Rais Jakaya Kikwete na mwenzake Rais Pierre Nkurunziza wa
Burundi wamezindua safari za treni tatu za mizigo ‘block train’ kutoka
Dar es Salaam kwenda Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC).
Uzinduzi wa treni hizo zenye mabehewa 15 hadi 20
ulifanyika jana jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Rais Kikwete
kuzindua mkutano wa marais wanachama wa nchi zinazounda ukanda wa kati.
Marais waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni
Rais Yoweri Museven wa Uganda, Rais wa Kenya aliwakilishwa na Waziri wa
Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Amina Mohamed, Rais wa DRC aliwakilishwa na
Waziri wa Usafirishaji, Justine Kanumba huku Rais wa Rwanda,
akiwakilishwa na Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, James Musoni.
Akizindua treni hizo, Rais Kikwete alisema,
“kuanzia sasa zitakuwa zikibeba mizigo ya nchi moja pekee yake kwa
wakati mmoja, kama ni mizigo ya Burundi itakuwa Burundi tu vivyo hivyo
kwa DRC na Uganda, kinyume na ilivyokuwa awali.
“Awali safari za treni za mizigo zilikuwa
zikichukua wiki mbili kufikisha mizigo kwenye nchi husika, lakini sasa
itakuwa inachukua siku mbili pekee,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake Rais Nkurunziza alisema Tanzania
imefanya jambo la maana kuisaidia nchi yake ambayo ipo mbali na bahari.
“Safari hizo zitasaidia kusafirisha mizigo mingi na kwa njia ya kwa
haraka.”
Vikwazo vya usafirishaji
Awali akifungua mkutano wa Ukanda wa Kati wa
Kibiashara jijini hapa, Rais Kikwete alisema Tanzania imeshapiga hatua
kubwa katika kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo
kwenda nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vizuizi
barabarani.
“Tumeamua kupunguza vizuizi vya polisi barabarani
kutoka 15 hadi vitatu na vituo vya mizani kutoka 10 hadi vitatu
vitakavyojengwa vigwaza mkoani Pwani, Manyoni (Singida) na Nyakahura
(Kagera),” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni jukumu la nchi kuonyesha kuwajibika
katika mradi huo kwa kuwa sehemu kubwa ya mradi ipo nchini, hivyo ni
vyema kuhakikisha nchi jirani zinasafirisha mizigo yao kutoka bandari ya
Dar es Salaam bila tatizo.
“Kama ambavyo nimesema inatuwezesha kukuza biashara za ndani na kimataifa na kukuza uchumi.”
Katika mradi huo, kilomita 2,707 za reli hiyo zipo
Tanzania, barabara ni kilomita 2,406, pia bandari kubwa tatu za Dar es
Salaam, Kigoma na Mwanza zipo Tanzania.
Kuhusu ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema
kuwa idadi ya mizigo inayosafirishwa imeongeka kutoka tani milioni 9.2
mwaka 2010 hadi tani milioni 14 mwaka 2014 na kufikia mwishoni mwa mwaka
huu inatarajiwa kufikisha tani milioni 18.
“Idadi ya siku za kutoa mzigo bandarini zimepungua
kutoka siku 21 hadi 9 na bado tunataka zipungue zaidi. Kuhusu wizi
hakuna taarifa ya tukio lolote kwa miaka miwili sasa…pia Serikali ina
mpango wa kujenga bandari mpya Bagamoyo itakayoweza kuhifadhi tani
milioni 240 kwa mwaka,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu reli, alisema kuwa vichwa 13 vya treni
vimeshanunuliwa na kati yake viwili viliwasili nchini wiki iliyopita.
Vichwa vitano vinatarajiwa kuwasili mwezi ujao na vilivyobaki vitaletwa
Mei mwaka huu. Pia mabehewa 274 yamenunuliwa kati yake 150 yaliwasili
nchini Februari mwaka huu.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema pamoja na
Tanzania kuingiza nchini mkongo wa mawasiliano ya intaneti, bado
haijanufaika kiasi cha kutosha kwa kuwa baadhi ya wananchi wanautumia
kwa ajili ya kutuma ujumbe na picha kwa njia ya mtandao wa kijami wa
WhatsApp.
Rais Museveni aliyekuwa kivutio kwa watu
wengi mkutanoni kutokana na muda mwingi kutoa matamshi ya utani, alisema
sababu mbalimbali zinazokwamisha biashara kufanikiwa kuwa ni pamoja na
ukosefu wa usalama, kutokuwapo kwa watendaji wenye ujuzi, kukosekana kwa
soko na kukosekana kwa faida kuwa ndiyo sababu zinazoweza kukwamisha
biashara kustawi.
Alisema ili mipango ya kibiashara inayopangwa na nchi hizo ifanikiwe lazima vikwazo vijulikane na kutafutiwa ufumbuzi mapema.
“Wataalamu wa uchumi wanasema gharama ya usafiri
katika biashara inapaswa kuwa asilimia 40, mtaji asilimia 20, kazi
asilimia 10, ukilitimba asilimia tano, lazima tujiulize kikwazo kipi
kinatukwaza,” alisema Museven.
Alisema hakuna namna ujenzi wa reli unaweza kuepukika kwa kuwa barabara zinapitika mara kwa mara huku zikigharimu fedha nyingi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed
alisema miradi iliyoanzishwa chini ya mradi huo itachangia sehemu kubwa
kuimarisha hali ya kiuchumi iliyokuwa imekwama katika baadhi ya miradi.

No comments:
Post a Comment