Sunday, 23 August 2015

Treni ya Mwakyembe kurejea tena

Miezi kadhaa baada treni ya kubeba abiria jijini Dar es Salaam kusitisha safari zake kutokana na ubovu, imeelezwa kuwa hali hiyo ni kutokana na uchakavu wa injini.
Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Reli Tanzania, Charles Ndenge alisema treni hiyo imekuwa ikiharibika mara kwa mara, kutokana na injini zake kutumika kwa muda mrefu, huku treni hiyo ikifanya kazi tofauti na ilivyoundwa.
Elizabeth Edward
Dar es Salaam. Miezi kadhaa baada treni ya kubeba abiria jijini Dar es Salaam kusitisha safari zake kutokana na ubovu, imeelezwa kuwa hali hiyo ni kutokana na uchakavu wa injini.
Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Reli Tanzania, Charles Ndenge alisema treni hiyo imekuwa ikiharibika mara kwa mara, kutokana na injini zake kutumika kwa muda mrefu, huku treni hiyo ikifanya kazi tofauti na ilivyoundwa.
“Treni hii ilitengenezwa kwa safari za mbali, hata hivyo imeshafanya kazi kwa muda mrefu na injini zake zimechoka ndiyo maana zinafanyiwa marekebisho niwahakikishie watumiaji huduma ya usafiri itarejea kama kawaida” alisema Ndenge.
Alifafanua mpaka sasa matengenezo yamefika katika hatua nzuri na wiki mbili zijazo huduma hiyo itaanza kufanya kazi tena.
Ili kuepukana na adha ya kusitishwa kwa huduma hiyo mara kwa mara, Ndenga alisema kwamba kunahitajika treni iliyotengenezwa maalumu kwa ajili ya safari za mjini.
“Usafiri wa treni kwa safari fupi unaweza kuwa imara endapo kutakuwa na treni zilizotengenezwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo mikakati ambayo inaendelea, lakini hatuwezi kuizungumzia kwa sasa”alisema.
Aliweka wazi kwamba matengenezo ya injini hizo yanaendelea na wiki mbili zijazo huduma hiyo ya usafiri inaweza kurejea.
Kusitishwa kwa huduma hiyo ya usafiri kumeleta kero kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakitegemea njia kukabiliana na changamoto ya foleni hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi wa watumiaji wa usafiri huo walidai kuwa kukosekana kwa treni kumesababisha kuathirika kwa shughuli zao za kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kwenye foleni.
“Treni ilikuwa inasaidia sana, lakini sasa hivi tunalazimika kupoteza muda mwingi kwenye foleni za daladala, hivyo tunaomba wahusika waliangalie suala hili kwa umakini zaidi usafiri wetu walala hoi urejee”alisema Erick Kivambala mkazi wa Ubungo Jasmine Ally mkazi wa Tabata alisema kukosekana kwa usafiri huo, kumeleta changamoto kubwa kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakipata wakati mgumu kwenye daladaa kutokana na kusumbuliwa makondakta.
“Ingawa hata watu wazima tumeathirika lakini wanafunzi ndiyo wameathirika zaidi, maana treni ndiyo ilikuwa inawabeba bila matatizo yoyote, siku hizi unawakuta kwenye vituo vya daladala wakikunjana mashati na makondakta”alisema.
Kwa upande wake Ofisa Habari Mkuu Wizara ya Uchukuzi, William Budoya Ndenge alikiri kuwepo kwa kadhia hiyo na kueleza kuwa treni maalum kwa ajili ya safari za mjini zinahitajika kukabiliana na changamoto za usafiri katika maeneo hayo.
“Ili usafiri huu uwe wa uhakika ni lazima ziwepo treni ambazo zimetengenezwa maalum kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri maeneo ya mijini,”alisema.
Kuhusiana na madai ya kuwepo kwa mvutano kati ya TRL na Wizara ya Uchukuzi katika suala la uendeshaji wa treni hiyo, Budoya alisema jambo hilo halina ukweli na wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega kuhakikisha huduma hiyo inarejea.
“Sisi tunatunga sera na TRL ni waendeshaji tunatambua fika kwamba treni hili ni mkombozi kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam, ndiyo maana tunaweka nguvu zote kuhakikisha linarejea”alisema Budoya

Unachopaswa kufanya siku ya uchaguzi



Dar es Salaam. Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu. Baadhi ya wananchi hasa vijana waliofikisha miaka 18 hivi karibuni hawajawahi kushiriki kwenye uchaguzi wowote na uchaguzi huu ni wa kwanza kwao.

Saa 1: Wananchi wanatakiwa kufika vituoni kuanzia saa moja asubuhi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura.
04:Jambo la nne, mwananchi akimaliza kupiga kura aende nyumbani kusubiri matokeo kutangazwa.
53:Kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi, wagombea urais na wagombea wenza wanayo haki ya kutumia vituo vya redio na televisheni vya Serikali wakati wa muda rasmi wa kampeni.
Peter Elias, Mwananchi
Dar es Salaam. Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu. Baadhi ya wananchi hasa vijana waliofikisha miaka 18 hivi karibuni hawajawahi kushiriki kwenye uchaguzi wowote na uchaguzi huu ni wa kwanza kwao.
Vijana hawa na watu wengine, wanahitaji kujifunza au kukumbushwa juu ya mambo ya kufanya siku ya uchaguzi ili kufanya zoezi la upigaji kura kuwa lenye mafanikio na kuepusha uvunjifu wa sheria unaoweza kumweka mtu matatani.
Kwa bahati mbaya, elimu kwa mpigakura haitolewi mara kwa mara kwa wananchi mpaka nyakati za uchaguzi. Hata wakati huo ukifika, baadhi ya watu hasa wale wa hali ya chini, hawafikiwi na elimu hiyo.
Elimu kwa mpiga kura bado inahitajika ili kila mwananchi afahamu haki na wajibu wake katika mchakato mzima wa uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ndiyo yenye jukumu la kutoa elimu hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine.
Hata hivyo, zoezi hili linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali za kufanikisha utoaji wa elimu kwa wapigakura. Vilevile, hakuna chombo maalumu cha kuratibu na kusimamia utoaji wa elimu ya uraia.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni pamoja na uhaba wa Asasi za kiraia zinazotoa elimu kwa wapigakura na kuwafikia wananchi wote nchi nzima.
Jaji Lubuva anasema Tume imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba elimu inawafikia wapigakura nchi nzima. Anasema watatumia vyombo vya habari vikiwamo vinavyomilikiwa na taasisi za dini ili kuwafikia wananchi haraka zaidi.
Zingatia haya siku ya uchaguzi
Mkurugenzi wa uchaguzi – Nec, Kailima Kombwey anafafanua mambo muhimu ambayo mpigakura anatakiwa kufanya siku ya uchaguzi bila kuathiri masharti ya sheria za uchaguzi na kanuni zake.
Wahi kituoni
Anasema jambo la kwanzana la msingi ni  kuwahi asubuhi katika kituo cha kupigia kura. Kombey anasema wananchi wanatakiwa kufika vituoni kuanzia saa moja asubuhi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura.
Anasema kila mpigakura anatakiwa kujua kituo atakachopigia kura na kuhakiki kama jina lake lipo kwenye orodha ya wapigakura kwenye kituo husika.
Panga foleni
Kombey anabainisha kuwa watu watapanga foleni kuingia chumba cha kupigia kura na vituo vitafungwa kuanzia saa 10 jioni. Anasema watakaokuwa kwenye mstari baada ya muda huo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura mpaka watakapomaliza.
“Tunasisitiza wananchi wajitokeze kwa wingi ili wawachague viongozi wao. Kupiga kura ni jambo la muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Wasipojitokeza basi wasilaumu kiongozi atakayechaguliwa na wengine,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi huyo anasema katika uchaguzi wa mwaka 2010, waliandikisha watu milioni 20 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa chini ya milioni 10. Kwa hiyo, anasisitiza zaidi kujitokeza kupiga kura siku hiyo.
Usivae sare za chama
Jambo la pili, mpigakura asivae nguo yenye nembo au alama yoyote ya chama cha siasa kwenye kituo cha kupigia kura. Kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za uchaguzi na mtuhumiwa anaweza kushitakiwa kwa kuhujumu mchakato wa upigaji kura.
Kombey anafananisha jambo hilo na akufanya kampeni siku ya kupiga kura, jambo ni kinyume na kanuni. Kwa hiyo, fulana, kofia, bendera au kanga au nguo yoyote inayovaliwa na chama chochote haitakiwi kwenye eneo la kupigia kura.
“Tunatoa muda wa kampeni ili wanasiasa na vyama vyao wajinadi kadri wanavyotaka lakini siku ya uchaguzi siyo siku ya kufanya kampeni, ni kinyume cha kanuni za uchaguzi,” anasema mkurugenzi huyo.
Anaendelea kubainisha kuwa Tume kupitia kifungu cha 124 (a) cha sheria ya taifa ya uchaguzi ya mwaka 1985 ilianda maadili ya uchaguzi ambayo yamefanyiwa mabadiliko madogo mwaka huu na kukubaliwa na vyama vyote.
Wahusika wakuu katika maadili haya ni Tume ya Uchaguzi, Serikali, wagombea na wanachama wote wa vyama vya siasa. Kombwey anasema wadau hawa kwa pamoja wana wajibu wa kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Usilete ushabiki
Jambo la tatu, wapigakura wasilete ushabiki kwenye vituo vya kupigia kura. Mambo ya ushabiki ni pamoja na kuongelea matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na mamlaka husika zilizokasimiwa jukumu hilo.
Mkurugenzi huyo anafafanua kwamba jambo hilo linajenga hisia tofauti miongoni mwa wapiga kura na linaweza kusababisha vurugu endapo matokeo yatakuwa kinyume chake. Anabainisha kuwa kura ni siri ya mpigakura mwenyewe.
“Sitarajii kuona watu wakitengeneza makundi ya kujadili mwenendo wa uchaguzi kwenye vituo. Hiyo ni sawa na kampeni siku ya uchaguzi, hatutaacha ufanyike kwa sababu utaharibu mchakato wa uchaguzi,” anasema.
Ukipiga kura nenda nyumbani
Jambo la nne, mwananchi akimaliza kupiga kura aende nyumbani kusubiri matokeo kutangazwa. Kuendelea kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kunasababisha msongamano usio wa lazima.
Kombwey anasema hakuna haja ya kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kulinda kura kwa sababu tayari mawakala wa vyama vya siasa wapo kwa ajili ya kuangalia mwenendo mzima wa uchaguzi.
“Ile dhana ya kutaka kulinda kura zisiibiwe ndiyo inayosababisha vurugu kwenye vituo. Hizo ni hisia tu, hakuna wa kuiba kura kwa sababu kuna mawakala wanaowakilisha vyama vyao,” anasema.
Tume ina jukumu la kutangaza matokeo
Anasema jukumu la kutangaza matokeo ya urais ni la Tume ya uchaguzi. Tume pia imekasimisha jukumu la kutangaza matokeo ngazi ya kata kwa msimamizi msaidizi wa kata na ngazi ya jimbo kwa msimamizi wa halmashauri.
Kombwey anasema kuna baadhi ya watu wanatishia kutangaza matokeo endapo Tume itachelewa kufanya hivyo. Anasisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha utaratibu kwa sababu hakuna mtu mwenye jukumu hilo zaidi ya Nec.
Anasema Nec imejipanga kutangaza  matokeo ya urais ndani ya siku tatu kwa sababu watatumia Mfumo wa Kusimamia Matokeo (RMS) ambao utawawezesha kupokea, kujumlisha na kutangaza matokeo.
Licha ya kutakiwa kisheria kutangaza matokeo hayo ndani ya siku saba, Nec imebainisha kwamba mfumo huo utasaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa matokeo kutoka sehemu mbalimbli nchini.
Mabadiliko ya sheria
Jaji Lubuva anasema mabadiliko makubwa ya sheria ya uchaguzi yalifanyika mwaka 2010, mwaka huu sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho isipokuwa kanuni za uchaguzi zimerekebishwa ili kuleta ufanisi katika uchaguzi ujao.

Sumaye ajitoa CCM, ajiunga Ukawa

Historia imeendelea kuandikwa katika siasa za Tanzania baada ya leo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujitoa CCM na kujiunga na chama kimojawapo kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-(Ukawa).
Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam leo katika mkutano na wanahabari Sumaye amesema chama alichojiunga miongoni mwa vinne (Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD) vinavyounda Ukawa kitajulikana baadaye.
Louis Kolumbia, Mwananchi Digital
Dar. Historia imeendelea kuandikwa katika siasa za Tanzania baada ya leo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kujitoa CCM na kujiunga na chama kimojawapo kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-(Ukawa).
Sumaye anakuwa Waziri Mkuu mstaafu wa pili kujiondoa chama tawala katika historia ya Tanzania, ambapo waziri mkuu wa kwanza kuhama CCM ni Edward Lowassa aliyejiunga Chadema miezi michache iliyopita.
Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam leo katika mkutano na wanahabari Sumaye amesema chama alichojiunga miongoni mwa vinne (Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD) vinavyounda Ukawa kitajulikana baadaye.
Waziri Mkuu huyo aliyehudumu Uwaziri Mkuu miaka yote 10 ya utawala wa awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema amejiunga Ukawa kwa kushirikiana na viongozi wa umoja huo awatumikie Watanzania kwa kasi kubwa baada ya uchaguzi kwa kuwa anaamini Ukawa utashinda.
Amesema kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM na kuvurugwa kwa mchakato wa uchaguzi kumechangia wananchi kukata tamaa hali iliyochochea uungwaji mkono wa upinzani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Na sasa kuzuia wimbi la mabadiliko ni kazi kubwa sana. Naamini Ukawa watashinda uchaguzi huu, CCM wamezubaa wakidhani watashinda wakati wananchi wamechoka, wanahitaji mabadiliko” alisema na kuongeza.
“Sijajiunga Ukawa kwa kuwa mgombea wake wa urais anatoka Kanda ya Kaskazini, wala kwa kuwa viongozi wengi waandamizi wanatokea huko la hasha bali kutaka kutoa uzoefu wangu nikishirishiana na Lowassa katika uongozi wa nchi, alisema na kudai dhana kwamba hakuna maisha ya kisiasa nje ya CCM imepitwa na wakati.

