Moja ya sababu kuu za kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), ni kutoa wigo mpana wa soko na shughuli za kiuchumi miongoni mwa
nchi wanachama.
Tanzania na Burundi ni kati ya nchi tano
zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi nyingine wanachama ni
Kenya, Uganda na Rwanda, wakati nchi ya Sudan Kusini ikiwa imetuma
maombi rasmi ya kujiunga.
Hivi karibuni, EAC iliandaa mafunzo ya siku tano
kwa waandishi 25 wa Ukanda huo, mafunzo yaliyoambatana na mkutano wa
pili wa siku tatu kuhusu Amani na Usalama miongoni mwa nchi wanachama.
Nilipata fursa ya kuwa kati ya waandishi watano
waliowakilisha Tanzania kwenye mafunzo hayo yaliyolenga kuwanoa
wanahabari namna ya kuandika habari za machafuko na migogoro bila kuleta
madhara kwa jamii.
Pamoja na mafunzo, waandishi wa habari kutoka
Tanzania walipata fursa ya kutembelea ubalozi wa Tanzania nchini
Burundi. Walipata fursa ya kujifunza mambo kadhaa, mojawapo ni fursa za
uwekezaji zinazopatikana nchini Burundi.
Katika mazungumzo yake na ujumbe wa waandishi wa
habari kutoka Tanzania, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk James
Mwasi Nzagi pamoja na mengine alizungumzia fursa ambazo Watanzania
wanapaswa kuzichangamkia hivi sasa.
Uwekezaji katika sekta ya elimu, hasa lugha ya Kiswahili
Burundi ikiwa moja ya nchi zinazoongea lugha ya
Kifaransa na Kirundi kama lugha rasmi ya kiofisi na mawasiliano, imeanza
kutilia mkazo lugha za Kiswahili na Kiingereza ambazo ni lugha rasmi ya
mawasiliano ndani ya EAC.
Serikali ya Burundi hivi sasa inahimiza wananchi
wake kujifunza na kumudu lugha za Kiswahili na Kiingereza. Lugha hizo
zinapaswa kufundishwa kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi Chuo
Kikuu.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa
ikizalisha idadi kubwa ya wahitimu katika sekta ya elimu kuanzia ngazi
ya cheti, diploma na shahada.
Uzalishaji nishati ya umeme
Baada ya kumalizika kwa vita na machafuko, nchi ya
Burundi hivi sasa inaelekeza nguvu nyingi kwenye kujenga na kuinua
uchumi wa Taifa hilo kwa kuhimiza uwekezaji katika sekta ya viwanda,
hasa vya uzalishaji.
Hata hivyo, juhudi hizo za serikali
zinakwamishwa kwa kukosekana kwa nishati ya umeme ya uhakika, hali
inayofanya viwanda vingi kutumia umeme unaozalishwa kwa kutumia
jenereta.
Matumizi ya umeme wa jenereta hunasababisha bei ya
bidhaa za viwandani kuwa kubwa kiasi cha kupunguza uwezo wa ununuzi kwa
wananchi wa kawaida wa Burundi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 9 milioni.
Huduma katika sekta ya hoteli za kitalii na kumbi za mikutano
Kutokana na kukua kwa kasi kwa uchumi wa Burundi
na uwepo wa mikutano ya kimataifa na wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa
na mabalozi wa nchi mbalimbali, ujenzi wa hoteli za kitalii nchini
humo, hasa Mji Mkuu, Bujumbura umeanza kwa kasi na hivyo kusababisha
uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi.
Sekta ya usafirishaji wa anga, barabara, reli na majini
Burundi ina mikoa 17 ambayo yote imeunganishwa kwa
barabara ya lami na hivyo kutoa fursa ya uwekezaji katika sekta ya
usafirisha wa mizigo na abiria kwa gharama nafuu.
Barabara za lami ambazo zote zimeunganishwa na Mji
Mkuu, Bujumbura ni fursa nyingine ya kibiashara kati ya mikoa mingine,
wilaya na vijiji vya Burundi kwa Watanzania wanaofanya biashara ya
usafirishaji abiria na mizigo kwa njia ya barabara.
Usafiri wa Anga
Hadi sasa hakuna ndege zinazofanya safari ya moja
kwa moja kutoka Bujumbura hadi Jijini Dar es Salaam ambapo abiria wote
hulazimika ama kupitia Nairobi Kenya, Kampala Uganda au Kigali Rwanda
ndipo waweze kufika Dar es Salaam au miji mingine nchini.
Usafiri wa maji (meli)
Tanzania na Burundi zinaunganishwa na Ziwa
Tanganyika na hivyo kutoa fursa ya uwekezaji kwenye sekta ya
usafirishaji kwa njia ya maji.
Hivi sasa meli pekee inayotoa huduma ya usafiri kati ya Burundi na Tanzania ni Mv Liemba ambayo umri wake ni zaidi ya miaka 50
Sekta ya Gesi, hasa za hospitalini
Kuna tatizo la upatikanaji wa uhakika wa gesi za
hospitalini ambapo wakati mwingine taifa hilo hulazimika kupata huduma
hiyo kutoka nchini Kenya.
Kutokana na Tanzania kufanikiwa kuwa na utajiri
mkubwa wa nishati ya gesi, hii ni fursa nyingine ya uwekezaji na
kibiashara kwa Watanzania wenye uwezo, ujuzi, utaalamu na uzoefu katika
biashara hii kujitanua katika soko la Burundi.
Uwekezaji katika viwanda vya Saruji
Hadi sasa, hakuna kiwanda cha Saruji nchini
Burundi. Saruji yote inayotumika nchini humo huagizwa kutoka nje ya nchi
na hivyo kufanya saruji kuwa moja ya bidhaa adimu na muhimu.
Kiwanda cha kutengeneza vyuma
Vyuma vyote vinavyotumika Burundi huagizwa kutoka
nje ya nchi, hasa nchini Ukraine. Mfanyabiashara atakayejenga kiwanda
cha chuma atakuwa na uhakika wa soko.
Kiwanda cha kutengeneza viatu
Kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, suala la
utengenezaji na uvaaji wa viatu nchini Burundi bado liko katika viwango
visivyoridhisha na siyo ajabu kukuta watu wazima wakitembea pekupeku
katika mitaa ya mji mkuu wa Bujumbura.
Siyo kwamba wananchi nchini Burundi wanatembea peku kwa kupenda. La hasha!
Bei ya viatu iko juu kiasi kwamba wananchi wenye
kipato cha chini hushindwa kumudu kununua viatu ambavyo vingi huagizwa
kutoka nje ya nchi.
Hii ni fursa mwafaka kwa Watanzania wenye uwezo
kuwekeza kwenye eneo hili kwani siyo tu watajihakikishia soko la Burundi
lakini pia wataweza kujipenyeza hadi kwenye soko la nchi jirani ya
Rwanda ambako tayari Rais wake, Paul Kagame amepiga marufuku watu
kutembea peku katika mitaa ya mji mkuu, Kigali.
Kushika soko la Burundi ni njia ya kuingia soko la DRC.
Kutoka mji mkuu wa Burundi, Bujumbura hadi mpakani
na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ni chini ya
Kilomita 20 pekee. Ukaribu huu unafanya wafanyabiashara nyingi
kuingiliana kati ya Burundi (Bujumbura) na DRC na hivyo kuongeza fursa
za kibiashara kwa Watanzania watakaowekeza Burundi.
Baadhi ya taarifa muhimu
Ukubwa wa nchi na idadi ya watu:
Nchi ya Burundi iliyopata uhuru Julai Mosi, 1962, ina ukubwa wa kilomita za mraba 28,000 na idadi ya watu zaidi ya 8 milioni.
Makabila Makuu Burundi
Wahutu: Hili ndilo kabila linaloongoza kwa kuwa na
idadi kubwa ya watu nchini Burundi kama ilivyo nchini Rwanda.
Inakadiriwa kuwa kabila hili ni asilimia 85 ya wananchi wote Burundi.
Kiasilia, Wahutu ni Wabantu ambao hujihusisha na kilimo kama njia kuu ya kipato pamoja na ufugaji kwa kiwango kidogo.
Watutsi: Hili ni kabila linalofuata kwa uwingi wa
watu nchini Burundi ikiwa na asilimia 14 ya wakazi wote wa nchi hiyo.
Asili yao ni ufugaji ingawa pia wanashiriki shughuli za kilimo.
Watwa: Hili ni kabila dogo lenye asilimia moja tu ya wakazi wa Burundi ingawa ndilo kabila la watu wa asili nchini humo.
Kiasilia Watwa ni wawindaji, warina asali na
waokota matunda (hunters and gatherers) kama walivyo makabila ya
Wahadzabe, Wandorobo, Wasandawe kwa hapa Tanzania.
Chakula: Chakula kikuu nchini Burundi ni ugali na
matoke inayoliwa kwa nyama, mboga za majani na samaki wanaopatikana Ziwa
Tanganyika, hasa mukake ambao kwa Tanzania, hasa kwa wakazi wa mikoa ya
Kigoma, Rukwa na Katavi hujulikana kwa jina la migebuka
Burundi pia imejaaliwa kuwa na uwingi wa aina mbalimbali za
matunda na vyakula vitokanavyo na mizizi kama mihogo, viazi vitamu na
viazi mviringo.
Kilimo:Mazao ya kilimo na chakula Burundi ni pamoja na kahawa, pamba, chai, mahindi, mtama, ndizi na viazi vitamu.
Muziki:Muziki maarufu unaopendwa na wananchi
Burundi ni ngoma ya Karyenda ambayo huchezwa kwa mtindo wa kuvutia
ukishirikisha wanawake na wanaume.
Ukiwa Burundi ekupa kuuliza zilipo kambi za jeshi
au ofisi za usalama. Tofauti na Tanzania ni kawaida kumsikia mtu akisema
kambi ya jeshi ya Mgulani, oohh Morogoro kuna kambi ya mizinga n.k.
Aidha, huruhisiwi kupiga picha mitaani bila kibali cha Meya wa mji, kwa
sababu za kiusalama.