Thursday, 26 March 2015

Utafiti: Hali ya uchumi ya mtu mmojammoja nchini ni mbaya kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita

Hivi karibuni, Taasisi ya Repoa ilitoa utafiti wake unaoonyesha kuwa hali ya kiuchumi ya wananchi inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, licha ya pato la taifa kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia saba, Watanzania wengi wanaamini kwamba hali ya uchumi nchini mbaya.
Utafiti huo wa Afrobarometer, awamu ya sita uliofanywa kati ya Agosti 26 na Septemba 29 mwaka jana, walihojiwa Watanzania 2,386 wa Tanzania Bara na Visiwani. Wananchi hao walisema kuwa hali ya maisha inazidi kuwa mbaya ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2003.
Akitoa ripoti ya utafiti huo, Dk Lucas Katera kutoka Repoa, anasema wananchi wanalalamika kuwa licha ya Serikali kusema kuwa uchumi ni mzuri na kwamba nchi inapiga hatua ikilinganishwa na ilivyokuwa, wanaona watu wachache tu ndiyo wanaonufaika na maendeleo hayo.
Akitoa mfano anasema mwaka 2003 asilimia 42 walisema hali ya uchumi ilikuwa mbaya, mwaka 2005 asilimia 38, utafiti uliofuata mwaka 2008 idadi ya wananchi iliongezeka na kufikia asilimia 57 huku mwaka jana walikuwa asilimia 67.
“Idadi ya wananchi wasioridhishwa na namna Serikali inavyotekeleza miradi ya huduma za kijamii imeongezeka. Wananchi wanne kati ya kumi hawafurahishwi na huduma ya maji inayotolewa,” anasema Dk Katera.
Mtafiti huyo anasema matokeo hayo yamebaini kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya hali mbaya ya kiuchumi na utoaji mbaya wa huduma za jamii.
“Wananchi saba kati ya kumi wanasema Serikali inafanya vibaya kwenye sekta ya maji na elimu jambo linalosababisha hali mbaya ya kichumi,” anasema.
Mtaalamu wa Sera na Bajeti, Gilead Teri anasema wananchi wanahoji juu ya sababu zinazofanya matumizi ya Serikali kutowekwa wazi. Wanapendekeza uwazi zaidi uongezwe kwenye masuala yanayohusu umma.
“Wengi wamekata tamaa, wanasema takwimu hizo haziendani na hali halisi ya kipato chao. Hapa Serikali inapaswa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii,” anasema.
Teri anasema kukithiri kwa rushwa ni moja ya changamoto zinazowafanya wananchi kutokuwa na imani na Serikali.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi anasema uchumi unaweza kukua, lakini kama hakutakuwa na matumizi sahihi ya fedha za umma wananchi wataendelea kuona kasoro za kiuchumi.
Dk Ngowi anasema, kama tatizo ni watendaji Serikalini, kununua vitu vyenye thamani kubwa visivyomlenga mwananchi wa kawaida, moja kwa moja, kunawafanya wananchi kutoona faida ya ukuaji wa uchumi.
“Sekta binafsi ndizo zinazochangia ukuaji wa uchumi kwa kutoa asilimia fulani ya faida waliyoipata kwa jamii. Ni vigumu wananchi kujua kiasi kilichotolewa kutokana na muundo wa sheria za uwekezaji nchini,” anasema.
Hata hivyo, wakati tafiti kutoka mashirika binafsi zikionyesha kuwa hali ya uchumi imekuwa mbaya kuliko ilivyokuwa mwaka 2003, Serikali kwa upande wake imekuja na matokeo yanayotoa taarifa tofauti.
Msimamo wa Serikali
Serikali daima umekuwa ikishikilia msimamo tofauti na tafiti hizo. Wao wanaamini wananchi wananeemeka kupitia miradi mbalimbali wanayoiendesha.
Akitangaza matokeo ya kwanza ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa mwaka 2013/14 Machi 13, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anasema ripoti ya mpango huo iliyotolewa na waangalizi kutoka nje ya nchi inaonyesha hali ya maisha kwa wananchi imeanza kuimarika.
Pinda anasema hali hiyo imeimarika kupitia sekta ya elimu iliyofanya vizuri zaidi kwa kupata asilimia 81, maji asilimia 80, Nishati asilimia 79, Kilimo asilimia 77, Uchukuzi asilimia 64 na Utafutaji Rasilimali Fedha asilimia 54.
Kwa matokeo hayo, anasema malengo ya BRN yanaonyesha dalili za kuleta ‘nuru’ katikati ya giza la umaskini linalowafunika wananchi wengi hasa waishio vijijini.
Waziri Mkuu anasema: “Kiu ya Watanzania kujiletea maendeleo endelevu imekuwa ni jambo lililochukuwa nafasi ya kipekee katika historia ya taifa letu.”
Akiwasilisha bungeni Hotuba ya mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya anasema umaskini wa kipato unaendelea kupungua nchini huku uchumi ukikuwa kwa kiwango cha kuridhisha.
“Ukuaji huu umeongeza pato halisi la wastani la kila Mtanzania hadi kufikia Sh1,186,200 mwaka 2013 kutoka Sh1,025,038 mwaka 2012 sawa na ongezeko la asilimia 14. “Umaskini wa kipato umeendelea kupungua ambapo kwa mujibu wa takwimu mpya za Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya Binafsi uliofanyika Mwaka 2012, umeonyesha kuwa umaskini wa kipato umepungua kwa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asilimia 34.4 hadi asilimia 28.2,” anasema Mkuya.
Vilevile, Waziri huyo anasema umaskini wa chakula umepungua kwa asilimia 2.1 kati ya mwaka 2007 na 2012 kutoka asilimia 11.8 hadi asilimia 9.7.
Mwandishi maarufu wa vitabu nchini Marekani, Mark Twain aliwahi kusema kuwa kufanikiwa katika maisha unahitaji vitu viwili; ujinga kidogo na ujasiri.
Anasema kuna wakati mwanadamu huhitaji kuwa mjinga kidogo ili aweze kufanya mambo anayoyaamini hata kama watu wote waliomzunguka wanampinga. Pia anahitaji ujasiri kufanya jambo ambalo wengine wanaliogopa.
Hata hivyo, ni wazi Watanzania wengi wanaamini kwamba kukua kwa uchumi wa nchi kunatokana na Serikali kuwabana kupita kiasi kwa kodi huku wafanyabiashara wakubwa na makundi machache wakineemeka zaidi kwa rasilimali za nchi.
Pato la Serikali linaongezeka lakini lile la wananchi walio wengi ni dogo ukilinganisha na gharama halisi za maisha.
Serikali inapaswa kuwa makini kubadili mwenendo huo. Hili litawezekana iwapo itawatumia wataalamu wake wa uchumi katika kuwashauri.

No comments: