Monday, 25 February 2013
Naibu Waziri aiomba Serikali kupunguza kodi
Kwa ufupi
“Serikali ifanye jitihada ya kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itapelekwa kwenye maendeleo ya jamii,”
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Janet Mbene ameiomba Serikali kuwatengenezea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itasaidia kuleta maendeleo ya taifa.
Waziri Mbene aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara ya kukagua nyumba 491 zilizopo eneo la Buyuni Kata ya Majohe Wilaya ya Ilala ambazo zimejengwa na Mradi wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF). Alisema lengo la kujengwa kwa nyumba hizo ni kuwanufaisha wanachama na wananchi na kwamba Serikali itakapoweka mazingira mazuri ya kazi kwa wananchi wake wataweza kulipa kodi ambayo itasaidia kuleta maendeleo katika jamii.
Aliongeza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuchangia kodi ambayo itafanya kazi ya kuibua miradi mbalimbali ya kuleta maendeleo ya jamii ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara
“Serikali ifanye jitihada ya kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wananchi ili waweze kulipa kodi kwa wakati ambayo itapelekwa kwenye maendeleo ya jamii,” alisema Mbene.
Pia, aliwataka wanachama wa PSPF kuchangamkia nyumba hizo waweze kununua au kukopa ili kujikwamua na adha ya kupanga ikiwamo kupata nyumba bora na za kisasa.
“Nyumba ni nzuri na zitawasaidia wananchi wa kawaida katika suala la ulipaji wa kodi, wamehakikisha haumizwi katika ulipaji, ndiyo maana wameamua mtu awe analipa kuanzia miaka 15 hadi miaka 20,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba PSPF kuhakikisha mahitaji muhimu yote yanayohitajika yanapatikana kama maji, umeme, usafiri na barabara iwekwe kiwango cha lami itamrahisishia mwananchi atakayehamia kuwa na uhakika wa usalama wake,” alisema Mbene. Kaimu Mkurugenzi wa PSPF, Adamu Mayunga alisema wamejipanga kuhakikisha miundombinu ya maji, umeme na barabara ambavyo ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa eneo hilo vinapatikana.
“Tumeshapata mkandarasi wa Manispaa ya Ilala ambaye amekubali kupeleka greda kwa ajili ya kuchonga barabara na kwa upande wa maji, Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) ilitujibu itachukua muda mrefu kufikisha mabomba kwenye eneo hili hivyo tumejipanga kuchimba visima vya maji,” alisema Mayunga.
Alisema nyumba hizo zimejengwa kwa awamu ya kwanza ambazo zipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro Shinyanga, Tabora na Mtwara hivyo wanachama hao wanatakiwa kununua popote wanakotaka.
Kwa mujibu wa Mayunga, nyumba hizo zitaanza kuuzwa kwa Sh64 milioni hadi Sh94 milioni kulingana na mahali nyumba ilipojengwa hiyo gharama ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la VAT.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment