Sunday, 14 June 2015

Zinakaribia siku za CCM kula gizani machungwa yaliyooza

Kuna kisa cha msafiri mmoja aliyeomba mahali pa kulala kwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa ili kesho yake aendelee na safari yake. Alifika saa 5.00 usiku na kwa kuwa mjumbe alikuwa amekwisha kula, alichofanya ni kumwandalia msafiri huyo mahali pa kulala, basi.
Alishukuru. Mlo wake usiku ule ulikuwa machungwa sita aliyonunua njiani. Loo, alipokata la kwanza, lilikuwa limeoza, alitupa kwenye kona. Lahaula, alipochukua la pili, nalo lilikuwa limeoza. Balaa, kumbe yote yalikuwa vivyo hivyo.
Haraka aligundua kwamba kilichosababisha akaona machungwa kuwa yameoza ni kibatari, hivyo, alikizima, akachukua machungwa yale na kuanza kula gizani, akalala. Heri angelala na njaa kabisa maana kesho yake aliharisha sana njiani na kutapika; we acha tu!
Kisa hicho kinakaribia kujirudia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho makada wake waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuwania urais wanachafuana na kujiozesha. Akisimama huyu anasema yeye tu anafaa, akisimama yule anadai wengine wote bomu, sasa atapatikana wapi aliye bora?
Edward Lowasa alijizuia alipotangaza nia, lakini Charles Makongoro alimshona barabara Stephen Wasira. “Mzee Wasira alifanya kazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Nyerere aliondoka yeye akabaki, bado yupo. Akaja Ali Hassan Mwinyi akaondoka, yeye yupo….na sasa huyu Mzee Wetu Jakaya Kikwete anaondoka, atamuaga yeye atabaki yupo!” Hebu jiulize, ikitokea ‘Bwana Yupo’ ameteuliwa itakuwaje?
Frederick Sumaye hakutafuna maneno, alisema; “Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni, nitampisha (katika mbio za urais).” Alishangiliwa na wafuasi wake huku wakimwambia; “Hakunaaaa.”
Bernard Membe aliwaambia wanaCCM mkoani Lindi; “Nimetafakari sana, nimeona ninatosha kwa nafasi hii nyeti…, nafasi adhimu na si ya mzaha japo naona wapo wanaofanya mzaha. Nimeangalia nikaona hakuna mwingine wa kufanana na mimi.” Halafua akadai, “Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere huko aliko atafurahi endapo nitakuwa rais.” Yaani Nyerere afurahie Membe kuwa rais kuliko hata mtoto wake Makongoro?
Prof Sospeter Muhongo alisema; “Nafahamu... sidhani kama kuna mtu mwingine anafahamu kama mimi. Mkinipa ridhaa yenu wanaCCM, nitahakikisha tunatumia vyema fursa hizo kwa ajili ya manufaa ya uchumi wa Taifa hili….Mtu wa kufanya yote haya ndani ya CCM ni mimi, mnanijua vizuri…”
Samuel Sitta alijipigie debe kwa kusema; “Kwa kifupi ninao uelewa na uzoefu unaolingana na changamoto za kipindi kigumu cha miaka mitano ijayo yenye mwelekeo wa kutikisa misingi ya utawala wa nchi yetu… kwa uimara wangu wa uongozi, nitajumuisha nguvu na maarifa ya wananchi ili tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za maendeleo kwa ufanisi na tija zaidi.”
Mwigulu Nchemba alisema; “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati.”
Kauli hizi zimetolewa kirejareja sana, lakini zitakuja kuwa na madhara makubwa mbele ya safari ndani na nje ya CCM kuwaaminisha wapigakura kwamba “chungwa teule” halijaoza kiviiile. Hapo watajitahidi kupiga msasa na kupinga methali isemayo “samaki mmoja akioza wote wameoza”.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na mkutano mkuu wa CCM walioshiriki mwezi huu, kuwaunga mkono makada wanaowapenda wawe marais, ndiyo mwezi ujao, watashiriki kumpitisha mmoja akapambane na wa Ukawa kutafuta tiketi ya kuishi Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Nani akemee? Wazee wa kukemea walijazana Arusha, Butiama, Mwanza, Lindi, Mbeya na kwingineko kuwapiga ‘tafu’ watangazania.
Kingunge Ngombale-Mwiru, mmoja wa makada wenye hekima wanaotegemewa kutoa ushauri ndani ya CCM yuko katika Timu Lowasa. Siku Lowasa alipotangaza nia mjini Arusha, Kingunge alikuwapo na alitoboa siri ya Halmashauri Kuu akisema, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete aliwataka wale wenye ugomvi kutafuta suluhu. Vyema. Je, yeye kuwa kwenye Timu Lowasa ni kusaidia suluhu ipatikane?
Lowasa mwenyewe yuko tayari kwa suluhu? Akijibu maswali ya wahariri kuhusu kutofautiana na wenzake alisema; “…Kama kuna mtu ambaye hanipendi ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi.” Siku alipochukua fomu alisema, “Naamini katika ushindi na sina mpango wa kushindwa.” Waandishi wa habari walipomuuliza kama yupo tayari kushirikiana na wanasiasa wanaompinga sasa, aliwajibu; “Nitavuka daraja nitakapofika.” Mmh!
Ndiyo maana nasema zinakaribia siku za CCM kula gizani chungwa lililooza na kununua msasa ili kulitakatisha kabla ya kuliuza kwa wananchi.
0658 383 979

Wagombea waisuta Serikali kwa rushwa

Dar es Salaam. Makada wa CCM waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na chama hicho kuwania urais, wameeleza jinsi rushwa, ufisadi na udhaifu katika ukusanyaji kodi huku wakijinadi kuwa wao ndiyo wataondoa uovu huo iwapo watapitishwa kushika nafasi hiyo ya juu kisiasa.
Lakini hakuna hata mmoja aliyeiponda Serikali kwa kushindwa kudhibiti rushwa, ambayo baadhi walishasema kuwa imekithiri hata kwenye chama hicho tawala, huku mmoja akisema kuwa iwapo CCM itampitisha mlarushwa, atajiondoa.
Kati ya waliotangaza nia na kuchukua fomu, makada 11 ni mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne wakiwamo mawaziri waandamizi walioshika nafasi za juu na waliofanya kazi katika awamu zote nne.
Pia wamo makada waliokuwamo kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, lakini wakaondoka kwa sababu tofauti, huku kundi jingine likihusisha watendaji wakuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Lakini bado tatizo hilo la rushwa limekuwa likitumiwa na makada hao wa CCM wanaowania urais wakati wakijinadi kwa wanachama wao kwamba watafumua mfumo uliopo, kusuka upya sheria na kuimarisha taasisi za fedha ili watuhumiwa wakubwa wa rushwa wafikishwe kortini na kufungwa, badala ya kuwakamata walarushwa wadogowadogo pekee.
Katika hotuba zao wakati wanatangaza nia mbele ya umati wa wafuasi wao na mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, makada hao, mbali ya kueleza mikakati tofauti ya namna ya kuimarisha uchumi wamekosoa mfumo wa sheria kwamba unawalinda mafisadi wakubwa ambao hawakamatwi hadi kwa kibali maalumu.
Kwa mfano, akitangaza nia ya kuwania urais kijijini kwao Butiama, Charles Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema anaomba kibali cha kuisaidia CCM ikomeshe rushwa, na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe Watanzania, anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.
“Kosa la Rais Jakaya Kikwete ni kuwapenda sana marafiki zake. Kwa bahati mbaya, baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka,” alisema Makongoro ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliwaambia wafuasi wake mkoani Lindi kwamba ili kutekeleza utawala bora, hawezi kukaa kimya kuona rushwa, ubadhirifu, ufisadi vikichukua nafasi katika utawala wake.
“Ninawatumia salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha Watanzania wanachukia rushwa na kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na mpokeaji rushwa. Kama ni watumishi wa umma, watakwenda na maji...,” alisema mbunge huyo wa Mtama.
Ahadi ya kukomesha rushwa pia ilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyesema kwamba anataka kulifanyia Taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
“Ili kukomesha tatizo la rushwa, hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” alisema Sitta kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, Tabora.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema akifika Ikulu, ili kupambana na rushwa, “nitafanya mabadiliko ya kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii ikiwamo kuipa meno Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani”.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira alionyesha kukiri kuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuwania urais, wamo wenye kashfa za rushwa, lakini akajitenga nao kujionyesha kuwa hana doa hilo.
“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea,” alisema waziri huyo mkongwe na kuongeza:
“Kumbukeni sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyinginezo.”
Wasomi wawashangaa
Lakini kauli na ahadi hizo za makada hao wa CCM wanaotaka kuingia Ikulu zimewashangaza wachambuzi waliofuatwa na Mwananchi ili kutoa maoni yao kuhusu hoja za wagombea.
Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema wengi waliotangaza nia ya kuwania urais wanatoka kwenye mfumo wa rushwa, hivyo itakuwa kazi ngumu kwao kuiondoa. “Tanzania imefikia ngazi ambayo rushwa imekuwa mfumo wa utawala. Ikifikia hatua hiyo kuindoa ni kazi kubwa kwa sababu kupiga vita mfumo si suala dogo, hawa watiania walishindwa huko serikalini, watawezaje sasa?” alihoji.
Alisema wengi kati ya wagombea hao wanatoka katika mfumo wa rushwa ambao wameujenga wenyewe, hivyo si kazi rahisi kuimaliza kwa sababu kuna kulindana na kustahimiliana.
“Kulindana ni utamaduni wa mfumo huo wa rushwa. Ndiyo wameujenga na walikuwa ndani ya mfumo, ndiyo maana wanashindwa kueleza watatumia mbinu gani
kuondoa mfumo huo,” alisema.
Alisema anahitajika mtu shupavu kuiondoa rushwa hapa nchini kwa sababu imeshaota mizizi kwenye mfumo wa utawala, na kwamba kusema tu wataimaliza hakuna ukweli wowote.
“Ufisadi unaofanywa na viongozi wa Serikali, vigogo na wanasiasa zina athari kubwa kwa uchumi wa nchi hii,” alisema Profesa Mpangala.
Mawazo hayo yanalingana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Hamad Salim ambaye alisema ni vigumu kwa wanaotaka kuwania urais kuimaliza rushwa kwa sababu wote wanafanya kazi katika mfumo uliojaa rushwa.
“Wao wenyewe wanaingia madarakani kupitia mfumo wa rushwa, sidhani kama wataweza kuung’ata mkono ambao unawalisha. Kama mchakato mzima wa kuingia madarakani kama vile kuchukua fomu, kupiga kura, kutafuta wadhamini wote umejaa rushwa, wataweza kuiondoa?” alihoji.
Alisema ahadi wanazozitoa watia nia ni vigumu kutekelezeka kwa sababu wanapambana na mfumo wao wenyewe na kazi ya kuumaliza ufisadi si ya mtu mmoja wala ya siku moja.
Salim alisema inashangaza baadhi ya watangazania kukusanya watu wanaowaunga mkono, kuandaa kampeni na kuandaa watu wa kuwashangilia.
Alisema watangazania hao wanatoa ahadi zao kama kampeni tu na wakiingia madarakani hawatafanya kazi kulingana na walichoahidi bali kwa kuangalia ilani ya CCM.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa UDSM, Dk Benson Bana aliwataka watangazania hao kuacha kutumia kigezo cha rushwa kama njia ya kupata kura na badala yake wazungumzie sera nyingine.
Dk Bana alisema Watanzania hawatamchagua kiongozi kwa sera zake za kutaka kuondoa rushwa kwani nao wanafahamu kuwa CCM imejaa rushwa.
“Watanzania hawamchagui mtu kwa kigezo cha kupambana na rushwa, hicho ni kimbelembele tu, waache kimbelembele,” alisema.
Dk Bana pia alisema watangazania hao waiache Takukuru ifanye kazi yake na wasiwadanganye wananchi kuwa wao ni mabingwa wa kupambana na tatizo hilo.
Lakini mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM) kitivo cha kompyuta na mifumo ya hesabu, Dk Eliamani Sedoyeka aliliangalia tatizo la rushwa kuwa ni silka na hivyo ni vigumu kuthibitisha iwapo mgombea ana au hana tatizo hilo.
Dk Sedoyeka alisema kiongozi anayesema atapambana na rushwa anatakiwa kupimwa kwa rekodi yake ya uongozi kwa kuangaliwa iwapo aliweza kukemea, kuadhibu, au kukataa rushwa katika mazingira yoyote yale.
“Kwa mfano wapo watu wanajiweka karibu na matajiri, wanapewa fedha na matajiri za kufanya kampeni, je watakuja kulipa vipi hisani za matajiri watakapoingia madarakani? Hayo ndiyo mazingira,” alisema

Wednesday, 3 June 2015

Ukawa wawaponda waliotangaza nia CCM

Sumbawanga/Dar. Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameponda tabia ya makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kufanya hafla zinazotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo.
Viongozi hao wamesema vitendo hivyo vinaonyesha kuwa chama hicho tawala hakichukii ufisadi na hivyo hakiwezi kuwa na mgombea safi.
Makada hao wamelipia muda wa matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya redio na televisheni, kufanya maandalilizi ya gharama kubwa kwenye sehemu walizotangazia nia, kuandaa vipeperushi na mabango ya thamani huku baadhi wakituhumiwa kusafirisha watu kutoka sehemu mbalimbali kuhudhuria hafla hizo.
Akihutubia wakazi wa Sumbawanga mkoani Rukwa, katibu mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa alisema Serikali ya CCM ni kama ya watu wa ukoo mmoja wenye tabia zinazofanana.
Alisema Serikali imejaa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi na kwamba, kinachotakiwa ni kuinyima kura zote wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Katibu huyo alisema wale wote wanaojitokeza kutangaza nia ni ‘mafisadi’ ndio maana wanatumia nguvu ya fedha kuwanunua Watanzania, jambo ambalo alisema ni kinyume cha maadili.
“Ni hatari sana kuwachagua viongozi kwa fedha, hawa wanataka kuliangamiza Taifa,” alisema.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema anashangaa chama kilichoasisiwa na mjamaa Mwalimu Julius Nyerere, vijana wake wanafanya sherehe kubwa kwenye jambo dogo.
“Hata mwanasiasa mkongwe Kingunge (ngombare Mwiru) anakwenda kuwa mpambe kwenye shughuli inayokiuka taratibu,” alisema na kuongeza kuwa hiyo ni ishara mbaya.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alihoji wanaotumia fedha nyingi kwenye jambo dogo, watazirudishaje.
Alisema kama makada hao walifanya kazi halali, hawawezi kuwa na fedha zinazoweza kugharimia sherehe kubwa kama hizo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mbaya wa CCM ndio unaonyesha chama hicho hakichukii mafisadi.“Kama chama kingekuwa kinachukia ufisadi, kingeandaa utaratibu wake ili watu wote wanaotangaza nia wawe na nguvu sawa,” alisema Mbatia.

Wednesday, 20 May 2015

Ufisadi huu sasa kiama

Dodoma. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amewasilisha ripoti tano za ukaguzi wa fedha kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2014 akibainisha ufisadi wa zaidi ya Sh600 bilioni katika maeneo mbalimbali na matumizi ya fedha ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ukaguzi huo ulifanywa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ufanisi wa maeneo mbalimbali.
Ripoti hizo zinaonyesha jinsi watumishi hewa wa umma wanavyoendelea kulipwa mishahara, wakiwamo wa balozi za Tanzania waliostaafu, misamaha ya kodi na ukiukwaji wa ununuzi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha katika Wizara ya Ujenzi na Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Amina Mwidau na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruk Mohamed walizichambua ripoti hizo na kueleza jinsi watumishi wa Serikali wanavyotafuna mabilioni ya fedha.
Akizungumzia ripoti hiyo katika mkutano wa pamoja na CAG, Mwidau alisema imeonyesha jinsi Sh285 bilioni za Kitengo cha Maafa zilivyotafunwa licha ya kuwa zilitengwa kwa ajili ya kufanya shughuli maalumu.
Kuhusu Wizara ya Ujenzi, alisema ililidanganya Bunge baada ya kueleza kuwa Sh262 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara, kitu ambacho kimebainika kuwa siyo kweli.
“Ukaguzi unaonyesha kuwa fedha hizo zimetumika katika mambo mengine kabisa, yaani zimetumika tofauti na hakuna maelezo ya kuridhisha,” alisema Mwidau huku akifafanua kuwa wizara hiyo inadaiwa na makandarasi Sh800 bilioni.
Misamaha ya kodi
Profesa Assad alisema ofisi yake ilibaini kasoro katika mfumo wa ufuatiliaji wa misamaha ya kodi na kusababisha ukiukaji wa matumizi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini.
Alisema mafuta yenye kodi ya Sh22.33 bilioni yaliyotakiwa kutumiwa na kampuni zilizosamehewa kodi, Geita Gold Mine na Resolute TZ Ltd, yalipelekwa kwa makandarasi wasiostahili msamaha na kusababisha hasara ya Sh22.33 bilioni,” alisema.
Alisema pia misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa, ilitolewa na kusababisha upotevu wa Sh392.7 milioni katika Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa imesamehewa kodi Sh465.2 ili kuingiza magari 28.
Hata hivyo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kati ya hizo kukusanya Sh72.5 milioni.
Pia, alisema misamaha ya Sh53.4 milioni ilitolewa kwa Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi hoteli katika Kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, lakini kampuni iliagiza magari matatu kwa kutumia msamaha na mengine matano ‘kuchepushwa’.
“Hata hivyo, ukaguzi ulithibitisha ununuzi wa gari moja tu ya Hyundai Santa. Magari mengine matano aina ya BMW na Toyota Land Cruiser Prado hayakufahamika yalipo,” alisema. CAG aliishauri Serikali izibe mianya ya upotevu wa kodi kupitia misamaha ya kodi aliyobaini katika ukaguzi wa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa misamaha ya kodi iliyotolewa.
Mashine za EFD
Alisema katika ukaguzi wa malipo na matumizi  ya mashine za kielektroniki (EFD), ofisi yake ilibaini kuwa kampuni binafsi hazitumii mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Alisema hali hiyo imesababisha malipo ya Sh4.4 bilioni kutokuwa na stakabadhi za kielektroniki kwa taasisi za Serikali Kuu na Sh4.6 bilioni kwa sampuli  22 ya mamlaka za serikali za mitaa.
“Katika suala hili, TRA ilitoza faini Sh440.8 milioni kwa wafanyabiashara ambao walishindwa kutumia mashine za EFD ambapo jumla ya Sh72 milioni zililipwa sawa na asilimia 16 na hivyo kufanya bakaa ya Sh369 milioni ambayo haikulipwa,” alisema.
Alisema pia ukaguzi ulibaini upungufu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali kama vile, malipo yasiyokuwa na nyaraka. Upungufu mwingine ni hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha zilizotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Alishauri taasisi za Serikali zisiendelee kanunua vifaa na huduma kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFD kutoa stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
“Hii iende sambamba na kuhakikisha kuwa maofisa masuuli wanaimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ikiwa pamoja na kuimarisha ukaguzi kabla ya malipo,” alisema.
Mishahara hewa
Alisema fedha zilizolipwa kwa watumishi hewa wa Serikali Kuu ni Sh141.4 milioni, “Hali hii inaendelea licha ya kuwa Serikali imewekeza kwenye mfumo wa Lawson kama njia mojawapo ya kudhibiti hali hiyo,” alisema. Hata hivyo, alisema suala hilo linazidi kupungua ikilinganishwa na mwaka jana. Lakini alisema Sh1.01 bilioni katika halmashauri 36 zililipwa kama mishahara kwa watumishi waliotoroka kazini, waliofariki, waliostaafu na kufukuzwa kazi.
Alisema kutokana na watumishi hewa, Sh845 milioni za halmashauri zililipwa kama makato ya taasisi mbalimbali kama vile mifuko ya pensheni, taasisi za fedha, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na TRA kwa ajili ya wafanyakazi hao hewa.
Katika balozi
CAG pia ameeleza jinsi Serikali ilivyolipa Sh543.7 milioni kutokana na kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani.
Watumishi hao ni wa balozi za Tanzania Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani).
Ripoti hiyo inaonyesha tarehe ambazo watumishi hao walistaafu, lakini Serikali iliendelea kuwalipa huku wakiwa katika maeneo yao ya kazi, zikijumuisha kodi za majengo huku baadhi ya watumishi hao wakifanya kazi licha ya kuwa mikataba yao kumalizika.
Ufisadi Tanesco
Ripoti hiyo pia ilibaini kuwapo kwa ununuzi wa Sh3.2 bilioni uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), bila kuzingatia kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ya Sh400 milioni.
“Katika zabuni nyingine, Tanesco iliingia mkataba wa Sh340 milioni ambayo ni zaidi ya bajeti iliyotengwa ya Sh154 milioni. Ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kuwapo kwa marejeo ya bajeti kwa kiasi kilichotumika nje ya makisio,” alisema
Vyama vya siasa
Kuhusu ukaguzi wa vyama vya siasa, CAG alisema hadi kufikia Juni, 2013 vyama 21 wakati vinakaguliwa, ni 12 tu ndivyo vilivyowasilisha taarifa za hesabu.Alisema kati ya vyama 12, tisa havikuwasilisha taarifa za hesabu ambavyo ni UPDP, Tadea, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa vyama sita vya siasa vilipata hati ya shaka ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na Chauma na vya vingine vilipata hati mbaya ambavyo ni NRD, UMD, ADC, APPT, NLD na SAU.
Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa akishirikiana na Mhasibu Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), waandae mwongozo wa aina ya muundo wa taarifa za fedha utakaotumiwa na vyama vyote vya siasa.
Bajeti
Kuhusu bajeti, alisema tathmini waliyofanya kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, programu na shughuli nyingine za maendeleo katika baadhi ya halmashauri, imeonyesha kuwa hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, halmashauri hizo zilikuwa na bakaa ya jumla ya Sh29.2 bilioni sawa na asilimia 28 ya jumla fedha zilizotolewa.
Alisema kubakia kwa kiasi kikubwa cha fedha bila kutumika katika utekelezaji wa miradi kunatokana na ucheleweshaji wa kutuma fedha katika halmashauri.
Deni la Serikali
Alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka jana, deni la mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia Sh1,699 milioni na Sh975.1 milioni zilipaswa kuwa zimereshwa, lakini hadi wakati wa kuandika ripoti hiyo zilikuwa bado hazijalipwa.
Alishauri mifuko na Serikali kuzingatia na kufuata mwongozo wa uwekezaji wa fedha za mifuko ambao pamoja na mambo mengine, unatoa ukomo wa aina za mali ambazo mifuko inaweza kuwekeza.

Monday, 18 May 2015

UCHAGUZI UPINZANI 2015: Anna Mghwira, Mwenyekiti ACT- Wazalendo

Historia yake
Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kipya cha siasa, ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23, 1959 katika hospitali ya Mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao Manispaa ya Singida Mjini. (Januari mwaka huu alitimiza miaka 56).
Baba mzazi wa Anna alikuwa diwani na kiongozi wa Tanu kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji na wazazi hawa kwa ujumla walipata watoto tisa, akiwamo Anna.
Mgwira alianza safari ya kielimu katika Shule ya Msingi Nyerere Road mwaka 1968 – 1974 akaendelea na sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka 1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya sekondari (kidato cha V na VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea na masomo ya chuo kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Thiolojia (Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu Shahada ya Thiolojia mwaka 1986.
Mwaka huohuo, alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea shahada ya Sheria.
Kati ya mwaka 1987 – 1998, aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa.
Safari ya elimu ya Mghwira ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex, Uingereza ambako alianza Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa, utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za binadamu.
Mghwira ana historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti ya hapa ndani ya nchi.
Alianza siasa tangu wakati wa Tanu akiwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu katika Tanu lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa kipindi kirefu, hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za uenyekiti wa baraza la wanawake  ngazi ya wilaya na katibu wa baraza la wanawake mkoa.
Machi mwaka huu alijiunga rasmi na ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa ACT.
Aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto watatu wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mumewe hivi sasa ni marehemu.
Mbio za ubunge
Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza Januari 2012 baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa. Hata hivyo, chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari (Josh) na Mghwira alikuwa na kazi ya kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia, amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Mbio za urais
Mghwira hajatangaza kuwa atagombea urais. Ila, tafiti kadhaa na maoni ya Watanzania zinaonyesha kuwa yeye ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa ambao wamejipambanua hivi karibuni na kuonyesha uwezo mkubwa katika uwanja wa kisiasa na hivyo anapewa nafasi kubwa kuwa anaweza kupewa majukumu makubwa na anaweza kuyahimili.
Nguvu yake
Jambo la kwanza linalompa nguvu mwanamama huyu ni umahiri katika elimu. Yeye ni msomi nguli wa masuala ya sheria lakini ana shahada tatu za vyuo vikuu. Nchi yoyote ingependa pamoja na sifa nyingine, iongozwe na Rais ambaye elimu si kikwazo kwake. Kwa nchi kama Tanzania ambayo mfumo dume umewakandamiza wanawake kwa kipindi kirefu, Mghwira anakuwa mmoja wa wanawake wachache wenye uwezo mkubwa.
Kwa sababu Mghwira ni mwanamke imara na anayepambana kwa muda mrefu sasa. Kitendo tu cha yeye kuwa mwanamke ni baraka tosha kwa siasa za kisasa ambazo zinaanza kuchangamkia, kukubali na kutafuta mchango wa wanawake katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Jinsia yake inampa fursa ya kuendelea kuaminiwa zaidi katika jamii ambayo inazidi kupoteza imani na uaminifu wa wanaume.
Lakini nguvu ya tatu ya Mghwira ni uthubutu. Ameniambia kuwa hata alipoingia katika ndoa bado alithubutu kujiendeleza kielimu bila kuchoka. Alipambana na changamoto za ndoa na shule. Wanawake wengi huchagua kufanya jambo moja na kuacha mengine, yeye alikwenda nayo yote na kuyakamilisha salama. Uwezo na uthubutu huu vinamfanya kuwa mwanamama imara anayeweza kukabidhiwa uongozi wa taasisi kubwa.
Mghwira ni mtu wa kuhoji kila jambo, si mwanamama “Ndiyo Mzee”. Wakati natafuta maoni ya watu waliowahi kufanya naye kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mtendaji mmoja aliniambia kuwa ukimpa Mghwira kazi ya harakati iliyo kwenye maandishi, hataondoka kwako hadi umpe taarifa za kina za kila jambo na atakuhoji hadi utachoka.
Hata mtaalamu mshauri wa chama hicho Profesa Kitila Mkumbo ameniambia kuwa wakati wanafanya marekebisho ya katiba ya chama cha ACT walikabidhi kazi hiyo kwa jopo maalumu la wataalamu akiwemo Mghwira.
Profesa Kitila ananiambia kuwa kwa kiasi kikubwa katika timu hiyo, Mghwira ndiye aliyehoji na kutoa mapendekezo ya masuala mengi kuliko hata wataalamu wengine wa sheria ambao walikuwa wanaume.
Nilipojaribu kumfikia Mghwira kwa ajili ya kupata taarifa zake za kina na maisha binafsi, nilijikuta nashushiwa maswali matano mfululizo kiasi kwamba nilirudi kujipanga na kumtafuta tena. Huyu ni mwanasiasa wa kisasa ambaye anahoji kila jambo lililoko mbele yake, sifa hii wanaikosa wakuu wengi wa nchi.
Pamoja na kuwa na elimu kubwa, uzoefu wa kutosha wa kukaa nje ya nchi na kufanya kazi na taasisi za kitaifa na kimataifa, Mghwira ni mwanamama wa kawaida sana. Watu wa karibu naye wanamtaja hivyo. Si mtu wa kupoteza muda na mambo yasiyo na tija, anapenda kuandika makala za kuelimisha jamii, kufanya kazi na jamii na kujitolea na kujichanganya na wananchi wasio na uwezo na wenye kuhitaji msaada. Sifa zote hizi ni nguvu muhimu kwa binadamu yeyote ambaye anahitaji uongozi mkubwa wa nchi.
Udhaifu wake
Udhaifu mkubwa nilioubaini na hata kujulishwa na watu wa karibu naye ni kuwa yeye ni mwanasiasa mpole sana. Nimeambiwa kuwa ni mpole kupita kiasi na mara nyingi huwa anakuwa msikilizaji mzuri kabla hajaanza kuhoji mambo mfululizo. Moja ya sifa muhimu za Rais ajaye ni uwezo wa kuwa mpole na mkali kutegemeana na mazingira.
Kiwango cha upole cha mwanamama huyu kinazidi kiwango cha ukali alionao na naliona kama ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu Taifa letu lilipofikishwa, mara kadhaa nimesisitiza kuwa tunahitaji kiongozi anayeweza kumudu hali zote mbili.
Lakini udhaifu wa pili mkubwa wa Mghwira ni kutojijenga kisiasa ndani ya nchi. Katika siasa, bado namuona kama mchanga, hajakomaa na kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kujipa jina kubwa kwa jamii.
Mchango wake katika jamii ni mkubwa kwa sababu amewahi kusimamia masuala mengi ya kijamii na kisheria yanayoonekana, lakini ninachokisema hapa ni kuwa, chama chochote kile kina jukumu la kusimamisha kiongozi ambaye anajulikana katika tasnia za siasa. Kutojijenga na kuwa juu tokea alipokuwa Chadema nakuchukulia kama udhaifu ambao anahitaji kuufanyia kazi.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kama ACT - Wazalendo kitampitisha mwanamama huyu kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, sababu ya kwanza ya kufanya hivyo inaweza kuwa ni ile dhana ya kumpa mwanamke nafasi.
Chama anachotoka ndicho peke yake kimeweza kumpa mwanamke nafasi ya juu ya uongozi, nadhani pia bado chama hicho kinaweza kumpa jukumu kubwa zaidi ya hilo kwa sababu tayari kimeshajijengea misingi ya kuwajenga kina mama.
Lakini ikiwa Mghwira atapitishwa, uzoefu wake kimataifa na katika masuala ya haki za binadamu na kushughulika na masuala ya kijamii kunaweza kuwa moja ya sababu.
Mwanamama huyu amefanya kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii hapa Tanzania, Sweden, Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Afrika. Amekuwa mwalimu wa vyuo vikuu hapa Tanzania na msimamizi wa miradi mbalimbali ya kitaifa ya mashirika ya ndani na nje ya nchi. Uwezo na uelewa wake vinampa fursa ya juu ya kuteuliwa kugombea urais na kuonyesha kuwa kina mama wanaweza ikiwa wanapewa fursa sawa na wanaume.
Nini kinaweza kumwangusha?
Dhana ileile ya kijinsia inayombeba, pia ndiyo inayoweza kumuangusha. Ikiwa ACT kitadhani kuwa vyama vingine washindani vitasimamisha wagombea wanaume imara ambao wanaungwa mkono na mfumo dume uliotawala nchi hii, chama hicho kinaweza kumuweka nje Mgwira na kutafuta mwanachama mwingine “mwanamume” ambaye atakuwa na fursa ya kupambana na wanaume wengine kutoka vyama vingine na kuangaliwa na jamii “ambayo kwa kiasi kikubwa bado inatawaliwa na wanaume”.
Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha ni ugeni wake katika masuala ya kisiasa. Kama nilivyoeleza, Mghwira hana uzoefu wa uongozi wa juu wa kisiasa katika vyama, nadhani nafasi aliyonayo ndani ya ACT - Wazalendo ndiyo inayompa uzoefu wa kwanza wa siasa za kitaifa.
Lakini uzoefu wa jumla unaonyesha kuwa vyama mbalimbali hapa Tanzania huteua wagombea urais wake miongoni mwa wanachama wazoefu au wale waliowahi kushika madaraka muhimu katika chama kwa muda mrefu. ACT ikipiga hesabu hizi inaweza kabisa kumuweka nje mwanamama huyu.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Ikiwa hatapewa fursa ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake, anaweza kuwa na mipango mitatu mezani:
Mpango wa kwanza ni kugombea ubunge katika jimbo mojawapo Tanzania. Bahati nzuri nimejulishwa kuwa moja ya majimbo anayojipanga kugombea ni pale Singida. Ikiwa ndivyo basi, mpango huu unaweza kumfaa kwa maana ya kuzidi kujifunza na kupata uzoefu wa siasa za Tanzania kwa upana.
Lakini mpango wa pili ni kuendelea kufundisha vijana katika vyuo vikuu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa wanafunzi na wa kisheria katika jamii. Katika masuala haya ana uzoefu mkubwa nayo na itakuwa tu ni kiasi cha kuendelea pale alipoishia.
Nadhani mpango wa tatu ni kuendelea kuongoza chama cha ACT - Wazalendo. Nimeambiwa kuwa uongozi (Uenyekiti wake) unapaswa kuisha Februari, 2020. Ikiwa ndivyo nadhani ana fursa njema ya kuendelea kufanya uongozi.
Hitimisho
Mgwira ni mwanasiasa na kiongozi wa chama kipya ambacho kimeanzishwa na wanachama wengi waliotoka Chadema. Safari yake kisiasa na hata ugombeaji wa nafasi nyingine kubwa za nchi kwa namna moja au nyingine, lazima utaathiriwa na ustawi au uzorotaji wa Chadema.
Ikiwa Chadema kitazidi kukubalika kwa Wwatanzania na kuwa chama kinachoimarika zaidi kuishinda ACT, ndiyo kusema kuwa yeye na wenzake watakuwa na wakati mgumu kujipambanua kisiasa na hivi ndivyo siasa za Afrika hutizamwa.
Pamoja na sintofahamu hizo, namuona Mgwira kama mmoja wanasiasa watulivu na wenye maono mapana katika Taifa hili. Kwa maneno yake yeye mwenyewe amenieleza kuwa “Natamani siku moja nchi hii iongozwe kwa misingi ya udugu na kusaidiana, kwa misingi ya malezi ya maadili bora kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Mimi nimekulia kwenye familia kubwa sana lakini wazazi wetu walitulea sote kama ndugu na tuliishi kwa furaha kubwa, nina ndoto kuwa Tanzania ijayo ipite katika njia hiyo.”
Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumwombea mama huyu nguli wa upinzani na kumtakia safari njema katika nia zake za kisiasa ikiwamo hii ambayo ametajwa kwamba ana sifa za kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.

Urais wawagonganisha NCCR-Mageuzi, Chadema

Dar es Salaam. Chama cha NCCR-Mageuzi kimeponda kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kwamba Katibu mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk Willibrod Slaa ndiye atakayekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema mjini Moshi, hivi karibuni, Lissu alikaririwa akieleza kuwa Dk Slaa, ndiye atakayepitishwa na Ukawa kugombea nafasi hiyo.
Lakini Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa ni makosa kudhani kwamba Chadema ndicho chenye nafasi ya kusimamisha mgombea urais kupitia Ukawa, wakati bado mchakato wa kumpata mgombea haujafanyika.
Sungura ambaye pia ni miongoni mwa waasisi na mwanzilishi wa mageuzi nchini, alisema kati ya vyama vinne vilivyounda Ukawa, tayari Chadema imepewa majimbo mengi ya ubunge. “Fursa hiyo pekee imeshawapa uwezekano wa kutoa waziri mkuu kama upinzani utashinda”, alisema.
“Kwa kawaida chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu, sasa kwa namna yoyote Chadema ndiyo itakayotoa waziri mkuu, hivyo haiwezekani watoe na mgombea urais. Nawashauri wachague nafasi mojawapo,” alisema Sungura.
Sungura alisema kauli hiyo ya Lissu siyo sahihi na hailengi kujenga Ukawa, bali kuubomoa kwa kuwa haiwezekani chama kimoja kitoe rais, makamu wake na waziri mkuu. “Ni vizuri ikaeleweka mapema kwamba, haiwezekani chama kimoja kati ya vyama vinne washirika wa Ukawa, kikatoa mgombea urais, makamu na waziri mkuu,” alisema Sungura  na kuongeza:
“Kwa kuwa CUF kina nafasi kubwa ya kumtoa mgombea urais wa Zanzibar, vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, kimoja kati ya vyama hivyo kitamtoa ama rais au waziri mkuu au spika wa Bunge, kinyume chake ni tamaa inayoweza kuua Ukawa.”
Kwa mujibu wa Sungura, mageuzi chanya hayawezi kuletwa kwa ubinafsi, bali nia ya dhati ya Ukawa katika kuyatafuta.

Asimamishwa kazi kwa kumtumia JK ‘meseji

Moshi. Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa  na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.
Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa Mei 15.
Hata hivyo, bado mhasibu huyo hajarejeshwa kazini na vikao vilikuwa vinaendelea kuhusu hatua za kinidhamu zinazostahili dhidi yake.
“Wakati hayo mambo mawili yanafanyiwa kazi, menejimenti imeamua kukusimamisha kazi. Kabla hujaondoka unatakiwa ukabidhi vitendea kazi pamoja na simu ya mkononi uliyokabidhiwa,” imedai.
Ofisa Uhusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo alipoulizwa kuhusu sakata hilo alisema kwa nafasi yake, hawezi kulizungumzia.
Mhumba alipotafutwa wiki iliyopita, alikiri kusimamishwa kazi kwa tuhuma za kumtumia Rais ujumbe wa simu ya mkononi, ingawa alikanusha kuhusika.
“Maudhui hayo kama ni kweli yalitumwa, hayana matatizo. Nimeongea na katibu mkuu kumuuliza kama alipokea sms kutoka kwa Rais na kuwapa KCMC na namba ya mtumaji amekanusha,” alidai.
Hata hivyo, alidai yeye akiwa mwenyekiti wa Tughe, amekuwa akionekana kama adui pale anapojaribu kutetea masilahi ya watumishi, likiwamo suala la kutopandishwa daraja tangu mwaka 2007 hadi 2015.
“Ni kweli, watumishi hawajapandishwa madaraja tangu 2007. Sisi (Tughe) tumekuwa tukilipigania kwa sababu linachangia wastaafu kulipwa pensheni ndogo,” alisema.
“Mimi kama kiongozi wa wafanyakazi, niko tayari kupeleka ushahidi kwa mambo ambayo Tughe tumekuwa tukipambana nayo, ikiwamo mahali zilipo fedha za mashine ya CT-Scan,” alisema Mhumba.
Tawi la Tughe KCMC, limemwandikia barua katibu mkuu wa Tughe, ikiomba Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aingilie kati suala hilo ili haki itendeke.
Gama alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupigiwa simu na Mhumba akimueleza lakini alimshauri aziandikie mamlaka husika.
Gama alisema akiwa mwakilishi wa Rais mkoani Kilimanjaro, atachunguza nini kimetokea baada ya kupata malalamiko rasmi kutoka kwa Mhumba au Tughe yenyewe.

Friday, 10 April 2015

Bakora sita za Ukawa kwa CCM

Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.
Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.
Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.
Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.
Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.
Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.
Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ufisadi 
Haitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia 70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa linaweza kukiathiri chama hicho.
Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.
Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi
Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa Taifa.
Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.
“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:
“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana na uzoefu uliopo.
“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu wa chama,” alisema Dk Mallya.
Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi kupigia kura vyama vya upinzani.
“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao na kuondolewa.
Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa, umewafanya wengi kugawanyika.
“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.
Kauli ya CCM 
Kupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.
Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.
“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema Simba.
Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko vyote.
Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na makandokando yake.

Mambo sita yaliyomshinda Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi  na zaidi ameacha manung’uniko na mgawanyiko.
Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.
Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi, vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na Mahakama ya Kadhi.
Sheria ya Habari
Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.
Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013 gazeti  la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni (Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).
Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.
Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa gazeti la The EastAfrican nchini.
Katiba Mpya
Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8,      2010 siku alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa Watanzania Katiba Mpya.
Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,  akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba. Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.
Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK, likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015 Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30. Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mahakama ya Kadhi
Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.
Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.
Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.
Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.
Mgogoro Zanzibar
Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani. Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani aliyepinduliwa mwaka 1964,  Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi mwaka 1964.
Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth, kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.
Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta ya ufugaji iwe ya kisasa.
Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.
Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji katika maeneo tofauti nchini.
Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo, waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira na uhasama vimetanda kila mahali.
Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.
Vita ya ufisadi
Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima ushahidi uwepo kwa asilimia 100.
Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa kuwashughulikia.
Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya, waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.

Friday, 27 March 2015

SHERIA: Sheria gharama za uchaguzi kung’ata zaidi

Dar es Salaam. Serikali inakusanya nguvu kuhakikisha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, inang’ata wagombea wote watakaojihusisha na rushwa katika harakati zao za kusaka uongozi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watendaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamesema, utekelezaji wa sheria hiyo ulikuwa na changamoto nyingi katika uchaguzi uliopita mwaka 2010.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ofisi yake ilikumbana na  changamoto nyingi zilizofanya ishindwe kuisimamia sheria hiyo ipasavyo.
“Mwaka 2010 changamoto zilikuwa nyingi lakini tumejifunza. Uchaguzi wa mwaka huu tumeshajipanga, tunajua jinsi gani ya kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, tunajua tunahitaji ushirikiano wa karibu wa wadau ili kuweza kufanikisha jambo hilo,” alisema Nyahoza.
Nyahoza alitaja wadau ambao ofisi hiyo inatarajia kushirikiana nao katika kuisimamia sheria hiyo kuwa ni pamoja na vyama vyote vya siasa, asasi za kijamii, waandishi wa habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Ushirikiano huu unaanza kuimarishwa kabla ya uchaguzi. tumebaini kwamba wadau hawa wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya namna wanavyoweza kushiriki kufanikisha utekelezaji wa sheria hii, pia kutakuwa na simu maalumu za kuripoti matukio yatakayokuwa kinyume,” alisema. 
Kauli ya Takukuru 
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikiri kuwepo kwa mkakati wa kuunganisha nguvu hizo, licha ya kukabiliwa na changamoto ya rasilimaliwatu.
“Ni kweli hata sisi tumeona kuna umuhimu wa kushirikiana katika kufanikisha jambo hili, ingawa kuna changamoto ya rasilimali watu, tunaamini kazi zitafanyika kwa namna ambayo itadhihirisha dhana ya kuwapo kwa Takukuru,” alisema Dk Hoseah.
Dk Hoseah pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuepuka kuuza haki zao za kuchagua viongozi bora kwa kudanganywa na zawadi za kanga, fulana, kofia na fedha. 
Sheria ikoje?
Ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake wa 18, uliofanyika Januari 2010. Sheria hiyo  imeweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato, matumizi  na gharama za kampeni na uchaguzi wa vyama vya  siasa na wagombea.
Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 17, 2010 ili iweze kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kwa lengo la   kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.
Madhumuni ya kuwekwa Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kujenga mazingira yatakayowezesha kuwapo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya kampeni, pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea na uchaguzi wenyewe kwa ujumla.
Sheria hii imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo ni jina, tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.
Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.
Sehemu ya  tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi, uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo vyama vya siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.
Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, matumizi ya gharama kwa vyama na taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.
Sehemu ya tano ya sheria hii inahusu masharti yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Sehemu ya sita ya sheria hii inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.
Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.
Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapigakura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.
Sehemu ya nane ya sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya vyama  vya siasa ili kuoanisha masharti  ya sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi.