye kupuuzwa.
Ni katika muktadha huo, Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 iliyoanzisha tozo ya kodi kwa laini za simu inapaswa kuangaliwa. Bunge kwa staili hiyohiyo ya ushabiki wa kisiasa na kiitikadi lilipitisha muswada wa sheria hiyo, huku wabunge wa upinzani wakipinga na kuainisha athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa. Ni kweli Rais alisaini muswada huo na kuwa sheria, lakini kutokana na athari zake kwa uchumi na wananchi kwa jumla, sasa  ameirudisha bungeni kwa hati ya dharura akitaka ifanyiwe marekebisho na kuifuta kodi hiyo mara moja.
Ni aibu kwa Bunge, Serikali na Kamati ya Bajeti iliyobuni tozo hiyo kutoona mapema madhara ambayo yangesababishwa na kodi hiyo ya Sh1,000 (kwa kila laini ya simu kila mwezi) kwa wananchi maskini ambao  wanahangaika kupata mlo mmoja kwa siku. Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutojua hali halisi ilivyo, hasa vijijini walikaririwa bungeni wakitetea kwa nguvu hoja ya kuwekwa kwa tozo hiyo,  wakidai kila mwananchi anao uwezo wa kuilipa kila mwezi.
Kutokana na utata uliosababishwa na tozo hiyo, kodi hiyo ilikuwa haijaanza kulipwa mpaka sasa, licha ya Bunge kupitisha muswada huo Julai, mwaka huu. Rais Kikwete baadaye aliingilia kati kwa kuagiza mamlaka zote husika  kukutana mara moja kumaliza mvutano wa kodi hiyo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya kodi ili kuziba pengo la Sh178 bilioni ambazo zingetokana na kodi kwenye laini za simu. Ni matarajio yetu kwamba Bunge letu litakuwa limepata somo la kutosha, hivyo litakuwa makini siku zijazo kwa kuhakikisha linapitisha miswada pasipo hila wala ushabiki wa kisiasa.

Wednesday, 18 December 2013

Wabunge waliokwepa safari watakiwa kurejesha posho

Dodoma.Sakata la wabunge waliochukua posho kwa ajili ya safari za mafunzo nje ya nchi na kuacha kusafiri, limeingia hatua mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wazirudishe.
Katika orodha ya wabunge wanaotajwa katika sakata hilo, wamo baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha NCCR-Mageuzi.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita mjini Dodoma na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).
Keissy alisema baadhi ya wabunge wanapaswa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kuchukua posho za safari za nje ya nchi lakini hawakwenda safari hizo.
Mbunge huyo alifafanua kuwa mbali na kutokwenda kabisa safari hizo, lakini wapo ambao walikwenda na hawakukaa siku zote zilizopangwa.
“Tunawajua na wapo humu ndani,” alisema huku baadhi ya wabunge wakipaza sauti wakitaka awataje, lakini yeye akasema siyo jukumu lake kuwataja kwani Ofisi ya Bunge inawajibika kufanya hivyo.
Mbunge huyo alienda mbali na kudai mbunge mmoja alikatisha safari ya kwenda Marekani na kuamua kwenda Dubai kwa safari binafsi ambayo haikuwepo katika ratiba ya ziara hiyo ya mafunzo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema wabunge wanane walichukua posho ya safari ya kati ya Sh5 milioni na Sh6 na Spika amewaandikia barua akiwataka warudishe fedha hizo.
Majina ya wabunge hao tunayo, lakini kwa sababu za maadili ya uandishi wa habari, gazeti hili halitaweza kuwataja kwa kuwa hawakupatikana ili kujibu tuhuma hizo kama maadili yanavyoelekeza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa Spika ameshaliona jambo hilo na kulichukulia hatua za kiutawala.
“Spika amewaandikia barua akiwataka kurejesha fedha zote za safari ambazo hawakwenda. Ni lazima wazirudishe hakuna namna,” alisema Joel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge.
Alipoulizwa kuhusiana na majina yao na kiasi walichochukua, Joel alisema hilo ni jambo la kiutawala na kwamba Spika ndiyehuarifiwa na kamati kuhusiana na wabunge ambao hawakusafiri.
“Spika ndiye anayearifiwa na wenyeviti wa kamati husika juu ya wabunge waliosafiri na wasiosafiri kwa sababu wao ndiyo wanapanga safari na sisi tunawapa posho,” alisema.
Akizungumzia malalamiko ya wabunge juu ya baadhi ya wabunge wasiofika bungeni kusaini ili wapate posho ya kikao, Joel alisema tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Lilikuwepo lakini limepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kugundua wakifika kwenye malipo majina yao waliosainiwa yamekatwa,” alisema Joel.
Alipoulizwa kuhusiana na tatizo hilo la kupokea posho za safari za nje ya nchi bila kwenda, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo.
“Lakini muhimu hapa ni Bunge kuandaa utaratibu wa kurejesha mrejesho wa jinsi walivyozitumia na hapo ndipo watagundulika wabunge wanaosafiri kweli na muda waliokaa mahali husika,” alisema Lissu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye anatajwa kuwemo kwenye orodha ya wabunge waliopokea posho bila kusafiri, alikiri na tayari alishamuandikia barua Katibu wa Bunge akimueleza kwamba hakusafiri na kuomba utaratibu wa kurejesha fedha hizo.
Nasari alisema yeye alikuwa Jimboni kwake kwa shughuli za wananchi wake, hivyo hakuweza kusafiri na suala hilo alilifikisha mapema kwa Katibu ili ampe maelekezo namna ya kurejesha fedha hizo.

