Monday, 18 May 2015

Asimamishwa kazi kwa kumtumia JK ‘meseji

Moshi. Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa  na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.
Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa Mei 15.
Hata hivyo, bado mhasibu huyo hajarejeshwa kazini na vikao vilikuwa vinaendelea kuhusu hatua za kinidhamu zinazostahili dhidi yake.
“Wakati hayo mambo mawili yanafanyiwa kazi, menejimenti imeamua kukusimamisha kazi. Kabla hujaondoka unatakiwa ukabidhi vitendea kazi pamoja na simu ya mkononi uliyokabidhiwa,” imedai.
Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema kwa nafasi yake, hawezi kulizungumzia.
Mhumba alipotafutwa wiki iliyopita, alikiri kusimamishwa kazi kwa tuhuma za kumtumia Rais ujumbe wa simu ya mkononi, ingawa alikanusha kuhusika.
“Maudhui hayo kama ni kweli yalitumwa, hayana matatizo. Nimeongea na katibu mkuu kumuuliza kama alipokea sms kutoka kwa Rais na kuwapa KCMC na namba ya mtumaji amekanusha,” alidai.
Hata hivyo, alidai yeye akiwa mwenyekiti wa Tughe, amekuwa akionekana kama adui pale anapojaribu kutetea masilahi ya watumishi, likiwamo suala la kutopandishwa daraja tangu mwaka 2007 hadi 2015.
“Ni kweli, watumishi hawajapandishwa madaraja tangu 2007. Sisi (Tughe) tumekuwa tukilipigania kwa sababu linachangia wastaafu kulipwa pensheni ndogo,” alisema.
“Mimi kama kiongozi wa wafanyakazi, niko tayari kupeleka ushahidi kwa mambo ambayo Tughe tumekuwa tukipambana nayo, ikiwamo mahali zilipo fedha za mashine ya CT-Scan,” alisema Mhumba.
Tawi la Tughe KCMC, limemwandikia barua katibu mkuu wa Tughe, ikiomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aingilie kati suala hilo ili haki itendeke.
Gama alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupigiwa simu na Mhumba akimueleza lakini alimshauri aziandikie mamlaka husika.
Gama alisema akiwa mwakilishi wa Rais mkoani Kilimanjaro, atachunguza nini kimetokea baada ya kupata malalamiko rasmi kutoka kwa Mhumba au Tughe yenyewe.

Friday, 10 April 2015

Bakora sita za Ukawa kwa CCM

Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.
Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.
Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.
Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.
Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.
Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.
Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ufisadi 
Haitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia 70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa linaweza kukiathiri chama hicho.
Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.
Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi
Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa Taifa.
Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:
“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana na uzoefu uliopo.
“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu wa chama,” alisema Dk Mallya.
Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi kupigia kura vyama vya upinzani.
“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao na kuondolewa.
Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa, umewafanya wengi kugawanyika.
“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.
Kauli ya CCM 
Kupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.
Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.
“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema Simba.
Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko vyote.
Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na makandokando yake.

Mambo sita yaliyomshinda Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi  na zaidi ameacha manung’uniko na mgawanyiko.
Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.
Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi, vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na Mahakama ya Kadhi.
Sheria ya Habari
Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.
Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013 gazeti  la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni (Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).
Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.
Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa gazeti la The EastAfrican nchini.
Katiba Mpya
Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8,      2010 siku alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa Watanzania Katiba Mpya.
Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,  akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba. Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.
Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK, likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015 Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30. Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mahakama ya Kadhi
Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.
Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.
Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.
Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.
Mgogoro Zanzibar
Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani. Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani aliyepinduliwa mwaka 1964,  Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi mwaka 1964.
Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth, kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.
Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta ya ufugaji iwe ya kisasa.
Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.
Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji katika maeneo tofauti nchini.
Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo, waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira na uhasama vimetanda kila mahali.
Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.
Vita ya ufisadi
Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima ushahidi uwepo kwa asilimia 100.
Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa kuwashughulikia.
Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya, waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.

Friday, 27 March 2015

SHERIA: Sheria gharama za uchaguzi kung’ata zaidi

Dar es Salaam. Serikali inakusanya nguvu kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, inang’ata wagombea wote watakaojihusisha na rushwa katika harakati zao za kusaka uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watendaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamesema, utekelezaji wa sheria hiyo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi uliopita mwaka 2010.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ofisi yake ilikumbana na  changamoto nyingi zilizofanya ishindwe kuisimamia sheria hiyo ipasavyo.
“Mwaka 2010 changamoto zilikuwa nyingi lakini tumejifunza. Uchaguzi wa mwaka huu tumeshajipanga, tunajua jinsi gani ya kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, tunajua tunahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau ili kuweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Nyahoza.
Nyahoza alitaja wadau ambao ofisi hiyo inatarajia kushirikiana nao katika kuisimamia sheria hiyo kuwa ni pamoja na vyama vyote vya siasa, asasi za kijamii, waandishi wa habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ushirikiano huu unaanza kuimarishwa kabla ya uchaguzi. tumebaini kwamba wadau hawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya namna wanavyoweza kushiriki kufanikisha utekelezaji wa sheria hii, pia kutakuwa na simu maalumu za kuripoti matukio yatakayokuwa kinyume,” alisema. 
Kauli ya Takukuru 
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikiri kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha nguvu hizo, licha ya kukabiliwa na changamoto ya rasilimaliwatu.
“Ni kweli hata sisi tumeona kuna umuhimu wa kushirikiana katika kufanikisha jambo hili, ingawa kuna changamoto ya rasilimali watu, tunaamini kazi zitafanyika kwa namna ambayo itadhihirisha dhana ya kuwapo kwa Takukuru,” alisema Dk Hoseah.
Dk Hoseah pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuepuka kuuza haki zao za kuchagua viongozi bora kwa kudanganywa na zawadi za kanga, fulana, kofia na fedha. 
Sheria ikoje?
Ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010. Sheria hiyo  imeweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato, matumizi  na gharama za kampeni na uchaguzi wa vyama vya  siasa na wagombea.
Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 17, 2010 ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kwa lengo la   kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.
Madhumuni ya kuwekwa Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hii imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo ni jina, tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.
Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.
Sehemu ya  tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sehemu ya sita ya sheria hii inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.
Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.
Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapigakura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.
Sehemu ya nane ya sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya vyama  vya siasa ili kuoanisha masharti  ya sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi.

Urais Ukawa, hesabu zinalalia Chadema

Dar es Salaam. Wakati wenyeviti wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na kamati zake za kitaalamu wanakutana Zanzibar kutafuta suluhu kuhusu mgawanyo nafasi za kugombea katika uchaguzi mkuu ujao, kuna uwezekano mkubwa vyama hivyo kuteua mgombea urais kutoka Chadema.
Tovuti hii inaweza kuripoti kwa uhakika kuwa uwezekano huo unatokana na vigezo vinavyotumiwa na vyama hivyo kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo na kwenye nafasi ya urais ambavyo vinaipa Chadema nafasi hiyo dhidi ya vyama vingine katika umoja huo ambavyo ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Vigezo hivyo ni matokeo ya uchaguzi 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba mwaka jana, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi kutoka ndani ya kamati ya ufundi ya Ukawa zinasema pamoja na kuwapo mvutano katika baadhi majimbo Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo hilo, jambo linaloipa CUF nafasi ya moja kwa moja kwenye ubunge, uwakilishi na hata urais wa visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi nzuri ya CUF kupita moja kwa moja Zanzibar bila ushindani ndani ya Ukawa, inatoa fursa kwa upande wa Bara, kwa vyama vilivyosalia kupitishwa kuwania urais wa Muungano.
Hata hivyo, kwa vigezo vilivyotajwa hapo juu, Chadema ndiyo inakuwa na nafasi isiyo na kipingamizi kutokana na rekodi vyama vilivyosalia Bara.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Chadema kilimsimamisha Dk Slaa na aliibuka wa pili baada ya Rais Jakaya Kikwete akiwa na kura 2,271,941 (asilimia 26.34) akifuatiwa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyepata kura 695,667 (asilimia 8.06) na Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 26,388 (asilimia 0.31). NLD haikusimamisha mgombea urais.
Kwa upande wa majimbo yaliyotokana na uchaguzi wa 2010, Chadema kiliongoza kikiwa na wabunge 24 (wote kutoka Bara), CUF 23 (wawili kutoka Bara, 21 Zanzibar) na NCCR-Mageuzi wanne (wote wa Bara).
Katika rekodi za uchaguzi wa mitaa zilitolewa na Tamisemi kabla ya chaguzi za marudio, Chadema ilipata mitaa 980, ikifuatiwa na CUF (mitaa 266), NCCR Mageuzi  (28)  na NLD mtaa mmoja. Kwa upande wa vijiji, Chadema kilishinda vijiji 1,754, CUF (516), NCCR-Mageuzi (67) na NLD vijiji viwili.
Hata kwa upande wa vitongoji Chadema kiliviongoza vyama hivyo kwa kupata vijiji 9,145 kikifuatiwa na CUF (2,561), NCCR-Mageuzi (339) na NLD vitongoji viwili.
Tayari NCCR-Mageuzi kimeonyesha nia ya kumteua Dk George Kahangwa kuwania urais wakati Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikaririwa na gazeti hili hivi karibuni akisema kuwa chama chake kimekwishamteua kuwania urais, hivyo jina lake litapelekwa Ukawa kushindanishwa.
Mvutano mkali
Hali ikiwa hivyo, wajumbe wa Ukawa leo watakumbana na wakati mgumu wa kufikia maridhiano ya kugawana majimbo 19 kutokana na taarifa za kuwapo mvutano mkali wa pande zote za vyama husika.
Wanaokutana leo ni wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka vyama hivyo.
Kabla ya kuanza kikao cha leo, jana asubuhi wajumbe 16 wa Kamati ya Ufundi walikutana na baadaye jioni wenyeviti wa umoja huo wakawa na kikao cha awali, ikiwa ni sehemu ya vikao vya hatua za kugawana maeneo ya kuwania ili kutoa ushindani na hatimaye ushindi dhidi ya CCM.
Chanzo cha habari kutoka ndani kimelieleza Mwananchi kuwa NLD nayo imeongeza mvutano ikihitaji majimbo matano.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuwa Ukawa ilikuwa imekamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 170 lakini ukawapo mvutano katika majimbo 19 ambayo vyama zaidi ya kimoja vilikuwa vinayataka.
Majimbo hayo ni Segerea, Kinondoni, Kigamboni na Ukonga ya Dar es Salaam, Morogoro Mjini na mengine ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.
“Mvutano ni kwamba, kuna vyama vinavyotaka uwakilishi tu wa majimbo hayo lakini kiukweli yanaweza kupotea bure tu endapo vitakabidhiwa. Wengine wanataka kuangalia zaidi ushawishi wa chama ndani ya jimbo husika ila wengine wanapinga, wakisema umoja huo hautakuwa na sababu kama watakosa uwakilishi,” kilieleza chanzo hicho.
“NLD wanahitaji majimbo matano, CUF na Chadema wanavutana zaidi, ila NCCR-Mageuzi wameonekana kushtushwa sana na hali hiyo,” kilisema chanzo kingine kutoka NCCR-Mageuzi.
Chanzo kingine kilieleza kuwa kamati ya wataalamu ilishakamilisha kazi yake ya uchambuzi wa majimbo hayo na kuwasilisha taarifa zake lakini kuna upinzani mkali ambao umeendelea kuibuliwa na wajumbe wa umoja huo.
“Kikao cha leo kinaashiria kuwa na mvutano, ninaamini kuna uwezekano wa kufikia mwafaka lakini ikishindikana kabisa kwa leo lazima vitaandaliwa vikao vingine,” kilieleza chanzo kingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu, Benson Kigaila (Chadema) alisita kuweka wazi juu ya mvutano uliopo huku akibainisha kuwa maridhiano yatapatikana.
Kigaila alisema kikao cha leo kina nafasi kubwa ya kumaliza mvutano huo na kueleza Watanzania juu ya mwelekeo wa safari yao.
Kigaila ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni ya Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chadema, alisema: “Kwa sasa siwezi kueleza chochote kwani vikao ndiyo vinafanyika kwa sasa, lakini naomba vikao vikishamalizika viongozi wetu watazunguza tu,” alisema.
Alipoulizwa juu ya NLD kuhitaji majimbo matano, Kigaila alikiri kuwa kweli wanataka mgawo wa majimbo lakini alikataa kutaja idadi yake.
“NLD wanayo haki kama vyama vingine, kwa nini wasipate? Watapata, lakini kuna taarifa sahihi zitakazoelezwa baada ya kikao cha leo.”
Jumanne wiki hii, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara, Magdalena Sakaya alilieleza gazeti hili kuwa kikao hicho kitakuwa na ajenda ya kukusanya maoni na mapendekezo ya wanachama, kujadiliana kwa pamoja ili kufikia muafaka wa majimbo hayo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema katika hatua za kutafuta maridhiano ya majimbo hayo, vyama vyote vinapaswa kutambua kila nafasi ya chama kilichoshiriki kwenye makubaliano ya Ukawa.
“Tukifuata kanuni, nadhani kuna vyama ambavyo havitakuwa na nafasi Ukawa na haitakuwa na maana ya kuungana, kwa hivyo lazima busara itumike zaidi. Haiwezekani chama fulani kilazimishe kuchukua majimbo mengi kuliko kingine,” alisema Nyambabe.
Alipoulizwa kuhusu utata katika mgawanyo wa majimbo, Dk Slaa alisisitiza kumalizika kwa mvutano kutokana na busara za viongozi wa vyama hivyo.

