Lindi. Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amefafanua sakata lake la kuchukuliwa na
askari wa Takukuru kwa mahojiano muda mfupi baada ya kuchukua fedha
benki, akisema alikuwa akielekea kulipa mawakala.
Nape,
anayewania ubunge wa Jimbo la Mtama, jana mchana aliamriwa na maofisa
wa Takukuru kufika ofisi zao baada ya kutoka kuchukua fedha benki ya NMB
eneo la Misonobarini mkoa Lindi.
“Ninadhani hawa jamaa
walipotoshwa. Mimi nimekwenda zangu benki kuchukua fedha, lengo langu
ni kuwalipa mawakala,” alisema Nape jana jioni alipopigiwa simu na
Mwananchi kutoa ufafanuzi wa sakata hilo.
“Wakaja hawa
jamaa, wakajitambulisha kuwa wanatoka Takukuru, wakaniuliza ‘mbona
ninachukua fedha nyingi kipindi hiki?’ Nikawaambia ‘nakwenda kulipa
mawakala, na fedha zenyewe ni hizi Sh3.6 milioni’.
“Basi,
tukatoka taratibu tukaenda ofisini kwao, ni karibu tu na benki.
Wakanihoji hata haikumalizika nusu saa, niliwaambia nataka kulipa
mawakala wangu, tena fedha zenyewe hazitoshi, wako zaidi ya 100.”
Nape aliongeza kusema kuwa walimkamata na akawaambia kuwa yeye ni mwadilifu.
“Halafu ninyi, mnaacha marushwa makubwa makubwa huko, watu wanahonga halafu mnamvizia Nape masikini kwa Sh3mil?,” alisema.
Nape
alielezea kufadhaishwa na tukio hilo akidai kuwa limetengenezwa kwa
ajili ya kumchafua hasa kwa kuwa leo kuna kura za maoni, lakini akasema
anaamini yeye ni msafi.
Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa
Lindi, Stephen Chami alikiri kumhoji Nape, lakini akasema walijiridhisha
kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kulipa mawakala.
“Unajua
tuna watu wetu, kwenye maeneo mbalimbali hasa kipindi hiki cha
uchaguzi, tumeweka watu wetu maeneo mengi, tunataka kukomesha rushwa,”
alisema.
Kilango ageuka ‘mbogo’
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne
Kilango Malecela juzi aligeuka mbogo baada ya kuzushiwa katika mitandao
ya kijamii kuwa anashikiliwa na polisi.
Taarifa hizo
zilizosambazwa jana, zilidai kuwa Kilango alikamatwa juzi saa 5:00 usiku
katika eneo la Dimbi, kijiji cha Bagamoyo kwa tuhuma za kutoa rushwa,
madai ambayo ameyakanusha.
Hata hivyo, Kilango
alipoulizwa jana alisema tuhuma hizo ni uzushi uliotengenezwa na baadhi
ya washindani wake wakiamini kwa kufanya hivyo watamvurugia katika kura
ya maoni inayofanyika leo.
“Sijakamatwa na wala sijaona
hata polisi mmoja nyumbani kwangu. Nimelala nyumbani kwangu jana (juzi)
na leo (jana) nimeamka nyumbani kwangu na niko kwenye mikutano ya
kuomba kura,” alisema.
Kilango aliongeza,”Sasa hivi
nimetoka kuomba kura Mtii nilikuwa peke yangu wagombea wanzangu
wameingia mitini. Niko Bombo sasa hivi (saa 9;00 alasiri) ndio wanakuja
nishapiga bao.”
Kwa mujibu wa Kilango, baadhi ya
wagombea wamekuwa wakifanya kampeni zisizo za kistaarabu kwa kuandaa
vijana aliodai wamepewa pombe ili wamzomee katika baadhi ya maeneo
aliyopita.

No comments:
Post a Comment