Slaa: Aliyeteua mawaziri mizigo awajibishwe

Tabora. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad Slaa amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisitafute dawa ya mawaziri ‘Mizigo’ badala yake wamwajibishe aliyewateua hao wanaowaita mzigo.
Alisema badala ya kuwahangaisha Watanzania kwa kujadili majina ya mawaziri mizigo, wanapaswa kuchukua hatua za kinidhamu kama wana uhakika na mawaziri hao na kushauri kuangalia upatikanaji wao hadi kufikia nafasi hizo nyeti za kuwatumikia watu.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui mjini Tabora juzi,Dk Slaa alisema kinachoendelea ndani ya Serikali hivi sasa ambacho kinaitwa ‘mawaziri mizigo’ ni moja ya dalili ya tatizo katika mamlaka ya uteuzi alibainisha pia kuwa, kuwatimua mawaziri hao siyo dawa bali kushughulikia chanzo cha tatizo.
Amesema kwa muda mrefu Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa lawamani kutokana na kushindwa kazi kwa mawaziri wake, jambo ambalo Dk Slaa amesema, limetokana na kutofanyika kwa umakini wa kuzingatia vigezo, bali uswahiba.
Alisisitiza kuwa kinachofanyika sasa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuzunguka nchi nzima na kutaja majukwaani mawaziri mzigo ni njia ya kusukuma agenda ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri,lakini rais anapaswa kuchukua uamuzi sahihi wakati wa kuwawajibisha hao ‘mizigo’ ambao ni maswahiba.
Dk Slaa anaendelea na ziara ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama hicho mkoani Tabora,juzi alitembelea maeneo ya Ugoweko, Kakola na Tabora mjini na kudai kuwa mabadiliko ya mara kwa mara ya Baraza la Mawaziri katika Serikali ya Rais Kikwete hayana tija kwa Watanzania na ni dalili za tatizo la ukosefu wa uwajibikaji.