Thursday, 26 March 2015

Marufuku kuvuta sigara hadharani

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid amesisitiaza tamko la kupiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma ili kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara.
Tamko la Waziri limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, moja ya magonjwa yanayosababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Agizo hilo limezingatia Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL, ya mwaka 2003, Kipengele cha 12(1) ambacho kinakataza matumizi ya bidhaa hiyo katika maeneo ya umma.
“Agizo hili linawataka wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku, kupunguza au kuacha kabisa, pia linaijumuisha jamii yote kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma,” alisema Waziri katika tamko lake.
Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara ya kwanza mwaka 1575 na Kanisa la Katoliki lakini katika karne ya 20 harakati dhidi ya uvutaji sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.
Sababu kubwa ya kupiga marufuku ni ukweli kwamba uvutaji sigara ni hiari wakati kuvuta pumzi ni lazima, hivyo mtu anayetumia kilevi hicho hana budi kukaa mbali ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa kama ya moyo na saratani kwa wasiotumia na ambao kuvuta pumzi ni lazima.
Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema nia ya marufuku hiyo ni kuhakikisha wizara inatimiza kwa vitendo sheria hiyo ya bidhaa za tumbaku kwa kupiga marufuku na kuchukua hatua za kisheria. “Jamii itusaidie kutoa elimu katika hili, kuna suala la kujenga maeneo maalum ya kuvuta sigara na elimu kwa wale wanaovuta,” alisema.
Sheria ya usimamizi wa bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003, inaeleza kuwa nia ni kuwalinda vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 na wale wasiovuta wasishawishike kuvuta.
Kuwalinda wasiovuta wasipate madhara, kuifahamisha jamii juu ya madhara ya tumbaku na madhara ya kuvuta moshi wa sigara inayovutwa na mwingine na kuhakikisha jamii haina wavutaji sigara.
Maeneo ambayo yamepigwa marufuku kuvuta sigara yametajwa katika tamko hilo kuwa ni katika ofisi zote za serikali na taasisi zake, hospitali za umma, vyuo vikuu na shule za umma, vituo vya usafiri wa anga, mabasi, bandari na treni, bustani, fukwe na katika maeneo ya kupumzika ya umma.
Pia tamko hilo la wizara limekataza uvutaji wa sigara katika mikutano yote ya kiserikali.
“Wizara inawataka wale wote ambao wanataka kuacha kabisa kuvuta sigara, wawatafute wataalamu wa afya ili wapate ushauri wa kitaalamu,” alisema waziri katika tamko hilo.
Kadhalika, agizo hilo limewataka wafanyakazi wa sekta ya afya na watumishi wa umma kuhakikisha wanafanyia kazi na wanasimamia agizo hili.
“Tunataka kila mmoja ashiriki katika agizo hili la kuzuia bidhaa za tumbaku, sekta binafsi, asasi za kidini na wadau wengine wa afya watusaidie katika kufanikisha hili,” alisema Waziri
Wakati wizara ikitoa tamko hilo, Kampuni ya Sigara (TCCL) imekuwa moja ya kampuni zilizoongoza kwa kulipa kodi mwaka jana.

Tanesco haiwezi kukwepa lawama hizi

Leo katika gazeti hili tuna habari kuhusu vifo vya watu watatu ambao umauti wao unaelezwa kusababishwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia kwenye nguzo ya Tanesco.
Ni tukio la kusikitisha kwa sababu miongoni mwa waliokufa ni wanafunzi wawili. Lakini huzuni inaongezeka pale inapobainika kuwa tukio hilo limechangiwa na uzembe wa Tanesco. Kwa mujibu wa Mjumbe wa Shina wa mtaa lilipotokea tukio, Kondo Namna, taarifa za hitilafu hiyo ziliripotiwa kituo cha Tanesco Kurasini tangu Agosti 2, 2014. Lakini tangu wakati huo hakuna matengenezo yaliyofanyika hadi vifo vilipotokea Jumapili.
Kwa mujibu wa Kondo pia zaidi ya nguzo saba zimeinamia kwenye nyumba za watu na wameshatoa taarifa Tanesco, lakini hadi wakati wa tukio hilo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Lakini baada ya vifo hivyo shirika hilo lilikwenda kutoa pole kwa wafiwa na baadaye Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema jambo hilo linatakiwa lifanyiwe uchunguzi wa kina na hawezi kuwachukulia hatua wafanyakazi wanaodaiwa kuzembea.
Tunashindwa kumuelewa Mramba anataka uchunguzi wa kina wa nini, wakati ni ukweli kwamba wenye wajibu wao hawakuwajibika ipasavyo. Kuna mfululizo wa matukio mengi yanayotokana na uzembe wa wahusika kutokelekeza wajibu wao ipasavyo.
Aprili 2014 tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero mkoani Morogoro, mtoto Amon Ndawala mwenye umri wa miaka mitano, alikufa baada ya kugusa nyaya za umeme ambapo Tanesco walitaarifiwa lakini walipuuza kurekebisha hitilafu hadi kifo kilipotokea. Kabla ya tukio kuna taarifa kwamba wananchi kwa muda mrefu walilalamikia hatari ya miundombinu ya umeme katika eneo hilo, ikiwamo nyaya za shirika hilo kugusa juu ya paa za baadhi ya nyumba za watu huku nyingine zikigusana na miti ama kuning’inia njiani. Wananchi hao walidai kuwa wamekuwa wakitoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi wa shirika hilo kuhusiana na mazingira ya hatari ya miundombinu ya Tanesco, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kurekebisha.
Agosti 2013 huko Mbalizi mkoani Mbeya, nyaya za umeme zilizokuwa zimening’inia mita moja kutoka usawa wa ardhi, zilisababisha kifo cha Neema Kipenya (26), baada ya kuteleza na kushika nyaya hizo kwa lengo la kujinusuru asianguke. Tukio hilo lilielezwa kusababishwa na uzembe wa kutoziondoa nyaya hizo na kuziacha hapo kwa miezi kadhaa.
Julai 2013 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro eneo la Sadala, kijana aliyefahamika kwa jina la Valerian Mosha alikufa baada ya kunaswa na umeme uliotokana na kulegea kwa nguzo ya Tanesco na kusababisha nyaya zinazopitisha umeme kuwa kimo cha chini. Hayo ni matukio machache kati ya mengi ambayo yamesababisha vifo kutokana na uzembe wa wafanyakazi wa Tanesco, ama kwa makusudi au kwa sababu wanazozifahamu wenyewe.
Leo mkurugenzi wa Tanesco anaibuka na kusema hawezi kumchukulia hatua mfanyakazi wake, hadi uchunguzi wa kina ufanyike. Ni uchunguzi gani anaoutaka Mramba, zaidi ya taarifa zilizotolewa kuhusu dharura na kushindwa kufanyiwa kazi na watendaji wake?
Tunahoji kitengo cha dharura cha Tanesco kina kazi gani? Tabia ya wafanyakazi wa Tanesco ya kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati inatoka wapi? Ni nani wa kuwajibika kutokana na uhai wa Watanzania kupotea bila sababu? Kwa nini viongozi wa Tanesco wanashindwa kuwachukulia hatua wafanyakazi wazembe?