Aliyeshindwa kurejesha fomu abomolewa nyumba

Nyumba ya mgombea ubunge jimbo jipya la

Nyumba ya mgombea ubunge jimbo jipya la Nanyamba,Twahil Saidi (CUF) iliyobomolewa na watu wasiojulikana kwa kile kilichodaiwa ni baada ya kushindwa kurudisha fomu hadi muda ulipoisha. Picha na Haika Kimaro  
Haika Kimaro
Mtwara. Kundi la watu wasiofahamika wamevamia na kubomoa nyumba ya mgombea ubunge wa jimbo jipya la Nanyamba kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) lililogawanywa kutoka Jimbo la Mtwara Vijijini, Twahil Saidi kwa kile kilichodaiwa kuwa amekihujumu chama hicho baada ya kushindwa kurejesha fomu.
Hali hiyo imempa fursa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimboni humo kuwa mgombea pekee.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku. Inadaiwa kuwa mgombea huyo alipotafutwa na viongozi wa chama hicho juzi baada ya kushindwa kutokea katika ofisi za halmashauri alikopaswa kufika kurejesha fomu, hakupatikana na simu zake za kiganjani inadaiwa pia kuwa zilikuwa zimezimwa.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wafuasi wa CUF, walidai kuwa hatua hiyo imewapunguzia thamani ya chama chao, lakini wataendelea kumtafuta ili kujua sababu iliyomfanya ashindwe kurejesha fomu.
Mkazi wa Nanyamba, Ally Jumbe alisema tukio la kubomolewa kwa nyumba hiyo huenda likahusishwa na kushindwa kurejesha fomu. “Tunahisi labda waliofanya hivi ni wanachama wenzake na wale wa vyama shirika vya Ukawa. Lakini mpaka tunapozungumza sasa, hakuna mtu aliyefahamika.”
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Nanyamba, Osca N’gitu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mji wa Nanyamba, alisema kati ya wagombea watatu waliochukua fomu za kuomba kugombea nafasi ya ubunge, ni mmoja kupitia CCM ndiye aliyerejesha fomu.
“Tulikuwa na wagombea watatu kutoka CUF, Chadema na CCM na kazi ya urudishaji fomu ilikuwa jana (juzi), ilianza saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni na mpaka inamalizika ni mgombea mmoja tu wa CCM, Abdallah Chikota ndiye aliyefanikiwa kurejesha fomu zake,” alisema na kuongeza:
“Baada ya hapo tuliendelea na utaratibu mwingine kama sheria zinavyoelekeza lakini leo (jana) asubuhi nikapata taarifa kuwa nyumba ya mgombea aliyechukua fomu kupitia CUF imebomolewa na watu wasiojulikana. Nilienda eneo hilo na kufanya kikao na viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, kata na viongozi wa CUF, kimsingi nimewaomba kufanya utafiti wa kina ili kubaini waliohusika na tukio hilo na pili, kubaini ni kipi kilichomsibu mgombea huyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe alipotafutwa alisema yuko nje ya ofisi ila ana taarifa ya kuwapo kwa tukio hilo.

Thursday, 13 August 2015

Mgeja, Guninita wajiengua CCM, wajiunga Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na aliyekuwa mwenyekiti mkoa wa Dar es Salaam John Guninita wametangaza leo kuachana na CCM na kujiunga Chadema.
Makada hao wa CCM wametangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam leo.
Wakizungumza katika mkutano huo, makada hao wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini CCM imepoteza mwelekeo na kwamba kinaendeshwa kibabe tofauti na misingi ya kuasisiwa kwake.
Wametolea mfano wa kukiukwa kwa demokrasia kulikofanywa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa chama hicho ambapo Dr John Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM.
Hatua ya makada hao imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu aliyekuwa mbunge wa chama hicho jimbo la Sikonge, Said Nkumba atangaze kuachana na chama hicho na kujiunga na Chadema.
Huo ni mwendelezo wa matukio ya makada na wabunge chama hicho kuhamia upinzani hasa Chadema kwani awali aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliachana na CCM baada ya jina lake kukatwa na kamati ya maadili ya chama hicho.
Wengine waliohama CCM ni aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, aliyekuwa mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga ambaye pia ni naibu waziri Kazi na Ajira, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliyekuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai na mbunge wa viti maalumu anayemaliza muda wake Esther Bulaya.

Wednesday, 12 August 2015

Said Nkumba ahama CCM, ajiunga Chadema. Nini hatima ya CCM 25 Oct?

Mbunge wa Sikonge, CCM, Said Nkumba ametangaza kukihama hicho na kujiunga na Chadema, kwa madai CCM ‘haina mapenzi na watu’.
Nkumba anakuwa mbunge wa sita kutoka CCM kutimkia upinzani katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja.
Wabunge waliokihama chama hicho ni Edward Lowassa (Monduli), Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi), Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya.
Lowassa ametimkia Chadema na ndiye aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho kwa mwavuli wa Ukawa, kugombea urais katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana kutoka Tabora, Nkumba alisema: “Sikushawishiwa, nimejiondoa CCM kwa uamuzi wangu na nimefanya hivi kwa kuwa sikuwa nasikilizwa kwa kile nilichokisema.
“Niliipenda CCM kwa dhati kabisa, lakini sikuona sababu ya kuendelea kubakia CCM, sisikilizwi, chama hakina mapenzi na watu, ndiyo maana tunaondoka.”
Nkumba aliyekuwa kinara wa kuipinga Ukawa ambao baada ya kutoka bungeni kwenye Bunge la Katiba, alisimama kidete na kuanzisha “Tanzania Kwanza, Mbili yatosha” alisema amejiunga na upinzani ili kujenga chama cha Chadema.
“Mimi najiamini, ninakubalika ndani ya chama, sasa nimekuja huku, nataka kuendelea mazuri ya Chadema, ninaona huku kunanifaa,” alisema Nkumba.
Akizungumzia kuwa wanaokwenda upinzani ni makapi, Nkumba alisema kuwa hata makapi bado yanakuwa na faida.
“Unajua kuwa wakati mwingine makapi ya asali labda ukamua sawasawa, lakini kwa hapa, sisi bado tuna asali, si makapi yasiyokuwa na kitu.”
Kuhusu hatma ya CCM na kuondokewa watu mbalimbali na kujiunga upinzani, Mbunge huyo alisema kuwa wakuu wa chama hicho, lazima washtuke na wasipokuwa makini, huu utakuwa mwisho wa CCM.
“Hivi wewe hushtuki, wanaona kabisa chama kikubwa lakini watu wanaondoka, wanaona kabisa mwelekeo haupo, halafu wanaendelea na yao, ni wazi kuwa wataanguka,” alisema.

Saturday, 1 August 2015

Nape afafanua sakata lake na Takukuru Lindi

Lindi. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amefafanua sakata lake la kuchukuliwa na askari wa Takukuru kwa mahojiano muda mfupi baada ya kuchukua fedha benki, akisema alikuwa akielekea kulipa mawakala.
Nape, anayewania ubunge wa Jimbo la Mtama, jana mchana aliamriwa na maofisa wa Takukuru kufika ofisi zao baada ya kutoka kuchukua fedha benki ya NMB eneo la Misonobarini mkoa Lindi.
“Ninadhani hawa jamaa walipotoshwa. Mimi nimekwenda zangu benki kuchukua fedha, lengo langu ni kuwalipa mawakala,” alisema Nape jana jioni alipopigiwa simu na Mwananchi kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.
“Wakaja hawa jamaa, wakajitambulisha kuwa wanatoka Takukuru, wakaniuliza ‘mbona ninachukua fedha nyingi kipindi hiki?’ Nikawaambia ‘nakwenda kulipa mawakala, na fedha zenyewe ni hizi Sh3.6 milioni’.
“Basi, tukatoka taratibu tukaenda ofisini kwao, ni karibu tu na benki. Wakanihoji hata haikumalizika nusu saa, niliwaambia nataka kulipa mawakala wangu, tena fedha zenyewe hazitoshi, wako zaidi ya 100.”
Nape aliongeza kusema kuwa walimkamata na akawaambia kuwa yeye ni mwadilifu.
“Halafu ninyi, mnaacha marushwa makubwa makubwa huko, watu wanahonga halafu mnamvizia Nape masikini kwa Sh3mil?,” alisema.
Nape alielezea kufadhaishwa na tukio hilo akidai kuwa limetengenezwa kwa ajili ya kumchafua hasa kwa kuwa leo kuna kura za maoni, lakini akasema anaamini yeye ni msafi.
Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Lindi, Stephen Chami alikiri kumhoji Nape, lakini akasema walijiridhisha kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kulipa mawakala.
“Unajua tuna watu wetu, kwenye maeneo mbalimbali hasa kipindi hiki cha uchaguzi, tumeweka watu wetu maeneo mengi, tunataka kukomesha rushwa,” alisema.
Kilango ageuka ‘mbogo’
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela juzi aligeuka mbogo baada ya kuzushiwa katika mitandao ya kijamii kuwa anashikiliwa na polisi.
Taarifa hizo zilizosambazwa jana, zilidai kuwa Kilango alikamatwa juzi saa 5:00 usiku katika eneo la Dimbi, kijiji cha Bagamoyo kwa tuhuma za kutoa rushwa, madai ambayo ameyakanusha.
Hata hivyo, Kilango alipoulizwa jana alisema tuhuma hizo ni uzushi uliotengenezwa na baadhi ya washindani wake wakiamini kwa kufanya hivyo watamvurugia katika kura ya maoni inayofanyika leo.
“Sijakamatwa na wala sijaona hata polisi mmoja nyumbani kwangu. Nimelala nyumbani kwangu jana (juzi) na leo (jana) nimeamka nyumbani kwangu na niko kwenye mikutano ya kuomba kura,” alisema.
Kilango aliongeza,”Sasa hivi nimetoka kuomba kura Mtii nilikuwa peke yangu wagombea wanzangu wameingia mitini. Niko Bombo sasa hivi (saa 9;00 alasiri) ndio wanakuja nishapiga bao.”
Kwa mujibu wa Kilango, baadhi ya wagombea wamekuwa wakifanya kampeni zisizo za kistaarabu kwa kuandaa vijana aliodai wamepewa pombe ili wamzomee katika baadhi ya maeneo aliyopita.

Sifa 10 za mgombea urais bora wa upinzani 2015


Ni jana tu nimemaliza uchambuzi wa watu wanaotajwa au waliojitokeza kugombea urais au wale ambao hawajajitangaza na hawana nia lakini jamii ndani na nje ya vyama vyao inawataja kama watu wenye sifa, uwezo na hata vigezo vya kuiongoza nchi yetu, kutoka vyama vya upinzani.
Lengo la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania waanze kuwafahamu viongozi wao wajao na hata aina ya sifa wanazoweza kuwa nazo. Inawezekana kabisa kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee mmoja wao kugombea au la, lakini hapa ninachoangalia ni kwamba tayari wananchi watakuwa “wamesogezwa karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata akiletwa mgombea kutoka wapi, walau wananchi watakuwa wanajua wafanye uamuzi wa namna gani.
Leo nahitimisha hoja ya wagombea wa upinzani kwa kutoa sifa 10 za mgombea urais bora kutoka upinzani ambaye anaweza kupigiwa kura nyingi na Watanzania na hatimaye kuwa rais mpya wa Tanzania:
1. Mwenye umaarufu/umashuhuri na anayekubalika
Sifa hii ni muhimu, unapokuwa nje ya dola na nje ya chama tawala siyo rahisi kukishinda chama kinachoongoza Serikali. Umaarufu, umashuhuri na kukubalika ni mambo ya lazima. Ukitizama historia ya dunia na hata Afrika, vyama vikongwe vilipoondolewa madarakani waliofanya hivyo walikuwa wapinzani mashuhuri. Umuhimu wa sifa hii ni kuwa walau mtu maarufu na mashuhuri au anayekubalika, tayari amewekeza “mbegu” kwenye mioyo ya wananchi, wanaweza kumwamini ili waondoe hatima ya nchi mikononi mwa chama kilichowaongoza kwa miaka 50 na kuiweka mikononi mwa watu wapya. Wananchi wasipomwamini kiongozi wa upinzani anayekuja kwa sababu wanamkubali, ndipo huzuka ile kasumba ya “tupige kura kwenye zimwi likujualo”.
Hatari ya sifa hii
Umaarufu, umashuhuri na kukubalika vitaweza kufanya kazi kwa upinzani ikiwa mgombea husika hatatumia mwanya wa kukubalika kwake kujenga kiburi na hatimaye kuwasaliti wananchi. Ndiyo kusema kuwa vyama vya upinzani vitapaswa kuchagua mtu bora ambaye atatimiza matakwa ya wananchi “hata kama ni maarufu kuliko jua”.
2. Atakayebeba ajenda bora na kuifafanua vizuri
Kubeba ajenda bora na kuwa na uwezo wa kuifafanua kwa lugha rahisi ni jambo la muhimu kwa mtarajiwa kutoka upinzani. Moja kati ya makosa makubwa ya vyama vya upinzani katika bara la Afrika ni kutaka kubeba ajenda nyingi na kumrundikia mgombea urais, nakubali kuwa Afrika ina matatizo katika kila sekta ya maisha ya mwanadamu, lakini lazima iwe na vipaumbele vinavyowaumiza wananchi. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na ajenda bora kuliko ile ya CCM na atapaswa kuwa na uwezo wa kuifafanua akaeleweka na mipango ya utekelezaji wake ikawa siyo ya “kusadikika”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale inapotokea kuwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani anazunguka nchi na ajenda iliyo bora kabisa lakini utekelezaji wake ukifanana au kushabihiana moja kwa moja na ule wa mgombea wa CCM. Wananchi wakiona upinzani unahubiri mipango na mbinu zilezile za CCM wataamua pia kuchagua “shetani wanayemjua” ili kujiweka kwenye mazingira ya usalama zaidi. Hivyo, ajenda ya mgombea bora wa upinzani na utekelezaji wake vinapaswa kuwa “vya kipekee”.
3. Mwenye uzoefu na rekodi ya uchapakazi
Uzoefu wa uongozi na uchapakazi unaofahamika ni jambo la msingi kwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani. Vyama vya upinzani haviwezi kushinda uchaguzi na mgombea bora vitakayekuwa naye ikiwa mtu huyo si mzoefu na mchapakazi anayefahamika, mtu mwenye kujali wengine katika kazi lakini ambaye wananchi wataamini kuwa huyu atasimama pamoja na sisi usiku na mchana kuleta mabadiliko ya nchi.
Katika siasa, wananchi hupaswa kwanza kuamini na kisha hufanya uamuzi. Ikiwa mgombea bora wa urais wa upinzani hatakuwa na rekodi za uzoefu wa utumishi (katika taasisi za dini, serikali, vyama vya siasa na nyinginezo) si rahisi kumuuza kwa wananchi. Pia, ni lazima awe ni mtu ambaye rekodi zake zinatajwa kuwahi kuleta mabadiliko makubwa mahali alipofanya kazi.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii hupaswa kuelezewa na kufahamika kwa wananchi kutoka kwa timu za kampeni za wagombea, wakati mwingine wapambe wa wagombea huchukua muda mwingi kutaja elimu ya mgombea wakidhani wananchi wanachagua elimu, kumbe elimu ni jambo moja tu kati ya sifa 100 za kiongozi. Ikiwa sifa hii muhimu haielezwi kwa uwazi kwa wananchi na hasa kwa kutaja rekodi bora za mgombea wa upinzani, wananchi wanaweza kumpa kisogo.
4. Mwenye uadilifu usio na shaka
Mgombea bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa kuwa na uadilifu uliotukuka, usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana kuwa, awe ni mtu ambaye uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa Taifa zima. Awe na rekodi za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina maana kuwa, wananchi wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka haraka wasimame na kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”. Marais wengi walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na Marekani kwa kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa hii.
Hatari ya sifa hii
Kigezo hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo uelewa wa wananchi vijijini na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu nao huweza kuchafuliwa ndani ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si ajabu mgombea akawa hata na uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili kimchafue mwenzake, sifa za mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope. Vyama vya upinzani vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha uadilifu wa mgombea wake unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na propaganda za CCM.
5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua uchumi
Moja ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania ni usimamizi wa uchumi. Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa kutekeleza mipango yetu kwa sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila dakika na ambao hauna dira. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu ambaye akisimama na kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote wanamwelewa, kwamba “naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa umaskini wa nchi”.
Hatari ya sifa hii
Ni pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango kabambe ya uchumi lakini yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa umaskini, lakini pia ni pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi. Katika nchi maskini, wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi ili kuwahakikishia wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza kutekelezeka kwa wakati
