Tuesday, 26 February 2013

Viongozi wapunguze anasa kunusuru maisha ya mama na mtoto

NI Jumatano nyingine tena, tunakutana katika safu yetu ya Jicho la Mtanzania. Jumatano ya leo safu hii itajikita katika suala la afya ya mama na mtoto kwa kuijadili hospitali yetu ya taifa Muhimbili.

Sote tunafahamu kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ndiyo hospitali mama katika nchi yetu. Ni hospitali ambayo magonjwa sugu hutibiwa, ina wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali za afya pamoja na uwepo wa vifaa vya kisasa.

Binafsi, pamoja na kuwa mkazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu, sijawahi kupata nafasi ya kufika katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu bali kusindikiza wagonjwa au kwenda kuona. Mara ya kwanza kufika hospitalini hapo nilimsindikiza rafiki yangu wa karibu aliyekuwa akiuguliwa na mtoto wake mchanga.

Mwanaye huyo, alizaliwa katika hospitali hiyo akiwa hajatimiza umri wa kuzaliwa (pre mature), kutokana na matatizo ya uvimbe tumboni mwa mama yake. Wakati mama wa mtoto anaruhusiwa kurudi nymbani aliambiwa na daktari wake kuwa ataendelea kuhudhuria kliniki chini ya uangalizi wa daktari bingwa wa watoto hapo Muhimbili mpaka daktari wake atakaporidhishwa na maendeleo ya mtoto ndipo atapewa ruhusu ya kuhudhuria kliniki nyingine.

Siku nilifika Muhimbili nikiwa na rafiki yangu, mwanaye alikuwa ameugua ghafla na hivyo kulazimika kuwahishwa hospitalini Muhimbili.

Tukiwa kitengo cha huduma za dharura, mama na mtoto walipokelewa na kuingizwa ndani kwa ajili ya kuonwa na daktari. Tulimsubiri mapokezi kwa takribani saa nne ndiyo akatoka huku akitueleza kuwa mtoto ameandikiwa kulazwa. Ilibidi tena tusubiri kwa karibu saa moja ili gari la kuwapeleka wodini kufika.

Tulipofika wodini tulikutana na daktari wa zamu ambaye naye alichukua maelezo kabla ya mama kuonyeshwa wodi. Baadaye alimwita muuguzi na kumwambia amtafutie kitanda lakini muuguzi baada ya kuzunguka huko na kule alirejea na kueleza hakukuwa na kitanda isipokuwa anaweza kutoa msaada wa kumtafutia kitanda ambacho itabidi atumie na mgonjwa mwingine.

Kitanda kilipopatikana tulimpeleka mtoto na mama yake wodini. Kitanda ambacho alitakiwa kukitumia kilikuwa tayari kina mtoto wa umri kama miaka miwili akiwa amelala na mama yake.

Muuguzi alimwamsha mama aliyekuwa amelala na kumwambia kuwa itabidi atumie kitanda hicho pamoja na mwenziye.

Wakati huo, nilikuwa nikijaribu kuangalia uwezekano wa kitanda kile ambacho ni kidogo kutumiwa na watu wanne. Kimsingi uwezekano ulikuwa mdogo kwani hata huyo mama tuliyemkuta akitumia na mwanaye walikuwa wamelala kwa kujibana.

Mama tuliyemkuta aliamka kwa upendo na kushauri mke wa rafiki yangu amlaze mtoto na wao wakae macho mpaka asubuhi kwa sababu isingewezekana kulala wote kitandani hapo kutokana na udogo wa kitanda.

Moyoni nilisikitishwa na hali ile. Rafiki yangu aliniomba ushauri wa kumuhamisha mgonjwa wetu pale kutokana na mazingira tuliyoyaona na baada ya kujadiliana tulikwenda kumwomba daktari atupe ruhusa na kurudi siku inayofuata asubuhi, jambo ambalo alilikubali baada ya kutazama hali ya mtoto na pia kuangalia mazingira ya pale wodini.

Nilijiuliza maswali mengi, lakini kubwa lilikuwa iwapo Serikali yetu ina dhamira ya dhati ya kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Jibu lililonijia haraka ni kwamba pamoja na tatizo la ufinyu wa bajeti ambalo nchi yetu inakabiliana nalo, bado Serikali haijaweza kuonyesha nia ya dhati ya kutokomeza vifo hivi ambavyo vinaweza kuepukika.

Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika uliofanyika Kampala nchini Uganda mwaka 2010, viongozi wa Afrika walikubali kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya afya kwa kupanua wigo wa afya ya mama na mtoto. Raisi Jakaya Kikwete, alitamka kuwa kupunguza vifo vya akina mama na wototo ni kipaumbele namba moja kwa Tanzania.

Lakini takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa vifo vya watoto wachanga bado viko juu. Jumla ya watoto 32 hufa kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa wakiwa hai ikiwa na maana kuwa vifo vya watoto wachanga 44,000 hutokea kila mwaka sawa sawa na asilimia 47 ya vifo vyote vya watoto wachanga.

Kimsingi, maisha ya watoto hasa chini ya mwaka mmoja hutegemea sana maisha ya mama zao au kwa lugha nyingine ni kuwa kama mtoto wa chini ya mwaka mmoja atafiwa na mama yake, uwezekano wa yeye kuishi unakuwa ni mdogo na ndiyo maana afya ya mama ina uhusiano wa karibu na ya motto.

Niliwaza mambo mengi kutokana na ile hali niliyoiona pale Muhimbili. Kwanza niliwaza kuwalaza watoto wawili wagonjwa ambao umri wao unapishana sana. Mmoja ana miaka miwili mwingine kwa wakati huo alikuwa hajafikisha hata umri ambao kwa kawaida mtoto anatakiwa kuzaliwa japokuwa tayari alikuwa ameshazaliwa akiwa na karibu mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa maelekezo ya daktari wake, mtoto huyo alitakiwa kupata uangalizi wa karibu sana na kuwekwa kwenye mazingira safi na salama bila ya kushikwa au kuonwa na watu tofauti na wazazi wake ambao walishapewa masharti ya kumtunza kwani mwili wake ulikuwa bado ni dhaifu, hivyo ni rahisi kwake kupata magonjwa, lakini siku hiyo alilazwa na mgonjwa mwingine.

Kwa upande mwingine sote tunafahamu kuwa, malaria ni ugonjwa namba moja unaosababisha vifo vya maelfu ya Watanzania kila mwaka. Kina mama wale ambao walikuwa wameamua kukesha wakiwaangalia watoto kutokana na kukosa vitanda vya kulalia, walikuwa kwenye hatari ya kupata malaria kutokana na mbu jambo ambalo siyo tu ni hatari kwa afya zao bali hata kwa afya za watoto wao ambao wanawategemea.

Tukitazama kwa pamoja hii ya Hospitali ya Taifa ikiwa katika hali hiyo, nyingine hali ikoje? Waliopata nafasi ya kutembelea Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke wanaweza kuwa mashahidi wazuri wa hali mbaya za hospitali hizo.

Haina shaka kwamba, kama viongozi wetu na familia zao wangekuwa wanatibiwa katika hospiali zetu hizi, pengine wangeona umuhimu wa kuboresha hali ya utoaji huduma kwa hospitali hizi.

Mameya wa Jiji na viongozi wengine wa manispaa zetu wanatembelea magari ya gharama aina ya Toyota VX V8. Haya ni magari ya kifahari na yenye gharama kubwa. Fedha hizi zinaweza kujenga wodi kubwa kwa ajili ya akina mama wajawazito pamoja na kuwawekea vitanda na vifaa vingine muhimu.

Hakuna sababu kwa viongozi wetu kutumia magari ya gharama kubwa kama haya kama taifa limekusudia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Viongozi wetu wakiamua akina mama na watoto wasife kwa kukosa huduma na vifaa tiba inawezekana iwapo watakubali kuachana na anasa walizozikumbatia sasa.

Mulugo: Michango ya CWT hulinda maslahi ya walimu

SERIKALI imesema fedha ambazo walimu huchangia katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hulinda na kutetea maslahi ya walimu wawapo kazini. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliliambia Bunge jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kiembesamaki, Waride Bakari Jabu.

“Kwa mujibu wa Sheria namba sita ya mwaka 2004 ya CWT inabainisha wazi kuwa, makato ambayo walimu hukatwa ni kwa ajili ya kulinda na kueteta maslahi wawapo kazini, lakini sheria hiyo haijaelezea mafao ya walimu mara wanapostaafu ama kufariki,” alisema Mulugo.

Aidha, alitoa wito kwa wabunge kuhakikisha wanatoa mapendekezo ya kuwapo kwa mabadiliko ya sheria hiyo na hatimaye walimu hao mara wanapostaafu ama kufariki waweze kupata mafao yao.

Katika swali lake la nyongeza, alitaka kujua walimu wananufaikia vipi pindi wanapostaafu ama kufariki kutokana na wao kuchangia kiasi cha Sh bilioni 2.2 ikiwamo makato ya NSSF kwa kila mwezi.

Alihoji fedha hizo ambazo walimu wanachangia kama zimekuwa zikikaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Akijibu swali hilo, Mulugo, alisema CWT hawakaguliwi na CAG bali hukaguliwa na mamlaka ambaye humchagua wao na wala fedha hizo hazikaguliwi na CAG na baada ya ukaguzi wa mtaalamu huyo ripoti zote za fedha zilizokaguliwa hupelekwa kwa Msajili wa Vyama.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati, alitaka maelezo ya Serikali kuhusiana na kuwapo kwa malalamiko toka kwa walimu kutokana na kukatwa asilimia mbili na Hazina wanapoajiriwa.

Akijibu swali hilo, alikiri kuwapo kwa suala hilo na kudai lipo katika Sheria ya CWT ya mwaka 2004 na fedha hizo hukatwa kutokana na chama hicho kufikisha wanachama zaidi ya asilimia 50.

Vyombo vya habari vyashutumiwa kesi ya Lulu


ARAZA la Habari Tanzania (MCT), limevishutumu vyombo vya habari kwa kuandika habari zenye mwelekeo wa kumhukumu msanii Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, kwamba amemuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Akisoma tamko la Kamati ya Maadili ya MCT Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema wamesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza kwa baadhi ya vyombo vya habari katika kuripoti kuhusu kifo cha msanii, marehemu Kanumba.

Alisema hatua hiyo ni ukiukwaji mkubwa uliovuka mipaka wa maadili ya uandishi wa habari.

Alisema vyombo hivyo vimemhukumu msichana Lulu kuwa amemuua msanii huyo bila kuzingatia kwamba kufanya hivyo ni kosa.

Alisema ukiukwaji huo umejitokeza baada ya msichana huyo kufikishwa mahakamani ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii yaliandika vichwa vya habari vinavyomhukumu moja kwa moja Lulu kama ni muuaji.

“Kwa mujibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari, mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa hadi atiwe hatiani na mahakama.

“Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika kwa waandishi na wahariri wote kujiepusha na habari au vichwa vya habari vinavyohukumu ambavyo vinaonekana kushawishi au kushinikiza uamuzi wa mahakama,” alisema Jaji Mihayo.

Aidha, alionya kesi ya msanii huyo si rahisi kama wengi wanavyofikiri na vyombo vya habari vifanye kazi yake kwa mujibu wa taaluma na viache kuongozwa na taarifa za pembeni, zikiwamo za katika mitandao.

Naye, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, aliwataka waandishi wa habari kuchunguza undani wa kifo cha marehemu Kanumba kwa sababu kinaingilia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Nawakumbusha waandishi wenzangu, tuzame zaidi kulitazama suala hili, tukio limetokea kwa utatanishi, habari ya kifo cha Kanumba inaingilia masuala ya kijinsia, maana jamii inalishwa sumu kwamba kuna mmoja ambaye ni malaya na mwingine sivyo, hii si sawa,” alisema Kajubi.

Serikali yafanya kufuru

*Yapandisha mishahara ya vigogo ghafla Waziri Kombani adai imefuata taratibu,Wengine waongezewa Sh milioni moja
SERIKALI imefanya marekebisho ya mishahara kwa watumishi wake kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Sambamba na hilo, mishahara ya viongozi wa Serikali kwa mwaka huo wa fedha, nayo imefanyiwa marekebisho.

Marekebisho hayo ni kwa mujibu wa waraka wenye kumbukumbu namba S/AC 205/ 399/ 01/ 44, kutoka Ofisi ya Rais Ikulu (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), uliotolewa Julai 25, mwaka huu.

Waraka huo, umesambazwa kwa wakuu wote wa idara za Serikali, wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wakurugenzi wa halmashauri zote za wilaya nchini.

Waraka huo, uliosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu (Utumishi), Hab Mkwizu, umehusisha pia marekebisho ya ngazi za mishahara kwa viongozi hao wa Serikali.

Kwa mujibu wa waraka huo, ngazi za mishahara zilizokuwa zinaanzia TGS I hadi TGS Q, zimebadilishwa na sasa zitasomeka LSS (E) 1 hadi LSS (E) 9.

Watumishi na viongozi wa Serikali walionufaika na marekebisho hayo, ni pamoja na makatibu wakuu wa wizara, manaibu wao pamoja na wakurugenzi wa idara zote za Serikali. Marekebisho hayo yameanza kutekelezwa Julai, 2012.

Hata hivyo, marekebisho hayo yamelalamikiwa na baadhi ya watumishi wa Serikali, wakidai kuwa hayana uwiyano unaoeleweka kati ya mishahara ya wamtumishi wa Serikali.

Marekebisho hayo yanaoneshwa katika kiambatanisho namba 1 cha waraka huo, ambapo watumishi na viongozi hao wameongezewa mshahara usiopungua 400,000.

Mfano mshahara wa mtumishi wa ngazi TGS P, umepanda kutoka Sh 3, 216, 000 hadi Sh 4, 500, 000 katika ngazi mpya ya LSS (E) 9, ongezeko ambalo ni zaidi ya Sh milioni moja.

Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikosoa marekebisho hayo na kusema kuwa, hayana uwiyano mzuri kati ya mshahara wa mtumishi na mtumishi mwingine.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, amekiri kuwapo kwa marekebisho hayo ya mishahara kwa watumishi na viongozi wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Kombani alisema, marekebisho hayo ni ya kawaida na kwamba yanawagusa watumishi wote wa Serikali bila kubagua.

“Serikali ikifanya marekebisho ya mishahara, inafanya hivyo kwa watumishi wake wote. Hatuchagui nani aongezewe nani asiongezewe ni wote,” alisema.

Alisema vigezo vilivyotumika katika marekebisho hayo, ni pamoja na aina ya kazi, uzoefu na muda aliotumia mtumishi kukaa kazini.

“Unauliza kwanini watumishi wengine wamepewa nyongeza kubwa na wengine kidogo, ndugu yangu sifa zinatofautiana, mtumishi anayeanza kazi leo, hawezi kulipwa mshahara na mtumishi aliyepo kazini kwa miaka 20,” alisema.

Alipoulizwa ni sababu zipi zilizoifanya Serikali kurekebisha ngazi ya mshahara kutoka TGS na sasa kutumia ngazi mpya ya LSS, Waziri Kombani alisema. “Hayo ni masuala ya kitaalamu zaidi.”

Kombani alikiri kima cha chini cha mshahara ni kidogo na kueleza kuwa, Serikali ipo katika majadiliano.

“Kima cha chini kilipanda kutoka Sh 130, 000 hadi Sh 170, 000. Tunajua kima hiki hakitoshi lakini tupo katika majadiliano,” alisema.

Chadema waonyesha picha za video alivyouawa Mwangosi



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonyesha picha za mnato na video zinazoonyesha jinsi Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Television cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alivyouawa.

Picha hizo zilionyeshwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichohudhuriwa pia na waandishi wa habari. Kikao hicho cha Kamati Kuu kilikuwa ni cha dharura na kilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.


Wakati picha hizo zikionyeshwa wazi wazi, viongozi wa CHADEMA na waandishi wa habari, walishindwa kujizuia kwani baadhi yao walijikuta wakiangua vilio wakionyesha kusikitishwa na jinsi Mwangosi alivyouawa.

Katika tukio hilo, Mbowe ni kati ya waliolia na ilifika wakati akanyanyuka kutoka meza kuu na kwenda nje ya ukumbi, ili asiendelee kushuhudia Mwangosi alivyouawa.

Wakati picha hizo zikionyeshwa kwa zaidi ya masaa mawili, askari polisi walioshiriki kumuua Mwangosi walionekana wazi wazi na pia Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alionekana pia eneo la tukio akishuhudia Mwangosi akiuawa.

Kwa mujibu wa picha hizo, mwandishi wa habari aliyeanza kukamatwa na askari polisi na kupata kipigo ni Godfrey Mushi wa Gazeti la Nipashe.

Picha hizo za video zilionyesha kuwa, baada ya Mushi kukamatwa, Mwangosi alikwenda kumuokoa mwenzake huyo na alipofika eneo la tukio, askari hao walianza kumpiga na hatimaye kumuua mbele ya Kamanda Kamuhanda.

Picha hizo zinaonyesha kuwa, kabla Mwangosi hajauawa, polisi mmoja alipitisha bunduki yake miguuni kwa polisi mwenzake kisha Mwangosi akauawa.

Baada ya tukio hilo, picha hizo zinaonyesha kuwa, baadhi ya askari polisi waliokuwa wakimpa kipigo Marehemu Mwangosi, walikimbia na kuacha mwili wa marehemu ukiwa vipande vipande.

Kwa mujibu wa picha hizo, polisi hao walipokuwa pembeni, wenyewe kwa wenyewe walianza kulaumiana huku baadhi yao wakimlaumu muuaji na kusema umefanya nini hicho?.

Baada ya hapo, mmoja wa polisi hao alisikika akisema twende tukamchukue mwenzetu na walipofika mahali alipokuwa mwenzao ambaye alikuwa amejeruhiwa kwa bomu lililomuua Mwangosi, gari ya Kamanda Kamuhanda ilisogea karibu na kumpakia askari polisi aliyejeruhiwa.

Picha hizo za video ambazo zinaonekana zilirekodiwa kwa umakini wa hali ya juu, zinaonyesha baada ya mauaji hayo, askari walishikwa na butwaa huku baadhi yao wakionekana kushika pua.

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya askari ambao ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walionekana katika mkanda huo wa video, wakifungua kofia zao zilizokuwa zimefunika uso na macho yao, ili waone vizuri maiti ya Mwangosi iliyokuwa vipande vipande.

Wakati wakivua kofia hizo, baadhi yao walikuwa wakinawa nyuso zao kutokana na moshi uliokuwa umesambaa eneo la tukio wakati walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA.

Pia picha hizo, zilionyesha askari polisi mmoja akiwa amevaa kiraia, huku shingoni akiwa na skafu ya CHADEMA lakini baada ya vurugu kuanza, askari huyo alionekana akiivua skafu hiyo na kuiweka mfukoni.

Alipoivua na kuiweka katika mfuko wa nyuma wa kaptula aliyokuwa amevaa, mwenzake mmoja akampa kofia ya kujikinga na moshi kisha askari huyo akachomoa bastola kwa ajili ya mapambano.

Pamoja na picha hizo kuwaonyesha askari polisi walivyotekeleza tukio hilo, Kamanda wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wa CHADEMA, Benson Kigaila, alionekana pia akijibizana na ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Iringa kuhusu wafuasi wa CHADEMA kuwepo katika Kijiji cha Nyololo kilichopo Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Vile vile, picha hizo za video, awali zilionyesha marehemu Mwangosi alivyokuwa akimuuliza Kamanda Kamuhanda kuhusu sheria ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na maswali hayo yalionyesha jinsi kamanda huyo wa polisi alivyokuwa amechukizwa nayo.

Kutokana na picha hizo, Mbowe alisema huo ni ushahidi wa kutosha kuonyesha jinsi Jeshi la Polisi lilivyokuwa limedhamiria kuua.

Kwa mujibu wa Mbowe, CHADEMA itatoa tamko zito leo kuonyesha ni hatua gani zitachukuliwa baada ya kifo cha Mwangosi.

Serikali yamwaga ajira kwa walimu

SERIKALI imetangaza kumwaga ajira mpya za walimu 28,746 katika shule za msingi na sekondari, kuanzia mwezi huu. Hatua hiyo, itapunguza nusu ya ukosefu wa walimu katika shule za Serikali.

Mpaka sasa, Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo Serikali inasema italimaliza katika miaka michache ijayo, kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbalimbali kuhitimu masomo.

Rais Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo mjini Igunga juzi, ambapo alisema kati ya walimu watakaoajiriwa na kusambazwa, 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu, Rais Kikwete alisema mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu, ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.

Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee inahitaji walimu 285.

Hii itakuwa mara ya pili, Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo hilo.

Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379, walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246, walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu.

Wakati shule za Serikali, zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459, hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.

Rais Kikwete aliwaambia wananchi kuwa Serikali, inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi.

Pia alizungumzia suala la huduma ya maji, akisema Serikali imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete alisema kufuatia kuzinduliwa kwa mradi wa Maji wa Bulenya, mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70.
CWT YAJIBU
Akizungumzia ajira mpya za walimu, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania, Ezekiel Oluochi, alisema Serikali imefanya jambo la maana, lakini imechelewa kuchukua hatua haraka.

“Naipongeza Serikali, lakini kimsingi natofautina na Serikali katika hili, imechelewa sana kutoa ajira kwani takwimu zinaonyesha kuna upungufu wa walimu 150,000 kwa shule za msingi na 50,000 shule za sekondari.

“Mpaka sasa walimu waliopo ni 234,054, tunahitaji walimu 200,000, kwa maana hiyo walimu waliopo hivi sasa ni asilimia 90,” alisema Oluochi.

Aliitaja mikoa ambayo, inakabiliwa na uhaba wa walimu, kuwa ni Shinyanga, Singida na Arusha katika wilaya za Ngorongoro, Longido na Monduli.

Aliitaja mikoa mingine na wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Dodoma (Kondoa), Kagera (Muleba), Mwanza (Ukerewe, Misungwi), Tabora (Uyui, Sikonge na Urambo), Lindi (Kilwa, Nachingwe, Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini na Lindi Vijijini).

Alisema mikoa ya Mtwara na Lindi, ina hali mbaya zaidi kuliko mingine Tanzania.

“Sababu kubwa ya mikoa hii kuwa na hali mbaya, inatokana na mazingira magumu wanayokutanayo walimu wapya wanaopangiwa huko.

“Asilimia 12 ya walimu wapya wanaoajiriwa, wanaacha kazi hasa wa shule za msingi na walimu wenye shahada ambao wengi wao wanapelekwa vijijini na kujikuta hawatimizi ndoto zao,” alisema Oluochi.

Alisema kama kweli Serikali imedhamiria kumaliza tatizo hilo, basi kuanzia sasa ihakikishe walimu wapya wote wanalipwa stahiki zao, ikiwa ni pamoja na nauli, posho ya siku saba na fedha za kusafirishia mizigo ya tani moja na nusu, kama sheria inavyotaka.

Monday, 25 February 2013

MAUAJI YA PADRI Z'BAR Pengo atoa tamko zito

SIKU moja baada ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki la Minara miwili Zanzibar, kuuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika, Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo Kuu
la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
ametoa tamko zito kwa Serikali.


Padri Mushi aliuawa juzi asubuhi wakati akishuka katika gari lake
ili kwenda kuongoza ibaada katika Kanisa la Betras ambapo tayari Jeshi la Polisi nchini, limeanza uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo, wanakamatwa kwa gharama yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Kardinali Pengo alivitupia lawama vyombo vya ulinzi na usalama
kwa kushindwa kuzuia mifarakano kati ya dini moja na nyingene.

Alisema vyombo hivyo vimeshindwa kusoma alma za nyakati kwani baada ya tukio la kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa kanisa hilo Parokia ya Mpendaye, Desemba 24,2012, wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar walisambaza vipeperushi vilivyokuwa na ujumbe uliokusudia kufanya jambo kubwa la uhalifu.

“Vipeperushi hivi vilikuwa na ujumbe unaosema, mapambano yataendelea hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vilipaswa
kufanya uchunguzi wa kina ili kuzuia ualifu uliopangwa
kufanywa na wafuasi hao.

Aliongeza kuwa, tukio la kuuawa Padri Mushi halikutokea kwa dharura bali vyombo hivyo vilikuwa vinafahamu mkakati wa
jumuiya hiyo lakini bado vilishindwa kuchukua hatua.

“Padri Mushi hakuuawa akiwa baa wala sehemu nyingine tofauti na eneo lake la kazi bali mauaji yamemkuta akiwa kanisani ambako alikwenda kutekeleza jukumu lake la kikzai,” alisema.

Alisema mauaji hayo ni pigo kubwa kwa Taifa ambapo usaalama
wa imani moja ukikosekana kutokana na imani ya dini nyingine
ni tatizo na haijulikani nini kitatokea siku za mbeleni.

Alivitaka vyombo hivyo kuwa makini, kusoma alama za nyakati
ili kuzuia machafuko yanayoendelea yasitokee tena na kuwakata
waumini wa kanisa hilo, kutolipiza kisasi badala yake watulie, kuomba amani na kumuombea Padri Mushi.

Aliwataka Mapadri wengine wa kanisa hilo kuchukua tahadhari
ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu dhidi yao na kusisitiza kuwa, umefika wakati wa viongozi wa nchi kulinusuru Taifa lisigawanyike kwa misingi ya imani za dini.

Kardinali Pengo, alisema Februari 24 mwaka huu, kanisa hilo litafanya ibada kubwa Zanzibar na Dar es Salaam kwa ajili ya kumuombea Padri Mushi.

Aliongeza kuwa, vipeperushi vilivyomfikia ambavyo alidai vimesambazwa na wafuasi wa jumuiya hiyo vina ujumbe
unaosema; “Kwa nguvu hizo, tumeweza kuyachoma makanisa
yao na kumtuliza kibaraka wa Kiislamu Soroga, alhamdulillah
hata nje hatoki (laanatullah).

“Lakini nguvu za ushindi mkubwa tulioupata ni huu wa kuwatuliza Makatoriki katika mkesha wao wanaoujua wenyewe (laanatullah), kumkosa Ambrose wa Kanisa la Mpendae, haijawa mwisho wa mapambano, tutahakikisha kila kiongozi wa Makanisa hapa
Zanzibar, hapati nafasi tena ya kuendeleza ujumbe wao”

“Wapenzi Waislamu, viongozi wetu (waliopo mahabusu), wanaendelea vizuri, ipo siku watatoka ishallah kwa nguvu za
allah, jambo kubwa la faraja viongozi wetu waliomo ndani ya Serikali na nje ya nchi, wametuhakikishia huu ndio mwisho wa kusherehekea sherehe za Mapinduzi (laanatullah)”

“Vijana wetu waliokuwa masomoni Somari, wametuhakikishia
kabla ya kusherehekea siku ya kuzaliwa Mtume Mohamed (s.a.w), kutatokeza sherehe nyingine yoyote,” ulisema ujumbe huo.

Katika ujumbe huo, Soroga ambaye ametajwa na wafuasi hao ni Katibu wa Mufti wa Zanzibar na jina lake kamili ni Shekhe Fadhil Soroga ambaye alimwagiwa tindikali na kukimbizwa Dar es Salaam ili kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kardinali Pengo alisema, kutokana na vyombo hivyo kukosa umakini, ndiyo maana vipeperushi vyenye ujumbe mzito kama
huo, vilisambazwa hadi kumfikia yeye ambaye ni kiongozi wa
ngazi ya juu katika kanisa hilo jambo ambalo kama hatua za
haraka hazitachukuliwa, kutatokea madhara makubwa.

Dkt. Shein ashtushwa

Kutokana na mauaji hayo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea msiba
huo kwa mshtuko mkubwa, kutoa pole kwa waumini, ndugu,
jamaa, marafiki na wananchi wote wa Zanzibar.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Dkt. Shein, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Bw. Mohamed Aboud Mohamed, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga upya kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na vyengine kutoka nchi za nje ili kuongeza nguvu ya kuwasaka wauaji.

“Zipo kasoro katika Jeshi la Polisi lakini limekuwa likifanya kazi nzuri, nawaomba wananchi mtoe ushirikiano ambao utafanikisha kukamatwa wahalifu wanaofanya matukio mbalimbali.

Alisema kutokana na jiografia ya Zanzibar, kuna maeneo
ambayo watu wanaweza kupitisha silaha lakini Jeshi la Polisi
kwa kushirikiana na Vikosi vya SMZ, litaziba mianya yote.

Bw. Mohamed, alikanusha taarifa zilizopo mitaani kuwa silaha nyingi zipo mikononi mwa wasiostahili kuwa nazo na kuwataka kuondoa hofu waliyonayo kwani hizo ni njama za watu wachache wanaotaka kuiingiza nchi katika machafuko ya kidini.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Dkt. Shein hawapendi kusikia vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani vikitokea nchini, kutokana na sababu hizo wameomba
msaada kwa nchi nyengine kuja kufanya uchunguzi wa
kuwabaini wahusika wanaofanya vitendo hivi,” alisema.

Maalim Seif alaani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amelaani mauaji ya Padri Mushi na kusema kitendo hicho kimevuruga sifa njema ya Zanzibar kuwa kisiwa cha amani.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyasema hayo Kisiwani Pemba wakati akifungua semina
ya madiwani wa chama hicho.

Alisema mauaji hayo hayakubaliki kwani Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa kuvumiliana hivyo ni wajibu wao kuendeleza sifa hiyo kwa kuendeleza upendo dhidi yao na kuwapa matumaini wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa shughuli mbalimbali.

Marekani walaani mauaji

Katika hatua nyingine, Serikali ya Marekani imelaani vikali tukio
la mauaji ya Padri Mushi na kutoa salamu za pole kwa ndugu,
jamaa na marafiki wa familia ya marehemu.

Balozi wa Marekani nchini, Bw. Alfonso Lenhardt, aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari na kusisitiza kuwa, nchi yake ipo tayari kushirikiana na Watanzania ili kukomesha matukio ya aina hiyo.

Alisema vurugu za kidini hazipaswi kupewa nafasi Tanzania nchi ambayo inasifika kwa amani na utulivu, umoja na mshikamano
wa Watanzania wote.

“Watanzania mnapaswa kupuuzia vurugu hizi ambazo zinachochewa na watu wachache wenye dhamira ya kusambaratisha amani, utulivu, usalama na taswira ya muonekano bora wa ardhi yenu,” alisema.

Jumuiya ya Maimamu

Nayo Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) imedai kupokea taarifa za mauaji hayo kwa masikitiko makubwa na kulaani kitendo hicho ambacho wamekihusisha na uharamia ili kuitia doa Zanzibar.

Taarifa waliyoitoa kwa vyombo vya habari jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Shekhe Juma Muhiddin, imesema Zanzibar ni
kisiwa cha amani na ukarimu tokea enzi na enzi.

Alisema kutokana na mauaji hayo, jumuiya hiyo inawataka Wanzanzibari wote pamoja na dini zote, kuwa watulivu katika
kipindi hiki kigumu, kutunza amani iliyopo na mshikamano
chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kanisa lapigwa moto tena Z'bar *Walianza kulipiga mawe, wahusika wasakwa *Utaratibu wa kuyalinda na polisi waandaliwa



Rushwa yatajwa kutawala ndani ya JWTZ nchini




Kwa ufupi

“Hakuna kitu kibaya kama la rushwa kwenye jeshi, maana kuna fedha nyingi inatembea kutokana na ughali wa vifaa vya kijeshi. Bado Serikali nyingi zinafanya mambo haya kuwa siri na kutoa mwanya kwa rushwa kutembea.

TANZANIA imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na tatizo la rushwa ndani ya jeshi.
Taasisi ya Transparency International (TI), ambayo hutafiti masuala ya rushwa duniani imeitaja Tanzania kwamba jeshi lake lina rushwa kubwa na ndogondogo.

Kwa mujibu wa gazeti dada la The Citizen la jana Jumapili, uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) umekanusha vikali taarifa ya taasisi hiyo.

TI inadai katika taarifa yake kuwa sekta ya ulinzi ya Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo na hiyo ni kutokana na mambo yake kuendeshwa kwa usiri mkubwa.

“Hakuna kitu kibaya kama la rushwa kwenye jeshi, maana kuna fedha nyingi inatembea kutokana na ughali wa vifaa vya kijeshi. Bado Serikali nyingi zinafanya mambo haya kuwa siri na kutoa mwanya kwa rushwa kutembea.
“Fedha inayotumika vibaya kwa masuala ya kijeshi, ingeweza kutumia vizuri zaidi katika masuala ya maendeleo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyoandikwa na Mark Pyman, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya Ulinzi cha Transperancy International.

Transparency International inaeleza kuwa fedha ya rushwa inayotembea kwenye sekta ya ulinzi inakadiriwa kufikia kiasi cha Dola 20 bilioni (Sh32 trilioni).

“Ripoti ya Transparency International itufungue macho Watanzania maana kwa kawaida huwa kila watu wakihoji mapato na matumizi ya jeshi tunaambiwa hatuwezi kujibiwa kwa madai ya woga wa kuhatarisha usalama wa taifa,” alikaririwa mbunge mmoja na gazeti la The Citizen.

Tanzania, hata hivyo, iko juu ya nchi nyingi za Afrika kwa tatizo la rushwa ingawa inatakiwa kurekebisha mianya mingi kwenye sekta hiyo.

“Tunaona Tanzania ina changamoto ya kuimarisha vyombo vya kutupa jicho kwenye jeshi. Mathalani, kuna Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Mambo ya Nje, lakini haina meno ya kuingia kwa undani masuala ya kijeshi,” iliongeza Transparency International.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, hata hivyo, alikaririwa na gazeti la The Citizen akidai kuwa taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kitaalamu na kimaadili akitolea mfano jinsi wanavyoajiri wanajeshi kwa kufuata vigezo.

Transparency International inasema kuwa kuna Kitengo cha Utawala Bora cha Serikali ambacho hufanya ukaguzi kwenye jeshi ingawa halijatoa ripoti ya aina yoyote kuhusiana na ukaguzi wa bajeti ya jeshi. “Mfano kuna taarifa kuwa Kitengo cha Kilimo cha Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT) kuna kinajishughulisha na uchimbaji madini na biashara nyingine lakini kuna udhibiti mdogo,” iliongeza taarifa yao.

Julai mwaka jana, maofisa saba waandamizi wa Bodi ya Zabuni ya Suma-JKT walifunguliwa mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi na uhamishaji usio wa halali wa zaidi ya Sh 3.8 bilioni.
Waliotuhumiwa ni pamoja na Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni Kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajini John Laizer, Meja Yohana Nyuchi na Luteni Kanali Felix Samillan wanaodaiwa kufanya makosa hayo mwaka 2009.

Tanzania imewekwa katika Kundi D kwenye orodha hiyo ya Transperancy International ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na vigezo vinavyoangaliwa ni sekta za siasa, fedha, utumishi wa Kundi la D ni nchi ambazo zinakabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na katika orodha hiyo zimo pia nchi za Russia na China.

Hata hivyo, nchi zenye kiwango cha juu cha rushwa ziko katika Kundi F wakati zile zenye kiwango cha chini cha rushwa ziko Kundi A.

“Inasikitisha kuona kuwa Tanzania bado hakuna uwazi katika matumizi ya fedha za jeshi. Hata Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya nje haina meno,” alikaririwa Semkae Kilonzo wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Policy Forum.

Haya yanatokea wakati hivi karibuni Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje iligawanywa. Sasa kutakuwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na nyingine itakuwa inashughulikia Mambo ya Nje.

Naibu Waziri aiomba Serikali kupunguza kodi


Kwa ufupi

“Serikali ifanye jitihada ya kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itapelekwa kwenye maendeleo ya jamii,”

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Janet Mbene ameiomba Serikali kuwatengenezea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itasaidia kuleta maendeleo ya taifa.

Waziri Mbene aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara ya kukagua nyumba 491 zilizopo eneo la Buyuni Kata ya Majohe Wilaya ya Ilala ambazo zimejengwa na Mradi wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF). Alisema lengo la kujengwa kwa nyumba hizo ni kuwanufaisha wanachama na wananchi na kwamba Serikali itakapoweka mazingira mazuri ya kazi kwa wananchi wake wataweza kulipa kodi ambayo itasaidia kuleta maendeleo katika jamii.

Aliongeza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuchangia kodi ambayo itafanya kazi ya kuibua miradi mbalimbali ya kuleta maendeleo ya jamii ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara
“Serikali ifanye jitihada ya kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itapelekwa kwenye maendeleo ya jamii,” alisema Mbene.

Pia, aliwataka wanachama wa PSPF kuchangamkia nyumba hizo waweze kununua au kukopa ili kujikwamua na adha ya kupanga ikiwamo kupata nyumba bora na za kisasa.

“Nyumba ni nzuri na zitawasaidia wananchi wa kawaida katika suala la ulipaji wa kodi, wamehakikisha haumizwi katika ulipaji, ndiyo maana wameamua mtu awe analipa kuanzia miaka 15 hadi miaka 20,” alisema na kuongeza:

“Nawaomba PSPF kuhakikisha mahitaji muhimu yote yanayohitajika yanapatikana kama maji, umeme, usafiri na barabara iwekwe kiwango cha lami itamrahisishia mwananchi atakayehamia kuwa na uhakika wa usalama wake,” alisema Mbene. Kaimu Mkurugenzi wa PSPF, Adamu Mayunga alisema wamejipanga kuhakikisha miundombinu ya maji, umeme na barabara ambavyo ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa eneo hilo vinapatikana.

“Tumeshapata mkandarasi wa Manispaa ya Ilala ambaye amekubali kupeleka greda kwa ajili ya kuchonga barabara na kwa upande wa maji, Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) ilitujibu itachukua muda mrefu kufikisha mabomba kwenye eneo hili hivyo tumejipanga kuchimba visima vya maji,” alisema Mayunga.

Alisema nyumba hizo zimejengwa kwa awamu ya kwanza ambazo zipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro Shinyanga, Tabora na Mtwara hivyo wanachama hao wanatakiwa kununua popote wanakotaka.

Kwa mujibu wa Mayunga, nyumba hizo zitaanza kuuzwa kwa Sh64 milioni hadi Sh94 milioni kulingana na mahali nyumba ilipojengwa hiyo gharama ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la VAT.