Leo katika gazeti hili tuna habari kuhusu vifo vya watu watatu
ambao umauti wao unaelezwa kusababishwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia
kwenye nguzo ya Tanesco.
Ni tukio la kusikitisha kwa sababu miongoni mwa
waliokufa ni wanafunzi wawili. Lakini huzuni inaongezeka pale
inapobainika kuwa tukio hilo limechangiwa na uzembe wa Tanesco. Kwa
mujibu wa Mjumbe wa Shina wa mtaa lilipotokea tukio, Kondo Namna,
taarifa za hitilafu hiyo ziliripotiwa kituo cha Tanesco Kurasini tangu
Agosti 2, 2014. Lakini tangu wakati huo hakuna matengenezo yaliyofanyika
hadi vifo vilipotokea Jumapili.
Kwa mujibu wa Kondo pia zaidi ya nguzo saba
zimeinamia kwenye nyumba za watu na wameshatoa taarifa Tanesco, lakini
hadi wakati wa tukio hilo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Lakini
baada ya vifo hivyo shirika hilo lilikwenda kutoa pole kwa wafiwa na
baadaye Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba
alisema jambo hilo linatakiwa lifanyiwe uchunguzi wa kina na hawezi
kuwachukulia hatua wafanyakazi wanaodaiwa kuzembea.
Tunashindwa kumuelewa Mramba anataka uchunguzi wa
kina wa nini, wakati ni ukweli kwamba wenye wajibu wao hawakuwajibika
ipasavyo. Kuna mfululizo wa matukio mengi yanayotokana na uzembe wa
wahusika kutokelekeza wajibu wao ipasavyo.
Aprili 2014 tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero
mkoani Morogoro, mtoto Amon Ndawala mwenye umri wa miaka mitano, alikufa
baada ya kugusa nyaya za umeme ambapo Tanesco walitaarifiwa lakini
walipuuza kurekebisha hitilafu hadi kifo kilipotokea. Kabla ya tukio
kuna taarifa kwamba wananchi kwa muda mrefu walilalamikia hatari ya
miundombinu ya umeme katika eneo hilo, ikiwamo nyaya za shirika hilo
kugusa juu ya paa za baadhi ya nyumba za watu huku nyingine zikigusana
na miti ama kuning’inia njiani. Wananchi hao walidai kuwa wamekuwa
wakitoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi wa shirika hilo kuhusiana
na mazingira ya hatari ya miundombinu ya Tanesco, lakini hakuna hatua
zozote zilizochukuliwa kurekebisha.
Agosti 2013 huko Mbalizi mkoani Mbeya, nyaya za
umeme zilizokuwa zimening’inia mita moja kutoka usawa wa ardhi,
zilisababisha kifo cha Neema Kipenya (26), baada ya kuteleza na kushika
nyaya hizo kwa lengo la kujinusuru asianguke. Tukio hilo lilielezwa
kusababishwa na uzembe wa kutoziondoa nyaya hizo na kuziacha hapo kwa
miezi kadhaa.
Julai 2013 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro eneo la
Sadala, kijana aliyefahamika kwa jina la Valerian Mosha alikufa baada
ya kunaswa na umeme uliotokana na kulegea kwa nguzo ya Tanesco na
kusababisha nyaya zinazopitisha umeme kuwa kimo cha chini. Hayo ni
matukio machache kati ya mengi ambayo yamesababisha vifo kutokana na
uzembe wa wafanyakazi wa Tanesco, ama kwa makusudi au kwa sababu
wanazozifahamu wenyewe.
Leo mkurugenzi wa Tanesco anaibuka na kusema
hawezi kumchukulia hatua mfanyakazi wake, hadi uchunguzi wa kina
ufanyike. Ni uchunguzi gani anaoutaka Mramba, zaidi ya taarifa
zilizotolewa kuhusu dharura na kushindwa kufanyiwa kazi na watendaji
wake?
Tunahoji kitengo cha dharura cha Tanesco kina kazi
gani? Tabia ya wafanyakazi wa Tanesco ya kushindwa kutekeleza majukumu
yao kwa wakati inatoka wapi? Ni nani wa kuwajibika kutokana na uhai wa
Watanzania kupotea bila sababu? Kwa nini viongozi wa Tanesco wanashindwa
kuwachukulia hatua wafanyakazi wazembe?

No comments:
Post a Comment