Dar es Salaam. Ndivyo alivyosema na bila shaka
ndivyo anavyoamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini kauli
ambazo amekuwa akizitoa tangu kuanza kwa mbio za urais zinamuweka katika
hali ngumu Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Lowassa alirudia moja ya kauli hizo juzi alipokuwa
Dar es Salaam kuendelea na kazi ya kutafuta wadhamini aliposisitiza
kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa “Watanzania wanataka
mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje,” akisisitiza
kuwa yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko hayo.
Mbunge huyo wa Monduli ametoa kauli hizo kabla ya
vikao vya juu vya kufanya uamuzi wa mgombea urais wa CCM
vitakavyoongozwa na Rais Kikwete. Vikao hivyo vitaanza Julai 8.
Tayari makada 42 wamejitokeza kuchukua fomu za
kuomba ridhaa ya chama hicho kikongwe kugombea urais na kutoa ahadi
mbalimbali, lakini Lowassa, ambaye amekuwa akipata wadhamini wengi
kuliko makada wengine, ndiye ambaye ametoa kauli zinazomuweka Kikwete
kwenye hali ngumu.
Tangu alipoanza kuzungumzia urais kwenye kikao cha
kwanza na wahariri Mei 25 mjini Dodoma, Lowassa amekuwa akitoa kauli
kadhaa katika mikoa mbalimbali nchini, akianzia Arusha ambako alitangaza
nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM na baadaye kwenye harakati za
kusaka wadhamini.
Asiyenipenda ahame CCM
Akijibu swali kwamba anaweza kuhama chama iwapo
jina lake litakatwa kwenye mchakato wa ndani ya CCM, Lowassa alieleza
jinsi alivyokitumikia chama na imani yake.
“Sina mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B.
Mimi ni Plan A tu. Tangu nimalize chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa
mwana-CCM. Sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa
vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano
Arusha. Maisha yangu yote ni CCM,” alisema Lowassa.
“Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiyo ahame, siyo mimi.”
Safari hii JK ataniunga mkono
Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid Mei 30 wakati akitiania, Lowassa alielezea tukio la
kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania urais mwaka 1995 wakati
alipofanya mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kikwete,
ambaye pia alichukua fomu hizo.
“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja
tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na
waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo
halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita
kati yetu, mwenzake ambaye hangefanikiwa angemuunga mkono mwingine,”
alisema Lowassa na kuongeza kuwa wakati ule alimuunga mkono
Kikwete...“Natarajia safari hii, Kikwete ataniunga mkono.”
Mwaka huo, Kikwete alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye
akawa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Mwaka 2005, Lowassa hakuchukua
fomu na badala yake alimuunga mkono Kikwete aliyeshinda na mbunge huyo
wa Monduli kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Pengine kauli hiyo ya Lowassa kutaka amuunge mkono
ndiyo iliyosababisha Rais Kikwete kutupiwa swali na mwanadiplomasia wa
Marekani Juni 9 wakati akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio
Uholanzi katika hoteli ya Chawnie Plaza. Rais Kikwete alijibu kuwa hana
mtu wake na kwamba wote ni wagombea wake, na kama ni suala la kuchagua,
ana kura moja tu kama wajumbe wengine.
Mabadiliko aliyotabiri Nyerere
Akiwa mjini Iringa Juni 20, Lowassa alitumia kauli hiyo ya Nyerere kuhusu mabadiliko ndani na nje ya CCM.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji
mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,”
alisema Lowassa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga
inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,”
alisema Lowassa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Pia aliwaambia wahariri mjini Dodoma kuwa hawezi
kuondoka CCM na kama kuna watu wanadhani hivyo, waondoke wao. Alikuwa
akijibu swali kama atakuwa tayari kuondoka CCM iwapo ataenguliwa kwenye
mchujo wa wagombea urais.
Hakuna wa kumkata jina
Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani
Ruvuma alisema hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM
vitakavyoketi kumteua mwanasiasa atakayepeperusha bendera ya chama hicho
katika kinyang’anyiro cha urais.
“Nimekuwa mwanaCCM tangu mwaka 1977 nilipomaliza
chuo kikuu, sijawahi kufanya kazi nje ya CCM hivyo nakijua chama na
hakuna mgombea atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika
chama, sasa leo anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa
sababu gani? Sioni kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo
msiwe na wasiwasi jina litarudi tu,” alisema Lowassa.
Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje
Siku ya kuchukua fomu Juni 5, Lowassa alijibu kwa
kifupi maswali ya wanahabari na kusema kama kuna mtu ana ushahidi wa
tuhuma za ufisadi dhidi yake amtaje jina.
“Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme na
anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za
matusi ila tu zijengwe hoja.
CCM ikijipanga itashinda
Juni 25, akiwa mjini Babati kutafuta wadhamini,
Lowassa alisema iwapo CCM itajipanga vizuri, ikamaliza migogoro na
kujiamini, itashinda mapema katika uchaguzi.
“Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha magomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu.”
Kwa kujipanga, Lowassa alikuwa akimaanisha kumteua
yeye kugombea urais kwa tiketi ya CCM, akisema kufanya hivyo kutamaliza
uchaguzi mapema.
Alichokisema Dar
Akiwa Dar es Salaam juzi kusaka wadhamini alirejea
kauli ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1995 kwamba mabadiliko yasipopatikana
ndani ya CCM, yatatafutwa nje ya chama hicho.
Kutokana na kauli hizo ni wazi kuwa rais Kikwete
atakuwa katika mtihani mzito wakati atakapokuwa akiendesha vikao vya
chama hicho vya kupata mgombea urais.
Kwa mujibu wa ratiba za CCM, kikao kitakachoanza
kitakuwa na Usalama na Maadili kitakachofanyika Julai 8 na kufuatiwa na
Kamati Kuu Julai 9 ambayo itawachuja wagombea hao 42 na kubaki watano
ambao majina yao yatawasilishwa Halmashauri Kuu (NEC) Julai 10 kuchuja
wagombea hao na kubaki watatu watakaopigiwa kura na mkutano mkuu kumpata
mmoja. Mkutano mkuu utafanyika Julai 11 na 12.
Vikao vyote isipokuwa cha Usalama na Maadili vitaongozwa na Rais Kikwete.
Jambo jingine linaloonekana kukitesa chama hicho
katika kupitisha mgombea ni idadi kubwa ya wana-CCM wanaojitokeza
kumdhamini waziri mkuu huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho kila mgombea
urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama 30 katika mikoa 15 nchini ili
kufikisha idadi ya wadhamini 450, lakini Lowassa amekuwa akipata
wanachama hadi 50,000 wanaotaka kumdhamini katika baadhi ya mikoa.
Makada, wasomi wazungumzia kauli
Pius Msekwa alisema chama kikongwe kama CCM
hakiwezi kutishika kwa kauli kama hizo ambazo zinaweza kuwa na tafsiri
tofauti kwa wananchi wa kawaida ambao hawafahamu taratibu za chama
wanaoweza kuamini kuna watu wanaonewa.
Alisema kwa taratibu za chama, mgombea anatakiwa
kueleza sera zake atakachowafanyia wananchi, lakini akiwa anatoa kauli
za vitisho anakuwa kero kwa wanaomsikiliza kwani haziwasaidii.
“Sidhani kama ni kauli nzuri, kinachotakiwa
wagombea wanadi sera zao na wasubiri kupitishwa na kamati itakayokaa kwa
ajili hiyo badala ya kutamka kauli zisizokuwa na tija wala faida kwa
mwananchi wa kawaida, ”alisema Msekwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Frank Tilya alisema ameshangazwa na tabia hiyo ya wagombea wa CCM
iliyoibuka kabla ya taratibu za uchaguzi kutangazwa kwani huko nyuma
haikuwapo.
Alisema anachofahamu CCM ina taratibu zake za
kupata wagombea kwa kuwachuja, hivyo kauli hizo zinaonyesha kuingilia
mamlaka hizo na wanaozisimamia.
Alisema ameshangazwa na kinachojitokeza katika
uchaguzi wa mwaka huu wagombea wa CCM badala ya kutangaza nia na kuomba
wadhamini wao wanafanya kampeni kabisa utafikiri wameshapitishwa.
“Hii ni hatari kwa siasa, watu kufanya mambo kwa
kutokuzingatia taratibu siyo jambo jema, nahisi kuna kitu hakipo sawa
huko, wanapaswa wajichunguze na kuacha wahusika wafanye kazi yao badala
ya wao kuwa majaji,” alisema Dk Tily.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema
anayachukulia hayo kama majigambo ya wanachama kutafuta nguvu na
kujiamini na kwamba haoni kama kuna shida, kwa sababu mwisho wa siku
watajulikana nani anabaki na nani anaondoka katika kinyang’anyiro hicho.
“Ninachoomba kifanyike hapa ni kamati kufanya kazi
yake bila kupindapinda wala kumuogopa mtu, kwani inaonekana wazi kuna
ambao wanajinadi wakiwa na lengo la kutafuta nafasi huko mbele ya safari
ili wasiachwe na atakayeshinda, kutengeneza historia katika maisha yao,
pia wapo wenye nia ya kweli,” alisema Dk Bana.