Mawaziri matumbo joto

Dodoma.Kamati ya Bunge ya kuchunguza athari za Operesheni Tokomeza Ujangili inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake leo, ambayo inaelezwa kuwa imependekeza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya vigogo kadhaa wa Serikali.
Taarifa ya kamati hiyo ndogo itasomwa leo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili itakapokuwa inawasilisha taarifa yake ya utendaji kazi bungeni.
Wajumbe wengi wa kamati hiyo ndogo wanatokana na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa uchunguzi wa kamati hiyo umegundua udhaifu mkubwa katika wizara na idara za Serikali.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli imependekeza kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya maofisa waandamizi wa Wizara za Maliasili na Utalii na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Mjumbe huyo alisema kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii, watakaoguswa na ripoti hiyo ni baadhi ya maofisa waandamizi wanaosimamia wanyamapori na hata wale wa maliasili.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Novemba 25, mwaka huu inawasilisha ripoti yake baada ya kumaliza kazi ya kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo mawaziri watatu ambao wizara zao zilihusika moja kwa moja na operesheni hiyo.
Mawaziri waliohojiwa katika Hoteli ya Bahari Beach, Dar es Salaam ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilisema kuna uwezekano mkubwa taarifa hiyo ‘ikamkaanga’ Dk Mathayo kutokana na mapendekezo ya wabunge katika mkutano wa 13.
Wabunge walikerwa zaidi na kauli ya Dk Mathayo alipopata fursa ya kuchangia taarifa ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili na kuishia kuwapa pole wafugaji ambao mifugo yao iliuawa kwa risasi.
Katika operesheni hiyo, wabunge walipaza sauti wakidai wapo raia wasio na hatia waliouawa na kuteswa, huku mifugo ikiporwa na mingine kama ng’ombe ikiuawa kwa kupigwa risasi.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ndiye aliyekuwa mwiba kwa mawaziri hao aliposema ana kitabu kilichosheheni ushahidi dhidi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Habari zaidi zinasema kamati hiyo ya uchunguzi imelazimika kutofanyia shughuli zake katika kumbi za Bunge ili kukwepa vishawishi kutoka kwa watu wa karibu na vigogo wanaotuhumiwa.
“Wamejificha katika hoteli moja tangu waliporudi Dodoma wiki iliyopita ili kuandaa ripoti yao kwa sababu hawataki kuingiliwa ingiliwa na hili ndilo linalowatia hofu mawaziri,” alisema mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, pamoja na kasoro za operesheni hiyo, ilisaidia kuwabaini maofisa walioko katika mtandao wa ujangili na baadhi yao walikamatwa na nyara za Serikali.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alithibitisha kuwasilishwa kwa ripoti hiyo leo wakati kamati itakapowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake... Hata hivyo, alisema hana uhakika wa asilimia 100. Ripoti hiyo itawasilishwa huku kukiwa na vuguvugu la kung’olewa kwa mawaziri saba wanaodaiwa mzigo katika utendaji wao na tayari wamehojiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana wiki iliyopita chini ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete.
Mbali na vuguvugu hilo, ripoti ya uchunguzi pia inawasilishwa wakati tayari Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri watatu wajipime kama bado wanatosha kuongoza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mawaziri hao ni Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Manaibu wake, Aggrey Mwanry na Kassim Majaliwa. Ripoti kama hiyo inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo na Lembeli ndiyo iliyochangia kumng’oa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kutokana na kashfa ya ugawaji vitalu vya uwindaji.

Upangaji madaraja kidato cha 4 gizani

Dodoma.Serikali bado haijaamua utaratibu utakaotumika katika kupanga madaraja ya watahiniwa wa mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwaka huu.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema juzi jioni katika Viwanja vya Bunge kuwa, uamuzi juu ya utaratibu utakaotumika kupanga matokeo hayo utaamuliwa katika vikao vya watendaji wa wizara hiyo.
“Baada ya mkutano wa Bunge kumalizika, tutakwenda kukaa na kuamua utaratibu tutakaotumia lakini sasa sina majibu,” alisema na kuongeza kuwa baada ya wiki mbili atakuwa katika nafasi ya kusema utaratibu utakaotumika kupanga matokeo hayo.
Hivi karibuni Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, katika taarifa yake ya utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha Machi hadi Desemba 2013, iliitaka Serikali kusitisha utaratibu mpya wa upangaji wa matokeo ya mitihani.
Mabadiliko hayo, daraja ziro ambalo kwa muundo wa zamani lilikuwa na alama 34-35 sasa litakuwa daraja la tano likiwa na alama 48-49.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alikaririwa na vyombo vya habari akisema muundo huo mpya utatumika kwa mzunguko katika kipindi cha miaka minne.
Daraja la kwanza halijaathiriwa na muundo mpya, kwani alama zake zimebaki pale pale ambazo ni 7-17. Daraja la pili alama za muundo wa zamani zilikuwa 18-21 na sasa ni 18-24. Alama za daraja la tatu zilikuwa 22-25 na chini ya muundo mpya zitakuwa 25-31, wakati daraja la nne alama zimebadilika.

Thursday, 5 December 2013

Wingu jeusi chadema: Zitto amlima barua Dk Slaa


Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika sura mpya baada ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari `Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni) huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha na kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza Zitto katika taarifa yake.


Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala hilo.
“Hasa pale ambapo tumeambiwa waraka huu umetoka makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti iliyosheheni watu mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu katika idara hii kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa yanayokigusa chama, vipi makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?” aliandika Dk Mkumbo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook jana na kuthibitisha kwa simu.
Dk Kitila alisema pamoja na umaskini wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
“Taarifa zinazosambazwa kuhusu mimi ni za uongo wa kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni wazi kwamba wanaosambaza habari chafu kunihusu hawanijui na ndiyo maana wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi Kitila Mkumbo naweza kuhongwa Sh200,000.”
Alihoji pia Chadema ilikuwa na siri gani za hatari kiasi cha kumfanya Zitto, ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi kuhongwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
“Zitto anajua kuwa Andrea Cordes aliniandikia baruapepe na nakala kwake nikawajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa na makao makuu ya chama na tukipokea malalamiko rasmi tutachunguza kwa sasa chama kinaichukulia ripoti hiyo kama ripoti nyingine zinazosambazwa mitandaoni,” alifafanua Mnyika.
Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo, Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa na malalamiko.
Alisema baada ya taarifa hiyo ya siri kusambaa mtandaoni, Zitto alitoa kauli na kama Dk Mkumbo hakuridhika, alipaswa kuonana na watu wa Idara ya Uenezi ya Chadema.
“Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema Mnyika.

Watanzania changamkieni fursa hizi Burundi

Moja ya sababu kuu za kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ni kutoa wigo mpana wa soko na shughuli za kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama.
Tanzania na Burundi ni kati ya nchi tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi nyingine wanachama ni Kenya, Uganda na Rwanda, wakati nchi ya Sudan Kusini ikiwa imetuma maombi rasmi ya kujiunga.
Hivi karibuni, EAC iliandaa mafunzo ya siku tano kwa waandishi 25 wa Ukanda huo, mafunzo yaliyoambatana na mkutano wa pili wa siku tatu kuhusu Amani na Usalama miongoni mwa nchi wanachama.
Nilipata fursa ya kuwa kati ya waandishi watano waliowakilisha Tanzania kwenye mafunzo hayo yaliyolenga kuwanoa wanahabari namna ya kuandika habari za machafuko na migogoro bila kuleta madhara kwa jamii.
Pamoja na mafunzo, waandishi wa habari kutoka Tanzania walipata fursa ya kutembelea ubalozi wa Tanzania nchini Burundi. Walipata fursa ya kujifunza mambo kadhaa, mojawapo ni fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Burundi.
Katika mazungumzo yake na ujumbe wa waandishi wa habari kutoka Tanzania, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk James Mwasi Nzagi pamoja na mengine alizungumzia fursa ambazo Watanzania wanapaswa kuzichangamkia hivi sasa.
Uwekezaji katika sekta ya elimu, hasa lugha ya Kiswahili
Burundi ikiwa moja ya nchi zinazoongea lugha ya Kifaransa na Kirundi kama lugha rasmi ya kiofisi na mawasiliano, imeanza kutilia mkazo lugha za Kiswahili na Kiingereza ambazo ni lugha rasmi ya mawasiliano ndani ya EAC.
Serikali ya Burundi hivi sasa inahimiza wananchi wake kujifunza na kumudu lugha za Kiswahili na Kiingereza. Lugha hizo zinapaswa kufundishwa kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikizalisha idadi kubwa ya wahitimu katika sekta ya elimu kuanzia ngazi ya cheti, diploma na shahada.
Uzalishaji nishati ya umeme
Baada ya kumalizika kwa vita na machafuko, nchi ya Burundi hivi sasa inaelekeza nguvu nyingi kwenye kujenga na kuinua uchumi wa Taifa hilo kwa kuhimiza uwekezaji katika sekta ya viwanda, hasa vya uzalishaji.

Hata hivyo, juhudi hizo za serikali zinakwamishwa kwa kukosekana kwa nishati ya umeme ya uhakika, hali inayofanya viwanda vingi kutumia umeme unaozalishwa kwa kutumia jenereta.
Matumizi ya umeme wa jenereta hunasababisha bei ya bidhaa za viwandani kuwa kubwa kiasi cha kupunguza uwezo wa ununuzi kwa wananchi wa kawaida wa Burundi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 9 milioni.
Huduma katika sekta ya hoteli za kitalii na kumbi za mikutano
Kutokana na kukua kwa kasi kwa uchumi wa Burundi na uwepo wa mikutano ya kimataifa na wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa na mabalozi wa nchi mbalimbali, ujenzi wa hoteli za kitalii nchini humo, hasa Mji Mkuu, Bujumbura umeanza kwa kasi na hivyo kusababisha uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi.
Sekta ya usafirishaji wa anga, barabara, reli na majini
Burundi ina mikoa 17 ambayo yote imeunganishwa kwa barabara ya lami na hivyo kutoa fursa ya uwekezaji katika sekta ya usafirisha wa mizigo na abiria kwa gharama nafuu.
Barabara za lami ambazo zote zimeunganishwa na Mji Mkuu, Bujumbura ni fursa nyingine ya kibiashara kati ya mikoa mingine, wilaya na vijiji vya Burundi kwa Watanzania wanaofanya biashara ya usafirishaji abiria na mizigo kwa njia ya barabara.
Usafiri wa Anga
Hadi sasa hakuna ndege zinazofanya safari ya moja kwa moja kutoka Bujumbura hadi Jijini Dar es Salaam ambapo abiria wote hulazimika ama kupitia Nairobi Kenya, Kampala Uganda au Kigali Rwanda ndipo waweze kufika Dar es Salaam au miji mingine nchini.
Usafiri wa maji (meli)
Tanzania na Burundi zinaunganishwa na Ziwa Tanganyika na hivyo kutoa fursa ya uwekezaji kwenye sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji.
Hivi sasa meli pekee inayotoa huduma ya usafiri kati ya Burundi na Tanzania ni Mv Liemba ambayo umri wake ni zaidi ya miaka 50

Sekta ya Gesi, hasa za hospitalini
Kuna tatizo la upatikanaji wa uhakika wa gesi za hospitalini ambapo wakati mwingine taifa hilo hulazimika kupata huduma hiyo kutoka nchini Kenya.
Kutokana na Tanzania kufanikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa nishati ya gesi, hii ni fursa nyingine ya uwekezaji na kibiashara kwa Watanzania wenye uwezo, ujuzi, utaalamu na uzoefu katika biashara hii kujitanua katika soko la Burundi.
Uwekezaji katika viwanda vya Saruji
Hadi sasa, hakuna kiwanda cha Saruji nchini Burundi. Saruji yote inayotumika nchini humo huagizwa kutoka nje ya nchi na hivyo kufanya saruji kuwa moja ya bidhaa adimu na muhimu.
Kiwanda cha kutengeneza vyuma
Vyuma vyote vinavyotumika Burundi huagizwa kutoka nje ya nchi, hasa nchini Ukraine. Mfanyabiashara atakayejenga kiwanda cha chuma atakuwa na uhakika wa soko.
Kiwanda cha kutengeneza viatu
Kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, suala la utengenezaji na uvaaji wa viatu nchini Burundi bado liko katika viwango visivyoridhisha na siyo ajabu kukuta watu wazima wakitembea pekupeku katika mitaa ya mji mkuu wa Bujumbura.
Siyo kwamba wananchi nchini Burundi wanatembea peku kwa kupenda. La hasha!
Bei ya viatu iko juu kiasi kwamba wananchi wenye kipato cha chini hushindwa kumudu kununua viatu ambavyo vingi huagizwa kutoka nje ya nchi.
Hii ni fursa mwafaka kwa Watanzania wenye uwezo kuwekeza kwenye eneo hili kwani siyo tu watajihakikishia soko la Burundi lakini pia wataweza kujipenyeza hadi kwenye soko la nchi jirani ya Rwanda ambako tayari Rais wake, Paul Kagame amepiga marufuku watu kutembea peku katika mitaa ya mji mkuu, Kigali.

Kushika soko la Burundi ni njia ya kuingia soko la DRC.
Kutoka mji mkuu wa Burundi, Bujumbura hadi mpakani na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ni chini ya Kilomita 20 pekee. Ukaribu huu unafanya wafanyabiashara nyingi kuingiliana kati ya Burundi (Bujumbura) na DRC na hivyo kuongeza fursa za kibiashara kwa Watanzania watakaowekeza Burundi.
Baadhi ya taarifa muhimu
Ukubwa wa nchi na idadi ya watu:
Nchi ya Burundi iliyopata uhuru Julai Mosi, 1962, ina ukubwa wa kilomita za mraba 28,000 na idadi ya watu zaidi ya 8 milioni.
Makabila Makuu Burundi
Wahutu: Hili ndilo kabila linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu nchini Burundi kama ilivyo nchini Rwanda. Inakadiriwa kuwa kabila hili ni asilimia 85 ya wananchi wote Burundi.
Kiasilia, Wahutu ni Wabantu ambao hujihusisha na kilimo kama njia kuu ya kipato pamoja na ufugaji kwa kiwango kidogo.
Watutsi: Hili ni kabila linalofuata kwa uwingi wa watu nchini Burundi ikiwa na asilimia 14 ya wakazi wote wa nchi hiyo. Asili yao ni ufugaji ingawa pia wanashiriki shughuli za kilimo.
Watwa: Hili ni kabila dogo lenye asilimia moja tu ya wakazi wa Burundi ingawa ndilo kabila la watu wa asili nchini humo.
Kiasilia Watwa ni wawindaji, warina asali na waokota matunda (hunters and gatherers) kama walivyo makabila ya Wahadzabe, Wandorobo, Wasandawe kwa hapa Tanzania.
Chakula: Chakula kikuu nchini Burundi ni ugali na matoke inayoliwa kwa nyama, mboga za majani na samaki wanaopatikana Ziwa Tanganyika, hasa mukake ambao kwa Tanzania, hasa kwa wakazi wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi hujulikana kwa jina la migebuka
Burundi pia imejaaliwa kuwa na uwingi wa aina mbalimbali za matunda na vyakula vitokanavyo na mizizi kama mihogo, viazi vitamu na viazi mviringo.
Kilimo:Mazao ya kilimo na chakula Burundi ni pamoja na kahawa, pamba, chai, mahindi, mtama, ndizi na viazi vitamu.
Muziki:Muziki maarufu unaopendwa na wananchi Burundi ni ngoma ya Karyenda ambayo huchezwa kwa mtindo wa kuvutia ukishirikisha wanawake na wanaume.
Ukiwa Burundi ekupa kuuliza zilipo kambi za jeshi au ofisi za usalama. Tofauti na Tanzania ni kawaida kumsikia mtu akisema kambi ya jeshi ya Mgulani, oohh Morogoro kuna kambi ya mizinga n.k. Aidha, huruhisiwi kupiga picha mitaani bila kibali cha Meya wa mji, kwa sababu za kiusalama.

Polisi yaituhumu Chadema moto Arusha,Lema aja juu

Arusha.Polisi mkoani Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama wa chama hicho ndio waliohusika.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amepinga kauli hiyo na kulipa jeshi hilo siku nne kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa watano baada ya kulipatia majina hayo akidai kuwa ndio wanaohusika na uchomaji moto ofisi za chama hicho.
“Tumewapatia polisi majina... tunaamini walihusika moja kwa moja la sivyo, chama kitatumia vijana wetu wa Red Brigade kuwakamata na kuwafikisha polisi,” Lema aliwaambia waandishi wa habari jana.
Ofisi cha Chadema zilizoko katika eneo la Ngarenaro, zilinusurika kuteketea kwa moto juzi baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya vyumba vyake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Japhet Lusinga alisema:
“Katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa hakuna mahali palipovunjwa kutoka nje ya uzio na kuruhusu watu kuingia ndani... tumegundua kuna tundu dogo darini eneo la kuelekea bafuni la upana wa futi moja na nusu kiasi haliwezi kuruhusu mtu kupita.
“Tumejiridhisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupita hapo na ndani tulikuta majivu na baadhi ya vitu vilivyoungua na vifaa vingine.”
Lema akiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro alisema: “Tumebaini polisi wanataka kulifanya jambo hili kama la siasa ndiyo sababu juzi badala ya kuanza kuchunguza waliohusika, waliwakamata Mtunza Ofisi na mlinzi wetu na kuwalaza rumande hadi leo (jana) asubuhi kwa madai eti wanawahoji.
“Hatukubaliani na taarifa yao, hii ni siasa. Kulitokea mauaji ya bomu, wakasema Chadema wamejilipua, leo ofisi imechomwa wanasema Chadema wenyewe, hili hatukubali, “ alisema.
Msajili alaani
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amelaani tukio la kuchomwa moto ofisi hizo za Chadema na kusisitiza kuwa wananchi hususan wanasiasa wasiwe wepesi kuingiza hisia kwenye makosa ya kijinai.
Alisema kuwa tukio hilo linapaswa kukemewa kwa hali yoyote ile kwa kuwa linavuruga na kuhatarisha amani ya nchi.
Dk Slaa aanza ziara
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amesema hakuna mtu yeyote mkubwa kuliko katiba ya chama hicho.
Dk Slaa aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa CDT, Kahama mkoani Shinyanga, alipokuwa akihutubia mamia ya wanachama na mashabiki wa chama hicho akiwa katika ziara yake kuimarisha chama katika mikoa ya Shinyanga na Kigoma.
“Chadema ni chama makini, kina kila kitu kwenye katiba yake kuliko hata CCM, kina itifaki, kina maadili hata mimi na Mwenyekiti Mbowe (Freeman) imetuwekea mipaka ya utendaji... “Chama hakiwezi kumwonea mtu, kinatenda haki na yanayotokea sasa ni msukumo wa baadhi ya vyombo vya usalama na hayakuanza leo.”
Kauli yake ilionekana kutoa ufafanuzi wa hatua ya Kamati Kuu ambayo ilimvua nyadhifa zake zote aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake wawili kwa madai ya kuandaa waraka kuhamasisha mabadiliko hatua iliyosababisha mvutano mkubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.