Utafiti: Hali ya uchumi ya mtu mmojammoja nchini ni mbaya kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita

Hivi karibuni, Taasisi ya Repoa ilitoa utafiti wake unaoonyesha kuwa hali ya kiuchumi ya wananchi inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, licha ya pato la taifa kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia saba, Watanzania wengi wanaamini kwamba hali ya uchumi nchini mbaya.
Utafiti huo wa Afrobarometer, awamu ya sita uliofanywa kati ya Agosti 26 na Septemba 29 mwaka jana, walihojiwa Watanzania 2,386 wa Tanzania Bara na Visiwani. Wananchi hao walisema kuwa hali ya maisha inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2003.
Akitoa ripoti ya utafiti huo, Dk Lucas Katera kutoka Repoa, anasema wananchi wanalalamika kuwa licha ya Serikali kusema kuwa uchumi ni mzuri na kwamba nchi inapiga hatua ikilinganishwa na ilivyokuwa, wanaona watu wachache tu ndiyo wanaonufaika na maendeleo hayo.
Akitoa mfano anasema mwaka 2003 asilimia 42 walisema hali ya uchumi ilikuwa mbaya, mwaka 2005 asilimia 38, utafiti uliofuata mwaka 2008 idadi ya wananchi iliongezeka na kufikia asilimia 57 huku mwaka jana walikuwa asilimia 67.
“Idadi ya wananchi wasioridhishwa na namna Serikali inavyotekeleza miradi ya huduma za kijamii imeongezeka. Wananchi wanne kati ya kumi hawafurahishwi na huduma ya maji inayotolewa,” anasema Dk Katera.
Mtafiti huyo anasema matokeo hayo yamebaini kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya hali mbaya ya kiuchumi na utoaji mbaya wa huduma za jamii.
“Wananchi saba kati ya kumi wanasema Serikali inafanya vibaya kwenye sekta ya maji na elimu jambo linalosababisha hali mbaya ya kichumi,” anasema.
Mtaalamu wa Sera na Bajeti, Gilead Teri anasema wananchi wanahoji juu ya sababu zinazofanya matumizi ya Serikali kutowekwa wazi. Wanapendekeza uwazi zaidi uongezwe kwenye masuala yanayohusu umma.
“Wengi wamekata tamaa, wanasema takwimu hizo haziendani na hali halisi ya kipato chao. Hapa Serikali inapaswa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii,” anasema.
Teri anasema kukithiri kwa rushwa ni moja ya changamoto zinazowafanya wananchi kutokuwa na imani na Serikali.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi anasema uchumi unaweza kukua, lakini kama hakutakuwa na matumizi sahihi ya fedha za umma wananchi wataendelea kuona kasoro za kiuchumi.
Dk Ngowi anasema, kama tatizo ni watendaji Serikalini, kununua vitu vyenye thamani kubwa visivyomlenga mwananchi wa kawaida, moja kwa moja, kunawafanya wananchi kutoona faida ya ukuaji wa uchumi.
“Sekta binafsi ndizo zinazochangia ukuaji wa uchumi kwa kutoa asilimia fulani ya faida waliyoipata kwa jamii. Ni vigumu wananchi kujua kiasi kilichotolewa kutokana na muundo wa sheria za uwekezaji nchini,” anasema.
Hata hivyo, wakati tafiti kutoka mashirika binafsi zikionyesha kuwa hali ya uchumi imekuwa mbaya kuliko ilivyokuwa mwaka 2003, Serikali kwa upande wake imekuja na matokeo yanayotoa taarifa tofauti.
Msimamo wa Serikali
Serikali daima umekuwa ikishikilia msimamo tofauti na tafiti hizo. Wao wanaamini wananchi wananeemeka kupitia miradi mbalimbali wanayoiendesha.
Akitangaza matokeo ya kwanza ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa mwaka 2013/14 Machi 13, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema ripoti ya mpango huo iliyotolewa na waangalizi kutoka nje ya nchi inaonyesha hali ya maisha kwa wananchi imeanza kuimarika.
Pinda anasema hali hiyo imeimarika kupitia sekta ya elimu iliyofanya vizuri zaidi kwa kupata asilimia 81, maji asilimia 80, Nishati asilimia 79, Kilimo asilimia 77, Uchukuzi asilimia 64 na Utafutaji Rasilimali Fedha asilimia 54.
Kwa matokeo hayo, anasema malengo ya BRN yanaonyesha dalili za kuleta ‘nuru’ katikati ya giza la umaskini linalowafunika wananchi wengi hasa waishio vijijini.
Waziri Mkuu anasema: “Kiu ya Watanzania kujiletea maendeleo endelevu imekuwa ni jambo lililochukuwa nafasi ya kipekee katika historia ya taifa letu.”
Akiwasilisha bungeni Hotuba ya mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya anasema umaskini wa kipato unaendelea kupungua nchini huku uchumi ukikuwa kwa kiwango cha kuridhisha.
“Ukuaji huu umeongeza pato halisi la wastani la kila Mtanzania hadi kufikia Sh1,186,200 mwaka 2013 kutoka Sh1,025,038 mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 14. “Umaskini wa kipato umeendelea kupungua ambapo kwa mujibu wa takwimu mpya za Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya Binafsi uliofanyika Mwaka 2012, umeonyesha kuwa umaskini wa kipato umepungua kwa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asilimia 34.4 hadi asilimia 28.2,” anasema Mkuya.
Vilevile, Waziri huyo anasema umaskini wa chakula umepungua kwa asilimia 2.1 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asilimia 11.8 hadi asilimia 9.7.
Mwandishi maarufu wa vitabu nchini Marekani, Mark Twain aliwahi kusema kuwa kufanikiwa katika maisha unahitaji vitu viwili; ujinga kidogo na ujasiri.
Anasema kuna wakati mwanadamu huhitaji kuwa mjinga kidogo ili aweze kufanya mambo anayoyaamini hata kama watu wote waliomzunguka wanampinga. Pia anahitaji ujasiri kufanya jambo ambalo wengine wanaliogopa.
Hata hivyo, ni wazi Watanzania wengi wanaamini kwamba kukua kwa uchumi wa nchi kunatokana na Serikali kuwabana kupita kiasi kwa kodi huku wafanyabiashara wakubwa na makundi machache wakineemeka zaidi kwa rasilimali za nchi.
Pato la Serikali linaongezeka lakini lile la wananchi walio wengi ni dogo ukilinganisha na gharama halisi za maisha.
Serikali inapaswa kuwa makini kubadili mwenendo huo. Hili litawezekana iwapo itawatumia wataalamu wake wa uchumi katika kuwashauri.

Miswada miwili ya habari kuwasilishwa ‘kimafia’ bungeni

Licha ya wadau wa habari kuwasilisha ombi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda wakitaka miswada miwili ya habari ya mwaka 2015 iwasilishwe kwa mfumo wa kawaida, Serikali imeing’ang’ania huku ikisema itawasilishwa chini ya hati ya dharura Jumanne ijayo.
Miswada hiyo ni kati ya minne yenye ‘utata’ ambayo ilikuwa iwasilishwe bungeni leo na kesho, lakini jana ofisi ya Bunge ilitoa ratiba mpya inayoonyesha kuwa itawasilishwa wiki ijayo chini ya hati ya dharura, ikiwa ni kinyume na maombi ya wadau wa habari.
Kaimu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu aliliambia gazeti hili jana kwamba Serikali inataka kufanya ubabe na imepanga kuiwasilisha Jumanne asubuhi licha ya wabunge kutojua nini kimeandikwa.
Miswada hiyo ni pamoja na ule wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa mwaka 2014, Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa mwaka 2015 na Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari.
Juzi, wadau hao walimwomba Spika Makinda atumie hekima kuishauri Serikali iiwasilishe katika mfumo wa kawaida miswada miwili ya habari, ili kutoa fursa kwa wananchi na wadau kutoa maoni kabla ya kupitishwa na kuwa sheria.
Imeelezwa kuwa Jumanne, Muswada utakaoanza kuwasilishwa bungeni ni ule wa Sheria ya Kupata Habari na utafuatiwa na wa Sheria ya Vyombo vya Habari.
“Tunajua kuwa miswada hii imelenga kuvifungia vyombo vya habari, maana huu ni mwaka wa uchaguzi. Wanachokifanya Serikali ni kuiwasilisha bungeni ‘kimafia’ tu. Sisi tutakachokifanya ni kuibana bungeni,” alisema Lissu.
Hata hivyo, alisema kutokana na wingi wa wabunge wa CCM, huenda miswada hiyo ikapitishwa, jambo alilodai kuwa litakuwa gumu kulizuia.
“Mpaka sasa hatujaipata miswada hii, kwa kweli jambo hili linatusikitisha maana hata katika kamati haijafika,” alisema Lissu.
Tangu mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea mjini hapa ulipoanza, kumekuwa na taarifa kuwa Serikali inakusudia kuwasilisha miswada hiyo chini ya hati ya dharura, lakini wadau wa habari wameendelea kuiomba ibadili msimamo huo kwani kufanya hivyo kutawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni juu ya miswada hiyo kabla ya kuwa sheria.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel juzi alilieleza gazeti hili kuwa miswada hiyo hata ikiwasilishwa itakuwa vigumu kujadiliwa kutokana na muda uliopo, huku akishindwa kuthibitisha kama kweli itawasilishwa ama laa.
Alipotafutwa tena jana, Kaimua Katibu huyo wa Bunge, Joel kufafanua mabadiliko ya ratiba hiyo na kama miswada hiyo pamoja na hati ya dharura vimeshafikishwa katika ofisi ya Spika, hakupatikana.

JK, Nkurunziza wazindua treni za mizigo kwenda Burundi, Uganda na DR Congo

Rais Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’ kutoka Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15 hadi 20 ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda, akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete alisema, “kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake kwa wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo hivyo kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini sasa itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema Tanzania imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na bahari. “Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa Kati wa Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga hatua kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura (Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha kuwajibika katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka bandari ya Dar es Salaam bila tatizo.
“Kama ambavyo nimesema inatuwezesha kukuza biashara za ndani na kimataifa na kukuza uchumi.”
Katika mradi huo, kilomita 2,707 za reli hiyo zipo Tanzania, barabara ni kilomita 2,406, pia bandari kubwa tatu za Dar es Salaam, Kigoma na Mwanza zipo Tanzania.
Kuhusu ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema kuwa idadi ya mizigo inayosafirishwa imeongeka kutoka tani milioni 9.2 mwaka 2010 hadi tani milioni 14 mwaka 2014 na kufikia mwishoni mwa mwaka huu inatarajiwa kufikisha tani milioni 18.
“Idadi ya siku za kutoa mzigo bandarini zimepungua kutoka siku 21 hadi 9 na bado tunataka zipungue zaidi. Kuhusu wizi hakuna taarifa ya tukio lolote kwa miaka miwili sasa…pia Serikali ina mpango wa kujenga bandari mpya Bagamoyo itakayoweza kuhifadhi tani milioni 240 kwa mwaka,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu reli, alisema kuwa vichwa 13 vya treni vimeshanunuliwa na kati yake viwili viliwasili nchini wiki iliyopita. Vichwa vitano vinatarajiwa kuwasili mwezi ujao na vilivyobaki vitaletwa Mei mwaka huu. Pia mabehewa 274 yamenunuliwa kati yake 150 yaliwasili nchini Februari mwaka huu.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na Tanzania kuingiza nchini mkongo wa mawasiliano ya intaneti, bado haijanufaika kiasi cha kutosha kwa kuwa baadhi ya wananchi wanautumia kwa ajili ya kutuma ujumbe na picha kwa njia ya mtandao wa kijami wa WhatsApp.
Rais Museveni aliyekuwa kivutio kwa watu wengi mkutanoni kutokana na muda mwingi kutoa matamshi ya utani, alisema sababu mbalimbali zinazokwamisha biashara kufanikiwa kuwa ni pamoja na ukosefu wa usalama, kutokuwapo kwa watendaji wenye ujuzi, kukosekana kwa soko na kukosekana kwa faida kuwa ndiyo sababu zinazoweza kukwamisha biashara kustawi.
Alisema ili mipango ya kibiashara inayopangwa na nchi hizo ifanikiwe lazima vikwazo vijulikane na kutafutiwa ufumbuzi mapema.
“Wataalamu wa uchumi wanasema gharama ya usafiri katika biashara inapaswa kuwa asilimia 40, mtaji asilimia 20, kazi asilimia 10, ukilitimba asilimia tano, lazima tujiulize kikwazo kipi kinatukwaza,” alisema Museven.
Alisema hakuna namna ujenzi wa reli unaweza kuepukika kwa kuwa barabara zinapitika mara kwa mara huku zikigharimu fedha nyingi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed alisema miradi iliyoanzishwa chini ya mradi huo itachangia sehemu kubwa kuimarisha hali ya kiuchumi iliyokuwa imekwama katika baadhi ya miradi.