Thursday, 18 June 2015

Serikali yatangaza nafasi za kazi 1,100

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi nafasi hizo za kazi ambazo zinapatikana katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ya www.ajira.go.tz ni kwa ajili ya waajiri mbalimbali wa ofisi za umma.
Katibu alifafanua kuwa nafasi 949 ni kwa ajili ya waajiri walioainishwa katika ofisi za wizara, halmashauri na nyingine 185 ni za taasisi na wakala mbalimbali za Serikali.
Aidha, amewataka waombaji wote wa fursa za ajira kufungua matangazo yote mawili ya kazi na kuzingatia masharti ya Matangazo yote kama yalivyo katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili kabla ya kutuma maombi yao Aprili 9, 2013.
Daudi alifafanua kuwa waajiri ambao watatoa ajira hizo ni makatibu wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo Jinsia na Watoto, Wizara ya Kazi na Ajira na Ofisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo.
Wengine ni Makatibu wakuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji na Katibu Ofisi ya Rais Maadili.
Wengine ni Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Pwani, Mara, Kilimanjaro, Lindi, Singida, Tabora, Tanga, Katavi na Arusha; pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za majiji na manispaa Mwanza, Iringa, Songea, Shinyanga, Morogoro, Singida, Kigoma/ Ujiji na Temeke.
Nafasi nyingine ni kwa ajili ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mufindi, Kyela, Rungwe, Mbeya, Chunya, Biharamulo, Bukoba, Muleba, Namtumbo, Songea, Morogoro, Makete, Mkuranga, Mbinga, Tunduru, Ukerewe, Sengerema, Ilemela, Busega, Maswa na Meatu.
Nyingine ni Wilaya za Shinyanga, Kishapu, Kilosa, Msalala, Rufiji, Rorya, Ruangwa, Lushoto, Mkinga, Mpanda, Monduli, Ngorongoro, Kigoma, Nachingwea, Rombo, Same, Singida, Urambo, Tabora, Babati, Mbulu, Simanjiro na Kiteto.
Pia zimo Wilaya za Handeni, Pangani, Kibondo, Chamwino Mtwara, Nanyumbu, Mpwapwa, Kongwa na Tandahimba pamoja na halmashauri za miji ya Njombe na Kibaha. Nafasi nyingine ni za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).
Nafasi hizo zilizotangazwa zimegawanyika katika kada zifuatazo; Mchambuzi Mifumo ya Kompyuta daraja la II – (nafasi 10), Ofisa Vipimo II – nafasi 6, Mpima Ardhi, daraja la II (nafasi 26), Mhandisi daraja la II – Ufundi Umeme – Nafasi 9, Ofisa Mipango Miji daraja la II– nafasi 13 na Mhandisi daraja la II - Ujenzi (Nafasi 16).
Pia wanahitajika wahandisi daraja la II - Maji (Nafasi 13), Ofisa Misitu daraja la II (nafasi 7), Ofisa wa Sheria daraja la II – nafasi 3, Mtakwimu daraja la II – nafasi 8 na nyingine mbalimbali.

Mbowe ahukumiwa, utata wa sifa ya kugombea waibuka

Hai. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amehukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwangalizi wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa. Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa faini hiyo iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi wa chama hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Wabunge waliochanga fedha hizo ni, Mustafa Akuney wa Mbulu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Cecilia Pareso, Joyce Mukya, Rose Kalili na Paulin Gekul wote wa Viti Maalumu.
Utata wa kupoteza sifa ya kugombea
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii juu ya uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuwania tena ubunge au urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, Mwanasheria, Alex Mgongolwa akinukuu Katiba ya Tanzania Ibara ya 67 (1)(c); 67(2) (c na d) alisema hukumu hiyo haiwezi kumzuia kugombea ubunge kwa sababu hakwenda jela na kosa lake halihusu kukosa utovu wa uaminifu, kukwepa kodi wala kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Suala hilo linafanana na lililotokea katika mchakato wa uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa mgombea urais wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake, Saidi Soud Said walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo jela, Mtikila akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said akitumikia chuo cha mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa. Hata hivyo, pingamizi hilo lilitupwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame (marehemu) baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila na Said, kuwa makosa waliyofungwa kwayo hayakuwa ya kukwepa kodi, kukosa uaminifu wala kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Mashtaka
Mbowe alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia shambulio la kawaida, mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, Nassir Yamin katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa ambaye amehamishiwa Bukoba, alisema kitendo kilichofanywa na Mbowe hakikubaliki na kinapaswa kukemewa.
“Kitendo alichokifanya mshtakiwa akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Hai ambaye alipaswa kuwa kioo cha jamii hakikubaliki na lazima kikemewe,” alisema.
“Kwa hiyo hukumu ya Mahakama ni kwamba atalipa faini ya Sh1,000,000 au akishindwa kulipa atakwenda magereza kwa mwaka mmoja,” alisema hakimu huyo.
Ushahidi
Akichambua ushahidi uliomtia Mbowe hatiani, Hakimu huyo alisema Mahakama imeegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza, Yamin na shahidi wa pili John Mushi aliyekuwa msimamizi wa kituo.
Alisema ushahidi huo ulieleza kuwa siku hiyo Mbowe aliingia katika Kituo cha Zahanati ya Lambo katika Jimbo la Hai na kuuliza uhalali wa mlalamikaji kuwapo kituoni hapo.
Mashahidi hao waliiambia Mahakama kuwa walimuona Mbowe akimkunja na kumtoa nje kwa nguvu mwangalizi huyo wa ndani na baadaye mbunge huyo kuondoka katika kituo hicho.
Alisema ushahidi wa mashahidi hao uliungwa mkono na shahidi wa nne wa mashtaka, ambaye ni daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, aliyemtibu mlalamikaji na kujaza fomu PF3.
Alisema ushahidi wa daktari huyo unaonyesha kuwa mlalamikaji alikuwa na michubuko katika shavu lake moja na shingoni iliyotokana na kupigwa na kitu butu.
Hata hivyo, aliukataa ushahidi wa shahidi wa saba, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Shafii aliyekuwa mpelelezi mkuu kuwa Mbowe alikiri kufanya kosa hilo alipoandika maelezo ya onyo polisi.
Hakimu Mpelembwa alisema japokuwa upande wa mashtaka uliwasilisha maelezo hayo kama kielelezo lakini baada ya kuyapitia, hakuna mahali ambako Mbowe alikiri kufanya kosa hilo.
Utetezi wa Mbowe
Hakimu Mpelembwa alisema wakati akijitetea mahakamani, Mbowe alikanusha kufanya tukio hilo lakini alikiri kufika katika kituo hicho na kumtaka mwangalizi huyo kumwonyesha kitambulisho chake.
“Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha kumpiga Nasir Yamin wala kumfanyia kitu chochote kibaya, bali alimwamuru atoke nje kwani hakuwamo kwenye orodha ya waangalizi iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”
Hakimu huyo alisema, Mbowe alieleza kuwa hakuwahi kuitwa polisi, bali alikwenda mwenyewe baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa amefunguliwa kesi ya aina hiyo.
Sababu za kutiwa hatiani
Hakimu Mpelembwa alifafanua dhana ya kosa la shambulio kuwa ni kitendo chochote chenye nia ya kudhuru mtu mwingine au hata kujaribu tu kumdhuru au kumtia hofu.
“Kwa maana nyingine ni kitendo cha kumtia mtu mwingine hofu na ili kosa hilo litimie ni lazima mshtakiwa awe na nia isiyo halali kisheria ya kutaka kutenda kosa nililolianisha,” alisema.
Hata hivyo, hakimu huyo alisema shahidi wa kwanza (Yamin) na wa Pili (msimamizi) waliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alimkunja na kumvuta nje mlalamikaji atoke nje ya kituo.
“Ushahidi wa Yamin na Mushi ni wa kuona kuwa mshtakiwa alimkunja na kumtoa nje mlalamikaji. Swali hapa ni je, kumvuta mtu na kumtoa nje kunapelekea kosa la shambulio?” alihoji.
Hakimu huyo alisema kwa tafsiri ya dhana nzima ya kosa la shambulio ni dhahiri kitendo alichokifanya mshtakiwa kinaangukia katika kosa hilo kwa mujibu wa sheria.
“Ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili wa upande wa mashtaka unashabihiana na ushahidi wa daktari kwamba kulikuwa na michubuko. Kwa mantiki hiyo Mahakama inakubali ushahidi huo. Kutokana na Mahakama kukubali ushahidi wa mashahidi hao watatu, inakutia hatiani kwa kosa la shambulio kama ulivyoshtakiwa nalo.”
Mwendesha mashtaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Feo Simon alisema ingawa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, aliiomba itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa jamii.
Wakili wa Mbowe, Issa Rajabu aliyekuwa akisaidiana na Albert Msando, aliomba Mahakama impe adhabu ndogo mteja wake kwani hajawahi kutenda kosa lolote la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Mpelembwa alisema kwa kutoa adhabu ya faini ya Sh1 milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela amezingatia ombi la wakili wa Mbowe.
Baada ya hukumu
Hukumu hiyo iliyoanza saa sita mchana hadi saa 7.20 mchana, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamefurika mahakamani hapo walitandika kanga chini na kuanza kuchangishana faini hiyo kazi ambayo ilisimamiwa na Kiwelu.
Wakati kazi hiyo ikiendelea, Mbowe aliendelea kushikiliwa ndani ya chumba cha Mahakama hadi wabunge hao walipokwenda Benki ya NMB, Tawi la Hai saa 7.40 mchana na kulipa faini hiyo na Mbowe kuachiwa saa nane mchana.
Mbowe azungumzia hukumu
Akizungumza nje ya chumba cha Mahakama hiyo, Mbowe aliwatoa hofu wanachama wa Chadema kwamba wasikatishwe tamaa na hukumu hiyo ambayo alisema alitegemea ingekuwa hivyo.
“Mnanipa pole ya nini? Kuna msiba hapa? Tupeane hongera. Sikutarajia cha tofauti na hiki kilichofanyika. Hakinivunji nguvu, bali kinaniimarisha katika mapambano,” alisema.
“Haki katika nchi hii itapiganiwa kwa watu wengine kuumia na wengine kuokoka. Nimesota mahakamani miaka mitano badala ya kufanya kazi ya wananchi. Hainivunji moyo,” alisema na kuongeza:
“Hainivunji moyo katika azma yangu ya kuikomboa nchi hii na ukombozi uko jirani. Mahakama ya nchi hii vimekuwa ni vyombo vya kutoa dhuluma kwa wananchi japo siyo mahakimu wote. Lakini iko siku Mahakama zitakuwa ni sehemu ya kutolea haki, kutenda haki na haki ionekane imetendeka. Mapambano yanaendelea na nawaomba msiwe wanyonge,” alisisitiza.
“Sitaki kuizungumzia Mahakama katika hatua ya sasa lakini ndani ya Mahakama kuna watu wanaotenda haki na ndani ya Mahakama kuna watu wasiotenda haki,” alisema Mbowe.
Alisema kesi hiyo haikustahili kuiendesha kwa miaka mitano na kwamba kodi za wananchi zinateketea pamoja na muda, akisema haiwezekani nchi ikaendeshwa katika utaratibu huo.
“Kama mimi mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mtunga sheria wa nchi hii naweza kusoteshwa mahakamani miaka mitano, mwananchi wa kawaida atafanywaje?” alihoji Mbowe.

Hizi ndizo ndoto za waowania urais za kuiondoa nchi kwenye umaskini

Oktoba mwaka huu Watanzania wanatarajia kumpokea rais mpya wa awamu ya tano kwa imani kuwa atakata kiu kubwa ya watu wanaopenda kuona wanawekewa mazingira mazuri ya kuondokana na umaskini.
Uzoefu wa awamu nne zilizopita, umeonyesha kuwa pamoja na vyama vinavyowasimamisha wagombea kwenye kiti cha rais kuwa na sera zao, kila aliyengia alikuwa na aina yake ya mabadiliko katika uchumi nchi.
Anayeingia madarakani katika kipindi hiki, anaweza akawa ana majukumu makubwa zaidi kuliko wengine waliopita maana Watanzania wengi wana mambo mengi ambayo wanahisi yangetatuliwa, nchi itaingia kwa haraka kwenye mafanikio na kuondokana na umaskini uliokithiri.
Hadi sasa, Watanzania zaidi ya 30 wamejitokeza kupitia CCM na CUF, wakiwa na mawazo mbalimbali ya kutatua matatizo ya Watanzania kiuchumi, iwapo watapewa ridhaa ya kukalia kiti cha rais.
Yafuatayo ni sehemu ya maelezo ya baadhi yao ambao katika maelezo yao wanawahakikishia Watanzania watazifanya ndoto zao za maendeleo kuwa kweli.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa anasema akifanikiwa kuingia Ikulu atahakikisha analiondolea taifa sifa mbaya ya kuombaomba na kulifanya kuwa ‘mkoba wa neema’ katika Afrika. “Tunapaswa kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi tunaouzungumzia unamnufaisha Mtanzania aliyeko mjini au kijijini na kwamba hali za Watanzania wa matabaka yote zinanyanyuka na kwamba wanaridhika na kuuona uhalisi wa ukuaji wa maendeleo tunayoyazungumzia,” anasema Lowassa.
Anasema anataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira ili kuwawezesha Watanzania kukabiliana na changamoto za maisha yao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anasema akipewa ridhaa hiyo, atazishirikisha sekta binafsi na umma katika kuendesha uchumi na kuziwezesha kupata mitaji mikubwa.
Anasema ana mpango wa kuvifufua viwanda na kuboresha kilimo, ili mazao yanayozalishwa yanunuliwe hapahapa nchini.
“Hatutaki tena kusafirisha malighafi nje halafu tunaletewa bidhaa zilezile zilizosindikwa. Haya mapinduzi ya viwanda ni lazima, mara tu nikiingia Ikulu Oktoba mwaka huu,” anasema.
Anasema kasi ya kufanikisha maendeleo ya viwanda itachochewa na uwepo wa gesi asilia iliyovumbuliwa mikoa ya Kusini, itakayopunguza gharama za upatikanaji wa nishati ya umeme.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba anasema atahakikisha anakukuza uchumi kwa kuwa na serikali ya watu waadilifu. Anasema atahakikisha kuwa Serikali inaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. “Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu. Nitaunda serikali ya mawaziri 18, ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au uwezo wake,” anasema Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina anasema anataka nafasi hiyo ya juu nchini ili akasimamia makusanyo ya kodi yatokanayo na rasilimali za taifa yanakuwa mara tatu. Anasema kuwa Tanzania ina uchumi mzuri lakini unaharibiwa na mfumo wa utawala uliopo. “Kwa sasa Taifa linakusanya Sh12 trilioni kwa mwaka, lakini mimi nitahakikisha makusanyo hayo yanaongezeka mara tatu ya hapo. Sasa makusanyo yanashindikana kutokana na kuwapo kwa mianya mingi ambayo inaruhusu wizi wa mali za umma,” anasema. Mpina anasema Tanzania siyo maskini ila umaskini uliopo unasababishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wizi, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu inayofanywa na watu binafsi na serikali.
Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala anaamini kuwa uchumi unajengwa kwa kuyapa umuhimu mambo makubwa matatu; huduma za jamii, elimu na maji. Anasema ataboresha miundombinu ya reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.
“Kazi ya kujenga uchumi na maendeleo ninaamini tunaiweza, tukiamua. Uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo; sema tuna upungufu katika kuchukua hatua za kutenda,” anasema.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira anasema Tanzania inahitaji miundombinu mingi kuanzia vinu vya kufulia umeme hadi mifumo ya usambazaji maji safi na mawasiliano ya simu. “Utawala wangu utaweka kipaumbele cha hali ya juu mpanguo huo ili kuhakikisha uwapo wa miundombinu ya uhakika na gharama nafuu kwa ajili ya wazalishaji na walaji kuendana na ukuaji wa juu unaomfaidisha kila mmoja,” anasema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anasema ili kufanikiwa kiuchumi nchi, inahitaji rasilimali watu, hivyo ameahidi kutumia nguvu katika kufanikisha jambo hilo. Anasema anataka nchi ipige hatua kutoka hapa ilipo iende mbali zaidi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo elimu na afya.
Waziri Nyalandu anaeleza atatumia nguvu kubwa kuwekeza katika rasilimali watu ambayo ni muhimu kama ilivyo kuongeza nguvu za kuwawezesha Watanzania kuwekeza katika jamii.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba anasema iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu, atawavusha Watanzania kutoka katika hali ya uchumi mdogo uliopo hivi sasa na kuwaingia katika ulio wa kati. “Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili, nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia,” anasema Nchemba.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Entrepreneurship Limited, Boniphace Ndengo anasema Tanzania inaweza kufikia kiwango cha uchumi mzuri utakaoleta ustawi kwa wananchi wengi.
Ndengo anasema alianza biashara ya mghahawa mdogo Mtaa wa Uhuru mjini Musoma, lakini hivi sasa anaitwa mwekezaji hivyo kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo nchini, anakusudia kujenga Tanzania kuwa kituo bora cha kimataifa cha utalii na kuifanya kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Mjumbe wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ally anasema atatokomeza rushwa kwa kuwa ni adui wa uchumi.
Amina anataja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuinua uchumi, kuongeza mapato, kupambana na rushwa, huduma za jamii kuondoa matabaka ya walionacho na wasionacho na kudhibiti mapato ili yaendane na matumizi.
Balozi Ally Karume anasema Tanzania ili iweze kujenga uchumi imara, inahitaji kiongozi mwenye mbinu na uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi kwa vile ndiyo adui wakubwa wa maendeleo yake.
“Uhuru wa kujituma ni muhimu sana kwa kila mtu. Siyo mtu anataka kuuza njugu wewe unamwambia huna leseni. Unamuuliza leseni kwani anataka kuendesha gari? Mtu akitaka kuendesha gari ndiyo mdai leseni, lakini siyo kuuza njugu lazima watu wapewe uhuru wa kujituma,” anasema Balozi Karume.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Enterpreneurship, Boniphace Ndengo anasema adui mkubwa wa taifa ni rushwa na ujinga ambao ‘umezaa’ ufisadi, hivyo atakapoingia madarakani anapiga vita rushwa ili kukuza uchumi.
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal anasema kwa kuwa yeye ni mwanasayansi atatumia taaluma hiyo kuleta maendeleo nchini. “Hakuna uamuzi uliokuwa sahihi zaidi ya uamuzi wa kisayansi. Mimi siku zote uamuzi wangu unafuata utaratibu huo, ndivyo nilivyolelewa na kufunzwa na nitaendelea kuongozwa kisayansi,” anasema.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema: “Nitahakikisha uchumi wa wanyonge unainuka. Kwa hiyo katika mpango wa miaka mingine mitano, tutajikita kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. Tukifanya hivi umaskini utapungua kwa kiwango kikubwa na ajira zitapatikana.” Monica Mbega anasema akifanikiwa kuwa rais wa Tanzania atafanyia utafiti changamoto za awamu zilizopita na kuhakikisha anazitafutia suluhu ya kudumu.
Monica anasema pia atakabiliana na viashiria vya uvunjifu wa amani ambavyo vinatishia kuvuruga mipango ya maendeleo. Viashiria hivyo anavitaja kuwa ni uhasama, mauaji ya albino, wizi, ubaguzi wa dini na ukabila.
“Tutazungumzia upendo na umoja kuanzia ndani ya familia ndio kitovu kitakachosaidia kujenga amani. Amani itajengwa na upendo misamaha na umoja,” anasema.
Waziri wa Ofisi wa Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya anasema atakuza uchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha kisasa, kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya shughuli za kilimo.
Anasema atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa kujisimamia na kwamba Serikali itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya Watanzania waone matunda ya kukua kwa uchumi. “Serikali itakuwa injini ya kukua Kwa uchumi kwa kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye kazi kwa ufanisi na kulipa kodi nzuri kwa Serikali,’’ anasema.
Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Sospeter Muhongo anasema ataondoa umaskini nchini kwa kutumia uchumi wa gesi. “Nitafuta umaskini kwa kutumia uchumi wa gesi ambao utakuwa unamilikiwa na Watanzania wenyewe. Gesi nimesomea kwa hiyo ninafahamu mambo haya vizuri. “Tena kutokana na juhudi zangu za kuhamasisha vijana wapelekwe nje kusoma masomo ya gesi, nategemea mwakani tutakuwa na wataalamu wengi zaidi watakaoweza kufanya kazi kwenye sekta hii.”
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja anasema atapambana na mambo sita aliyoyaita maadui wakuu wa nchi, ambayo ni umaskini, ujinga, maradhi, rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili. “Maendeleo ya kweli ya nchi yetu hayawezi kuletwa na sekta ya umma peke yake, bali yataletwa kwa kushirikisha kikamilifu sekta binafsi. Ni muhimu rais wa awamu ya tano awe na weledi wa kutosha kuhusu utendaji wa sekta ya umma na binafsi,” anasema.

Sunday, 14 June 2015

Hali halisi ya nchi na rais tunaye mtaka, Taifa lifanye nini


Wengi mtakubaliana nami kwamba kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi kimekwenda kwenye kiwango kingine kabisa, na hasa ukizingatia mpaka sasa kuna makada zaidi ya 30 ambao wameonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama.
Wengi wamekuwa na maswali ya kiuchokozi hapa na pale kwamba unadhani wimbi hili kubwa la wagombea tafsiri yake ni nini? Nimejitahidi mara zote kusema kuna tafsiri zaidi ya moja, mosi ni uhalisia kwamba wana CCM wako huru kuweka mawazo yao hadharani, pili, demokrasia iko pana katika chama kwamba yeyote ambaye anaona anaenea katika nafasi basi anayo fursa ya kujitokeza na kutangaza nia na hatimaye kuomba kukubalika na chama.
Tatu, ni kwamba huenda watu hawajui maana hali ya tafsiri ya urais kama taasisi na Rais kama kiongozi mkuu wa nchi na majukumu yake, huenda watu wanauona urais kwa maana ya kusafiri kila pahala, kufungua miradi, kutoa hotuba, kutoa maelekezo, kupita kwenye msafara wakati wengine tunasubiri foleni, kutuma watu wakafanye kazi kana kwamba watu hawajui wanalopaswa kutenda.
Wengine wanadhani pia ukiwa Rais kazi ya kuwashughulikia wauza dawa za kulevya, kushughulikia wala rushwa na ufisadi ndio hasa itakuwa kazi yao, hawa nawaona wakitembea na pingu, bakora za mibungo na magereza yanayotembea ili kila watakaye mbaini basi watamfunga papo hapo, wapo watangaza nia ambao nikienda kwenye vichwa vya kwa kutafakari nawaona wakiwaza hivi.
Nne, ni kwamba huenda kuna watu wahuni pia, watu wasio na mapenzi mema na taifa hili, watu ambao wamegeuza nafasi ya urais bidhaa ya mnadani. Hawa wako pale kuhakikisha wanakuwa Rais, haijalishi sote tunajua urais mtu hupewa kama dhamana na wananchi, lakini wapo ambao tayari wameshajiona marais, hii ni kuwakosea wapigakura, na zaidi kukikosea heshima Chama cha Mapinduzi.
Hawa watu wa namna hii wao hawajali demokrasia kwa maana ya utawala wa watu kwa watu na watu wenyewe yaani kiingereza “democracy”, watu hawa ni genge la wajanja wachache ambao wanataka kushika madaraka ya nchi, maslahi yao ya msingi ni wao wenyewe kiingereza mtindo huu tunaita “mobocracy”.
Kisiasa- Tanzania iko Njiapanda
Wengi wanahoji dira ya Taifa hili ni ipi? Taifa halina dira, ninaposema hivi wengi mtasema kwamba mbona tunayo ile inaitwa “vision 2025”, ni kweli lakini ile ni dira ya Tanzania Bara pekee, na Tanzania Bara si Taifa, utaniambia pia “vision 2020” nakubali lakini hiyo inahusu Zanzibar pekee, sasa na mimi nitakuuliza je iko vision moja ambayo inazungumzia Taifa la Tanzania?
Kwanza nikitizama vision 2020 na 2025 utagundua bado hazina sifa ya kuwa Dira. Dira ni waraka ambao, Taifa kwa mwafaka limesema huko ndiko tunakotaka kwenda. Ukisoma vizuri hizi nyaraka mbili kila moja iko huru, nikimaanisha Ukisoma vision 2025 inazungumza kana kwamba Tanzania Bara ndio Jamhuri na Muungano na vivyo hivyo ukisoma vision 2020 unaona Zanzibar inajizungumza yenyewe kana kwamba ni huru. Kwangu mimi kitendo cha nchi moja kuwa na dira mbili na zisizosomana ni sawasawa kabisa na kuwa na ndege moja yenye marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja wa wanakwenda wapi. Juzi juzi hapa kule nchini Ujerumani kitendo cha kuwa na marubani wawili wasio na uelewa wa pamoja ndege inapaswa kwenda wapi kilipelekea ajali mbaya kabisa, rubani mmoja anajua tunatakiwa kuwafikisha salama abiria wakati rubani mwingine ana mipango ya kutoa uhai wa abiria na yeye mwenyewe kwa kuigongesha kwa makusudi ndege kwenye milima.
Mzee Warioba alijaribu kututengenezea dira katika Rasimu ya Katiba Toleo la Pili, lakini Katiba Inayopendekezwa ikasema hata serikali isipofanya chochote katika utekelezaji wake isihojiwe kokote hata mahakamani na mtu yeyote asiwe na mamlaka ya kuhoji juu ya utekelezwaji wa dira hiyo, sasa hapo ni dira au kiini macho?
Taasisi za Mamlaka ya nchi hasa Bunge ni dhaifu, unakumbuka wakati wa Bunge Maalum wengi ya wabunge walitaka mikataba isipelekwe Bungeni, baada ya Bunge maalum wakazinduka wakataka mikataba ya TPDC, wakanyimwa, roho ikawauma sana hata wakatenda kinyume na mamlaka yao na kuelekeza Polisi iwakamate viongozi wa shirika la mafuta, walitenda kwa hasira, kiko wapi leo? Kitendo kile kikawafanya watake mikataba ipitie bungeni kupata ukubalifu, hawa ni wale wale ambao wengi wao walifuta masharti ya rasimu ya Warioba yaliyosema mikataba ya madini iridhiwe na bunge.
Wakati Bunge likiwa na mtanziko wa kimamlaka, hali iko dhahiri shahiri kwamba kuna upungufu wa utamaduni wa kidemokrasia (democratic culture), tumeacha kuwa watu wa majadiliano (dialogue), hatujengi hoja bali tunapiga makelele na kushutumiana wakati wote, Mwalimu Nyerere alipata kusema “argue, don’t shout”. Hatujengi muafaka, hatufanyi maridhiano, hatuna uelewa wa pamoja katika masuala ya msingi, hatuna uhimilivu (tolerance) lakini inaonekana tuna uhimilivu kwa mambo kama rushwa, ufisadi, mauaji ya albino na vikongwe n.k.
Tumeanza kushuhudia roho mbaya ya utengano (negative devisive force), ukabila, ukanda, udini, ubara na uzanzibari. Umeshuhudia hata watangaza nia tayari wameanza kujipanga kikanda hii ni hatari kwa ustawi wa umoja wa kitaifa.
Inaanza kuonekana uongozi si dhamana tena bali mali ya watu fulani. Utumishi wa umma unafanya kazi kwa woga. Maadili ya Taifa, binafsi na ya viongozi ni tatizo kubwa, hata pale Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi inapowafuatilia wale wanaokiuka miiko ya uongozi utagundua nguvu zake zina ukomo mkubwa.
Kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili, angalia namna ambavyo watangaza nia wanatumia fedha nyingi, swali la kujiuliza ni fedha zao binafsi? Na kama si zao waliowapa wana maslahi gani na nafasi ambayo watangaza nia hawa wanaitafuta? Muungano wetu bado una changamoto nyingi, Serikali mbili hazieleweki, siyo tu kwenye Katiba ya 1977 bali hata kwenye Katiba Inayopendekezwa. Watu wa Tanzania Bara wanauona Muungano kama mzigo na watu wa Tanzania Zanzibar wanauona Muungano kama Kero. Kuvurugwa kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ni huzuni nyingine inayoongeza njia panda ya kisiasa
Kiuchumi- Tanzania njiapanda
Umma wa watanzania hauna mali za pamoja, tulibinafsisha kila kitu na mashirika ya umma yaliyosalia ni hohehahe, mfano ni shirika la ndege la Taifa “Air Tanzania”, Shirika la Reli (TRL) ni shida nyingine kubwa licha ya kwamba tuna ubia na watu wengine.
Tuna Shirika la Nyumba (NHC), hili linakimbia kwa kasi baada ya maboresho makubwa ya kiutendaji, lakini nawapa indhari kwamba uchumi wa Marekani ulianguka kwa uwekezaji usiotabirika katika makazi na nyumba, tuwe macho.
Sekta binafsi ni dhaifu, sekta binafsi imeingia katika huduma na si uzalishaji, tizama kampuni ambazo zinaonekana vinara ni makampuni ya simu.
Haya hayazalishi, haya yanatoa huduma na yanachukua fedha za Watanzania maskini zaidi kuliko hata faida ambayo tunanufaika nayo moja kwa moja kama wananchi maskini na wasio na ajira.
Angalia ongezeko kubwa la mabenki, unadhani wanufaikaji ni wakulima na wafanyabiashara ndogondogo ambao kwa kiasi kikubwa wanaangukia katika sifa za watu wasio kopesheka, Tuamke, benki ni nzuri lakini lazima tuwe na uchumi ambao unabeba watu wake.
Hakuna viwanda vya kutosha vya uzalishaji kunakopelekea tatizo la ajira na kupoteza fedha za kigeni (hakuna exports za kutosha), mchele wa mbeya na kwingineko tunao lakini tunaagiza, sukari ya kutoka Mtibwa, Kilombero na Kagera tunayo lakini tunaagiza, tunayo gesi lakini bado tunaagiza mafuta mazito. Halafu dola ya kimarekani ikifika zaidi ya shilingi 2000 tukiuliza tunaambiwa huko duniani dola imeimarika zaidi, kweli?
Sekta binafsi iliyo dhaifu haiwezi kusimamia demokrasia na kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwapo.
Na hapa niwaseme kidogo Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwamba wameona Bunge Maalum lilivyoendeshwa na namna ambavyo Katiba Inayopendekezwa imedhoofisha maadili ya viongozi na kuvuruga Dira ya Taifa kwa kuiwekea vikwazo, lakini kwani umesikia wakikemea au wakishauri kitaalamu madhara ya kubomoa misingi ya maadili na uwajibikaji katika Katiba? Nawapa changamoto, na wao wajitafakari.
Mkazo haujawekwa katika uchumi wa kujitegemea unaozingatia ukuaji wa kilimo kinachotoa malighafi kwa ajili ya viwanda ambavyo vinachakata malighafi kuwa bidhaa zilizochakatwa au bidhaa kamili ambazo ziko tayari kurudi na kutumika katia sekta nyinginezo ikiwemo kilimo
Kukosekana kwa uchumi imara unaojitegemea kunazalisha watu masikini wengi zaidi katika Taifa letu. Tuna walipakodi wachache na tuna walaji wengi katika Taifa lakini pia mianya ya wanaokula zaidi yaw engine kinyume cha sheria ni wengi zaidi na kusababisha chakula wanachokusanya wachache wetu ama kinaliwa na wachache wetu kinyume na sheria na matokeo yake hakitoshelezi mahitaji yetu kama Taifa. Tunalo pia Tatizo la kuwa na vyanzo mbadala mbali na hivi vya sasa vya mapato ya Taifa na Serikali, na bado tunalo tatizo la kampuni za madini kutokutoa kodi ya mapato kutoka faida zao.
Wengi wanasema wanatoa kodi lakini ni kodi wanazokatwa wafanyakazi wao na sio kodi inayokatwa kutokana na shughuli za ushalishaji wa kampuni. Kwenye gesi ni eneo linguine ambalo ukiachia kwamba limegubikwa na sintofahamu juu ya namna mikataba yake imefungwa hasa katika ngazi ya utafutwaji wa gesi ni kizungumkuti kingine kinachotuweka kwenye njiapanda kama Taifa.
Rais tunayemtaka awamu ya tano
Tunataka Rais ambaye anajua tuko njia panda, ana ana uwezo na mamlaka ya kukemea kwasababu na yeye ni mwadilifu “moral authority”. Tunataka kiongozi ambaye anakubalika na jamii na jamii inamwona kama sehemu ya majibu ya changamoto zao. Hatutaki watu wajitembeze kwetu, tunajua tunataka Rais ambaye atasimamia masilahi yetu.
Leo karibu kila mtia nia, nasikia huyu kapata pesa kule, huyu kapata pale, huyu hela za wizi, huyu kapokea fedha chafu, huyu kachukua za watu wabaya na kadharika. Watanzania tuache ushabiki, tusimame na tuwe wamoja katika hili. Rais wetu akiletwa na watu maana yake si wetu ni wao. Tafakari

Zinakaribia siku za CCM kula gizani machungwa yaliyooza

Kuna kisa cha msafiri mmoja aliyeomba mahali pa kulala kwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa ili kesho yake aendelee na safari yake. Alifika saa 5.00 usiku na kwa kuwa mjumbe alikuwa amekwisha kula, alichofanya ni kumwandalia msafiri huyo mahali pa kulala, basi.
Alishukuru. Mlo wake usiku ule ulikuwa machungwa sita aliyonunua njiani. Loo, alipokata la kwanza, lilikuwa limeoza, alitupa kwenye kona. Lahaula, alipochukua la pili, nalo lilikuwa limeoza. Balaa, kumbe yote yalikuwa vivyo hivyo.
Haraka aligundua kwamba kilichosababisha akaona machungwa kuwa yameoza ni kibatari, hivyo, alikizima, akachukua machungwa yale na kuanza kula gizani, akalala. Heri angelala na njaa kabisa maana kesho yake aliharisha sana njiani na kutapika; we acha tu!
Kisa hicho kinakaribia kujirudia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho makada wake waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuwania urais wanachafuana na kujiozesha. Akisimama huyu anasema yeye tu anafaa, akisimama yule anadai wengine wote bomu, sasa atapatikana wapi aliye bora?
Edward Lowasa alijizuia alipotangaza nia, lakini Charles Makongoro alimshona barabara Stephen Wasira. “Mzee Wasira alifanya kazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Nyerere aliondoka yeye akabaki, bado yupo. Akaja Ali Hassan Mwinyi akaondoka, yeye yupo….na sasa huyu Mzee Wetu Jakaya Kikwete anaondoka, atamuaga yeye atabaki yupo!” Hebu jiulize, ikitokea ‘Bwana Yupo’ ameteuliwa itakuwaje?
Frederick Sumaye hakutafuna maneno, alisema; “Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni, nitampisha (katika mbio za urais).” Alishangiliwa na wafuasi wake huku wakimwambia; “Hakunaaaa.”
Bernard Membe aliwaambia wanaCCM mkoani Lindi; “Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.” Halafua akadai, “Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere huko aliko atafurahi endapo nitakuwa rais.” Yaani Nyerere afurahie Membe kuwa rais kuliko hata mtoto wake Makongoro?
Prof Sospeter Muhongo alisema; “Nafahamu... sidhani kama kuna mtu mwingine anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu wanaCCM, nitahakikisha tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa ya uchumi wa Taifa hili….Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi, mnanijua vizuri…”
Samuel Sitta alijipigie debe kwa kusema; “Kwa kifupi ninao uelewa na uzoefu unaolingana na changamoto za kipindi kigumu cha miaka mitano ijayo yenye mwelekeo wa kutikisa misingi ya utawala wa nchi yetu… kwa uimara wangu wa uongozi, nitajumuisha nguvu na maarifa ya wananchi ili tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za maendeleo kwa ufanisi na tija zaidi.”
Mwigulu Nchemba alisema; “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati.”
Kauli hizi zimetolewa kirejareja sana, lakini zitakuja kuwa na madhara makubwa mbele ya safari ndani na nje ya CCM kuwaaminisha wapigakura kwamba “chungwa teule” halijaoza kiviiile. Hapo watajitahidi kupiga msasa na kupinga methali isemayo “samaki mmoja akioza wote wameoza”.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na mkutano mkuu wa CCM walioshiriki mwezi huu, kuwaunga mkono makada wanaowapenda wawe marais, ndiyo mwezi ujao, watashiriki kumpitisha mmoja akapambane na wa Ukawa kutafuta tiketi ya kuishi Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Nani akemee? Wazee wa kukemea walijazana Arusha, Butiama, Mwanza, Lindi, Mbeya na kwingineko kuwapiga ‘tafu’ watangazania.
Kingunge Ngombale-Mwiru, mmoja wa makada wenye hekima wanaotegemewa kutoa ushauri ndani ya CCM yuko katika Timu Lowasa. Siku Lowasa alipotangaza nia mjini Arusha, Kingunge alikuwapo na alitoboa siri ya Halmashauri Kuu akisema, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete aliwataka wale wenye ugomvi kutafuta suluhu. Vyema. Je, yeye kuwa kwenye Timu Lowasa ni kusaidia suluhu ipatikane?
Lowasa mwenyewe yuko tayari kwa suluhu? Akijibu maswali ya wahariri kuhusu kutofautiana na wenzake alisema; “…Kama kuna mtu ambaye hanipendi ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.” Siku alipochukua fomu alisema, “Naamini katika ushindi na sina mpango wa kushindwa.” Waandishi wa habari walipomuuliza kama yupo tayari kushirikiana na wanasiasa wanaompinga sasa, aliwajibu; “Nitavuka daraja nitakapofika.” Mmh!
Ndiyo maana nasema zinakaribia siku za CCM kula gizani chungwa lililooza na kununua msasa ili kulitakatisha kabla ya kuliuza kwa wananchi.
0658 383 979

Wagombea waisuta Serikali kwa rushwa

Dar es Salaam. Makada wa CCM waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na chama hicho kuwania urais, wameeleza jinsi rushwa, ufisadi na udhaifu katika ukusanyaji kodi huku wakijinadi kuwa wao ndiyo wataondoa uovu huo iwapo watapitishwa kushika nafasi hiyo ya juu kisiasa.
Lakini hakuna hata mmoja aliyeiponda Serikali kwa kushindwa kudhibiti rushwa, ambayo baadhi walishasema kuwa imekithiri hata kwenye chama hicho tawala, huku mmoja akisema kuwa iwapo CCM itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Kati ya waliotangaza nia na kuchukua fomu, makada 11 ni mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne wakiwamo mawaziri waandamizi walioshika nafasi za juu na waliofanya kazi katika awamu zote nne.
Pia wamo makada waliokuwamo kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, lakini wakaondoka kwa sababu tofauti, huku kundi jingine likihusisha watendaji wakuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Lakini bado tatizo hilo la rushwa limekuwa likitumiwa na makada hao wa CCM wanaowania urais wakati wakijinadi kwa wanachama wao kwamba watafumua mfumo uliopo, kusuka upya sheria na kuimarisha taasisi za fedha ili watuhumiwa wakubwa wa rushwa wafikishwe kortini na kufungwa, badala ya kuwakamata walarushwa wadogowadogo pekee.
Katika hotuba zao wakati wanatangaza nia mbele ya umati wa wafuasi wao na mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, makada hao, mbali ya kueleza mikakati tofauti ya namna ya kuimarisha uchumi wamekosoa mfumo wa sheria kwamba unawalinda mafisadi wakubwa ambao hawakamatwi hadi kwa kibali maalumu.
Kwa mfano, akitangaza nia ya kuwania urais kijijini kwao Butiama, Charles Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema anaomba kibali cha kuisaidia CCM ikomeshe rushwa, na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe Watanzania, anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.
“Kosa la Rais Jakaya Kikwete ni kuwapenda sana marafiki zake. Kwa bahati mbaya, baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka,” alisema Makongoro ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliwaambia wafuasi wake mkoani Lindi kwamba ili kutekeleza utawala bora, hawezi kukaa kimya kuona rushwa, ubadhirifu, ufisadi vikichukua nafasi katika utawala wake.
“Ninawatumia salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha Watanzania wanachukia rushwa na kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na mpokeaji rushwa. Kama ni watumishi wa umma, watakwenda na maji...,” alisema mbunge huyo wa Mtama.
Ahadi ya kukomesha rushwa pia ilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyesema kwamba anataka kulifanyia Taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
“Ili kukomesha tatizo la rushwa, hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” alisema Sitta kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, Tabora.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema akifika Ikulu, ili kupambana na rushwa, “nitafanya mabadiliko ya kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii ikiwamo kuipa meno Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani”.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira alionyesha kukiri kuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuwania urais, wamo wenye kashfa za rushwa, lakini akajitenga nao kujionyesha kuwa hana doa hilo.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea,” alisema waziri huyo mkongwe na kuongeza:
“Kumbukeni sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyinginezo.”
Wasomi wawashangaa
Lakini kauli na ahadi hizo za makada hao wa CCM wanaotaka kuingia Ikulu zimewashangaza wachambuzi waliofuatwa na Mwananchi ili kutoa maoni yao kuhusu hoja za wagombea.
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema wengi waliotangaza nia ya kuwania urais wanatoka kwenye mfumo wa rushwa, hivyo itakuwa kazi ngumu kwao kuiondoa. “Tanzania imefikia ngazi ambayo rushwa imekuwa mfumo wa utawala. Ikifikia hatua hiyo kuindoa ni kazi kubwa kwa sababu kupiga vita mfumo si suala dogo, hawa watiania walishindwa huko serikalini, watawezaje sasa?” alihoji.
Alisema wengi kati ya wagombea hao wanatoka katika mfumo wa rushwa ambao wameujenga wenyewe, hivyo si kazi rahisi kuimaliza kwa sababu kuna kulindana na kustahimiliana.
“Kulindana ni utamaduni wa mfumo huo wa rushwa. Ndiyo wameujenga na walikuwa ndani ya mfumo, ndiyo maana wanashindwa kueleza watatumia mbinu gani
kuondoa mfumo huo,” alisema.
Alisema anahitajika mtu shupavu kuiondoa rushwa hapa nchini kwa sababu imeshaota mizizi kwenye mfumo wa utawala, na kwamba kusema tu wataimaliza hakuna ukweli wowote.
“Ufisadi unaofanywa na viongozi wa Serikali, vigogo na wanasiasa zina athari kubwa kwa uchumi wa nchi hii,” alisema Profesa Mpangala.
Mawazo hayo yanalingana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Hamad Salim ambaye alisema ni vigumu kwa wanaotaka kuwania urais kuimaliza rushwa kwa sababu wote wanafanya kazi katika mfumo uliojaa rushwa.
“Wao wenyewe wanaingia madarakani kupitia mfumo wa rushwa, sidhani kama wataweza kuung’ata mkono ambao unawalisha. Kama mchakato mzima wa kuingia madarakani kama vile kuchukua fomu, kupiga kura, kutafuta wadhamini wote umejaa rushwa, wataweza kuiondoa?” alihoji.
Alisema ahadi wanazozitoa watia nia ni vigumu kutekelezeka kwa sababu wanapambana na mfumo wao wenyewe na kazi ya kuumaliza ufisadi si ya mtu mmoja wala ya siku moja.
Salim alisema inashangaza baadhi ya watangazania kukusanya watu wanaowaunga mkono, kuandaa kampeni na kuandaa watu wa kuwashangilia.
Alisema watangazania hao wanatoa ahadi zao kama kampeni tu na wakiingia madarakani hawatafanya kazi kulingana na walichoahidi bali kwa kuangalia ilani ya CCM.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa UDSM, Dk Benson Bana aliwataka watangazania hao kuacha kutumia kigezo cha rushwa kama njia ya kupata kura na badala yake wazungumzie sera nyingine.
Dk Bana alisema Watanzania hawatamchagua kiongozi kwa sera zake za kutaka kuondoa rushwa kwani nao wanafahamu kuwa CCM imejaa rushwa.
“Watanzania hawamchagui mtu kwa kigezo cha kupambana na rushwa, hicho ni kimbelembele tu, waache kimbelembele,” alisema.
Dk Bana pia alisema watangazania hao waiache Takukuru ifanye kazi yake na wasiwadanganye wananchi kuwa wao ni mabingwa wa kupambana na tatizo hilo.
Lakini mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM) kitivo cha kompyuta na mifumo ya hesabu, Dk Eliamani Sedoyeka aliliangalia tatizo la rushwa kuwa ni silka na hivyo ni vigumu kuthibitisha iwapo mgombea ana au hana tatizo hilo.
Dk Sedoyeka alisema kiongozi anayesema atapambana na rushwa anatakiwa kupimwa kwa rekodi yake ya uongozi kwa kuangaliwa iwapo aliweza kukemea, kuadhibu, au kukataa rushwa katika mazingira yoyote yale.
“Kwa mfano wapo watu wanajiweka karibu na matajiri, wanapewa fedha na matajiri za kufanya kampeni, je watakuja kulipa vipi hisani za matajiri watakapoingia madarakani? Hayo ndiyo mazingira,” alisema

Wednesday, 3 June 2015

Ukawa wawaponda waliotangaza nia CCM

Sumbawanga/Dar. Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.
Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na mgombea safi.
Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo.
Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.
Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili.
“Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere, vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo.
“Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru) anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje.
Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi.“Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.

Wednesday, 20 May 2015

Ufisadi huu sasa kiama

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.
Pia, alisema misamaha ya Sh53.4 milioni ilitolewa kwa Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, lakini kampuni iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha na mengine matano ‘kuchepushwa’.
“Hata hivyo, ukaguzi ulithibitisha ununuzi wa gari moja tu ya Hyundai Santa. Magari mengine matano aina ya BMW na Toyota Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema. CAG aliishauri Serikali izibe mianya ya upotevu wa kodi kupitia misamaha ya kodi aliyobaini katika ukaguzi wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa misamaha ya kodi iliyotolewa.
Mashine za EFD
Alisema katika ukaguzi wa malipo na matumizi  ya mashine za kielektroniki (EFD), ofisi yake ilibaini kuwa kampuni binafsi hazitumii mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Alisema hali hiyo imesababisha malipo ya Sh4.4 bilioni kutokuwa na stakabadhi za kielektroniki kwa taasisi za Serikali Kuu na Sh4.6 bilioni kwa sampuli  22 ya mamlaka za serikali za mitaa.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini Sh440.8 milioni kwa wafanyabiashara ambao walishindwa kutumia mashine za EFD ambapo jumla ya Sh72 milioni zililipwa sawa na asilimia 16 na hivyo kufanya bakaa ya Sh369 milioni ambayo haikulipwa,” alisema.
Alisema pia ukaguzi ulibaini upungufu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile, malipo yasiyokuwa na nyaraka. Upungufu mwingine ni hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha zilizotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Alishauri taasisi za Serikali zisiendelee kanunua vifaa na huduma kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD kutoa stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Hii iende sambamba na kuhakikisha kuwa maofisa masuuli wanaimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ikiwa pamoja na kuimarisha ukaguzi kabla ya malipo,” alisema.
Mishahara hewa
Alisema fedha zilizolipwa kwa watumishi hewa wa Serikali Kuu ni Sh141.4 milioni, “Hali hii inaendelea licha ya kuwa Serikali imewekeza kwenye mfumo wa Lawson kama njia mojawapo ya kudhibiti hali hiyo,” alisema. Hata hivyo, alisema suala hilo linazidi kupungua ikilinganishwa na mwaka jana. Lakini alisema Sh1.01 bilioni katika halmashauri 36 zililipwa kama mishahara kwa watumishi waliotoroka kazini, waliofariki, waliostaafu na kufukuzwa kazi.
Alisema kutokana na watumishi hewa, Sh845 milioni za halmashauri zililipwa kama makato ya taasisi mbalimbali kama vile mifuko ya pensheni, taasisi za fedha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na TRA kwa ajili ya wafanyakazi hao hewa.
Katika balozi
CAG pia ameeleza jinsi Serikali ilivyolipa Sh543.7 milioni kutokana na kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani.
Watumishi hao ni wa balozi za Tanzania Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani).
Ripoti hiyo inaonyesha tarehe ambazo watumishi hao walistaafu, lakini Serikali iliendelea kuwalipa huku wakiwa katika maeneo yao ya kazi, zikijumuisha kodi za majengo huku baadhi ya watumishi hao wakifanya kazi licha ya kuwa mikataba yao kumalizika.
Ufisadi Tanesco
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo kwa ununuzi wa Sh3.2 bilioni uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bila kuzingatia kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ya Sh400 milioni.
“Katika zabuni nyingine, Tanesco iliingia mkataba wa Sh340 milioni ambayo ni zaidi ya bajeti iliyotengwa ya Sh154 milioni. Ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kuwapo kwa marejeo ya bajeti kwa kiasi kilichotumika nje ya makisio,” alisema
Vyama vya siasa
Kuhusu ukaguzi wa vyama vya siasa, CAG alisema hadi kufikia Juni, 2013 vyama 21 wakati vinakaguliwa, ni 12 tu ndivyo vilivyowasilisha taarifa za hesabu.Alisema kati ya vyama 12, tisa havikuwasilisha taarifa za hesabu ambavyo ni UPDP, Tadea, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa vyama sita vya siasa vilipata hati ya shaka ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na Chauma na vya vingine vilipata hati mbaya ambavyo ni NRD, UMD, ADC, APPT, NLD na SAU.
Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa akishirikiana na Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), waandae mwongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
Bajeti
Kuhusu bajeti, alisema tathmini waliyofanya kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, programu na shughuli nyingine za maendeleo katika baadhi ya halmashauri, imeonyesha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, halmashauri hizo zilikuwa na bakaa ya jumla ya Sh29.2 bilioni sawa na asilimia 28 ya jumla fedha zilizotolewa.
Alisema kubakia kwa kiasi kikubwa cha fedha bila kutumika katika utekelezaji wa miradi kunatokana na ucheleweshaji wa kutuma fedha katika halmashauri.
Deni la Serikali
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia Sh1,699 milioni na Sh975.1 milioni zilipaswa kuwa zimereshwa, lakini hadi wakati wa kuandika ripoti hiyo zilikuwa bado hazijalipwa.
Alishauri mifuko na Serikali kuzingatia na kufuata mwongozo wa uwekezaji wa fedha za mifuko ambao pamoja na mambo mengine, unatoa ukomo wa aina za mali ambazo mifuko inaweza kuwekeza.

Monday, 18 May 2015

UCHAGUZI UPINZANI 2015: Anna Mghwira, Mwenyekiti ACT- Wazalendo

Historia yake
Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini. (Januari mwaka huu alitimiza miaka 56).
Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.
Mgwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Thiolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea shahada ya Sheria.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa.
Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake  ngazi ya wilaya na katibu wa baraza la wanawake mkoa.
Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.
Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.
Mbio za ubunge
Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Josh) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Mbio za urais
Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila, tafiti kadhaa na maoni ya Watanzania zinaonyesha kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonyesha uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.
Nguvu yake
Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Mghwira anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.
Kwa sababu Mghwira ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.
Lakini nguvu ya tatu ya Mghwira ni uthubutu. Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.
Mghwira ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”. Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa Mghwira kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka.
Hata mtaalamu mshauri wa chama hicho Profesa Kitila Mkumbo ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalumu la wataalamu akiwemo Mghwira.
Profesa Kitila ananiambia kuwa kwa kiasi kikubwa katika timu hiyo, Mghwira ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa wanaume.
Nilipojaribu kumfikia Mghwira kwa ajili ya kupata taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake, sifa hii wanaikosa wakuu wengi wa nchi.
Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Mghwira ni mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na watu wa karibu naye ni kuwa yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.
Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu Taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.
Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Mghwira ni kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa, bado namuona kama mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kujipa jina kubwa kwa jamii.
Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana, lakini ninachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kile kina jukumu la kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana katika tasnia za siasa. Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa Chadema nakuchukulia kama udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama ACT - Wazalendo kitampitisha mwanamama huyu kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa mwanamke nafasi.
Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Mghwira atapitishwa, uzoefu wake kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu.
Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, Sweden, Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa vyuo vikuu hapa Tanzania na msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea urais na kuonyesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na wanaume.
Nini kinaweza kumwangusha?
Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo inayoweza kumuangusha. Ikiwa ACT kitadhani kuwa vyama vingine washindani vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Mgwira na kutafuta mwanachama mwingine “mwanamume” ambaye atakuwa na fursa ya kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii “ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Mghwira hana uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi aliyonayo ndani ya ACT - Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa siasa za kitaifa.
Lakini uzoefu wa jumla unaonyesha kuwa vyama mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje mwanamama huyu.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Ikiwa hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango mitatu mezani:
Mpango wa kwanza ni kugombea ubunge katika jimbo mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa za Tanzania kwa upana.
Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha vijana katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na wa kisheria katika jamii. Katika masuala haya ana uzoefu mkubwa nayo na itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia.
Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama cha ACT - Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa kuisha Februari, 2020. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea kufanya uongozi.
Hitimisho
Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka Chadema. Safari yake kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi nyingine kubwa za nchi kwa namna moja au nyingine, lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa Chadema.
Ikiwa Chadema kitazidi kukubalika kwa Wwatanzania na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye na wenzake watakuwa na wakati mgumu kujipambanua kisiasa na hivi ndivyo siasa za Afrika hutizamwa.
Pamoja na sintofahamu hizo, namuona Mgwira kama mmoja wanasiasa watulivu na wenye maono mapana katika Taifa hili. Kwa maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “Natamani siku moja nchi hii iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Mimi nimekulia kwenye familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu na tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika njia hiyo.”
Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu nguli wa upinzani na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa ikiwamo hii ambayo ametajwa kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.

Urais wawagonganisha NCCR-Mageuzi, Chadema

Dar es Salaam. Chama cha NCCR-Mageuzi kimeponda kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kwamba Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk Willibrod Slaa ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk Slaa, ndiye atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa ni makosa kudhani kwamba Chadema ndicho chenye nafasi ya kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa, wakati bado mchakato wa kumpata mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa waasisi na mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne vilivyounda Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”, alisema.
“Kwa kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu, sasa kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa waziri mkuu, hivyo haiwezekani watoe na mgombea urais. Nawashauri wachague nafasi mojawapo,” alisema Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo sahihi na hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani chama kimoja kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni vizuri ikaeleweka mapema kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama vinne washirika wa Ukawa, kikatoa mgombea urais, makamu na waziri mkuu,” alisema Sungura  na kuongeza:
“Kwa kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea urais wa Zanzibar, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati ya vyama hivyo kitamtoa ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge, kinyume chake ni tamaa inayoweza kuua Ukawa.”
Kwa mujibu wa Sungura, mageuzi chanya hayawezi kuletwa kwa ubinafsi, bali nia ya dhati ya Ukawa katika kuyatafuta.