6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa
Rushwa ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa mtu wa kipekee ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano dhidi ya rushwa, ndogo na kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba anapiga vita rushwa, bali anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu ambaye yuko mbali kabisa na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani watatafuta mgombea wa namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule wa CCM, kwamba ukiwaweka pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme “…naam huyu wa upinzani anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”
Hatari ya sifa hii
Ikiwa upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika mapambano ya rushwa lakini ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya mipango ya upinzani inapaswa kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya ya usimamizi wa mapambano dhidi ya rushwa na hata kueleza watu watakaokuwa na sifa za kufanya kazi na mifumo hiyo.
7. Asiyependa kulipiza visasi na atakayefuata sheria
Jambo hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka upinzani anapaswa kuwa na sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa kutokuwa na tabia ya kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa ya sheria katika utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya kisheria ambayo ni lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate, mfano, wizi wa pesa za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi upo, lazima watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala kupotea”. Lakini kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo yalikuwa yanatendwa na uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na zisizo na maana, hayana haja ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.
Hatari ya sifa hii
Wananchi wengi huhofia masuala ya usalama iwapo vyama vipya vitaingia madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo hupoteza usalama ni “kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani vinawajibika kuwa na mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya nyuma ya kiutendaji, ila atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa makusudi na kwa kutofuata sheria.
8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi
Tangu tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika kwa kuwa na mifumo mibovu na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni janga kubwa. Rais bora ajaye kutoka upinzani ana kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi katika kila eneo ili mifumo ifanye kazi kwa mbio na kwa tija kubwa zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka ya 1990 na bado wako gerezani bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari Kilombero na huko bei ya sukari ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni matatizo makubwa ya kimfumo. Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuja kubadilisha kabisa mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa bahati nzuri, upinzani unaweza kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo havikuwahi kuongoza Serikali na vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.
Hatari ya sifa hii
Ubadilishaji wa mifumo ukifanywa haraka na kwa pupa, utaingilia na kuvunja hata mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na kukomaa kwa upande chanya. Ni jukumu la mgombea bora wa upinzani na timu zake kutambua mifumo yote ya utendaji katika sekta za jamii na kubainisha tangu wakati wa kampeni, ipi itavunjwa na ipi itarekebishwa ili kutoleta hofu yoyote kwa wapiga kura.
9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba
Suala la katiba mpya ni ajenda muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe kuwa na busara za kutosha na msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba na hasa mchakato wa Katiba Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na misimamo ya wananchi katika suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama katiba itapitishwa au la na hatuelewi kama wananchi wanaikubali au wanaikataa. Nani atatuvusha na kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo mgombea bora wa urais kutoka upinzani.
Hatari za sifa hii
Msimamo wowote ule wa mgombea urais wa upinzani katika jambo hili unaweza kuwa na athari chanya au hasi kulingana na namna wananchi wanavyolitazama suala la katiba. Kama mgombea huyu atakuwa na msimamo katika kuikataa Katiba Inayopendekezwa na kwamba ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi, jambo hili peke yake litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa kinyume chake, litakuwa na athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama athari yenyewe ni chanya au hasi.
10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa
Moja ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni kuliwakilisha Taifa katika masuala ya kimataifa. Rais bora kutoka upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya masuala ya kimataifa, si kuishi Ulaya na Marekani, lakini kuwe na ushahidi wa kutosha kuwa amewahi kushiriki katika baadhi ya shughuli muhimu za kimataifa na kwamba huenda hata kimataifa yeye ni mtu bora. Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea mwenye sifa hii pia, ni jukumu la upinzani pia kuwa na mtu ambaye amejipanga vyema kimataifa na mambo aliyoyasimamia kimataifa pia yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali, yanaweza kuwa ya kijamii, ya kitaasisi au ya kitaaluma.
Hatari ya sifa hii
Sifa hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za kuisaidia CCM, kwamba ndicho chama pekee chenye watu waliofanya kazi za kimataifa na wataifanya Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea ambaye tayari wananchi wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na shaka ili kusiwe na tabu ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura juu ya eneo hili.
HITIMISHO
Andiko hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote muhimu za kiongozi bora kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha Taifa. Nimechokoza mjadala wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya kuongoza Serikali si nyepesi, inataka kujipanga kila idara na kuwathibitishia wapigakura kuwa mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura huwa ni kutafuta namna gani watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati nzuri vyama vya upinzani katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya kupigiwa mfano inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji